Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 6/22 kur. 26-27
  • Roboti Yachunguza Mihiri

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Roboti Yachunguza Mihiri
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuchunguza Mihiri
  • Ujasiri na Uchunguzi
  • Kuzuru Tena Sayari Nyekundu
    Amkeni!—1999
  • Kuitazama Mihiri kwa Ukaribu
    Amkeni!—2009
  • Kujua Yaliyo Katika Habari
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Dini Yangu Ilikuwa Sayansi
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 6/22 kur. 26-27

Roboti Yachunguza Mihiri

MIMI na familia yangu tulisisimka tulipotazama roketi iliyobeba chombo cha angani kiitwacho Mars Pathfinder ikifyatuka kwenda angani kutoka Cape Canaveral, Florida. Tukajiuliza, ‘Je, itafanikiwa kutua kwenye Mihiri? Ni mambo yapi mapya yatakayogunduliwa?’

Kulikuwa na wasiwasi juu ya mafanikio ya Pathfinder kwa sababu safari mbili za awali za kwenda Mihiri, zilizofanywa na vyombo vya angani viitwavyo Mars Observer na Mars 96, hazikufua dafu. Isitoshe, Pathfinder ilikuwa ijaribu ugumu usio na kifani wa kutua.

Chombo hicho kilianza kuingia katika anga la Mihiri kwa mwendo wa karibu kilometa 27,000 kwa saa. Baada ya kutoa mwavuli ili kupunguza mwendo wake na kisha kufikia meta 98 kutoka ardhini, kilifyatua roketi-saidizi ili kipunguze mwendo zaidi. Wakati huo, mifuko mikubwa ambayo ilikuwa imejaa hewa ilikuwa imeandaliwa ili kukilinda chombo hicho. Siku ya Julai 4, 1997, ikienda kwa mwendo wa kilometa 65 kwa saa, Mars Pathfinder ilitua juu ya Mihiri.

Chombo hicho kiliinuliwa meta 15 hivi hewani kilipogonga Mihiri mara ya kwanza. Baada ya kuruka-ruka kama mpira mkubwa mara nyinginezo 15 hivi, kikatulia. Kisha ile mifuko ya hewa ikatoa hewa na kujirudisha ndani. Ingawa ilikuwa imetengenezwa ili iweze kujirekebisha yenyewe ikihitajika, Pathfinder ilitua kwa njia nzuri. Hatimaye ikajifungua, ikifunua vifaa vya kisayansi, antena za redio, paneli za jua, na gari dogo lililoitwa Sojourner.

Kuchunguza Mihiri

Punde si punde, kamera ya Pathfinder ikachunguza mandhari ya huko. Ikiwa katika uwanda mpana uitwao Chryse Planitia, linalomaanisha “Nyanda za Dhahabu,” karibu na eneo liitwalo Ares Vallis, au “Bonde la Mihiri,” Pathfinder ilifunua eneo lenye mawemawe lenye miinuko na mabonde na milima iliyo mbali—lililofaa sana kuchunguzwa na Sojourner. Roboti hiyo ndogo yenye uwezo sana, ambayo inatoshana na sentimeta 65, ingefanya uchunguzi kupitia kamera na vilevile kutumia spektrameta kupima kiwango cha kemikali za elementi katika miamba na udongo.

Wanasayansi na wahandisi wa safari hiyo walianzisha uchunguzi wa Sojourner. Kwa kuwa mawimbi ya redio huchukua dakika nyingi kusafiri kati ya Dunia na Mihiri, wasimamizi wa safari hiyo hawangeweza kuendesha Sojourner moja kwa moja. Kwa hiyo, Sojourner ilitegemea sana uwezo wake wa kuepuka hatari za ardhi ya Mihiri. Iliepuka hatari hizo kwa kutumia miale ya leza ili kuamua ukubwa na mahali penye miamba katika njia yake. Kisha kompyuta yake ingeiongoza ipande hiyo miamba kama ilikuwa midogo ama kuizunguka kama ilikuwa mikubwa.

Ujasiri na Uchunguzi

Ripoti katika magazeti zilionyesha mamilioni ya watu picha za Pathfinder za uso wa Mihiri. Picha mpya kutoka Mihiri zilipofika, watu duniani walitumbuizwa kwa vioja vya hiyo roboti iliyokuwa ikitangatanga, wakivutiwa na rangi za ardhi yenye mawemawe na milima-milima, na kuvutiwa na picha za mawingu na machweo kwenye anga la Mihiri. Katika mwezi wa kwanza wa safari hiyo, mahali pa Pathfinder katika Internet palijaa “maombi” milioni 500 ya watu waliotaka kujua utendaji wa chombo hicho.

Pathfinder ilitokeza habari nyingi sana, hata kushinda matazamio ya wanasayansi waliyoipeleka. Ilifanya hivyo japo ilikuwa inatenda katika hali za baridi kali kati ya digrii 0 Selsiasi hadi digrii 80 Selsiasi chini ya sufuri. Safari hiyo ilifunua nini?

Kamera na vifaa vilionyesha miamba, udongo, na vumbi zilizokuwa hewani zenye kemikali, rangi, na miundo mbalimbali, ikionyesha kwamba kumekuwa na utendaji wa miamba kwenye Mihiri. Mafungu madogo ya mchanga katika mandhari hiyo yalithibitisha kwamba pepo za kaskazini-mashariki zimekuwa zikikusanya mchanga. Anga lilionyesha mawingu ya alfajiri yaliyofanyizwa kwa barafu ndogo-ndogo. Mawingu yalipotawanyika na kukapambazuka, anga likawa na rangi nyekundu kwa sababu ya kuwapo kwa vumbi laini angani. Pindi kwa pindi, tufani za vumbi zilikuwa zikipita juu ya chombo hicho cha angani.

Hiyo Mars Pathfinder imetuonyesha mambo ya anga la nje. Marekani na Japani zinapanga kuwe na safari nyinginezo za kwenda Mihiri katika mwongo wote ujao. Chombo kingine, Mars Global Surveyor, tayari kimefika Mihiri ili kufanya uchunguzi zaidi wa kisayansi. Kwa kweli, tutapata kufahamu Mihiri zaidi tuzurupo sayari hiyo nyekundu kupitia picha zilizo katika chombo hicho cha angani cha roboti.—Imechangwa.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kuondoka

Kutua

Kwenye Mihiri

[Hisani]

Picha zote: NASA/JPL

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki