KUUTAZAMA ULIMWENGU
Umaskini na Mazingira
Japo ukuzi wa kiuchumi, zaidi ya watu bilioni 1.3 ulimwenguni pote bado hutegemea mapato yasiyofikia dola mbili kwa siku. Ripoti ya UM yasema kwamba umaskini unadumu na unazidi kuwa mbaya. Zaidi ya watu bilioni moja huchuma pesa kidogo zaidi kuliko walivyochuma miaka 20, 30, au hata 40 iliyopita. Hali hiyo nayo huchangia uharibifu wa mazingira, kwa kuwa “umaskini hufanya watu watumie maliasili zinazopatikana wakati huohuo na kuvuruga jitihada za muda mrefu za kuhifadhi maliasili,” lasema gazeti UNESCO Sources. “Kwa makadirio ya sasa, misitu katika Karibea itakuwa imetoweka kabisa katika muda upunguao miaka 50 . . . Kwa kiwango cha mataifa, hali ni mbaya hata zaidi: Filipino ina misitu itakayodumu kwa miaka 30 tu, Afghanistan miaka 16, na Lebanoni miaka 15.”
Hatari ya Kukata Tumaini
“Wanasayansi . . . wasema kwamba kukata tumaini kwaweza kudhuru moyo kama kuvuta sigareti 20 kwa siku,” laripoti The Times la London. “Uchunguzi wa miaka minne uliofanyiwa wanaume wa Finland wapatao 1,000 ambao wana umri wa makamo ulipata kwamba kukata tumaini kuliongeza hatari ya mishipa ya damu kuwa minene na migumu.” Uchunguzi huo ulionyesha kwamba hali ya akili ya mtu yaweza kuathiri sana afya yake. “Tunaendelea kupata kwamba hali za kiakili na za kihisia-moyo huchangia sana afya,” asema Dakt. Susan Everson, aliyeongoza utafiti huo. “Matabibu wanahitaji kutambua kwamba kukata tumaini kunaathiri afya na kuzidisha mzigo wa kushikwa na maradhi. Watu wahitaji kutambua kwamba wanapohisi kukata tamaa na kukata tumaini, wao wanapaswa kujaribu kutafuta msaada.”
Miaka Mingi Ndani ya Magari
Wakazi wa majiji makubwa ya Italia hutumia muda mwingi sana wakisafiri kwenda na kurudi kutoka nyumbani hadi kazini au shuleni. Wanatumia muda gani? Kulingana na Legambiente, shirika moja la mazingira la Italia, wakazi wa Naples hutumia dakika 140 safarini kila siku. Tukidhania kuwa wastani wa muda wa kuishi ni miaka 74, Mkazi wa Naples atapoteza miaka 7.2 ya maisha yake ndani ya gari. Mkazi wa Rome, ambaye hutumia dakika 135 kusafiri kila siku, atapoteza miaka 6.9. Hali hiyo bado ni mbaya katika majiji mengine. Watu katika Bologna watapoteza miaka 5.9, na wale wa Milan miaka 5.3, laripoti gazeti La Repubblica.
Saa ya Mashariki ya Kati
Mabadiliko ya saa yaweza kuzusha matatizo sana katika Mashariki ya Kati. Mfano mmoja ni Iran, ambayo kwa miaka mingi “imepima saa yake iwe muda wa saa tatu na nusu mbele ya saa ya ulimwengu badala ya kupima saa kamili bila dakika zozote juu, kama ilivyo na nchi nyingi,” lasema The New York Times. “Kwa mfano, ili kuweza kusikiliza Habari za Ulimwengu za Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC za saa 11:00 alfajiri, ni lazima ufungue redio saa 2:30 asubuhi na kujaribu kupuuza kengele za saa ya Uingereza ambayo haiambatani na yako.” Ingawa desturi ya huko ni kuokoa saa moja katika mwisho-juma wa mwisho wa mwezi wa Septemba, mwaka uliopita Israeli ilifanya badiliko hilo Septemba 13. Ni vigumu kujua pia siku zipi ndizo mwisho-juma. Nchi nyingi katika Ghuba ya Uajemi huchukua Alhamisi na Ijumaa kuwa siku za mapumziko. Lakini, nchini Misri na jirani zake, Ijumaa na Jumamosi ndizo siku za mwisho-juma, na Lebanoni ni Jumamosi na Jumapili. “Kwa mfano, msafiri anayepanga kufika Abu Dhabi Jumatano adhuhuri, kisha aende Beirut Ijumaa jioni atafurahia mwisho-juma wenye siku nne. Mtu apendaye kufanya kazi ahitaji tu kupanga safari yake kinyume,” lasema Times.
Hofu kwa Lugha ya Kifaransa
Wawakilishi kutoka nchi zinazosema Kifaransa hivi majuzi walihudhuria mkutano wa siku tatu uliofanywa Hanoi, Vietnam, ili kusherehekea “kutumika kwingi kwa Kifaransa,” laripoti gazeti la kila siku la Paris Le Figaro. Kifaransa huzungumzwa kwa ukawaida na zaidi ya watu milioni 100. Kifaransa kilipotia fora katika karne ya 17, kilikuwa lugha iliyopasa kutumiwa na mabalozi wa kimataifa. “Katika Ulaya iliyogawanyika, vita na mapigano madogo yalimalizwa kwa mikataba iliyoandikwa katika Kifaransa,” lasema gazeti hilo. Lakini, sasa lugha ya Kifaransa “inang’ang’ana itambuliwe ulimwenguni.” Kuvuma kwa Kiingereza hasa kikiwa lugha ya biashara kumeangusha Kifaransa. Ili kujaribu kuinua Kifaransa, rais wa Ufaransa alitia moyo kuendelezwa kwa lugha ya Kifaransa katika mfumo mkuu wa kompyuta wa habari. Lakini, mwanasiasa mmoja akihofia wakati ujao wa Kifaransa, alisema: “Umma, vyombo vya habari, au wanasiasa hawana hamu kuzungumza Kifaransa ulimwenguni kote. Ukosefu huo wa upendezi umejitokeza zaidi katika Ufaransa kuliko nchi nyinginezo zote.”
Kujaribu Kumaliza Rushwa
Nchini China rushwa huitwa huilu; nchini Kenya, kitu kidogo. Mexico hutumia neno una mordida; Urusi, vzyatka; na Mashariki ya Kati, baksheesh. Katika nchi nyingi, rushwa ni jambo la kawaida, na nyakati nyingi ndiyo njia ya pekee ya kutimiza mambo yako, kupata vitu, au hata kutekelezewa haki. Lakini, hivi karibuni mataifa 34 yalitia sahihi mkataba uliokusudiwa kuondoa rushwa katika shughuli za kibiashara za kimataifa. Nchi hizo zinatia ndani washiriki 29 wa Shirika la Ushirikiano na Maendeleo ya Kiuchumi, pamoja na Argentina, Brazili, Bulgaria, Chile, na Slovakia. Mashirika makubwa ya kifedha ulimwenguni, Benki ya Ulimwengu na Shirika la Fedha Ulimwenguni, pia yanachukua hatua ya kumaliza ufisadi serikalini. Hatua hizo zilichukuliwa baada ya uchunguzi wa Benki ya Ulimwengu kuonyesha kwamba asilimia 40 ya mashirika ya kibiashara katika nchi 69 yalikuwa yakitoa rushwa. Mashirika hayo mawili sasa yanakataa kuzipa fedha nchi ambazo zinapuuza ufisadi.
Kupenda Viwavi
Viwavi aina ya mopane wamekuwa wakiliwa kwa muda mrefu na maskini katika sehemu za mashambani za Afrika Kusini, ambako viwavi hao wamekuwa chanzo cha protini. Wao ni wazao wa nondo na wamepata jina lao kutokana na mti uitwao mopane ambao wao hujilisha kwake. Miezi ya Aprili na Desemba, wanawake huwakusanya viwavi, huwatoa matumbo, huwachemsha, na kuwakausha kwenye jua. Protini zake, mafuta yake, vitamini zake, na ubora wake walingana na zile za nyama na samaki. Lakini, sasa viwavi wa mopane wanaanza kupendwa sana katika mikahawa ya Afrika Kusini. Kupendwa kwa chakula hicho kumeenea hata Ulaya na Marekani, na jambo hili limewashtua wakazi wa sehemu za mashambani wa Afrika. Kwa nini? “Viwavi wazidipo kutakikana, kuna wasiwasi kwamba viwavi hao watakuja kutoweka,” lasema gazeti The Times la London. Tayari “viwavi hao wametoweka katika sehemu kubwa za nchi jirani za Botswana na Zimbabwe.”
Je, Madhara ya Sigareti Hayawezi Kurekebishwa?
Madhara ya mishipa ya damu yatokanayo na kuvuta sigareti yaweza kudumu daima, wasema uchunguzi mmoja wa majuzi. Katika jarida The Journal of the American Medical Association, watafiti waliripoti kwamba kuvuta sigareti na kuvuta moshi unaotolewa na mtu mwenye kuvuta sigareti kwaweza kusababisha madhara yasiyoweza kurekebishwa kwenye mishipa ya damu. Uchunguzi huo ulifanyiwa wanaume na wanawake 10,914 wenye umri wa kati ya miaka 45 hadi 65. Kikundi hicho kilitia ndani wavutaji wa sigareti, watu ambao zamani walikuwa wavutaji wa sigareti, na watu ambao hawavuti sigareti lakini ambao mara nyingi hupumua moshi unaotolewa na wavutaji wa sigareti. Watafiti walipima unene wa mshipa wa damu ulio katika shingo. Nao walipima tena mshipa huo miaka mitatu baadaye.
Kama ilivyotarajiwa, mishipa ya wavutaji wa kawaida ilikuwa imekuwa migumu—asilimia 50 kwa watu ambao walikuwa wakivuta wastani wa paketi moja ya sigareti kila siku kwa miaka 33. Mishipa ya damu ya watu ambao zamani walikuwa wavutaji ilifinyaa pia, kwa kiwango cha asilimia 25 kuliko ya watu wasiovuta—wengine hata miaka 20 baada ya wao kuacha kuvuta. Watu ambao hawavuti sigareti na ambao walipumua moshi wa sigareti uliotoka kwa wavutaji walipatwa na kunenepa kwa mshipa wa damu kwa kiwango kizidicho asilimia 20 kuliko watu ambao hawapumui moshi huo. Kulingana na uchunguzi huo, yawezekana kwamba vifo vya watu wapatao 30,000 hadi 60,000 kila mwaka Marekani pekee vyaweza kuwa vimesababishwa na moshi wa sigareti uliotoka kwa wavutaji.
Hakuna Marekebisho
Baada ya miaka saba ya kazi ya urekebishaji, ile sanamu ya simba-mtu katika Misri hatimaye imeondolewa ngazi zilizokuwa zimeizunguka. “Mawe elfu mia moja yalitumiwa kati ya 1990 na 1997 ili kuifanyia marekebisho hiyo sanamu ya simba-mtu,” akasema Ahmad al-Haggar, mkurugenzi wa mambo ya kale katika eneo hilo. Lakini aliongezea kusema kwamba kazi hiyo ngumu ya kuirekebisha haikutia ndani sehemu ya uso ambayo ilikuwa imeharibika ya “sanamu hiyo kubwa ya simba-mtu ambayo ilikuwa imefanyizwa kwa chokaa.”