Kujitibu—Manufaa na Hatari
Na Mleta-habari Wa Amkeni! Katika Brazili
“ULIMWENGUNI pote soko la dawa za kujitibu linapanuka,” adai msimamizi wa kampuni kubwa ya madawa. “Watu wanataka kudhibiti afya yao wenyewe.” Ingawa yaweza kuwa hivyo, je, kuna hatari zozote unazopaswa kujua?
Bila shaka, dawa zaweza kutibu zikitumiwa vizuri. Kwa kielelezo, insulini na dawa za viuavijasumu na vilevile hata mchanganyiko usio ghali na ulio sahili wa chumvi, sukari na maji safi huokoa uhai wa wengi. Ugumu wa kujitibu huwa ni kujua wakati ambapo manufaa ni bora kuliko hasara.
Ni kweli kwamba katika nchi fulani matabibu wanostahili waweza kuwa mbali sana au ghali sana. Kwa sababu hiyo, watu wengi hutegemea maoni ya marafiki na jamaa au vitabu vya mwongozo ili kupata habari kuhusu tiba. Pia, “matangazo ya biashara hutoa wazo la kwamba kwa kununua tembe fulani tu ya dawa, unaweza kuwa na afya nzuri na hali njema,” asema Fernando Lefèvre, profesa katika Chuo Kikuu cha São Paulo, Brazili.a Matokeo yanakuwa kwamba wengi huanza kutumia dawa ili kuondoa athari za kufanya kazi kupita kiasi, lishe isiyofaa, na hata matatizo ya kawaida ya kihisiamoyo. Lefèvre aongezea hivi: “Badala ya kuboresha maisha yao, watu hujaribu kutatua matatizo yao kwa dawa za kujinunulia.” Na ni nani ajuaye ikiwa wagonjwa hata hutambua ugonjwa wao?
Mbali na kutumia dawa kutibu magonjwa kama vile kuumwa kichwa, msongo wa damu, na kuchafuka tumbo, wengi hutumia dawa ili kukabiliana na hangaiko, hofu, na upweke. “Watu hutafuta msaada wa daktari kwa sababu wao hufikiri kwamba tembe itawatibu,” asema Dakt. André Feingold. “Hata wataalamu wa kitiba huelekea kutoa maagizo ya dawa za kutumia na kupendekeza kupimwa mara nyingi. Hakuna jitihada inayofanywa ya kufahamu malezi ya mgonjwa, ambaye mara nyingi huwa na mtindo-maisha uliovurugika, uliojaa mkazo, na usiofaa.” Akiri hivi Romildo Bueno, wa Baraza la Ulimwengu la Kuzuia Matumizi Mabaya ya Madawa Yanayoathiri Akili: “Daktari huwa na muda mfupi wa kumwona mgonjwa mmoja mmoja, na daktari humwacha upesi mtu aende nyumbani, akitibu dalili peke yake.” Kutumia dawa “ndiyo njia ya [kutatua] matatizo ya jamii.” Hata hivyo, daktari mwingine atahadharisha kwamba wagonjwa wengi wahitaji maagizo yenye uangalifu ya kutumia dawa zinazoathiri akili.
Baada ya kuzungumzia “mtindo wa kutumia dawa ya Prozac,” gazeti la kila siku la Brazili O Estado de S. Paulo lasema hivi: “Tiba ambayo huwa mtindo wa muda tu, kama vile mtindo mpya wa nywele, kwa kweli, ni ya ajabu.” Gazeti hilo lamnukuu tabibu wa magonjwa ya akili Arthur Kaufman akisema: “Ukosefu wa maoni sawa ya akilini na kusudi maishani hutokeza jambo ambalo hufanya tiba yenye matokeo kuwa suluhisho la magonjwa yote.” Kaufman aongezea hivi: “Binadamu anajishughulisha zaidi na zaidi na tiba za mara moja, na kwa hiyo, kwa kuwa hapendezwi na kutafuta visababishi vya matatizo yake, yeye hupendelea kutumia tembe ili kuyatatua.” Lakini je, ni salama kujitibu?
Kujitibu—Je, ni Hatari?
“Jambo moja lenye kutokeza sana katika karne ya 20 katika uwanja wa tiba limekuwa kutokezwa kwa dawa mpya,” yasema The New Encyclopædia Britannica. Lakini pia yasema: “Labda kutiwa sumu kwingi husababishwa na matumizi mabaya ya dawa kuliko chanzo kingine chochote.” Kwa kweli, kama vile dawa iwezavyo kutibu, ndivyo iwezavyo kudhuru pia. Tembe za kupunguza hamu ya chakula “huathiri mfumo wa neva na kwa hiyo zaweza kuchochea dalili zisizofaa kama ukosefu wa usingizi, mabadiliko katika tabia, na katika visa fulani hata kuona vitu ambavyo havipo,” aeleza mwandishi Cilene de Castro. Aongezea hivi: “Lakini mtu yeyote ambaye hufikiri kwamba tembe hizo hupunguza tu hamu ya chakula anajidanganya. Tembe moja yaweza kuwa mwanzo wa tiba nyingi zisizokoma, kila tiba ikiondoa athari ya nyingine.”
Dawa nyingi zinazotumiwa kwa ukawaida zaweza kusababisha mwasho wa tumbo na hata kichefuchefu, kutapika, na kutokwa damu. Dawa fulani zaweza kuanzisha mazoea au kusababisha madhara kwa mafigo na ini.
Hata dawa za kiafya zipendwazo zaweza kudhuru. “Mtindo huu wa kutumia vitamini za ziada ni hatari sana,” aonya Dakt. Efraim Olszewer, msimamizi wa shirika la kitiba la Brazili. “Watu hawajitibu tu bali madaktari fulani wasio na ujuzi kamili wanatoa maagizo yenye kutiliwa shaka, bila kujali hatari zinazohusika.” Hata hivyo, daktari mwingine ataarifu kwamba vitamini za ziada katika viwango vinavyofaa zaweza kuwa za lazima au zenye kunufaisha katika kutibu magonjwa na upungufu fulani.
Tiba ya Kibinafsi Iliyo Salama—Jinsi Gani?
Kwa kuwa hatuwezi kumwona daktari wakati wote tunaposumbuka, elimu ya kitiba na njia zifaazo za kujitibu zaweza kunufaisha familia zetu. Hata hivyo, kabla ya kutumia utibabu wowote, ni muhimu kutambulisha ugonjwa kwa usahihi na kwa njia yenye matokeo. Ikiwa hakuna daktari karibu au huwezi kugharimia kumwona, kuchunguza kitabu kinachofaa cha kitiba kwaweza kukusaidia kutambulisha dalili za kweli. Kwa kielelezo, Shirika la Kitiba la Marekani huchapisha mwongozo wa kitiba kwa familia unaotia ndani sehemu yenye kurasa 183 juu ya chati za dalili. Hizi humsaidia mgonjwa apitie maswali ambayo yaweza kujibiwa ama ndiyo ama la. Kwa kutumia njia hii, mara nyingi tatizo laweza kutambulishwa.
Lakini namna gani daraka la madaktari? Ni wakati gani tuhitajipo kutafuta msaada wa daktari? Twaweza kuepukaje kuwa wenye wasiwasi mwingi kupita kiasi juu ya afya yetu au wenye kuipuuza? Kwa kweli, katika ulimwengu ambao maradhi na magonjwa ya kiakili yameenea, twaweza kufurahiaje afya njema ya kadiri fulani?
[Maelezo ya Chini]
a Katika nchi nyingi, hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la matangazo ya “kupatikana kwa urahisi” kwa dawa zilizokuwa zikipatikana tu kwa agizo la daktari licha ya madaktari wengi na mashirika mengi ya kitiba kuchambua hali hiyo.
[Blabu katika ukurasa wa 4]
“Hakuna jitihada inayofanywa ya kufahamu malezi ya mgonjwa, ambaye mara nyingi huwa na mtindo-maisha uliovurugika, uliojaa mkazo, na usiofaa.”—Dakt. André Feingold
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
Tiba za Mitishamba za Nyumbani
Kwa maelfu ya miaka, watu katika tamaduni mbalimbali wametibu magonjwa yao kwa mitishamba, wakitumia mimea inayopatikana shambani na misituni. Hata dawa nyingi za kisasa hutengenezwa kutokana na mimea, kama vile digitali, ambayo hutumiwa kutibu matatizo ya moyo. Hivyo, Penelope Ody, mshiriki wa Taasisi ya Kitaifa ya Dawa za Mitishamba katika Uingereza, ataarifu katika kitabu chake kwamba “kuna tiba salama zaidi ya 250 za kusaidia kutibu matatizo ya kawaida—kutoka kikohozi cha kawaida, mafua, na kuumwa kichwa kufikia matibabu maalumu ya ngozi, matatizo ya umeng’enyaji tumboni, na magonjwa ya watoto.”
Aandika hivi: “Sikuzote tiba ya mitishamba imeonwa kuwa ‘dawa ya watu wa kawaida’—tiba sahili zinazoweza kutumiwa nyumbani kwa magonjwa madogo-madogo au kuongezea tiba zaidi zenye nguvu zinazoagizwa na madaktari kwa ajili ya hali mbaya na zenye kudumu.” Aendelea kusema: “Ingawa kwa asili mitishamba mingi ni salama sana, inapaswa kutumiwa kwa uangalifu. Usipitishe vipimo vilivyowekwa au kuendelea na tiba za nyumbani ikiwa ugonjwa unadumu, unakuwa mbaya zaidi, au ikiwa ugonjwa wako haujajulikana vizuri.”—The Complete Medicinal Herbal.