Vifaru Mayatima wa Kenya
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KENYA
NI NINI hutukia porini mtoto wa mnyama akitenganishwa na wazazi wake? Yaelekea atauawa na wanyama-wawindaji. Ili kuzuia jambo hili, walinzi wa wanyama katika Kenya huokoa wanyama hao wachanga na kuwapeleka kwenye makao ya kutunzia wanyama mayatima. Mojawapo ya makao yanayojulikana sana ni yale yanayosimamiwa na Daphne Sheldrick katika Mbuga ya Taifa ya Wanyama ya Nairobi. Kwa miongo kadhaa, Sheldrick amelea na kurudisha porini wanyama wengi, kutia ndani nyati, paa, fungo, ngiri, nguchiro, tembo, na vifaru.
Mwaka jana alikuwa akiwatunza watoto wawili wa kifaru mweusi, walioitwa Magnette na Magnum. Magnette ni ndama wa kifaru anayeitwa Edith wa Mbuga ya Wanyama ya Nairobi, ambaye bado yu hai. Ndama huyu aliletwa kwenye makao ya kutunzia mayatima katikati ya mwezi wa Februari mwaka wa 1997, baada ya kutenganishwa na mama yake kwa njia fulani. Walinzi wa wanyama walipompata mamake Magnette mwishowe, siku tano zilikuwa zimepita. Kufikia wakati huo, uwezekano wa mama huyo wa kumkubali huyo ndama ulikuwa mdogo sana kwa sababu ya muda uliokuwa umepita baada ya kutengana, na harufu ya wanadamu aliyopata ndama huyo.
Magnum alizaliwa mnamo Januari 30, 1997, na ni ndama wa kifaru aitwaye Scud, aliyevunjika mguu wa mbele wa kuume, yaelekea alitumbukia shimoni akiwa kwenye mbio kali sana. Ijapokuwa jitihada kubwa sana zilifanywa ili kuponesha jeraha hilo, mifupa yake iliambukizwa, na Scud akahitaji kuuawa ili asiteseke majuma matatu baada ya kumzaa Magnum.
Kulea Kifaru
Ni rahisi kupendeza na kushughulikia vifaru wachanga, lakini kuwalea si kazi inayoweza kufanywa nyumbani. Kila baada ya saa nne wakati wa mchana, wao hunyweshwa chupa kubwa sana iliyojaa maziwa ya mtindi. Pia hula vichaka. Ingawa vifaru wachanga wana kimo cha sentimeta zipatazo 40 tu na uzani wa kati ya kilogramu 30 hadi 40 wanapozaliwa, wao huongeza uzani kwa kiwango cha kustaajabisha—wakiongeza kilogramu moja kwa siku! Kifaru aliyekomaa kabisa huwa na uzani uzidio tani moja.
Walinzi wao huandamana na Magnette na Magnum katika matembezi marefu kupitia kwenye mbuga kila siku. Matembezi haya si mazoezi tu; hutumikia kusudi la maana—kuwafanya vifaru wafahamiane na pori. Ebu tuone jinsi jambo hili hufanywa.
Vifaru hawaoni vizuri, lakini wana uwezo mkubwa sana wa kunusa na kumbukumbu la ajabu. Hivyo, vifaru hujuana kwa mara ya kwanza kwa harufu. Vifaru huweka mipaka ya eneo lao kwa kunya marundo ya mavi na kwa kunyunyizia vichaka mkojo wao.
Katika hali za kawaida, ndama hulindwa na mamake, harufu yake ya kipekee ikichangamana na ya mamake mpaka ndama mwingine azaliwapo. Kufikia wakati huo, kifaru huyo mchanga atakuwa amezoewa na kukubaliwa na jumuiya ya vifaru. Kwa wageni kama Magnette na Magnum, hali ni tofauti. Lazima waongezee mavi yao kwenye marundo ya mavi ya vifaru wanaoishi katika eneo hilo kabla ya kukutana nao ana kwa ana. Kwa hiyo wakati wa matembezi yao marefu ya kila siku, vifaru mayatima huongezea mavi yao kwenye marundo ya mavi yaliyo vichakani. Kwa njia hii harufu yao hutambuliwa, huchunguzwa, na hatimaye hukubaliwa na vifaru wa eneo hilo. Kwa hiyo, kuhamisha vifaru waliolelewa na wanadamu kwenye makao mapya ya porini, ni hatua ngumu iwezayo kuchukua miaka kadhaa.
Kuna Wakati Ujao wa Aina Gani kwa Mayatima?
Kulingana na Hazina ya Wanyama wa Pori ya Ulimwengu, katika mwaka wa 1970 kulikuwako vifaru weusi wapatao 65,000 katika Afrika. Leo wanapungua 2,500. Upungufu huu mkubwa umesababishwa na majangili ambao wamewauwa vifaru ili kupata ngozi na pembe zao. Katika biashara ya magendo, pembe ya kifaru iliyo na uzani sawa na dhahabu ni ghali zaidi. Kwa nini ni ghali sana hivyo?
Jambo moja ni kwamba katika nchi fulani katika Mashariki ya Mbali, watu wengi huamini kwamba pembe iliyosagwa yaweza kupunguza homa. Majaribio ya kemikali yameonyesha kwamba huenda kukawa na ukweli katika jambo hili ikiwa inatumiwa katika viwango vikubwa zaidi ya vipatikanavyo katika tiba za kisasa. Bila shaka, kuna dawa nyingi sana ambazo hupunguza homa.
Pembe za kifaru hutafutwa pia kwa sababu za kitamaduni. Katika nchi moja ya Mashariki ya Kati, jambia ni ishara ya uanaume inayotamaniwa sana. Jambia iliyo na mpini wa pembe ya kifaru ni yenye thamani sana hivi kwamba wanunuzi huwa tayari kulipa dola 580 kwa mpini wa pembe mpya na kulipa dola 1,200 kwa mpini wa pembe ya kale.
Kwa sababu ya ujangili, Kenya ilipoteza zaidi ya asilimia 95 ya vifaru wake kwa kipindi kinachopungua miaka 20. Mapema katika miaka ya 1990, idadi hiyo ilipungua kutoka elfu 20,000 kufikia 400 tu. Tangu wakati huo, kwa sababu ya hatua kali za ulinzi, idadi ya vifaru imeongezeka kufikia karibu 450. Sasa Kenya ni moja ya nchi tatu pekee za Kiafrika ambazo idadi ya vifaru weusi imeimarika au inaongezeka. Kwa hiyo wakati ujao wa Magnette na Magnum ni wenye kutumainika, na walinzi wao wanatumaini kwamba hatimaye watajiunga na jumuiya ya vifaru wa eneo hilo na kuishi maisha marefu ya raha mustarehe.
[Picha katika ukurasa wa 12]
Magnum (kushoto) na Magnette wakiwa na umri wa miezi minne