Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 8/8 kur. 25-27
  • Yule Mnyama Mwenye Hizo Pembe Zenye Bei

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Yule Mnyama Mwenye Hizo Pembe Zenye Bei
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kipitisha-Wakati Kipendwacho Sana
  • Ni Yupi Mweupe na Yupi Mweusi?
  • Pembe Hizo Zenye Bei
  • Vifaru Mayatima wa Kenya
    Amkeni!—1998
  • Je! Kuna Nafasi ya Kutosha Mwanadamu na Mnyama?
    Amkeni!—1993
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1990
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2015
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 8/8 kur. 25-27

Yule Mnyama Mwenye Hizo Pembe Zenye Bei

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AFRIKA KUSINI

KWA ghafula, kifaru alikuwa akishambulia kwa kasi sana. Huyo mwanamume alijirusha upande mmoja na kukimbia kuelekea mti mdogo uliokuwa karibu. Lakini kifaru alizunguka kwa wepesi wa kushangaza, bila kumpa wakati wa kuparamia ili kupata usalama. Yeye alifukuzwa kuzunguka huo mti mara kadhaa kabla ya kukamatwa na pembe yake na kurushwa hewani. Chini akaja huyo mwanamume wa kuhurumiwa, akidunda kwanza kwenye mabega ya kifaru kabla ya kugonga ardhi. Akalala hapo, akitarajia kukanyagwa au kudungwa pembe hadi kifo. Kifaru alipopiga hatua mbele, huyo mwanamume aliinua mguu wake, lakini kifaru aliunusa tu na kuenda zake!

Huyu ni kifaru mweusi wa Afrika—mdadisi, mkali, mwenye kuvutwa na jambo kwa urahisi. Ikiwa hisi ya kifaru ya kunusa au kusikia iliyo bora zaidi inamvuta fikira kwa kitu ambacho hawezi kukiona (mwono wake ukiwa usio mzuri), kwa hisia zenye nguvu atashambulia kuelekea chanzo—iwe ni chochote kikubwa kuanzia gari-moshi hadi kipepeo! Ingawa ana kimo cha meta 1.5 mabegani na uzito mwingi kufikia kilogramu 1,000, yeye aweza kwenda shoti kwa yapata kilometa 55 kwa saa na kugeuka kwa ghafula kwa digrii 180!

Nyakati fulani shambulio lake ni wonyesho tu wa nguvu au hata raha tu. Yuilleen Kearney, mhodhi wa wakati mmoja wa kifaru mchanga mweusi aliyeitwa Rufus, aelezea kwamba “kadiri wingi wa vumbi ulivyopepea, ndivyo Rufus alivyohisi furaha.” Yeye akumbuka kwa shauku pindi fulani ambapo Rufus alikuja “akikoroma, kutweta na kukimbia kwa kishindo” akipita kichakani, “akija kwa kasi kuelekea bustanini na kusimama kwa ghafula tu mbele ya varanda, kutembea polepole akipanda ngazi na kulala chini kando ya kiti chake [Joan] cha kukunjwa.”

Shauku hii kwa kifaru mweusi hushirikiwa na wengi ambao wamefanya uchunguzi wake. Ingawa hivyo, wote hukubali kwamba miongoni mwa kifaru nyutu hutofautiana tu kama zinavyotofautiana miongoni mwa binadamu. Jihadhari, basi na jamaa huyo mwenye hasira mbaya! Mwongoza watu mbugani aliye mashuhuri katika kusini mwa Afrika aonya kwamba kifaru mweusi “hapaswi kamwe kutumainiwa hivihivi, na apaswa kupewa kiwango cha umbali wa kadiri inayofaa.” Kwa kuhuzunisha, usumbuaji wa binadamu mara nyingi ndio kisababishi cha ukali wake. Profesa Rudolf Schenkel, mwokokaji wa shambulizi la kifaru lililofafanuliwa mapema, asikitikia uhakika wa kwamba mwanadamu amejifanya mwenyewe adui pekee ambaye kifaru anayo.

Namna gani kifaru mwingine wa Afrika, yule mweupe? Hali yake ya kawaida ya utulivu humfanya awe tofauti kadiri fulani na binamu yake mwenye kujigamba. Huyo pia ana ukubwa wa karibu mara mbili kuliko yule mweusi, akiwa mnyama wa bara aliye wa tatu kwa ukubwa kuliko wote ulimwenguni. Kichwa chake kikubwa ni kizito mno hivi kwamba huchukua wanaume wanne kukiinua! Na bado, ana wepesi tu kama binamu yake mweusi.

Anapokabiliwa na mtu mbugani, kifaru mweupe kwa kawaida atakimbia kwa woga aonapo, kusikia, au kuhisi harufu ya binadamu. Hata hivyo, katika kitabu chao Rhino, Daryl na Sharna Balfour huonya dhidi ya kupuuza hilo. “Maumizo mengi yamesababishwa na kifaru mweupe zaidi ya mweusi katika miaka ya majuzi,” wao waandika, wakiongeza kwamba hili labda ni kwa sababu ya “ukosefu wa staha” wa mwanadamu kwake.

Kipitisha-Wakati Kipendwacho Sana

Kuna upendo hususa ambao kifaru wa Afrika hushiriki. Ni upendo wa matope—mengi mno! Wengi wataharakisha mwendo wao wakikaribia kidimbwi chao cha matope wakipendacho sana na kutoa vilio vyembamba vya furaha kwa taraja lililoko mbele. Akina Balfour, ambao mara nyingi walitazama hili, wanaelezea kwamba kifaru alikuwa akizama polepole matopeni, “halafu mtweto ungesikika, na huyo mnyama aliyetosheka angelala kwa upande mmoja kwa dakika chache . . . kabla ya kuendelea na miogesho yake, mara nyingi akibingirika kwa mgongo wake, miguu ikirusha mateke angani.”

Spishi zote mbili za kifaru nyakati fulani zitashiriki kidimbwi kimoja cha matope na zitapeana heshima yote katika upendo wao wa kipitisha-wakati cha matope. Rufus mchanga, aliyetajwa juu, alikuwa mwenye idili mno kuhusu uogaji wake wa matope hivi kwamba “angeruka nje kabla ya huo kwisha, ili tu akimbie bustanini, akirukaruka kama farasi, kabla ya kurudi kwenye kidimbwi ili kufurahia mara nyingine tena.”

Hata hivyo, hayo matope hutumika kwa mambo mengine zaidi ya raha tu. Hayo huandaa mahali pa vikusanyiko vya kijamii pamoja na vifaru wenzao na wanyama wengine wapenda-matope, humpunguzia kifaru miumo yenye kuwasha-washa ya wadudu warukao, na hupoza miili yao kutokana na joto la jua. Kwa hivyo haishangazi kwamba vifaru wanaweza nyakati fulani kuonekana wakikawia katika mahali pa matope kwa saa zisizo na mwisho.

Ni Yupi Mweupe na Yupi Mweusi?

Mtu aweza kutofautishaje kifaru mweupe na kifaru mweusi? Je, kweli mmoja ni mweusi na yule mwingine mweupe? La. Wote ni wa kijivu—lakini namna zenye tofauti ndogo za kijivu—ikiwa kwa vyovyote utapata kuona hiyo rangi ya kijivu. Kile utakachoona hasa ni rangi ya matope waliyoogea mwisho, ambayo sasa yamefunika ngozi.

Lakini umbo la kinywa litakueleza mara moja ni yupi mweusi na yupi mweupe. Kifaru mweusi, akiwa mtafunaji-majani, ana mdomo wa juu uliochongoka ambao huutumia kupinda au kuvuta majani na vitawi vya vichaka. Kwa hivyo jina lake sahihi zaidi ni kifaru mwenye mdomo-ndoana. Kwa upande ule mwingine, kifaru mweupe, ni mlaji-nyasi. Hivyo, pua yake haijachongoka, hivi kwamba hukata nyasi kama mashine ya kufyeka nyasi. Si ajabu kwamba, jina lake sahihi zaidi ni kifaru mwenye mdomo-mraba. Lakini kwa sababu fulani utofautisho wa weusi-au-weupe, ambao yaonekana ulianza na masetla wa mapema Wadachi katika kusini mwa Afrika, umebaki.

Pembe Hizo Zenye Bei

Jina kifaru latokana na maneno mawili ya Kigiriki yanayomaanisha “mwenye pembe-pua.” Na pembe za kifaru zimefanyizwa kwa kitu gani? Watu fulani huzifafanua kuwa nywele zilizoambatishwa, kwa kuwa zaelekea kuchakaa karibu na sehemu ya chini. Hata hivyo, si nywele halisi, asema Dakt. Gerrie de Graaff, mshauri wa kisayansi kwenye Baraza la Mbuga za Kitaifa la Afrika Kusini, lakini hizo “zafanana kihadubini na kwato za wanyama.”

Pembe huendelea kukua, kama tu vile kucha zifanyavyo. Kifaru mweusi aliyejulikana sana aliyeitwa Gertie alikuwa na pembe iliyokuwa na urefu wa zaidi ya meta 1.4, na pembe ya kifaru mmoja mweupe ilikua hadi meta mbili! Na iwapo pembe yavunjika, kama inavyotukia nyakati fulani, itajirudisha yenyewe kwa kiwango cha sentimeta nane hivi kwa mwaka.

Kwa nini pembe za kifaru zina bei mno? Watu wengi huzitumia kwa dawa, na wengine hufurahia umashuhuri wa kuwa na jambia lenye kishikio cha pembe ya kifaru. Uhitaji ni mkubwa sana, na hiyo biashara ni yenye faida nyingi sana, hivi kwamba maelfu ya vifaru yamechinjwa na watu wenye pupa ya faida.

Kifaru mweupe, aliyekuwa wakati mmoja kwenye ukingo wa kutoweka, sasa amerudia hali nzuri kwa kadiri fulani, kwa sababu ya jitihada nyingi za wahifadhi. Lakini sivyo ilivyo na binamu yake mweusi. Miradi mbalimbali iliyopo ili kusimamisha wimbi la uwindaji haramu yatia ndani kukata pembe za huyo mnyama. Lakini kazi hii kubwa mno yathibitika kuwa na thamani ndogo. Pembe za kifaru zikichuma hadi dola 2,000 kwa kilogramu, wawindaji haramu wanahisi kwamba hata vigutu vya kifaru aliyetolewa pembe vinastahiki kung’olewa. Ingawa hivyo, inatumainiwa kwamba pupa ya mwanadamu haitafaulu, ili vizazi vijavyo pia viweze kupata furaha katika kujuana na mnyama huyu mwenye kupendeza.

[Blabu katika ukurasa wa 27]

Waweza kutofautishaje kifaru mweusi na kifaru mweupe, kwa kuwa wote ni wa kijivu?

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kifaru mweupe na mtoto wake

[Hisani]

National Parks Board of South Africa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki