Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 8/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uchawi Miongoni mwa Wakimbizi
  • Mapadri “Wakatiwa Simu”
  • Nzuri kwa Akina Mama —Mbaya kwa Watoto
  • Mapigano ya Bunduki Yaongezeka Katika Japani
  • Viepeo vya Tekinolojia na Sabato
  • Majitu Yaliyo Hatarini
  • “Death by Government”
  • Nyungunyungu Wenye Manufaa
  • Kanisa na Vita
  • Biashara ya Dawa za Kulevya Ni Biashara Kubwa
  • Uchawi Waenea Pote—Je! Ni Hatari?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Kanisa Othodoksi la Kigiriki—Dini Iliyogawanyika
    Amkeni!—1996
  • Unajua Nini Kuhusu Uchawi?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • Idadi Yenye Kuongezeka ya Wakimbizi
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 8/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Uchawi Miongoni mwa Wakimbizi

Wakimbizi kutoka Rwanda iliyokumbwa na vita wanakumbwa na tatizo jingine tena katika kambi zao katika Ngara, magharibi mwa Tanzania: uchawi. Kulingana na shirika la habari la Reuters, UNHCR (Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi) imetoa uangalifu wa pekee kwa uchawi kuwa “tatizo zito” katika kambi mbalimbali. Kila usiku, kulingana na mnenaji wa UNHCR Chris Bowers, watu wawili au watatu wanauawa katika desturi za kichawi. Yeye aeleza hivi: “Twajua kwamba uchawi wahusika kwa sababu twapata maiti zikiwa zimekatwa viungo katika njia fulani.” Kufikia mwishoni mwa 1994, watu wapatao 580,000 walikuwa wakiishi katika kambi za Ngara, huku wakimbizi wapya 2,000 wakiwasili kila siku. Shirika la habari la Reuters lanukuu chanzo kimoja cha UM kikisema: “Kuna ongezeko la uchawi na hatujui jinsi ya kupambana nalo.”

Mapadri “Wakatiwa Simu”

Simu ziwezazo kuchukulika kila mahali zaweza kutokeza kiwango cha juu katika uwasiliano ufaao, lakini askofu mmoja katika Finland ameamua kwamba kitu chaweza kuwa kibaya kikipita kiasi. Kulingana na shirika la habari la Reuters, huyo askofu alidai kwamba “simu ya kuchukulika yapaswa kutumikia, si kutumikisha, mtumizi wayo” naye akaamrisha wafanyakazi wa kanisa na wahudumu wapunguze utumizi wa hivyo vidude. Yaonekana kwamba malalamiko ya wanaparokia yalikuwa yamemfikia askofu—makasisi fulani walikuwa wakipokea simu wakati wa ibada za kanisa. Ilisemekana kwamba simu moja kama hiyo ilikuja katikati kabisa ya ibada ya maziko. Vivyo hivyo, gazeti la Kikatoliki katika Italia hivi majuzi lilishauri mapadri wasiende na simu zao katika vyumba vya kuungamia—baada ya mwanamke fulani kulalamika kwamba angeweza kusikia simu ya padri ikilia alipokuwa akiungama dhambi zake.

Nzuri kwa Akina Mama —Mbaya kwa Watoto

Wanawake wengi humeza tembe za madini kwa ajili ya afya yao ili kusaidia damu ya wagonjwa wa anemia, lakini wengine hawajui jinsi tembe hizohizo ziwezavyo kuwa hatari kwa watoto wanaozimeza. Kulingana na gazeti Safety+Health, tembe za madini ndizo kisababishi kikuu cha vifo vya kusumishwa miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka sita. Serikali ya Marekani imependekeza kwamba tembe zote kama hizo zipakiwe moja-moja katika viwekeo vya plastiki vilivyo vigumu kufungua badala ya chupa. Ingawaje, katika hali yoyote, akina mama wanashauriwa kuweka tembe za madini mahali ambapo watoto wadogo hawawezi kuzifikia, kama tu wafanyavyo na tembe nyinginezo na dawa.

Mapigano ya Bunduki Yaongezeka Katika Japani

Japani lajulikana kuwa moja ya mataifa yenye usalama kuliko yote ulimwenguni. Kiwango chalo cha uuaji wa kimakusudi kwa mwaka ni mtu 1 tu kwa watu 100,000, ilhali kiwango kama hicho ni karibu mara kumi juu zaidi katika nchi kama vile Thailand na Marekani. Ingawa hivyo, hivi majuzi Japani imekumbwa na ongezeko katika mauaji ya kimakusudi yaliyohusisha bastola, laripoti gazeti Asiaweek. Tangu 1990 hadi 1993, kulikuwa na mipigo ya bunduki 180 kila mwaka, yote ya hiyo ikihusisha washiriki wa vikundi vya uhalifu. Lakini kwa kuogopesha, katika 1994 idadi ya mipigo ya bunduki iliongezeka, na saba wa majeruhi walikuwa wananchi wa kawaida. Ingawa Japani ina sheria kali dhidi ya mtu binafsi kuwa na bunduki, polisi wametaarifu kwamba kuna yapata bastola 100,000 zisizo halali katika hiyo nchi. Baada ya daktari mmoja kupigwa risasi katika kituo cha gari la moshi kilichojaa watu, yaelekea na mgonjwa wake wa zamani aliyeudhika, mwanafunzi mmoja wa koleji alitoa maelezo haya katika mahojiano: “Nilifikiri kwamba hili lingetukia katika Marekani tu.”

Viepeo vya Tekinolojia na Sabato

Katika Israeli, kushika Sabato katika ulimwengu wa tekinolojia ya hali ya juu hutokeza magumu fulani halisi kwa wale ambao huishi kwa kushika sana ile Halakah, au kikundi cha kale cha sheria za Kiyahudi. Kwa kielelezo, Wayahudi Waothodoksi wanahangaikia kutembea kupitia kivumbua-metali. Funguo zikiwasha hicho kivumbua-chuma, basi wamekamilisha mzunguko wa kiumeme bila kutaka—na hili, wao wanasababu, lingevunja amri ya Halakah dhidi ya kuwasha moto. Kwa hiyo shirika liitwalo Tsomet limebuni kivumbua-metali ambacho hakiitikii vitu vya kawaida kama vile funguo, hivyo kutoweka hatari yoyote katika ushikaji Sabato. Vivyo hivyo, shirika jingine limetatua tatizo la madaktari wa Othodoksi ambao huhitaji kufanya uandishi wa kikawaida wakati wa Sabato. Wamebuni kalamu yenye ncha iliyo na nyuzinyuzi ambayo huandika kwa wino utakaofutika baada ya siku chache. Hilo husaidiaje? Halakah huzuia kuandika wakati wa Sabato lakini hufafanua kuandika kuwa kukiacha alama ya kudumu. The New York Times lamnukuu rabi mmoja mashuhuri akisababu hivi: “Ikiwa [Mungu] aliacha kiepeo, alikiweka pale ili kitumiwe.”

Majitu Yaliyo Hatarini

Kobe-jitu wa Visiwa Galápagos anajulikana sana kimataifa na hulindwa akiwa aina iliyo hatarini. Ingawa hivyo, hivi majuzi imekuwa wazi kwamba wanyama-watambazi hawa wakubwa mno wanakabili hatari mpya. Kwa mwezi mzima moto uliendelea bila kuzuiwa kotekote katika Kisiwa Isabela cha jamii-visiwa vya Galápagos. Wafanyakazi wa kuokoa walichimba mitaro ili kulinda idadi ya hicho kisiwa ya kobe 6,000 na hata wakahamisha 400 wa hao hadi kwenye hifadhi ya pekee. Hatua hii ya baadaye ilichukuliwa ili kulinda hao kasa hasa kutokana na watu badala ya moto. Kulingana na The Unesco Courier, “uwindaji-kobe, ingawa si halali, yaelekea ni zoea la kimapokeo. Nyama ya kobe, hasa kobe wa kike, na damu yao huchukuliwa kuwa zina manufaa za kitiba, kando na kuwa tamu.” Waokoaji walipata masalio 42 ya majitu hawa ambao walikuwa wameliwa na wanadamu.

“Death by Government”

Maneno yaliyo juu ni kichwa cha kitabu kipya kilichoandikwa na R. J. Rummel wa Chuo Kikuu cha Hawaii. Wakati wa kipindi cha miaka minane, Bw. Rummel alikusanya habari kutoka “maelfu ya vyanzo” juu ya mada ya fungu la serikali katika machinjo ya binadamu wakati wa karne hii. Kulingana na The Honolulu Advertiser, hicho kitabu chataarifu hivi: “Karibu wanaume, wanawake na watoto milioni 170 wamepigwa risasi, kupigwa viboko, kuteswa, kudungwa kisu, kuchomwa, kunyimwa chakula, kugandishwa kwenye barafu, kupondwa, au kufanyishwa kazi hadi kifo; kuzikwa wakiwa hai, kuzamishwa majini, kunyongwa, kulipuliwa kwa bomu au kuuawa katika nyingineyo yote ya njia nyingi mno ambazo kwazo serikali imetokeza kifo cha wananchi na wageni wasio na silaha na wasio na uwezo.” Rummel asema hivi: “Ni kana kwamba jamii ya binadamu imeharibiwa na Tauni Nyeusi ya kisasa.” “Hakuna karne nyingine imeona machinjo ya kiwango cha juu kama hicho,” laripoti hilo gazeti la habari kuhusu matokeo ya uchunguzi wa Rummel.

Nyungunyungu Wenye Manufaa

“Nyungunyungu wa udongoni ni silaha ya siri ya India katika kuzuia pigo lingine la tauni,” laripoti gazeti New Scientist. Takataka zinaporundamana, panya na visumbufu vingine ambavyo huwa na magonjwa mabaya huongezeka. Sasa aina ya kienyeji ya nyungunyungu mwenye kuchimba chini sana udongoni, Pheretima elongata, imetumiwa ili kubadili takataka kuwa lundamano lenye mafaa. Wanapowekwa katika viwekeo vya takataka, nyungunyungu hawa hula takataka wanapopita na kutokeza rundamano zuri ambalo huchanguka kwa haraka. Ufundi huu, unaotumiwa tayari katika Bombay, hutengeneza tani nne za uchafu wa kichinjio kila siku. Mamlaka za mitaa ambazo kwa sasa hutegemea tanuri na mashimo ya kuzikia takataka sasa zafikiria kwa upendezi nyungunyungu hawa wenye mafaa.

Kanisa na Vita

Kanisa Othodoksi la Serbia limekuwa na fungu gani katika mizozo ya Balkani? Swali hilo lilishughulikiwa kwenye mazungumzo ya mkutano wa majuzi miongoni mwa viongozi wa kanisa la Othodoksi na Protestanti kutoka Marekani, Serbia, Sweden, Ugiriki, Uingereza, Ujerumani, Urusi, na Uswisi. Christ in der Gegenwart (Mkristo wa Wakati Huu), gazeti la Kikatoliki linalochapishwa katika Ujerumani, liliripoti kwamba hayo mazungumzo yalipangwa na Shirika la Ulimwenguni la Makanisa na yalifanywa katika Geneva, Uswisi. Hayo mazungumzo yalifuatia mashtaka ya kwamba Kanisa Othodoksi la Serbia lilionyesha upendeleo katika vita, “likitoa utegemezo mkubwa mno” kwa upande lililopendelea. Licha ya hayo mashtaka mazito, wengi wa washiriki katika hayo mazungumzo walipiga kura kuruhusu Kanisa Othodoksi la Serbia kubaki na uanaushirika katika Shirika la Ulimwenguni la Makanisa, ingawa “si tofauti zote za maoni [zingeweza] kutatuliwa.”

Biashara ya Dawa za Kulevya Ni Biashara Kubwa

“Ulanguzi wa kimataifa wa dawa za kulevya,” lasema gazeti la habari la Australia The Sydney Morning Herald, “umekuwa biashara ya pili yenye faida nyingi kuliko zote ulimwenguni baada ya biashara ya bunduki, ikichuma dola za Marekani milioni elfu 400 kila mwaka na ikiharibu mifumo ya kisiasa katika Asia.” Kiwango hiki cha pesa, asema katibu-mkuu wa Interpol (Shirika la Polisi wa Kimataifa), “kina nguvu ya kufisidi karibu kila mtu.” Asia yatokeza wazi sana kwa sababu zaidi ya asilimia 80 ya heroini ya ulimwenguni inatokezwa katika lile eneo la Golden Triangle karibu na mipaka ya Myanmar, Thailand, na Laos, na vilevile katika eneo la Golden Cresent la Afghanistan na Pakistan. Ofisa mkuu wa dawa za kulevya wa Interpol aongeza hivi: “Biashara ya dawa za kulevya imekuwa njia kuu ya kutegemeza kifedha uharamia.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki