Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 8/22 kur. 8-9
  • Uwezo wa Matangazo ya Biashara

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Uwezo wa Matangazo ya Biashara
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Tabia za Wanunuzi
  • Uwezo Wake Juu Yako
  • Kupotoshwa na Matangazo Mengi ya Biashara
    Amkeni!—1998
  • Ustadi wa Kushawishi
    Amkeni!—1998
  • Tumbako na Uchunguzi wa Kama Yafaa Kutumiwa
    Amkeni!—1990
  • Je, Unaweza Kuamini Ripoti za Habari?
    Amkeni!—2013
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 8/22 kur. 8-9

Uwezo wa Matangazo ya Biashara

ZAMANI sana, tangazo la biashara katika televisheni lingetangulizwa kwa maneno haya, “Na sasa pata ujumbe mfupi kutoka kwa mdhamini wetu.” Wadhamini ni kampuni zinazolipia ili bidhaa zao zitangazwe. Ingawa “ujumbe mfupi kutoka kwa mdhamini wetu” umekuwa mrefu, wadhamini bado wanategemeza kifedha vyombo vya habari na vya vitumbuizo—televisheni, magazeti, na redio. Na basi, wadhamini hujaribu kutawala kile kinachotokea katika vyombo vya habari na kile kisichopaswa kutokea.

Kwa mfano: Mnamo 1993 kampuni moja ya Ujerumani inayotengeneza magari ya anasa iliandikia magazeti 30 ikiyaamuru kwamba matangazo ya gari lao yanapasa kuwekwa “katika ukurasa ufaao tu wa uhariri.” Barua hiyo ilisema kwamba matoleo ya magazeti yenye matangazo yao ya biashara hayapaswi kuwa na habari yoyote inayochambua gari lao, bidhaa za Ujerumani, au kuchambua Ujerumani yenyewe. Hiyo haishangazi kamwe kwa kampuni hii, ambayo hutumia dola milioni 15 kwa matangazo katika magazeti, kutaka “ukurasa ufaao wa uhariri.”

Pia haishangazi kwamba magazeti yanayotangaza mavazi mapya ya bibi-arusi hayakubali matangazo ya mavazi ya mitumba ya bibi-arusi au magazeti yanayoorodhesha majina ya wakala wa ununuzi wa nyumba hayakuambii jinsi ya kununua nyumba ikiwa huna. Hivyohivyo, hatushangai wakati vyombo vya habari vinavyotangaza sigareti au kamari havishutumu kuvuta sigareti au kucheza kamari.

Tabia za Wanunuzi

Basi uwezo wa matangazo ya biashara si kuuza tu bidhaa. Huongoza mtindo wa maisha wa mnunuzi, tabia iliyoko duniani pote inayozingatia ufuatiaji wa vitu vya kimwili.

Je, kuna ubaya wowote na jambo hilo? Inategemea unauliza nani swali hilo. Watangazaji husababu kwamba watu hupenda kununua na kumiliki vitu; matangazo ya biashara hutumikia mapendezi yao. Isitoshe, wao wasema, matangazo ya biashara hutokeza kazi, hudhamini michezo na sanaa, husaidia kufanya vyombo vya habari viwe vya gharama nafuu, hutokeza ushindani, huboresha bidhaa, hufanya bei ziwe nafuu, na kuwaarifu watu juu ya ununuzi.

Wengine hudai kwamba matangazo ya biashara huwafanya watu wasitulie na wasiridhike na kile walicho nacho, wakikuza tamaa nyingi zisizokoma. Mtafiti mmoja Alan Durning aandika: “Matangazo ya biashara, kama ilivyo na kizazi chetu, ni yenye msukosuko, yenye kupenda anasa, yenye kujaa mambo ya kufuatiwa, na kusukumwa na mitindo ya karibuni; hutukuza watu, hutukuza ununuzi wa vitu kuwa ndiyo njia ya kupata uradhi wa kibinafsi, na kusisitiza kuwa maendeleo ya kitekinolojia ndilo jambo kuu.”

Uwezo Wake Juu Yako

Je, matangazo ya biashara huchangia kufanyiza utu wetu na tamaa zetu? Labda. Lakini, iwe uvutano huo ni mkubwa au mdogo wategemea mambo mengine.

Tukiongozwa na kanuni za Biblia na maadili, tutatambua kwamba hakuna ubaya wa kuwa na vitu vya kimwili. Kwani, Mungu alimbariki Abrahamu, Yobu, Solomoni, na wengine kwa mali tele.

Kwa upande mwingine, tukitumia kanuni za Kimaandiko, tutaepuka kutoridhika kwa wale ambao wanatafuta uradhi na furaha katika mbio zisizoisha za kutafuta vitu vya kimwili. Ujumbe wa Biblia si “Nunua mpaka uchoke.” Badala yake, inatuambia hivi:

Mtumaini Mungu. “Uwape maagizo wale walio matajiri katika mfumo wa mambo uliopo wasiwe wenye kunia ya juu, na waweke tumaini lao, si juu ya mali zisizo hakika, bali juu ya Mungu, ambaye hututolea sisi vitu vyote kwa utajiri kwa ajili ya ufurahio wetu.”—1 Timotheo 6:17.

Ridhika. “Hatukuleta kitu katika ulimwengu, wala hatuwezi kupeleka kitu chochote nje. Kwa hiyo, tukiwa na riziki na cha kujifunika, tutakuwa wenye kuridhika na vitu hivi.”—1 Timotheo 6:7, 8.

Uwe mwenye kiasi. “Natamani wanawake wajirembe wenyewe katika mavazi yenye mpangilio mzuri, pamoja na kiasi na utimamu wa akili, si kwa mitindo ya kusuka nywele na dhahabu au lulu au mvao ulio ghali sana, bali katika njia inayofaa wanawake wanaodai kumstahi Mungu, yaani, kupitia kazi zilizo njema.”—1 Timotheo 2:9, 10.

Jua kwamba hekima ya kimungu ni bora kuliko mali. “Heri mtu yule aonaye hekima, na mtu yule apataye ufahamu. Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi. Yeye ana thamani kuliko marijani, wala vyote uvitamanivyo havilingani naye. Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume, utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto. Njia zake ni njia za kupendeza sana, na mapito yake yote ni amani. Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana; ana heri kila mtu ashikamanaye naye.”—Mithali 3:13-18.

Zoea kutoa. “Kuna furaha zaidi katika kutoa kuliko kulivyo katika kupokea.”—Matendo 20:35.

Mtu aweza kubisha kwamba makala hizi zenyewe ni aina fulani ya matangazo, tangazo ambalo “huuza” wazo la kwamba mambo ya kiroho hayapasi kusukumwa kando na mambo ya kimwili. Bila shaka unakubaliana na mkataa huo.

[Sanduku katika ukurasa wa 9]

Kutangaza Ufalme wa Mungu

Ni ipi mojawapo ya njia bora zaidi za kuwafikia watu kwa ujumbe wenye kushawishi? Kitabu Advertising: Principles and Practice chasema: “Katika ulimwengu mzuri kila mtengenezaji wa bidhaa angeweza kuzungumza ana kwa ana na kila mnunuzi kuhusu bidhaa au utumishi unaotolewa.” Wakristo wa kweli wamekuwa wakitangaza kwa hiari Ufalme wa Mungu kwa njia hii kwa karibu miaka 2,000. (Mathayo 24:14; Matendo 20:20) Kwa nini mashirika mengi ya kibiashara hayatumii njia hii ya kuwafikia watu? Kitabu hicho chaeleza hivi: “Ni ghali mno. Ziara zinazofanywa na wauzaji hugharimu zaidi ya dola 150 kwa kila ziara.” Bila shaka, Wakristo “hutangaza” Ufalme wa Mungu kwa hiari. Hiyo ni sehemu ya ibada yao.

[Picha katika ukurasa wa 8]

Ujumbe wa Biblia si “Nunua mpaka uchoke”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki