Kupotoshwa na Matangazo Mengi ya Biashara
“BABA, mwezi unatangaza nini?” Swali hilo la ajabu lililoulizwa na mtoto lilitokea katika shairi lililoandikwa na Carl Sandburg miaka 50 hivi iliyopita. Wakati ujao, swali kama hilo huenda lisionekane kuwa la ajabu. Kulingana na gazeti New Scientist, wakuu wawili wa matangazo ya biashara huko London wanafanya mpango wa kuakisi nuru ili ionyeshe matangazo kwenye mwezi.
Ebu wazia kutumia mwezi kama bango la matangazo ya biashara! Ebu fikiria kutangaza bidhaa fulani ya kibiashara ulimwenguni pote, ujumbe ambao watazamaji hawawezi kuzima, kukata, kutupa, au kuuondolea sauti. Huenda jambo hilo lisikupendeze, lakini wengine wametamani sana lifaulu.
Ingawa matangazo ya biashara hayajafika kwenye mwezi, tayari yamejaa tele duniani. Magazeti mengi ya Marekani huhifadhi asilimia 60 ya kurasa zake kwa matangazo ya biashara. Toleo la Jumapili la The New York Times pekee linaweza kuwa na kurasa 350 za matangazo ya biashara. Vituo fulani vya matangazo hutumia dakika 40 kwa kila muda wa saa moja kwa matangazo ya biashara.
Kisha kuna televisheni. Kulingana na kadirio moja, vijana wa Marekani hutazama matangazo ya biashara katika televisheni kwa muda wa saa tatu kila juma. Kufikia wakati wanapomaliza shule ya sekondari, wao watakuwa wametazama matangazo 360,000 ya biashara kwenye televisheni. Televisheni hutangaza katika viwanja vya ndege, vyumba vya kungojea katika hospitali, na shuleni.
Michezo mikubwa sasa ni matangazo makubwa ya biashara. Magari ya mashindano hubandikwa matangazo. Wanariadha fulani hupokea pesa nyingi zaidi kutoka kwa watangazaji wa biashara. Mchezaji mmoja mashuhuri wa mpira wa vikapu alipokea dola milioni 3.9 kwa kucheza mchezo huo. Wenye matangazo ya biashara walimlipa mara tisa zaidi ya mapato hayo ili atangaze bidhaa zao.
Huwezi kuhepa matangazo ya biashara. Matangazo ya biashara yamebandikwa kwenye kuta, basi, na malori. Yamejaa ndani ya teksi na katika reli za chini ya ardhi—hata kwenye milango ya vyoo vya umma. Twasikia matangazo ya biashara katika vipaza-sauti katika maduka, lifti—na tunaposhikilia simu tukingoja kuunganishwa. Katika nchi fulani matangazo mengi hupokewa kwa njia ya barua na watu wengi wenye kuzipokea huzitupa.
Kulingana na Insider’s Report, iliyochapishwa na McCann-Erickson, ambalo ni shirika la matangazo ya biashara la duniani pote, inakadiriwa kwamba kiasi cha pesa kilichotumiwa kwa matangazo ya biashara ulimwenguni pote katika mwaka wa 1990 kilikuwa dola bilioni 275.5. Tangu wakati huo kumekuwa na ongezeko kubwa kufikia dola bilioni 411.6 katika mwaka wa 1997 na inatarajiwa kufikia dola bilioni 434.4 katika mwaka wa 1998. Pesa chungu nzima!
Matokeo ya hayo yote ni nini? Mchunguzi mmoja asema: “Matangazo ya biashara ni mojawapo ya kani zenye nguvu zaidi katika utamaduni. . . . Matangazo ya biashara hayashawishi tu watu wanunue bidhaa fulani. Hayo hutangaza mienendo, maadili, miradi, dhana za sisi ni nani na twapaswa kuwa nani . . . Yanaathiri mitazamo yetu ambayo huathiri mwenendo wetu.”
Kwa kuwa huwezi kuepuka matangazo ya biashara, mbona usijue jinsi matangazo ya biashara hufanya kazi na jinsi yawezavyo kukushawishi?