TV—Ni “Mwalimu Mjanja”
TELEVISHENI inaweza kuwa kifaa chenye nguvu cha kufundishia. Inaweza kutufundisha kuhusu watu na nchi ambazo huenda hatutawahi kuzitembelea. Ni kana kwamba sisi hutembelea misitu mikubwa na maeneo yenye barafu, vilele vya milima na bahari zenye kina. Tunachunguza mambo ya ajabu kuhusu atomu na nyota. Tunatazama habari za matukio yanayotukia wakati huohuo upande mwingine wa dunia. Tunajifunza kuhusu siasa, historia, matukio ya sasa na utamaduni. Televisheni huonyesha maisha ya watu wanaokumbwa na misiba na wale wanaopata ufanisi. Inaburudisha, inafundisha, na hata inachochea.
Hata hivyo, vipindi vingi vya televisheni havifai wala havifundishi. Yamkini wachambuzi wengi wa televisheni ni watu ambao hupinga vikali picha nyingi zinazoonyesha jeuri na ngono waziwazi. Kwa mfano, uchunguzi mmoja uliofanywa nchini Marekani ulionyesha kwamba vipindi 2 hivi kati ya 3 vina maonyesho ya jeuri, na huo ni wastani wa maonyesho sita kwa saa. Kijana anapokuwa mtu mzima, atakuwa ametazama maelfu ya vipindi vyenye jeuri na mauaji. Pia habari za ngono huonyeshwa kwa wingi. Asilimia 66 ya vipindi vyote vya televisheni vinahusisha mazungumzo kuhusu ngono na asilimia 35 huhusisha tabia za kingono ambazo huonyeshwa kuwa hazina madhara, ni jambo la kiasili, na huhusisha watu ambao hawajaoana.a
Ulimwenguni pote vipindi vinavyoonyesha mambo ya ngono na jeuri vinapendwa sana. Sinema zinazotayarishwa Marekani na ambazo hatimaye huonyeshwa katika televisheni zinaweza kuuzwa kwa urahisi nje ya nchi hiyo. Si lazima zitayarishwe na kuigizwa kwa ustadi sana, nazo hueleweka kwa urahisi. Watayarishaji hutegemea vita, mauaji, madoido, na ngono ili kuwafanya watu waendelee kutazama vipindi hivyo. Hata hivyo, ili waendelee kuwavutia kwa muda mrefu, mabadiliko fulani yanahitajiwa. Watazamaji huchoka kutazama mambo yaleyale kwani baada ya muda mambo yanayosisimua huishia kuwa ya kawaida. Ili kuendelea kuwavutia watazamaji, watayarishaji wa vipindi hivyo hujitahidi wawezavyo kuwashtua na kuwasisimua watazamaji kwa kuongeza matendo ya jeuri na kuonyesha mambo wazi zaidi, kuhusisha ngono zaidi, na kuongeza ukatili.
Mjadala Kuhusu Athari za Televisheni
Watazamaji huathiriwaje kwa kutazama kwa ukawaida vipindi vya televisheni vyenye jeuri na ngono? Wachambuzi hudai kwamba jeuri inayoonyeshwa katika televisheni huwafanya watu watende kwa ukatili na wasiwahurumie sana watu wanaotendwa jeuri. Wanadai pia kwamba picha za ngono huchangia ukosefu wa maadili na kushusha viwango vya maadili.
Je, kweli utazamaji wa televisheni una matokeo hayo yote? Kwa miaka mingi kumekuwa na mjadala mkali sana kuhusu jambo hilo. Uchunguzi mwingi na maelfu ya vitabu na makala zimelizungumzia. Mojawapo ya sababu kuu za mjadala huo ni ugumu wa kuthibitisha kwamba hali moja hutokeza nyingine. Kwa mfano, ni vigumu kuthibitisha kwamba mtu anapotazama jeuri kwenye televisheni anapokuwa mchanga atakuwa katili atakapokuwa mtu mzima. Si rahisi kuthibitisha kwamba kuna uhusiano kati ya kisababishi na matokeo. Kwa kielelezo: Ukimeza dawa fulani kwa mara ya kwanza, kisha baada ya saa kadhaa utokwe na vipele, haitakuwa vigumu kukata kauli kwamba dawa hiyo ndiyo imekuathiri. Hata hivyo, nyakati nyingine athari zinaweza kutokea polepole. Ikitukia hivyo, huenda ikawa vigumu sana kuhusianisha athari na dawa fulani kwani watu huathiriwa na vitu mbalimbali.
Hali kadhalika, imekuwa vigumu kuthibitisha kwamba jeuri inayoonyeshwa kwenye televisheni husababisha uhalifu na tabia ya kujitenga na wengine. Uchunguzi mwingi umedokeza kwamba kuna uhusiano kati ya mambo hayo. Isitoshe, wahalifu wengi wamesema kwamba mtazamo na tabia yao ya jeuri inategemea mambo waliyoona kwenye televisheni. Kwa upande mwingine, watu huathiriwa na vitu mbalimbali maishani. Michezo ya video yenye jeuri, maadili ya marafiki na familia, hali za maisha—yote hayo yanaweza pia kumfanya mtu awe katili.
Basi haishangazi kwamba watu hawaafikiani kuhusu jambo hilo. Mwanasaikolojia Mkanada aliandika: “Uthibitisho wa kisayansi hauonyeshi kwamba kutazama jeuri kwenye televisheni huwafanya watu wawe wajeuri au huwafanya wasishtuliwe nayo.” Hata hivyo, Kamati ya Shirika la Saikolojia la Marekani Kuhusu Vyombo vya Habari na Jamii inasema: “Hakuna shaka yoyote kwamba watu ambao hutumia wakati mwingi wakitazama jeuri kwenye televisheni husumbuliwi sana na mtazamo au tabia za kikatili.”
Jinsi Televisheni Inavyoathiri Fikira
Kumbuka kwamba wataalamu wanajadiliana kuhusu uthibitisho, yaani, ikiwa inaweza kuthibitishwa kwamba kutazama jeuri humfanya mtu awe katili. Hata hivyo, ni watu wachache tu wanaoweza kudai kwamba televisheni haiwezi kuathiri jinsi tunavyofikiri na kutenda. Wazia hili. Picha moja inaweza kutufanya tukasirike, tulie, au tushangilie. Muziki pia huchochea hisia zetu sana. Maneno, hata yale yaliyoandikiwa, hutufanya tufikiri, tuhisi, na tutende. Basi sinema, muziki, na maneno yanapoambatanishwa kwa ustadi yanaweza kutuathiri hata zaidi! Haishangazi kwamba televisheni inavutia wee! Nayo inapatikana kwa urahisi. Mwandishi mmoja anasema hivi: “Wanadamu waliathiriwa sana walipojifunza kuandika . . . lakini tangu hapo hakuna mbinu nyingine ya kupitisha habari ambayo imewaathiri zaidi kuliko televisheni.”
Wafanyabiashara hutumia mabilioni ya dola kila mwaka kutangaza biashara kwani wanajua kwamba watazamaji huathiriwa na wanachoona na kusikia. Hawatumii pesa hizo kwa sababu wanadhani kwamba matangazo hayo yanaweza kuwa na matokeo, bali wana hakika kwamba yana matokeo. Matangazo hayo huwafanya watu wanunue bidhaa zao. Mnamo 2004, Kampuni ya Coca-Cola ilitumia dola bilioni 2.2 kutangaza bidhaa zake ulimwenguni pote kupitia habari zilizochapishwa, redio, na televisheni. Je, walifaidika kwa kutumia pesa hizo zote? Mwaka huo, kampuni hiyo ilipata faida ya karibu dola bilioni 22. Watangazaji wa biashara wanatambua kwamba huenda tangazo moja lisibadili tabia za watu. Badala yake, wao hufahamu kwamba likirudiwa-rudiwa kwa miaka mingi litakuwa na matokeo.
Ikiwa tangazo la sekunde 30 huathiri mtazamo na tabia zetu, tunaweza kuwa na hakika kwamba kutazama televisheni kwa saa nyingi kutatuathiri pia. Mwandishi wa kitabu Television—An International History anasema: “Kupitia burudani nyingi ndogo ambazo ni za kawaida, televisheni hutenda kama mwalimu mjanja.” Kitabu A Pictorial History of Television kinasema: “Televisheni inabadili kufikiri kwetu.” Swali ambalo tunahitaji kujiuliza ni, ‘Je, kile ambacho ninatazama kinaathiri kufikiri kwangu kwa njia ninayotaka?’
Swali hilo ni muhimu sana kwa wale wanaomtumikia Mungu. Mambo mengi yanayoonyeshwa katika televisheni hupingana na kanuni na viwango bora vya maadili vinavyofundishwa katika Biblia. Mitindo ya maisha na mazoea ambayo Maandiko hushutumu huonyeshwa kuwa yanakubaliwa, ya kawaida, na ya kisasa. Wakati huohuo, kanuni za Kikristo na wale wanaozifuata hupuuzwa, hudhihakiwa, na kudharauliwa katika vipindi vya televisheni. Mwandishi mmoja wa vitabu alisema: “Haitoshi tu kufanya mambo yaliyopotoka yaonekane kuwa ya kawaida. Mambo ya kawaida yanafanywa yaonekane kuwa mapotovu.” Mara nyingi sana huyo “mwalimu mjanja” husema hivi: “Wema ni ubaya na ubaya ni wema.”—Isaya 5:20.
Tunapaswa kuwa waangalifu kuhusu kile tunachotazama, kwa kuwa kitaathiri kufikiri kwetu. Biblia inasema: “Anayetembea na watu wenye hekima atakuwa na hekima, lakini anayeshirikiana na wajinga atapatwa na mabaya.” (Methali 13:20) Msomi wa Biblia Adam Clarke anasema hivi: “Kutembea na mtu kunamaanisha kumpenda na kushikamana naye; na hatuwezi kamwe kukosa kuwaiga watu tunaowapenda. Hivyo tunasema, ‘Nionyeshe rafiki zake, nami nitakuambia yeye ni mtu wa aina gani.’ Niambie rafiki zake ni nani, nami nitakuambia maadili yake yakoje.” Kama tulivyoona, watu wengi hutumia muda mrefu sana pamoja na watu wasio na hekima wanaoigiza kwenye vipindi vya televisheni, watu ambao Mkristo mnyoofu hangethubutu kuwaalika nyumbani kwake.
Daktari akikuandikia dawa yenye nguvu, yaelekea ungefikiria kwa makini faida na madhara ya kutumia dawa hiyo. Kutumia dawa isiyofaa au hata kutumia kiasi kikubwa sana cha dawa inayofaa kunaweza kudhuru afya yako. Inaweza kusemwa hivyo kuhusu kutazama televisheni. Hivyo, ni jambo la hekima kufikiria kwa uzito kuhusu vipindi tunavyotazama.
Mtume Paulo aliyeongozwa kwa roho aliwahimiza Wakristo wafikirie mambo yaliyo ya kweli, ya hangaiko zito, ya uadilifu, yaliyo safi kiadili, ya kupendeka, yanayosemwa vema, yenye wema wa adili, na yenye kustahili sifa. (Wafilipi 4:6-8) Je, utatii shauri hilo? Utakuwa mwenye furaha ukifanya hivyo.
[Maelezo ya Chini]
a Takwimu za Marekani zinafanana na za nchi nyinginezo kwani vipindi vya televisheni na sinema za Marekani huonyeshwa ulimwenguni pote.
[Blabu katika ukurasa wa 5]
“Televisheni ni chombo kinachokuwezesha kuburudishwa kwako na watu ambao hungewakaribisha kamwe nyumbani kwako.”—David Frost, Mtangazaji wa habari Mwingereza
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
VIPI MASIMULIZI YA NGONO NA JEURI KATIKA BIBLIA?
Kuna tofauti gani kati ya jeuri na ngono inayotajwa katika Biblia na ile inayoonyeshwa katika televisheni? Sababu ya kutaja kuhusu ngono na jeuri katika Biblia ni kufundisha, si kuburudisha. (Waroma 15:4) Neno la Mungu hutaja mambo hakika ya kihistoria. Linatusaidia kufahamu maoni ya Mungu kuhusu mambo na kutuwezesha kujifunza kutokana na makosa ya wengine.
Katika nchi nyingi ambako matangazo ya biashara huonyeshwa, ngono na jeuri kwenye televisheni haionyeshwi ili kufundisha. Inaonyeshwa ili kuchuma pesa. Watangazaji wa biashara wanataka kuwavutia watu wengi iwezekanavyo, na ngono na jeuri huteka akili za watazamaji. Matokeo: Watu hutazama matangazo ya biashara na kununua bidhaa zinazotangazwa. Watangazaji wa habari hufuata kanuni hii: “Habari inayovutia zaidi ni ile yenye jeuri zaidi.” Kwa ujumla, hadithi zenye kuogofya kama zile zinazohusu uhalifu, misiba, na vita hupewa kipaumbele.
Ingawa Biblia ina masimulizi yanayohusu jeuri, inawatia watu moyo waishi kwa amani, wasilipize kisasi bali watatue matatizo kwa amani. Inapohusu ngono, Biblia huwahimiza watu tena na tena wafuate maadili mema. Jambo hilo halikaziwi katika habari nyingi zinazoonyeshwa katika televisheni.—Isaya 2:2-4; 1 Wakorintho 13:4-8; Waefeso 4:32.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
TELEVISHENI INAVYOATHIRI WATOTO
“Kwa kutegemea uthibitisho uliokusanywa katika uchunguzi mbalimbali ambao umefanywa kwa miaka kadhaa, wanasayansi na watu wanaoshughulikia afya wanasema kwamba kutazama vipindi vya televisheni vyenye jeuri kunaweza kuwadhuru sana watoto.”—The Henry J. Kaiser Family Foundation.
“[Tunakubaliana na] Chuo cha Marekani cha Tiba ya Watoto kwamba ‘watoto wenye umri wa miaka miwili kwenda chini hawapaswi [kutazama televisheni].’ Watoto hao, ambao wakati huo ubongo wao unakua kwa haraka sana, wanahitaji kucheza na kushirikiana na watu ili kuwachochea waboreshe ustadi wao wa kimwili, ukuzi, na kushirikiana na watu.”—Taasisi ya Kitaifa ya Kuchunguza Athari za Vyombo vya Habari kwa Familia.
[Picha katika ukurasa wa 6, 7]
Je, kile ambacho ninatazama kinabadili kufikiri kwangu kwa njia ninayotaka?