TV—Je, Ni Mwizi wa Wakati?
IKIWA mtu angekupa dola milioni moja ili uache kutazama televisheni kwa maisha yako yote, je, ungekubali? Uchunguzi uliofanywa miaka kadhaa iliyopita ulionyesha kwamba asilimia 25 ya watu nchini Marekani hawangekubali. Katika uchunguzi mwingine wanaume waliulizwa kile ambacho wangependa zaidi. Wengi walisema wanatamani kuwa na amani na furaha. Lakini hilo halikuwa jambo walilopenda zaidi. Kitu walichopenda zaidi maishani ni televisheni kubwa!
Watu wengi sana ulimwenguni wanapenda televisheni. Huko nyuma katika mwaka wa 1931, televisheni ilipokuwa imetoka tu kuvumbuliwa, mwenyekiti wa Shirika la Redio la Marekani alisema hivi: “Televisheni ikiisha kufanyiwa maendeleo makubwa kuna uwezekano mkubwa sana kwamba watu wote ulimwenguni watakuwa wakiitazama.” Huenda wakati huo maneno hayo yalionekana kuwa yametiliwa chumvi, lakini sivyo ilivyo leo. Inakadiriwa kwamba kuna televisheni bilioni 1.5 ulimwenguni pote. Lakini kuna watazamaji wengi zaidi. Tupende tusipende, televisheni hutimiza sehemu muhimu katika maisha ya watu.
Muda ambao watu wengi hutumia kutazama televisheni unashangaza. Hivi karibuni, uchunguzi uliofanywa ulimwenguni ulionyesha kwamba, kwa wastani, watu hutazama televisheni kwa saa tatu hivi kila siku. Watu wanaoishi Amerika Kaskazini huitazama kwa muda wa saa nne na nusu kila siku. Wajapani ndio huitazama kwa muda mrefu zaidi kwani wao hutumia saa tano kila siku. Hiyo ni jumla ya saa nyingi sana. Ikiwa tutaitazama kwa saa nne kila siku, tutakuwa tumetazama televisheni kwa miaka kumi tunapofikia umri wa miaka 60. Hata hivyo, hakuna yeyote kati yetu ambaye angependa kukumbukwa kwa kutumia asilimia 17 ya maisha yake kutazama televisheni.
Je, watu hutazama televisheni kwa muda mrefu kwa sababu wanaifurahia? Haiwi hivyo nyakati zote. Wengi huona kuwa wanatumia muda mrefu sana kutazama televisheni nao huhisi vibaya kwamba hawakutumia wakati wao kwa njia nzuri zaidi. Wengine husema kwamba wao ni “waraibu wa televisheni.” Ingawa kuna ufanani, huwezi kuwa mraibu wa televisheni kama mtu anavyokuwa mraibu wa dawa za kulevya. Waraibu hupoteza wakati mwingi sana kutumia dawa ya kulevya. Ijapokuwa wanataka kupunguza wakati au kuachana na zoea hilo, wao hushindwa kufanya hivyo. Wao hukosa shughuli muhimu za jamii na za familia ili watumie dawa hizo, nao hupatwa na athari za kuacha zoea hilo. Watu ambao hutazama televisheni kwa muda mrefu sana huwa na dalili hizohizo.
“Si vizuri kula asali nyingi mno,” akaandika Mfalme Solomoni mwenye hekima. (Methali 25:27) Kanuni hiyohiyo inahusu utazamaji wa televisheni. Ijapokuwa televisheni huonyesha mambo mengi mazuri, kutumia wakati mwingi kuitazama kunaweza kupunguza wakati unaotumiwa na familia, kuwazuia watoto wasisome na kufanya vizuri shuleni, na kuchangia kumfanya mtu awe mnene kupita kiasi. Iwapo unatumia wakati mwingi sana kutazama televisheni, inafaa ufikirie manufaa unazopata kwa kufanya hivyo. Wakati tulio nao ni wenye thamani sana hivi kwamba hatupaswi kuupoteza. Vilevile ni jambo la hekima kufikiria vipindi tunavyotazama. Tutazungumzia jambo hilo katika makala inayofuata.