Je! Televisheni Imekubadili Wewe?
“KIDIRISHA cha ulimwengu.” Hivyo ndivyo televisheni imeweza kuelezwa. Katika kitabu Tube of Plenty—The Evolution of American Television, mwandikaji Erik Barnouw aandika kwamba katika miaka ya mapema ya 1960, “kwa watu wengi [televisheni] ilikuwa imekuwa dirisha lao la kuchungulia ulimwengu. Picha ilizoonyesha zilionekana kuwa ndiyo ulimwengu. Wao waliamini uhalali na ukamili wayo.”
Hata hivyo, dirisha la kawaida tu haliwezi kuchagua picha litakazokuonyesha; haliwezi kuamua kiasi cha mwangaza au pembe ya mtazamo; wala haliwezi kubadili picha ghafula ili kuendeleza upendezi wako. Televisheni yaweza. Mambo mbalimbali kama hayo yanaunda hisia zako na mkataa wako kuhusu kile unachotazama, na bado yanadhibitiwa na watu wale wanaotayarisha vipindi vya televisheni. Hata habari ambazo haziegemei upande wowote ule pamoja na vipindi vinavyoonyesha mambo mbalimbali ya jamii huwa chini ya uvutano kama huo, hata iwe bila kukusudia jinsi gani.a
Mdanganyi Mwenye Ufundi
Hata hivyo, mara nyingi, wale wanaodhibiti televisheni wanajaribu kwa vyovyote vile kuwavuta watazamaji. Kwa mfano, katika matangazo, wana uhuru kutumia kila njia ya udanganyifu wawezayo kutumia ili kukushawishi ununue. Rangi. Muziki. Watu warembo. Umahaba. Mandhari fupi zenye kuvutia kuhusu matukio mbalimbali. Mbinu zao ni nyingi, na wanazitumia kwa ustadi.
Mmoja aliyekuwa mtangazaji mwenye cheo aliandika hivi kuhusu miaka yake 15 katika shughuli hiyo: “Mimi nilijifunza kwamba inawezekana kusema kupitia vyombo vya habari [kama vile televisheni] moja kwa moja ndani ya vichwa vya watu halafu, kama na mfanya mizungu yeyote yule, uwaache na picha akilini mwao ambazo zaweza kufanya watu watende kile ambacho hawangefikiria kufanya.”
Kwamba televisheni ina uwezo mkubwa hivyo juu ya watu iliweza kuonekana wazi katika miaka ya 1950. Kampuni moja ya rangi ya midomo ambayo ilikuwa inapata dola 50,000 kwa mwaka ilianza utangazaji katika televisheni ya U.S. Katika miaka miwili, mauzo yalipanda hadi kufikia dola 4,500,000 kwa mwaka! Benki moja ilipata akiba tele ya dola 15,000,000 baada ya kutangaza utumishi inayotoa katika kipindi kimoja kinachopendwa na wanawake wengi.
Leo, Mwamerika wa kadiri hutazama matangazo ya kibiashara 32,000 kila mwaka. Matangazo hayo hudanganya hisia za moyo. Kama vile Mark Crispin Miller alivyoandika katika Boxed In—The Culture of TV: “Ni kweli kwamba sisi tunadhibitiwa kwa werevu na kile tunachotazama. Matangazo ya biashara ambayo huenea katika kila sehemu ya maisha ya kila siku yanatuvutia bila kikomo.” Yeye aongezea kwamba udhibiti huu wa werevu, “ni hatari hasa kwa sababu mara nyingi inakuwa vigumu kuutambua, na hivyo hautakosa kufanikiwa mpaka tujifunze kuutambua.”
Lakini televisheni huuza zaidi tu ya rangi za midomo, maoni ya kisiasa, na utamaduni. Hiyo huuza maadili pia—au ukosefu wayo.
Televisheni na Maadili
Ni watu wachache wanaoweza kushangaa kufahamu kwamba tabia za kingono zinaonyeshwa mara nyingi zaidi na zaidi katika televisheni ya Amerika. Uchunguzi mmoja uliochapishwa katika 1989 katika Journalism Quarterly ulipata kwamba katika saa 66 za ule wakati ambapo televisheni inatazamwa na wengi zaidi, kulikuwako na maonyesho 722 ya tabia za ngono, iwe ni kwa kudokezwa, kutajwa kwa maneno, au kuonyeshwa kihalisi. Mifano ilianzia kupapasana kimahaba hadi kufanya ngono, punyeto, kulalana kwa watu wa jinsia moja, na ngono ya maharimu. Wastani ulikuwa maonyesho 10.94 kwa kila saa moja!
United States si peke yake katika jambo hilo. Sinema za televisheni za Ufaransa huonyesha waziwazi ngono za ukatili. Maonyesho ambapo mchezaji huvua nguo moja baada ya nyingine huonyeshwa katika televisheni ya Italia. Maonyesho ya masaa ya usiku sana katika televisheni ya Hispania huonyesha filamu za ujeuri na za mahaba. Orodha hiyo yaendelea bila kikomo.
Jeuri ni aina nyingine ya ukosefu wa adili katika televisheni. Katika United States, hivi karibuni mchambuzi wa televisheni wa gazeti Time aliusifu “ucheshi mzuri wa kuogofya” katika programu kadhaa zenye maogofyo. Mwendelezo huo wa vipindi ulionyesha vituko vya kukatwa kichwa, kukatwakatwa kwa viungo, kutundikwa, na kupagawa na roho waovu. Bila shaka, wingi wa jeuri katika televisheni unafanya iwe isiyoogofya sana—na hufanya ichukuliwe kwa urahisi zaidi kuwa ya kikawaida tu. Wakati maonyesho ya televisheni ya Magharibi yalipofanywa hivi karibuni katika kijiji kimoja cha ndani-ndani mashambani katika Côte d’Ivoire, Afrika Magharibi, mzee mmoja mwanamume aliyefadhaika angeweza tu kuuliza: “Kwa nini weupe hudungana visu, kufyatuliana risasi na kupigana ngumi kila wakati?”
Jibu, bila shaka, ni kwamba watayarishi na wadhamini wa vipindi vya televisheni wanataka kuwapatia watazamaji kile watazamaji wanachotaka kuona. Jeuri huwavutia watazamaji. Ngono pia hufanya hivyo. Kwa hiyo televisheni hutoa kiasi cha kutosha cha mambo hayo mawili—lakini si kiasi kikubwa sana kwa haraka sana, au watazamaji watachukizwa. Kama vile Donna McCrohan alivyoliweka wazo hilo katika Prime Time, Our Time: “Kwa kadiri ile viwezavyo, vipindi vingi maarufu hutumia lugha, ngono, jeuri, au kiini cha habari yenyewe; halafu, baada ya kufika ukingoni, wanauondoa ukingo huo. Hivyo basi, umma wanakuwa tayari kwa ukingo mpya.”
Kwa mfano, lile wazo la kulalana kwa watu wa jinsia moja lilifikiriwa wakati mmoja kuwa limepita “mpaka” wa kuweza kuonyeshwa kwenye televisheni. Lakini watazamaji walipozoeleana nalo, walikuwa tayari kupokea zaidi. Mwandishi wa magazeti wa Ufaransa alisema: “Hakuna mtayarishaji vipindi anayeweza kujaribu kamwe kutokeza ngono ya waume kwa waume kama kwamba ni upotovu leo . . . Badala yake ni jamii na kutovumilia kwayo kuliko na kasoro.” Kuhusu televisheni ya Amerika ipitishayo vipindi kwa nyuzi za simu, ‘kipindi-mfululizo cha wanaume wenye kulalana’ kilitokea mara ya kwanza katika majiji 11 katika 1990. Kipindi hicho kilionyesha tamasha za wanaume wakiwa kitandani pamoja. Mtayarishaji wa kipindi hicho aliliambia gazeti Newsweek kwamba tamasha kama hizo zilitayarishwa na wanaume wanaolalana ili kugandisha hisi za watazamaji watambue kwamba sisi ni kama mtu mwingine yeyote.”
Kabiliano Kati ya Msisimuko Bandia na Uhalisi
Waandishi wa uchunguzi ulioripotiwa katika Journalism Quarterly walionelea kwamba kwa sababu karibu wakati wote televisheni huwa haionyeshi matokeo ya ngono haramu, “miminiko la daima la ngono zenye kusisimua” ni kama tu kampeni ya kueneza habari bandia. Wao walitaja uchunguzi mwingine na kumalizia kwamba vipindi-mfululizo vinavyodhaminiwa na biashara ya sabuni huandaa ujumbe huu mkuu: Ngono ni ya wenzi wasiooana, na hakuna anayepatwa na ugonjwa kutokana nayo.
Je! kweli hivyo ndivyo mambo ya ulimwengu yalivyo kwa kadiri wewe ujuavyo? Je! eti ngono za kabla ya ndoa hufanyika bila mimba za utineja au magonjwa yenye kuambukizwa kwa kufanya ngono? Eti watu wa jinsia tofauti na wa jinsia zote mbili wakalalana bila hofu ya kuambukizwa UKIMWI? Eti jeuri na fujo zitendeke na kuwaacha mabingwa wakiwa washindi na wakora wakiwa wameaibishwa—lakini wote mara nyingi wakiwa bila majeraha isivyo kawaida? Televisheni huonyesha ulimwengu wa vitendo vibaya vikiwa na matokeo ya raha mustarehe. Mahali pa kanuni za dhamiri, na za adili, na za kujidhibiti huchukuliwa na kanuni ya utoshelezo wa papo hapo.
Kwa wazi, televisheni si “dirisha la kuchungulia ulimwengu”—angalau si la kuuchungulia ulimwengu ulio halisi. Kwa kweli, kitabu cha hivi karibuni kuhusu televisheni kinaitwa The Unreality Industry. Waandishi wacho wanadai kwamba televisheni “imekuwa moja ya kani zenye uvutano mwingi zaidi katika maisha yetu. Kama tokeo, si kwamba tu televisheni inatoa maana ya uhalisi wa mambo, bali lililo la maana zaidi na lenye kutia hangaiko zaidi ni kwamba, televisheni hufutilia mbali ule upambanufu, ule utofautiano, ulio kati ya mambo halisi na yasiyo halisi.”
Maneno haya huenda yakasikika kuwa ya kuogofya bila sababu nzuri kwa wale wanaofikiri kuwa wao hawawezi kudhuriwa na uvutano wa televisheni. ‘Mimi siamini kila kitu ninachoona,’ wengine hubisha. Ni kweli, huenda tukaelekea kutoamini televisheni. Lakini wastadi wanaonya dhana hiyo ya kujiamulia moja kwa moja haiwezi kutulinda kutokana na njia za udanganyifu ambazo televisheni huvutavuta hisia zetu za moyoni. Kama vile mwandikaji mmoja alivyoliweka jambo hilo: “Hila moja ya maana sana ya televisheni ni kutotoa siri juu ya kadiri ya athari inayopata uwezo wetu wa kufikiri.”
Mashine Yenye Uvutano
Kulingana na 1990 Britannica Book of the Year, Waamerika hutazama televisheni kwa wastani wa saa saba na dakika mbili kila siku. Kisio lingine la kiasi husema hesabu yenyewe ni saa mbili hivi kila siku, lakini hilo bado lingejumlika kuwa miaka saba ya kutazama televisheni katika muda wote wa maisha ya mtu! Ingewezekanaje ufyonzaji mkubwa hivyo wa televisheni ukose kuathiri watu kwa njia fulani?
Huwa haishangazi hata kidogo tunaposoma juu ya watu wanaopata ugumu wa kutenganisha televisheni na uhalisi. Uchunguzi mmoja uliochapishwa katika jarida la Uingereza Media, Culture and Society ulipata kwamba kwa kweli televisheni huwashawishi watu fulani kuanzisha “mwono mwingine badala ya ulimwengu halisi,” ukiwaongoza kufikiri kwamba tamaa zao kuhusu uhalisi huwa ni sehemu ya uhalisi wenyewe. Uchunguzi mwingine, kama ule uliofanyizwa na Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Akili U.S., unaonekana ukiunga mkono matokeo hayo.
Televisheni ingeshindwaje kuwa na uvutano juu ya maisha zenyewe za watu na matendo yao, ikiwa hiyo ina uvutano juu ya maisha yenyewe hasa na vitendo vya watu? Kama vile Donna McCrohan anavyoandika katika Prime Time, Our Time: “Wakati kipindi fulani cha televisheni kilicho maarufu kivunjapo miiko au vizuizi vya lugha, sisi huhisi tukiwa na uhuru mkubwa zaidi wa kuvivunja sisi wenyewe. Vivyo hivyo, sisi huathiriwa wakati . . . ngono za ovyoovyo ziwapo jambo la kikawaida tu, au wakati mwanamume mwenye kiburi cha uume atajapo kwamba yeye hutumia mipira ya kuzuia uzazi. Katika kila pindi, televisheni huwa—kwa msingi wa kitendo kilichokawizwa—kama kioo cha kutuonyesha yule tunayeweza kusadikishwa kwamba sisi ndiye, na kwa hiyo tunakuwa hivyo sana-sana.”
Ni kweli, kutokea kwa muhula wa televisheni kumeandamwa na kutokea kwa ukosefu wa adili na jeuri. Jambo lenye kutokea kiajabu-ajabu? La sivyo. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba kiasi cha uhalifu na jeuri katika nchi tatu kiliongezeka baada tu ya televisheni kuanzishwa katika kila moja ya nchi hizo tatu. Mahali ambapo televisheni ilianzishwa mapema, kiasi cha uhalifu kiliongezeka mapema.
Kwa kushangaza, televisheni hata haihesabiwi kuwa starehe ya kupishia wakati kama watu wengi sana waelekeavyo kufikiri. Uchunguzi uliofanywa juu ya habari 1,200 kwa muda wa kipindi cha miaka 13 ulipata kwamba kati ya starehe zote za kupishia wakati, utazamaji televisheni ndiyo uliokuwa wenye uwezo mdogo zaidi wa kustarehesha watu. Badala yake, ilielekea kuwaacha watazamaji wakiwa wasiotenda mambo lakini wenye mkazo wa mawazo na wasioweza kukaza fikira juu ya jambo moja. Hasa vipindi virefu vya utazamaji viliwaacha watu katika hali ya moyo iliyo mbaya zaidi kuliko wakati walipoanza kutazama. Kwa kutofautiana, kusoma kuliwaacha watu wakiwa wamestarehe zaidi, wakiwa katika hali nzuri zaidi za moyoni, na wenye uwezo zaidi wa kukazia mambo fikira!
Lakini hata iwe usomaji wa kitabu kizuri waweza kujenga namna gani, televisheni, huyo mwivi mwepesi wa wakati, aweza kwa urahisi kusukuma vitabu nje ya habari kabisa. Wakati televisheni ilipoanzishwa kwa mara ya kwanza katika Jiji la New York, maktaba za vitabu za umma upesi ziliripoti mshuko katika mwenezo wa vitabu. Bila shaka, hii haimaanishi kwamba ainabinadamu karibuni itaacha kusoma kabisa. Walakini, imesemwa kwamba watu leo husoma wakiwa na kadiri ndogo ya subira, kwamba uangalifu wao hudhoofika ikiwa picha zenye kutokeza hazimo mbele yao. Huenda takwimu na uchunguzi mbalimbali usiweze kutokeza ithibati madhubuti juu ya mambo hayo yenye mashaka. Bado, sisi tunapoteza nini kwa habari ya utu wetu wa ndani na nidhamu ikiwa tunategemea kufurahishwa daima na mtiririko mwendelevu wa burudisho la televisheni ambalo kila dakika yalo imepangwa kwa njia yenye kunasa uangalifu wa hata mtu yule mwenye uwezo mfupi zaidi wa kukazia fikira juu ya jambo?
Watoto wa Sanduku Hilo
Hata hivyo, ni kwa habari ya watoto kwamba jambo hilo la televisheni linakuwa la muhimu sana. Kwa kufikiria mambo yote yanayohusika, kwa vyovyote ambavyo televisheni yaweza kuathiri watu wazima, yaweza pia kuwaathiri watoto—lakini kwa kiasi kikubwa zaidi. Kwa vyovyote, watoto ndio wanaoelekea kuamini ulimwengu wa ndoto wawezao kuuona katika televisheni. Gazeti la Ujerumani Rheinischer Merkur/Christ und Welt lilionyesha uchunguzi wa hivi majuzi uliopata kwamba watoto mara nyingi “hushindwa kutofautisha maisha halisi kutokana na yale wayaonayo katika televisheni. Wao huhamisha yale wayaonayo katika ulimwengu usio halisi hadi kwenye ulimwengu halisi.”
Uchunguzi mbalimbali wa kisayansi ulio zaidi ya 3,000 uliofanywa kwa miongo mingi ya utafiti umeunga mkono mkataa kwamba vipindi vya televisheni vyenye jeuri vina matokeo hasi kwa watoto na matineja. Mashirika yenye kusifika kama vile Chuo cha Afya ya Watoto cha Amerika, Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Akili U.S., na Shirika la Kitiba la Amerika yote hukubali kwamba jeuri ya televisheni huwafanya watoto wawe na tabia ya kuanzisha ugomvi na nyingine isiyokubalika kijamii.
Uchunguzi mbalimbali umeonyesha matokeo mengine yenye kusumbua. Kwa mfano, unene wakati wa uchanga umefungamanishwa na utazamaji wa televisheni wa kupita kiasi. Kwa wazi kuna sababu mbili. (1) Saa zinazotumiwa kukaa tu mbele ya sanduku hilo huchukua mahali pa saa zenye utendaji wa kucheza. (2) Matangazo ya kibiashara katika televisheni hufanikiwa sana kuwafanya watoto wale chakula cha mafuta kisichofaidi mwili. Utafiti mwingine umedokeza kwamba watoto wanaotumia wakati mwingi sana kutazama televisheni hawafanyi vema shuleni. Hali mkataa ukiwa wenye kubishaniwa, gazeti Time hivi karibuni liliripoti kwamba madaktari wengi wa magonjwa ya akili na waalimu wanailaumu televisheni kwa mshuko mkubwa katika stadi za watoto za kusoma na utendaji wao wa shuleni.
Tena, wakati ni jambo la maana. Kufikia wakati ambapo mtoto wa kadiri wa Amerika afikiapo kuhitimu kutoka shule ya sekondari, yeye ametumia saa 17,000 akiwa mbele ya televisheni ikilinganishwa na saa 11,000 akiwa shuleni. Kwa watoto wengi, kutazama televisheni huwa ndio utendaji wao wa maana kwa wakati usio na kazi ikiwa sio utendaji ulio wa maana zaidi wa wakati wote. Kitabu The National PTA Talks to Parents: How to Get the Best Education for Your Child kinasema kwamba nusu ya wale walio katika darasa la tano (wa miaka kumi) hutumia dakika nne kila siku wakisoma nyumbani, lakini dakika 130 wakitazama televisheni.
Mwisho, huenda kukawa na wachache sana wanaoweza kubisha kwa uzito kwamba televisheni haitoi hatari halisi sana kwa watoto na watu wazima pia. Lakini hilo linamaanisha nini? Je, wazazi wanapaswa kupiga marufuku utazamaji wa televisheni nyumbani? Je, watu kwa ujumla wapaswa wajilinde kutokana na uvutano wayo kwa kuitupa nje au kuipakia na kuiweka mahali karibu na paa ya nyumba?
[Maelezo ya Chini]
a Ona “Je! Kweli Kweli Unaweza Kuziamini Habari?” katika toleo la Amkeni! la Aprili 8, 1991.
[Blabu katika ukurasa wa 7]
“Kwa nini weupe hudungana visu, kufyatuliana risasi na kupigana ngumi kila wakati?”
[Picha katika ukurasa wa 9]
Zima televisheni, fungua vitabu