Dhibiti Televisheni Kabla Haijakudhibiti Wewe
TELEVISHENI ina uwezo mkubwa sana wa mambo. Wakati kiwanda cha televisheni cha Amerika kilipokuwa kikihimiza mataifa yanayoendelea yatumie televisheni, kilitoa ndoto za televisheni zisizowezekana. Nchi nzima nzima zingebadilishwa kuwa madarasa, huku hata sehemu za ndani-ndani mashambani zikihusishwa kusikiliza vipindi vya elimu juu ya mambo ya maana kama vile ustadi wa kilimo, uhifadhi wa udongo, na mpango wa uzazi. Watoto wangeweza kujifunza fizikia na kemia na wafaidike kutokana na mbadilishano wenye kukua wa tamaduni.
Bila shaka, ndoto kama hizo zilitoweka kwa kiwango kikubwa kwa uhalisi uliofuata wa televisheni yenye matangazo ya kibiashara—lakini si kabisa. Hata Newton Minow, mkuu wa Baraza la Mawasiliano aliyeita televisheni kuwa “bara kubwa lililo tupu,” alikiri katika hotuba hiyo hiyo ya 1961 kwamba televisheni ilikuwa na sifa ya kutimiza makuu na kuandaa tafrija zenye kupendeza.
Hapana shaka kwamba hilo bado ni kweli hata leo. Habari zinazotangazwa katika televisheni hutuarifu juu ya matukio ya ulimwengu. Vipindi vya televisheni vinavyohusu maumbile hutuwezesha kuona kwa ufupi vitu ambavyo labda hatungeweza kuviona kamwe: uzuri dhahiri wa ndege kivumi anayechukuliwa picha akiwa na mwendo wa polepole, akionekana kana kwamba anaogelea hewani; au ule mtingishiko wa ajabu wa maua yaliyopigwa picha ya mwendo wa kasi kuyafanya yaonekane yakikua mbio-mbio, huku yakichomoza udongoni yakiwa na urangirangi wa kupendeza. Halafu kuna tamasha za kitamaduni, kama vile dansi za kujirusha na kuzunguka kwa hatua za mwendo wenye fahari na haiba, michanganyo ya mivumo kutoka ala mbalimbali za kimuziki, na tamthilia za kimuziki. Tena kuna michezo ya kuigiza, sinema, na vipindi vingine—baadhi yavyo vikiwa vya kuelimisha sana na kutia mwono-ndani, vingine vikiwa ni burudisho zuri tu.
Kuna vipindi vya kuelimisha kwa watoto. Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Akili yaripoti kwamba kama vile watoto wawezavyo kujifunza ugomvi kutokana na jeuri ya televisheni, wao waweza pia kujifunza kujitoa wasaidie wengine bila kutazamia faida za kibinafsi, kuwa na urafiki, na wenye kujidhibiti kutokana na mifano mizuri kwenye televisheni. Vipindi juu ya jinsi ya kutenda wakati wa dharura hata vimeokoa maisha za watoto. Hivyo, Vance Packard aandika katika Our Endangered Children: “Wazazi wanaochukizwa au kusumbuliwa wanaoweka mbali televisheni zikiwa mahali fulani karibu na paa ya nyumba huwa labda wanatenda kwa kupita kiasi, isipokuwa kama hali ya watoto ni ya kushindwa kabisa kujidhibiti.”
Kuidhibiti
Kwa wazi, iwe tunazungumzia juu ya watu wakubwa au watoto, ufunguo ni huo tu—udhibiti. Je, sisi hudhibiti televisheni, au televisheni ndiyo hutudhibiti? Kama vile Bw. Packard adokezavyo, kwa wengine njia pekee ya kudhibiti televisheni ni kwa kuiondolea mbali. Lakini wengine wengi wamepata njia za kuidhibiti hali bado wakitumia manufaa zayo. Yafuatayo ni baadhi ya madokezo.
✔ Kwa juma moja au mawili, weka rekodi nzuri ya utazamaji wa televisheni wa familia yako. Jumlisha saa hizo mwishoni mwa kipindi hicho halafu ujiulize kama televisheni inastahili wakati inaochukua.
✔ Tazama vipindi vya televisheni—si televisheni tu. Chunguza orodha ya vipindi ili uone kama kuna lolote linalostahili kutazamwa.
✔ Weka na ulinde nyakati fulani fulani za maongezi ya familia na upamoja.
✔ Wataalamu fulani huonya dhidi ya kuruhusu watoto au matineja wachanga wawe na televisheni katika vyumba vyao. Huenda ikawa vigumu zaidi kujua kile mtoto wako anachotazama.
✔ Ikiwa una uwezo wa kupata VCR (video-kaseti-rekoda), inaweza kusaidia. Kwa kukodisha ukanda mzuri wa video au kwa kunakili vipindi vizuri na kuvitazama wakati ufaao, unaweza kutumia VCR kudhibiti yale yaliyo katika televisheni yako—na wakati ambao televisheni yako imewashwa. Hata hivyo, kuna tahadhari. Ikiwa haidhibitiwi, VCR yaweza tu kuongeza wakati unaotumiwa mbele ya televisheni au ifanyize njia ya kanda za video zisizo za adili.
Mwalimu Wako ni Nani?
Binadamu ni kama mashini yenye kujifunza. Hisi zetu wakati wote huwa zinafyonza habari, zikipeleka vipande vya habari 100,000,000 kwenye ubongo kwa kila sekunde. Kwa kiwango fulani tunaweza kuwa na uvutano juu ya kilicho katika habari zenyewe kwa kuamua kile tutakacholisha hisi zetu. Kama vile hadithi ya televisheni ionyeshavyo waziwazi, akili na roho ya binadamu yaweza kuchafuliwa kwa kile tutazamacho kama vile tu ilivyo rahisi kwa mwili kuchafuliwa kwa kile tunachokula na kunywa.
Sisi tutajifunzaje juu ya ulimwengu unaotuzunguka? Ni vyanzo vipi vya habari tutakavyochagua? Ni nani au nini kitakachokuwa mwalimu wetu? Maneno ya Yesu Kristo yanatoa wazo lenye busara kuhusu jambo hilo: “Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake.” (Luka 6:40) Ikiwa tunatumia wakati mwingi sana tukitazama televisheni kama mwalimu wetu, huenda tukaanza kuiiga—tukifuata thamani na viwango itoavyo. Kama vile Mithali 13:20 iwekavyo wazo hilo: “Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; bali rafiki wa wapumbavu ataumia.”
Hata wakati ambapo televisheni haileti watu wapumbavu au wasio na adili nyumbani mwetu, bado inakosa jambo la maana. Ni vipindi vichache sana kati ya vile vionyeshwavyo katika televisheni ambavyo huzungumzia uhitaji wa kila binadamu: uhitaji wa kiroho. Televisheni yaweza kuonyesha vizuri sana jinsi ulimwengu huu ulivyo katika hali ya mchafuko wenye kusikitisha, lakini hiyo hufanya nini ili kutueleza kwa nini mwanadamu anaonekana kama kwamba hawezi kujitawala? Televisheni yaweza kuonyesha uzuri wa uumbaji, lakini hiyo hufanya nini ili kutuvuta kwa Muumbaji wetu? Televisheni yaweza kutuchukua hadi kwenye pembe nne za tufe hili, lakini je, hiyo yaweza kutueleza kama mwanadamu ataishi kamwe juu yake kwa amani?
Hakuna “dirisha [lolote] la kuchungulia ulimwengu” lililo kamili bila kujibu maswali hayo ya kiroho yenye maana. Hilo ndilo hasa hufanya Biblia iwe yenye thamani sana. Hiyo hutoa “dirisha la kuchungulia ulimwengu” kulingana na mwono wa Muumbaji wetu. Imefanyizwa kitusaidie kuelewa kusudi letu maishani na kutupa sisi tumaini hakika la wakati ujao. Majibu yenye kuridhisha juu ya maswali yanayosumbua sana kuhusu maisha yanapatikana kwa urahisi. Hayo yanangoja kusomwa humo katika kurasa za Biblia zenye kuvutia daima.
Lakini ikiwa sisi hatuidhibiti televisheni, tutaupata wapi wakati?