Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 9/22 kur. 15-17
  • Cock-of-the-Rock—Mrembo wa Msitu wa Amazon

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Cock-of-the-Rock—Mrembo wa Msitu wa Amazon
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mabishano ya Mipakani na Ugomvi wa Urithi
  • Na Mshindi Ni . . .
  • Kizazi Kifuatacho
  • Kuwatazama Ndege—Je, Kwavutia Kila Mtu?
    Amkeni!—1998
  • “Mkazi wa Msituni Mwenye Kuvutia Kuliko Wote”
    Amkeni!—2000
  • Manyoya—Ubuni wa Ajabu
    Amkeni!—2007
  • Je, Wanataka Tu Kujirembesha?
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 9/22 kur. 15-17

Cock-of-the-Rock—Mrembo wa Msitu wa Amazon

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Brazili

KWA kweli wapenda-asili hatimaye huwa washairi wanapomfafanua cock-of-the-rock wa Guiana, ndege mwenye kupendeza na asiyejulikana sana wa msitu wa mvua wa Amazon.a “Ni mwale mwangavu,” akaandika mtu mmoja. “Ni nyotamkia yenye rangi ya moto,” akasema mwingine. “Ni vigumu kumpita kwa . . . uvutio,” akamalizia mtu wa tatu. Wote walikubaliana kwamba uvutio wake hausahauliki. Lakini, ni nini hasa hufanya ndege huyu anayetoshana na njiwa aweze kukumbukwa sana? Sababu moja ni umaridadi wake.

Ndege wa kiume wa cock-of-the-rock hujivunia kishungi chenye rangi ya machungwa kinachofanana na kipepeo na hufunika mdomo wake wote. Mstari wenye rangi ya kijivujivu na nyekundu, unaofuata sehemu za pembeni, unatokeza waziwazi kishungi chenye umbo la nusu-duara lisilo na kasoro. Kutoka kwenye kishungi hadi kwenye kucha, ndege huyo amefunikwa na manyoya yenye rangi ya machungwa. Mabawa yake meusi yenye viraka vyeupe, yanafunikwa na tabaka la manyoya yenye rangi ya kidhahabu na kimachungwa, ambayo humfanya aonekane kana kwamba amefunikwa kwa shali. “Umbo lao na mwonekano wao,” chasema kifupi kitabu Birds of the Caribbean, “ni uzuri usioweza kufafanuliwa.” Ndege huyu huvutia si kwa sababu ya mwonekano wake tu. Manyoya yake pia hudhihirisha tabia yake. Katika njia gani?

Ndiyo, utakubali kwamba katika msitu wa rangi ya kijani kibichi, ikiwa hungependa kutambuliwa, hungevalia nguo ya rangi ya machungwa nyangavu. Hata hivyo, ndege huyu maridadi wa msituni ataka kuonekana. Yeye hutumia urembo wake ili kuwafukuza wapinzani na kuvutia wenye kumtamani.

Mabishano ya Mipakani na Ugomvi wa Urithi

Mapema mwakani, wakati wa majira ya kujamiiana, cock-of-the-rock wa kiume huteremka hadi kwenye maeneo ya misitu yaliyo na mipaka dhahiri yanayoitwa lek, ambayo ni nyanja za ndege hao kuchezea dansi za uchumba za kila mwaka. Labda neno hili “lek” linatokana na kitenzi cha Kisweden att leka, kinachomaanisha “kucheza.” Kwa kweli, kwa miaka mingi wapenda-asili walielewa kurukaruka huko kwa furaha kwa uchumba kuwa mchezo tu—maonyesho yenye kupendeza kwenye msitu. Ingawa hivyo, hivi karibuni walipata kujua kwamba lek si ukumbi wa dansi tu bali uwanja wa mweleka na maonyesho. Kwa nini?

Baada ya kikundi cha cock-of-the-rock wa kiume kuvamia lek, kila ndege hutia alama kisehemu fulani cha msitu kuwa eneo lake la kibinafsi kwa kuondoa majani yaliyoanguka hapo. Pia hudai vitulio vilivyo juu ya ua, hivi kwamba eneo lake hufanyiza mcheduara upatao meta moja na nusu kwa upana na meta mbili kwa urefu. Ndege wapatao 50 wakiwa wamesongamana ndani ya lek moja, asema mtafiti Pepper W. Trail, nyua zao ni “miongoni mwa zile zilizosongamana zaidi kuliko aina yoyote ya ndege wa lek.” Kwa matokeo gani? Mabishano ya mipakani na ugomvi wa urithi.

Mabishano yao ya mipakani hufanana na ngoma za vita zenye kusisimua lakini zisizodhuru—kuinua kichwa kwa ghafula na kukitikisa-tikisa, kupiga-piga mdomo, kutikisa mabawa, na kuvumisha manyoya, yanayochangamana na kuwika na kuruka juu hewani. Baada ya dakika moja au mbili, wakati kila ndege ahisipo kuwa amemtisha mwingine, wote hurudi kwenye maeneo yao. Lakini, wakati ndege wawili watakapo kunyakua lek ileile moja ambayo iliachwa na ndege mwingine aliyekufa, bishano hugeuka kuwa pigano halisi la urithi.

“Ndege hao huunganisha kucha zao zenye nguvu, huchapana kwa mabawa yao, na mara kwa mara huunganisha midomo yao. Mechi kama hizo,” aandika Trail katika gazeti National Geographic, “zaweza kuchukua muda wa saa tatu na kuacha wapiganaji wakihema.” Ikiwa hakuna mshindi dhahiri baada ya duru hii ya kwanza, ndege hao hupumzika, lakini baada ya hapo, pigano huanza tena na huendelea mpaka mrithi atakapojulikana wazi.

Punde baada ya vita, mwanamweleka huyo mkali hubadili tabia yake na kusimama tuli, na lek hugeuka kuwa wonyesho. Kwa nini onyesho hili jipya? Sehemu ya mwisho ya jina la ndege huyu, cock-of-the-rock, hutoa jibu.

Na Mshindi Ni . . .

Wakati ndege wa kiume wanapozozana kwenye sakafu ya msitu, ndege wachache wasio na rangi yenye kuvutia wanakarabati viota vyao kwa ukimya katika sehemu zilizokingwa za miamba iliyo karibu. Ndiyo, wao ni ndege wa kike cock-of-the-rock. Tofauti na ndege wa kiume, wa kike si warembo. Mtafiti David Snow aandika kwa busara kwamba ndege huyo ni wa “aina tofauti kabisa.” Kichwa chake kina taji dogo, ambalo “ni mwigizo wa kishungi chenye fahari cha ndege wa kiume, ambacho hufanya kichwa chake kiwe chenye sura ya kupendeza.” Ndege huyo wa kike ana miguu mifupi na nyayo kubwa, mwili wenye rangi hafifu ya kikahawia wenye “umbo zito lisilopendeza.”

Hata hivyo, yeye ni mrembo kwa wale wa kiume. Anapoingia ndani ya matawi juu ya lek, kwa sauti ya juu kiuoou, husababisha kila ndege wa kiume amtazame na kutokeza maonyesho ambayo ni “baadhi ya maonyesho ya uchumba yenye kupendeza na kuvutia zaidi miongoni mwa ndege wote.” (The Life and Mysteries of the Jungle) Ni nini hutukia? Mtafiti Trail asema kwamba ndege wa kike aonekanapo tu, “lek hujaa rangi, mwendo, na sauti,” kila ndege wa kiume ajaribupo kuwashinda wengine na kuvutia uangalifu wa ndege wa kike. Kisha, ndege wa kiume huruka kutoka kwenye vitulio vyao na kutua kwa kishindo na kilio kwenye nyua zao. Mabawa yao yanapopigapiga huvutia uangalifu wa ndege wa kike na kufagilia mbali majani yaliyoanguka uani. Kisha kwa ghafula, vurugu hukoma. Wakati wa kukata maneno umefika.

Kila ndege wa kiume huinama kwa ugumu, manyoya yake yakiwa yamesambaa, na kuganda kana kwamba amepagawa. Kishungi chake kilichojitokeza kama feni huuficha mdomo wake huku manyoya yake yakisitiri umbo la mwili wake, na kumfanya aonekane kama ua la rangi ya machungwa lililoanguka msituni. Kitabu kimoja chasema kwamba “mwonekano wa cock-of-the-rock ni wa kustaajabisha sana, hivi kwamba mara ya kwanza ni vigumu kuamini kwamba ni ndege.”

Ingawa hivyo, ndege wa kike aweza kupambanua kati ya ua na mchumba na huteremka akielekea kwa ndege wa kiume watatu au wanne walio kimya, ambao huweka miili yao ikiwa bapa na migongo yao ikiwa imegeuzwa kuelekea ndege wa kike. Hata hivyo, wamegeuza vichwa vyao hivi kwamba jicho moja linaangalia juu, likielekezwa kwa ndege wa kike. Dakika kadhaa zapita ndege wa kike afanyapo uamuzi, lakini mwishowe, ateua mshindi. Yeye hutua nyuma ya ndege wa kiume ambaye anampenda zaidi, huruka akielekea kwake, huegama mbele, na kudonoa unyoya wake. Kisha ndege wa kiume huanza kutenda tena. Wanajamiiana katika ua wake au kwenye kitulio kilicho karibu. Baada ya hayo, ndege wa kike hupuruka na kwenda zake. Majira ya kujamiiana yafikapo, ndege wa kike hurudia mwenzi yuleyule.

Mpaka wakati wa majira ya uchumba, ndege wa kiume husahau mwenzi wake wala hashughuliki kutunza wazao. Bila kujali, hujitayarisha kwa maonyesho yatakayofuata, huku ndege wa kike akilea familia akiwa peke yake. Kwa kweli, jambo hilo laonekana kana kwamba kazi haikugawanywa kwa njia ya haki, lakini ni afadhali kwa ndege wa kike na makinda yake kwamba ndege wa kiume akae mbali. Kwani, kuwa na ndege mwenye rangi ya machungwa akizunguka karibu na kiota chako halingekuwa jambo la hekima, kama vile lisingelikuwa jambo la busara kutangaza kwa wazi maficho yako.

Kizazi Kifuatacho

Manyoya hafifu ya kike hufaa sana kufunika mayai mawili ya rangi ya kikahawia, na yenye madoa ambayo huyataga ndani ya kiota kikubwa cha matope ambacho hushikiliwa kwenye ukuta wa mawe na mate ya ndege huyo. Baada ya mama kuatamia mayai hayo kwa majuma manne, huangua makinda. Ingawa si warembo wanapoanguliwa, wanakuwa tayari kukabiliana na siku watakazokaa ndani ya kiota. Muda mfupi baada ya kutoka kwenye makaka ya mayai, aeleza mtafiti Trail, wanashika kwa kucha zao kali sehemu ya ndani ya kiota na, kwa miguu yao yenye nguvu, wananing’inia kwa uthabiti wakati wowote mama anapong’ang’ana kupata mahali pa kusimama.

Kwa bidii mama huwalisha makinda yake matunda na mara moja moja wadudu au mjusi. Baada ya mwaka mmoja, manyoya ya ndege wa kiume bado huwa ya rangi ya kikahawia, lakini tayari kichwa chake huwa na kishungi kidogo. Anapofikia umri wa miaka miwili, manyoya yake ya kikahawia hubadilika kuwa ya rangi ya kidhahabu na ya kimachungwa ambayo humbadilisha kuwa “mmojawapo wa ndege maridadi zaidi ulimwenguni” kama aandikavyo mpenda-asili mmoja.

Ujapokuwa uharibifu wa msitu ulio makao ya cock-of-the-rock, wapenda-asili wanatumaini kwamba watu hawatamnyang’anya mchezaji huyu mwenye kupendeza wa Amazon uwezekano wa kuendelea na dansi yake yenye kuvutia ya kujamiiana.

[Maelezo ya Chini]

a Aina hii ya ndege hutofautiana na cock-of-the-rock wa Peru, ambaye huishi katika miteremko ya Milima ya Andes katika Bolivia, Ekuado, Kolombia, na Peru.

[Sanduku katika ukurasa wa 17]

Kitambulisho cha Cock-of-the-Rock

Jina la Kisayansi: Rupicola rupicola, au “mkaaji wa mahali penye mawemawe”

Familia: Cotingidae

Eneo la makao: Kaskazini mwa Amerika ya Kusini, ndani ya bonde la Amazon na kulizunguka

Urefu: Karibu sentimeta 30

Kiota: Kimefanyizwa kwa matope na mimea iliyoshikanishwa kwa mate, kina uzito wa kilogramu 3.9

Ndege mchanga: Kwa kawaida mayai mawili kwa mwaka; muda wa kuatamia mayai ni siku 27 hadi 28—“kipindi kirefu zaidi kinachojulikana miongoni mwa ndege wakubwa”

[Ramani katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Makao ya “cock-of-the-rock” wa Guiana

AMERIKA KUSINI

[Hisani]

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Kenneth W. Fink/Bruce Coleman Inc.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki