Kutafuta Maisha Yenye Usalama
USALAMA wamaanisha mambo tofauti kwa watu mbalimbali. Kwa mtu mmoja usalama wamaanisha kuwa na kazi ya kuajiriwa; kwa mwingine, ni kuwa na mali; na kwa mtu wa tatu, usalama wamaanisha mazingira yasiyokuwa na uhalifu. Je, wamaanisha jambo tofauti kwako?
Hata maoni yako yaweje, bila shaka unachukua hatua za kujaribu kufanya maisha yako yawe kama utakavyo. Fikiria wanavyofanya watu katika Ulaya ili kujipatia usalama wa kibinafsi wa kiasi fulani.
Elimu ya Juu
Kulingana na Jacques Santer, msimamizi wa Tume ya Ulaya, asilimia 20 ya vijana katika Muungano wa Ulaya hawana kazi za kuajiriwa. Kwa sababu hiyo, kwa kikundi hicho, mengi yategemea swali moja, Nitapataje kazi itakayonipa usalama maishani? Wengi wanaamini kwamba mradi huu waweza kutimizwa vizuri kwa kupata elimu ya juu, ambayo, kama lielezavyo The Sunday Times la London, huwapa wanafunzi “uwezo muhimu wa kupata kazi ya kuajiriwa.”
Mathalani, katika Ujerumani, “tamaa ya elimu na hadhi ya utaalamu imekuwa kubwa kuliko wakati mwingine wowote,” laripoti Nassauische Neue Presse. Ndivyo hali ilivyo licha ya kwamba gharama za elimu ya chuo kikuu katika nchi hiyo ni karibu dola 55,000 kwa wastani.
Vijana wanaochukua elimu kwa uzito na wanaotamani usalama wa kazi wapaswa kupongezwa. Na mara nyingi mtu aliye na stadi na aliyehitimu ana uwezekano wa kupata kazi. Lakini je, sikuzote elimu ya juu hutoa usalama wa kazi? Mwanafunzi mmoja alisema hivi: “Tangu mwanzo nilijua kwamba mtaala wa masomo yangu haungenisaidia kupata kazi ya kitaalamu na haungeniletea usalama.” Kisa chake si cha kipekee. Katika mwaka mmoja wa hivi karibuni, idadi ya wanafunzi waliohitimu katika vyuo vikuu katika Ujerumani ilifikia kilele kikubwa kabisa.
Kulingana na gazeti moja la habari, katika Ufaransa, vijana hujiunga na vyuo vikuu kwa sababu cheti cha shule ya sekondari hakina thamani kwa sababu ya idadi kubwa ya vijana wasiokuwa na kazi za kuajiriwa. Hata hivyo, wanafunzi wengi wa chuo kikuu wanatambua kwamba wamalizapo masomo yao, “hawatafanikiwa hata ingawa watakuwa na digrii.” Gazeti The Independent laripoti kwamba katika Uingereza “mikazo ya maisha ya kitaaluma inaathiri wanafunzi sana.” Inaripotiwa kwamba mkazo badala ya kusaidia wanafunzi wakabiliane na ukosefu wa usalama wa maisha, nyakati fulani maisha katika chuo kikuu husababisha matatizo kama vile mshuko-moyo, hangaiko, na kutojistahi.
Mara nyingi, kujifunza ufundi fulani au kupata mazoezi yanayotumika katika uwanja fulani wa kutokeza vitu humwezesha mtu ajipatie kazi ya kuajiriwa kwa utayari zaidi kuliko kuwa na digrii ya chuo kikuu.
Je, Mali Zatosha?
Wengi wanaamini kwamba siri ya maisha yenye usalama ni mali. Jambo hilo laweza kuonekana kuwa zuri, kwa sababu kuwa na pesa nyingi kwenye benki ni akiba inayoweza kutumiwa nyakati za magumu. Biblia hueleza kwamba ‘fedha ni ulinzi.’ (Mhubiri 7:12) Hata hivyo, je, sikuzote mali nyingi huboresha usalama wa kibinafsi?
Si lazima iwe hivyo. Fikiria namna mali zimeongezeka katika miaka 50 iliyopita. Mwishoni mwa Vita ya Ulimwengu ya Pili, Wajerumani wengi hawakuwa na mali. Leo, kulingana na gazeti la habari la Ujerumani, Mjerumani wa kawaida ana vitu 10,000. Ikiwa matabiri ya kiuchumi ni sahihi, vizazi vijavyo vitakuwa na mali nyingi hata zaidi. Lakini je, kukusanya mali hufanya maisha yawe salama zaidi? Hapana. Uchunguzi uliofanywa nchini Ujerumani ulifunua kwamba watu 2 kati ya 3 wanaona maisha yakiwa bila usalama kuliko yalivyokuwa miaka 20 au 30 iliyopita. Kwa hiyo, kuongezeka sana kwa mali hakujafanya watu wahisi kuwa salama zaidi.
Jambo hili laeleweka kwa sababu, kama ilivyotajwa katika makala iliyotangulia, kuhisi ukosefu wa usalama ni mzigo wa kihisia-moyo. Na mzigo wa kihisia-moyo hauwezi kuondolewa kabisa na mali za kimwili. Kweli, mali hupunguza madhara yaletwayo na umaskini na husaidia wakati wa shida. Lakini chini ya hali fulani, kuwa na pesa nyingi ni mzigo mkubwa unaotoshana na kuwa na pesa chache.
Kwa sababu hiyo, mtazamo uliosawazika kuelekea vitu vya kimwili utatusaidia tukumbuke kwamba ingawa mali zaweza kuwa baraka, si jambo la msingi la kuwa na usalama maishani. Alipokuwa duniani, Yesu Kristo aliwatia moyo wafuasi wake akisema: “Hata wakati mtu ana wingi uhai wake hautokani na vitu alivyo navyo.” (Luka 12:15) Ili mtu apate usalama kamili katika maisha, anahitaji mambo mengine mbali na vitu vya kimwili.
Kwa wazee-wazee, mali ni za maana si kwa sababu ya thamani yake ya kimwili bali kwa sababu ya jinsi wazee-wazee wanavyoziona. Linalowahangaisha zaidi wazee-wazee kuliko mali ni kutendwa kijeuri.
Jihadhari!
“Uhalifu . . . umekuwa tatizo linalokua ulimwenguni pote kwa miaka 30 iliyopita,” chasema kijitabu Practical Ways to Crack Crime, kilichochapishwa Uingereza. Polisi wanafanya kazi kwa bidii sana. Watu wengine wanakabilianaje?
Usalama wa kibinafsi huanzia nyumbani. Kwa kielelezo, katika Uswisi, msanifu-ujenzi mmoja hubuni nyumba zilizoimarishwa dhidi ya wezi zenye vifuli vya usalama, milango iliyoimarishwa, na madirisha yenye fito. Wenye kumiliki nyumba hizi huuchukua kihalisi msemo huu ujulikanao sana: “Nyumba yangu ndiyo buruji langu.” Kulingana na gazeti la habari Focus, nyumba hizi ni ghali, lakini wengi wanazitaka.
Ili kuzidisha usalama wa kibinafsi ndani na nje ya nyumba, wakazi wa jumuiya fulani wamepanga watu wa kulinda ujirani usiku. Wakazi wa viunga fulani huchukua hatua za kutahadhari hata zaidi kwa kulipa makampuni ya ulinzi ili kulinda eneo lao kwenye saa fulani. Watu wengi wanahisi kwamba haifai kuwa peke yako usiku katika barabara za jiji zilizo ukiwa. Na wazazi ambao kiasili huhangaikia hali njema ya watoto wao, waweza kuchukua tahadhari zaidi ili kuwalinda. Fikiria madokezo yanayopatikana katika sanduku kwenye ukurasa huu.
Lakini si kila mtu awezaye kugharimia nyumba iliyoimarishwa dhidi ya wezi. Mbali na hilo, mipango ya ujirani na walinzi wenye kushika doria huenda wasipunguze kabisa uhalifu; wao waweza kuhamisha tu uhalifu kwenye maeneo yasiyolindwa. Kwa hiyo uhalifu ungali tisho kubwa kwa usalama wa kibinafsi. Ili maisha yetu yawe salama, mengi zaidi yahitajiwa kuliko jitihada zote za kuondoa uhalifu.
Tibu Maradhi—Si Dalili Tu
Kila mmoja wetu ana tamaa ya asili ya kutaka maisha salama, na twafanya vema kuchukua hatua zifaazo ambazo zinaweza kutumika ili kufikia mradi huu. Lakini uhalifu, ukosefu wa kazi, na mambo mengine yote yafanyayo maisha yetu yasiwe salama ni dalili tu za hali inayoathiri wanadamu wote. Ili kutibu hali hii, ni muhimu kushambulia, si dalili tu, bali chanzo chenyewe.
Ni nini chanzo cha ukosefu wa usalama katika maisha yetu? Twaweza kukiondoaje na hivyo kumaliza ukosefu wa usalama katika maisha yetu milele? Jambo hili litazungumziwa katika makala inayofuata.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Njia za Kulinda Watoto Wachanga
Kwa sababu ya watoto kushambuliwa mara nyingi, kutekwa nyara, na mauaji, wazazi wengi wameliona kuwa jambo linalosaidia kuwafundisha watoto wao kufanya mambo yafuatayo:
1. Kukataa katakata ikiwa mtu yeyote anajaribu kuwafanya wafanye jambo wanalohisi ni baya.
2. Kukataza mtu yeyote asiguse sehemu zao za siri ila tu—iwe ni daktari au muuguzi—mzazi akiwepo.
3. Wakimbie, wapige yowe, au wamwombe mtu mzima msaada wanapokuwa hatarini.
4. Waambie wazazi kuhusu kisa au mazungumzo yoyote yasiyomstarehesha mtoto.
5. Wasikubali kuwaficha mambo wazazi.
Jambo la mwisho, wazazi hufanya vyema kuwa waangalifu wanapoteua mtu wa kumtunza mtoto wao.
[Picha katika ukurasa wa 5]
Ili maisha yetu yawe salama twahitaji mengi zaidi kuliko elimu, mali, au jitihada zote za kushinda uhalifu