Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 10/8 kur. 21-25
  • Je, Reli Itadumu?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, Reli Itadumu?
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maendeleo ya Karne ya 19
  • Mabadiliko ya Magari-Moshi
  • Reli Yaimarishwa na Tramu
  • Je, Magari-Moshi Ni Kasi na Salama Zaidi?
  • Wakati Ujao wa Kutumia Sumaku?
  • Reli Inayoenea Kotekote India
    Amkeni!—2002
  • “Reli ya Kichaa” ya Afrika Mashariki
    Amkeni!—1998
  • Reli Iliyochukua Zaidi ya Miaka 120 Kujengwa
    Amkeni!—2008
  • Gari-Moshi Lisilo na Magurudumu
    Amkeni!—2008
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 10/8 kur. 21-25

Je, Reli Itadumu?

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Uingereza

JINSI ya kusafirisha mizigo na watu katika nchi kavu kwa bei nafuu na kwa haraka ni tatizo la kudumu. Tangu enzi za mvuvumko wa viwanda ziongeze mahitaji ya mali ghafi, reli imechangia sana kusuluhisha tatizo hilo. Kwa sababu ya kuendelea kutegemea zaidi injini za petroli na hangaiko kuhusu uchafuzi, wengi wanachunguza tena reli.

Reli ilianzaje? Inachangia nini katika jumuiya ya kisasa? Ina wakati ujao wa aina gani?

Maendeleo ya Karne ya 19

Mnamo 1804 gari-moshi lililotengenezwa na mhandisi wa Cornwall Richard Trevithick, lilikokota tani kumi za fito za chuma kwenye reli ya kilometa 14 kwa mwendo wa kilometa 8 kwa saa. Lakini ufanisi huo wa awali wa reli haukudumu kwa sababu reli hizo dhaifu ziliporomoka upesi kutokana na uzito wa gari-moshi. Kukawa na tatizo wakati huo la kuunda gari-moshi ambalo lingekuwa na uzito wa kutosha wa kushika reli za chuma na kulizuia lisiteleze kutoka kwenye reli na ambalo pia halingeharibu reli.

Miaka minane baadaye, John Blenkinsop, alitengeneza reli zenye meno za kutumiwa katika machimbo ya makaa-mawe ya Yorkshire. Kisha, William Hedley akatatua tatizo la kuteleza kwenye reli kwa kutumia nguvu za mvuke kupitia gia ili kusogeza jozi moja-moja ya magurudumu ya gari-moshi. Baada ya hapo, kwa ukawaida magari-moshi yakawa yakienda kwenye reli laini. Kufikia mwaka wa 1820, reli za chuma-mfuo zenye urefu wa meta sita-sita zilitegemeza magari-moshi makubwa na mazito zaidi ambayo yalikuwa yakitengenezwa.

Reli ya Uingereza ya Stockton & Darlington ikawa maarufu sana katika mwaka wa 1825 wakati ambapo gari-moshi la abiria la kwanza kabisa ulimwenguni lilipokokota tani 69 za mizigo na zaidi ya abiria 600 kwenye reli ya kilometa 34 likifikia kilele cha mwendo wa kilometa 24 kwa saa. Mmojawapo wa abiria hao, Mmarekani Evan Thomas kutoka Baltimore, Maryland, alirudi nyumbani kwao na kuwashawishi wafanya-biashara wenzake watumie reli badala ya mfereji wa maji jijini mwao. Basi Reli ya Baltimore & Ohio ikaanzishwa mwaka wa 1827.

Reli za chuma cha pua, ambazo ni thabiti mara zipatazo 60 kuliko chuma-mfuo zikawa zinatumiwa zaidi. Jambo hilo lilitukia Uingereza tokea mwaka wa 1857 na kuendelea. Kufikia 1870 reli za nchi hiyo zilienea kupita kilometa 20,000. Kukawa na tofauti “kubwa sana,” lasema The Times la London. “Kabla ya reli kuwapo, watu wengi hata hawakuwa wamepata kusafiri nje ya vijiji vyao.”

Kwingineko, pia, reli zilikuwa zinaenea. Kwa mfano, mnamo 1847 matajiri wa Zurich, Uswisi, walianza kutuma watumishi wao kwenye mji wa Baden ambapo kulikuwa na reli mpya ili wakalete mikate midogo ya Hispania waliyoipenda (brötli). Huo ukawa ndio mwanzo wa miaka 150 wa Waswisi kupenda reli.

Reli zilichangia sana maendeleo ya Marekani. Mnamo 1869, reli ya kwanza iliyovuka bara ilimalizika katika Amerika ya Kaskazini, tokea Pwani ya Mashariki hadi Pwani ya Magharibi. Ilifanya sehemu za magharibi za Marekani zikaliwe haraka. Mnamo 1885 reli ya kwanza ya kuvuka bara ilimalizika nchini Kanada, tokea Montreal, Quebec, hadi Vancouver, British Columbia. Kwa kweli, ulimwenguni pote, reli zilisitawi.

Mabadiliko ya Magari-Moshi

Kadiri wakati ulivyopita, mameneja wa reli walianza kutafuta njia za kutumia magari-moshi kwa njia bora zaidi. Walipata kwamba magari-moshi ya dizeli na umeme, ambayo yalikuwa bora kwa mara mbili na nusu hivi kuliko magari-moshi ya mvuke, hayakuwa na gharama sana yakitumiwa. Ingawa ilikuwa ghali zaidi kutengeneza magari-moshi ya dizeli kuliko magari-moshi ya mvuke, uwezo wao wa kutumika kwa njia nyingi ulimaanisha kwamba ni machache tu yangehitajiwa. Magari-moshi ya umeme yalikuwa bora kwa sababu yalikuwa na mwendo wa kasi na vilevile hayakuwa yakichafua mazingira. Hata hivyo, magari-moshi yakaendelea kutumiwa katika nchi nyingi sana.

Nchini Ufaransa, hata kabla ya Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, magari-moshi ya umeme yalitumiwa kwenye vitongoji vya miji, na baada ya vita yalitumiwa kwenda sehemu za mbali. Vilevile, nchini Japani, mabadiliko ya kuacha magari-moshi ya mvuke hadi magari-moshi ya dizeli hadi magari-moshi ya umeme ni kama yamekamilika. “Gharama ya mafuta inayozidi kuongezeka na wafanyakazi ndizo sababu kubwa,” lasema Steam Locomotives of Japan, likiongezea hivi: “Sababu nyingine kuu yaweza kuwa kwamba gari-moshi ni kitu cha kale na kisichopendeza watu wa kisasa. Abiria wa kawaida hafurahii kusafiri akiwa na moshi usoni pake; yeye anataka starehe na mwendo wa kasi.” Msemaji wa reli ya India akubali. “Hatuwezi kuendelea kutumia magari-moshi. Kila mtu anataka kusafiri haraka. Magari-moshi ni vitu vya kale. Nayo yanaharibu mazingira.”

Kwa sababu mwendo wa kasi na uwezo ni mambo muhimu ya kufanikiwa kwa reli ya kisasa, mameneja wamechunguza maendeleo mengine. Nchini Uingereza, magari-moshi ya kisasa ya umeme ya kubebea abiria yamepangwa kwa kufuata utaratibu wa kichwa upande mmoja na gadi upande mwingine na mabehewa katikati.

Kutumiwa kwa umeme katika reli hakujakosa matatizo. Reli za tatu zinazoandaa umeme na mifumo ya juu yenye kutumia umeme huhitaji vituo vidogo vingi vya kudumisha umeme. Mifumo ya kubadili mkondo wa umeme wenye nguvu nyingi sana na ambayo hutumia nyaya za juu imetengenezwa. Mifumo hiyo imeunganishwa na mota ndogo-ndogo za umeme zinazofanya reli isiwe na gharama nyingi. Sasa magari-moshi ya umeme yanayoenda mbali hutumia vituo vya umeme kwenye reli zao bila kukatizwa-katizwa.

Reli Yaimarishwa na Tramu

Eneo moja ambapo reli inarudi ni ukuzi wa tramu.a Mifumo mipya ya tramu inatokea katika miji inayoendelea kukua ulimwenguni pote. Katika Sydney, Australia, ambako inaripotiwa kuwa wakuu wa usafiri walikuwa wameamini kwamba walikosea kuondoa tramu za jiji hilo, hizo tramu zimerudi.

Tofauti na mambo yaliyotokea katika miji mingi ya Uingereza mapema katika karne hii, majiji mengi ya Ulaya yalidumisha reli za tramu ambazo zimedumu kwa miaka 100. ‘Katika Zurich, tramu ndiyo njia kuu ya usafiri,’ laripoti gazeti la habari The Independent. “Tramu inapokaribia taa za kuongoza magari, inachochea taa hizo ziangaze rangi ya kijani-kibichi na hivyo basi haingoji. . . . Tramu hutunza wakati daima.”

Ingawa mifumo ya reli za chini ya ardhi hufaa sana katika majiji yenye mamilioni ya wakazi, tramu hufanikiwa zaidi katika majiji yenye wakazi nusu-milioni au wachache, adai mwanamazingira mmoja wa Italia.

Tramu zaweza kukimbia kama tu magari mengine ya barabarani. Kwa kuwa tramu huwa na ekseli isiyo nzito kama magari-moshi na mabehewa ya kawaida, reli zao na madaraja yao si mazito sana. Mambo yanayoendelea ndani ya tramu yaweza kuonekana kupitia madirisha yake makubwa, jambo linaloongezea usalama wa abiria. “Kutokana na uwezo wake usio na kifani wa kutumika kwa njia nyingi kwa sababu ya muundo wake, tramu ya kisasa inaweza kwenda kwa mwendo wa gari-moshi na kupatikana kwa urahisi kama basi,” wasema uchunguzi wa uchukuzi wenye kichwa Tram to Supertram, wa Sheffield, Uingereza. Tramu ni “safi, ni bora na hazichafui mazingira.” Gazeti The Times lasema: “Tramu hufanya haraka kuliko magari ya kawaida wakati wa msongamano, na hazichafui mazingira.”

Je, Magari-Moshi Ni Kasi na Salama Zaidi?

Kuna aina nyingi sana za magari-moshi yenye kwenda kwa kasi sana—Train à Grande Vitesse (TGV), InterCity Express, Eurostar, Pendolino, na Shinkansen ya Japani (New Trunk Line). Wakitaka kutoa mwendo wa kasi zaidi na usalama zaidi, watengenezaji wa magari-moshi wametokeza njia mpya za kukabiliana na magari-moshi yenye kwenda kwa kasi. Reli zilizojengwa bila mipindo mikali kwenye reli zao ambazo zimechomelewa pamoja hufanya magari-moshi ya Ufaransa ya TGV yasafiri kwa mwendo uzidio kilometa 200 kwa saa.

Magari-moshi ya Eurostar sasa husafiri kati ya London na Paris na Brussels kupitia Handaki la Mlango-Bahari la Uingereza. Baada ya kuacha reli za zamani za Uingereza ambazo zinazuia mwendo wake wa kasi, Eurostar hupitia Ufaransa na Ubelgiji kwa mwendo wa kilometa 300 kwa saa. Muda wa kusafiri wa saa tatu kutoka London hadi Paris na wa saa mbili na dakika 40 kutoka London hadi Brussels umefanya reli ishindane sana na feri na ndege. Lakini imewezekanaje kwa gari-moshi kwenda kasi hivyo?

Ili kuhakikisha kuna mshiko mzuri wa reli, wahandisi nchini Japani walitengeneza gari-moshi jepesi lenye mabehewa ambayo hayawezi kupinduka kwa urahisi. Tofauti na njia ya kawaida ya kuwa na seti kadhaa za magurudumu chini ya kila behewa, magari-moshi ya Eurostar (yenye mabehewa 18 kati ya injini mbili) yana mabehewa mawili-mawili kwenye mfumo mmoja wa magurudumu. Jambo hilo hupunguza mtetemeko na uzito na kuruhusu gari-moshi liende kwa uanana na kwa kasi.

Njia za kutoa ishara za gari-moshi lenye kwenda kwa kasi ni tofauti sana na viashiria vya miaka iliyopita au hata taa za kando za reli ambazo zingali zinatumiwa sana katika reli nyingi za kawaida. Kompyuta zilizo kwenye gari-moshi huonyesha mambo ambayo dereva ahitaji kujua gari-moshi linapoenda kwa kasi. Njia tata za kuwasiliana huruhusu vituo vikuu vyenye kutoa ishara vidhibiti njia zote.

Wapangaji wa reli pia wamechunguza jinsi ya kuongeza mwendo wa magari-moshi yanayotumia reli za kawaida. Jambo moja ambalo wametokeza ni kuinamisha gari-moshi. Magari-moshi ya Pendolino, ambayo hupitia Italia na Uswisi, hutumia tekinolojia hii, kama ilivyo na X2000 ya Sweden. Hilo gari-moshi la Sweden husafiri kwenye mipindo kati ya Stockholm na Göteborg kwa mwendo wa kasi wa kilometa 200 kwa saa. Kwa sababu ya kutumia kwa werevu shokomzoba na mabogi yenye kujielekeza yenyewe, abiria hawahisi vibaya gari-moshi linapojipinda-pinda njiani.

Ripoti zinazopokewa za miendo ya kasi sana za magari-moshi na kuanguka kwa magari-moshi huzusha swali hili, Je, usalama unapuuzwa? Kufuatia aksidenti mbaya ya reli iliyoua watu nchini Uingereza mwaka wa 1997, Sunday Times liliripoti kwamba katika wakati ujao “reli zitawekewa vidhibiti ambavyo vingeweza kutambua hali za dharura haraka zaidi.” Mfumo mpya wa Transmission Based Signalling utawasilisha jumbe za redio moja kwa moja hadi mahali pa dereva kutoka kwenye kituo cha usimamizi. Kwa kuongezea, tekinolojia ya kushika breki iitwayo Automatic Train Protection itatumiwa kwa kawaida katika magari-moshi ya Uingereza, kama ilivyo katika nchi nyingi za Ulaya na kwingineko. Dereva akishindwa kuitikia ishara zenye kuonya kando ya reli, gari-moshi lenyewe lajishikia breki na kusimama salama salimini.

Wakati Ujao wa Kutumia Sumaku?

Kwa abiria ambaye amezoea kelele za usafiri wa reli wa kawaida kwenye reli nzito au kwenye reli za chini ya ardhi, inafurahisha sana kusafiri kwa ukimya na kwa utulivu. Mabehewa ya magari-moshi yenye magurudumu ya mpira katika reli fulani za Reli ya Chini ya Ardhi ya Paris huwatuliza wakazi wa jijini. Lakini njia hiyo haifikii hata kidogo uvumbuzi mpya wa reli.

Reli za chuma cha pua ambazo magari-moshi ya kawaida hutumia hupunguza mwendo wake. Ili kwenda kwa kasi sana, wahandisi sasa wanatokeza magari-moshi yenye kuinuliwa na sumaku (maglevs), ambayo huelea juu ya metali yenye kuyaongoza. Kwa kuwa hayagusi reli, magari-moshi hayo hutumia sumaku-umeme zenye nguvu sana ambazo huyainua juu ya reli na kuyafikisha kwenye mwendo wa kilometa 500 kwa saa. Gazeti The Times la London liliripoti kwamba, mnamo Desemba 13, 1997, maglev ya Japani iliweka rekodi mpya ya ulimwengu ya mwendo wa kasi zaidi wa kilometa 531 kwa saa katika majaribio yenye kuendeshwa na watu na yasiyoendeshwa na watu.

Kwa kuona mambo kupitia wapenzi wa magari-moshi na wengine ambao hutetea magari-moshi ya dizeli na yenye kutumia umeme, wakati ujao wa reli u salama. Hatujui jinsi magari-moshi na reli zake zitakavyokuwa ama kama zitabadilika kabisa. Angalau kwa sasa, reli itadumu.

[Maelezo ya Chini]

a Hizo zinaweza kukimbia kwenye reli na vilevile barabarani.

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

Mabehewa Yenye Fahari

Jumba la Makumbusho la Reli la Uingereza lililo katika jiji la York lina mabehewa mengi ya zamani yaliyotumiwa na watu wa kifalme. Kati ya 1842 na 1977, magari-moshi ya kifalme 28 yalitumiwa nchini Uingereza. Wakati wa utawala wa Malkia Victoria (1837-1901), angalau magari-moshi 21 yalitengenezwa ayatumie. Baada ya kumaliza safari yake ya kwanza kwa gari-moshi, alitangaza kwamba ‘alifurahia sana’ safari hiyo.

Mwana wa Victoria Mfalme Edward wa saba aliamua kutotumia magari-moshi ya mamake. Badala yake alitumia magari-moshi mapya matatu. Baadaye, Mfalme George wa tano na Malkia Mary waliyarekebisha yawe ya kisasa na kuweka vyoo ndani kwa mara ya kwanza.

[Sanduku katika ukurasa wa 24]

Usalama Ni Jambo la Kwanza

Ili kukabiliana na uhalifu, reli zinazidisha usalama na matumizi ya kamera na vifuli. Lakini unaweza kufanya nini ili usafiri kwa usalama zaidi katika gari-moshi? Hapa pana madokezo machache:

• Usionyeshe-onyeshe vitu vyenye thamani.

• Ukiwa ndani ya chumba, funga mlango kwa ufunguo na kufunga vizuri dirisha.

• Weka vitu vyenye thamani kwenye sehemu mbalimbali za mizigo yako na nguo zako.

• Usipigane ukitishwa.

• Fikiria kubeba kibeti kingine chenye kupotosha chenye fedha chache.

• Beba fotokopi za hati zako.

[Hisani]

The Daily Telegraph, Machi 22, 1997.

[Picha katika ukurasa wa 22, 23]

1. “Lake Shore Flyer,” 1886, Marekani

2. Schweizer Centralbahn, 1893

3. Class B1, 1942, Uingereza

4. Bödelibahn “Zephir,” 1874

[Hisani]

Early American Locomotives/Dover Publications, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 25]

1. Shinkansen, Model 500, Japani;

2. Eurostar, Ufaransa;

3. Train à Grande Vitesse (TGV), Ufaransa;

4. Gari-moshi la THALYS PBA, Ufaransa

[Hisani]

Copyright: Eurostar/SNCF-CAV/Michel URTADO

Copyright: Thalys/SNCF-CAV/Jean-Jacques D’ANGELO

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki