Uwongo wa Kawaida Kuhusu Nyoka
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA INDIA
Fira mwenye mwili unaoteleza-teleza alitambaa kumwelekea msichana mmoja, akivutiwa na marashi ya maua ya asmini ambayo yalikuwa kwenye nywele zake. Mwili mrefu wa nyoka huyo ukasonga ukiinuka na kushuka kama mawimbi ya bahari. Msichana huyo akaona mmweko katika kipaji cha fira uliofanana na kito chenye kung’aa huku nyoka huyo akimpumbaza akili kwa macho yake. Kwa ghafula fira akajirusha kwenye msichana huyo na kuuma mkono wake.
NI KWELI au uwongo? Ufafanuzi huo wote si wa kweli, ukitegemea dhana isiyo ya kweli ambayo wengi wameshikilia. Ebu ona baadhi ya uwongo huo.
1. Asmini, sandali, na marashi mengine huvutia nyoka. SI KWELI. Manukato huvutia wadudu, wadudu huvutia vyura, na vyura ambao huliwa na nyoka, huvutia nyoka.
2. Nyoka husonga kwa kuinua-inua miili yao wima. SI KWELI. Jambo hilo hudhaniwa mtu akiona nyoka akisonga juu ya mawe makubwa. Mwendo wa kawaida wa fira na nyoka wengine ambao hutambaa kwenye ardhi ni wa mlalo, kwa mwendo ulionyooka. Ama nyoka huvuta sehemu ya mbele ya mwili wao na kuvuta sehemu ya nyuma, ama kwa msaada wa vitu vilivyoko kwenye ardhi, wao huenda upande-upande kisha mbele, wakifanyiza herufi S.
3. Nyoka fulani wana kito chenye thamani kichwani. SI KWELI. Ni ngano, pamoja na itikadi ya kwamba mashujaa katika India ya kale walilindwa na fira.
4. Fira hupumbaza mawindo yake. SI KWELI. Kwa kawaida nyoka hutazama bila kugeuza macho anapokuwa mwoga, basi wanapokutana na nyoka watu hudhani kwamba ule mtazamo usiogeuka unakuwa wa kupumbaza. Hata hivyo, hiyo si njia wanayotumia kushika windo.
5. Fira hujirusha kwenye windo lake. SI KWELI. Fira hurusha sehemu ya mbele ya mwili wake ili kushambulia windo lake, lakini sehemu kubwa ya mwili wake hubaki kwenye ardhi ili kuutegemeza mwili wake. Sanasana, ni thuluthi tu ya mwili wake ambayo huweza kuinuliwa ili kushambulia.
6. Ngozi ya nyoka, kutia ndani fira, daima huteleza-teleza na ni baridi. SI KWELI. Ngozi ya nyoka, ikiwa na magamba yanayolaliana, ni kavu na ni kama ngozi laini. Nyoka ni viumbe wenye damu inayobadilikana na hali; halijoto za mwili wao hubadilika kulingana na halijoto ya nje.
7. Fira ni viziwi. SI KWELI. Dhana isiyo ya kweli ambayo wengi huamini. Watu hawa hufikiri kwamba nyoka husikia tu kutokana na mitikisiko ardhini ambayo mwili wake huhisi. Kwenye Zaburi 58:4, 5, Biblia yadokeza kwa kweli kwamba fira si viziwi. Utafiti wa karibuni umeonyesha kwamba fira wanaweza kusikia sauti zinazopitia hewani na kwamba wao waweza kuvutiwa na muziki wa watu ambao hucheza na nyoka.—Ona pia Amkeni! la Julai 22, 1993, ukurasa wa 31.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
Nyoka aliye juu: Animals/Jim Harter/Dover Publications, Inc.