Je, Ungependa Kukutana na Fira?
Na mleta-habari wa Amkeni! katika India
NAAM, wewe ungependa? Watu wengi walio wazima huenda wakajibu la. Lakini sivyo ilivyo kwa mtoto. Kuogopa nyoka, kutia ndani fira, si tabia ya kiasili katika watoto wachanga au hata katika wanyama. Kuwachukia nyoka kwaweza kusababishwa na habari isiyotegemeka, hadithi zilizotiwa chumvi, ngano, na maoni yasiyofaa.
Bila shaka, tunapokualika ukutane na fira, twamaanisha ukiwa umbali ulio salama! Fira wana sumu kali sana, nasi hatungetaka kumwendea mmoja na kumnyoshea mkono wetu ili kumpapasa. Wala fira haelekei kukaakaa karibu ili akutane nasi; atusikiapo tukikaribia, ataondoka mara moja na kukimbilia mahali salama pa kujificha. Basi acheni turidhike na kukutana na fira kwa kujifunza habari mbalimbali za kweli zenye kuvutia juu ya kiumbe huyu mwenye kupendeza.
Fira ni wamyama-watambazi wa daraja la chini la Serpentes na familia ya Elapidae, jina wanalopewa nyoka wenye sumu kali na wenye meno yaliyopindika. Kuna karibu aina 12 za fira waliotapakaa toka Australia kupitia tropiki za Asia na Afrika hadi Arabia na sehemu za dunia zisizo na joto wala baridi kali. Fira anayeogopwa sana ni yule mfalme fira, au hamadryad. Akiwa na urefu wa meta tatu hadi tano, yeye ndiye nyoka mwenye sumu aliye mkubwa zaidi ulimwenguni. Kwa kuwa anapenda kukaa mahali penye mimea mingi na iliyosongamana au kwenye majimaji, ambako kuna mvua nyingi, yeye aweza kupatikana kusini mwa China, Filipino, Indonesia, Malasia, Myanmar, na sehemu za India. Mkia mweusi sana, mwili wenye mistari yenye rangi kijani-kibichi-manjano, inayogeuka na kuwa rangi nzito ya kijani kibichi kadiri anavyozeeka, na vidoadoa kwenye sehemu ya juu ya kichwa chake humfanya kuwa mwenye kupendeza sana.
Aina nyingine za fira zina wastani wa meta moja hadi mbili kwa urefu. Mwenye asili katika India na aliyesambaa sana huko, ni fira-miwani ambaye ana alama za pekee kwenye kichwa chake, zinazofanana na miwani. Aweza kuwa mweusi, mwenye rangi nzito ya kahawia, au nyeupe-manjano akiwa na mstari mweusi mkubwa shingoni na mistari myeupe na ya rangi ya manjano yenye madoadoa kwenye urefu wa mwili wake. Fira-rodi, apatikanaye Sri Lanka na pia sehemu za mashariki na kaskazini-mashariki mwa India, ni mwenye rangi nyepesi zaidi na mwenye kichwa kidogo, kilicho mviringo zaidi na chenye mviringo mmoja mweupe, unaompa jina lake. Kaskazini-magharibi mwa India na Pakistan, twamkuta fira aliye mweusi sana. Miongoni mwa fira walio Afrika mna, swila, au koboko-mate, na koboko-mkubwa wa Misri. Huyu wa pili, nyoka mweusi na mwenye kichwa kidogo, huenda ndiye nyoka mdogo anayefikiriwa kuwa alisababisha kifo cha Malkia Cleopatra.
Nyoka hujamiiana na nyoka wa aina zao tu, wakivutiwa na harufu ya kipekee ya meski. Fira huonyesha kupendezwa na familia kuliko nyoka wengine, wa kiume na kike mara nyingi hubaki pamoja. Mfalme-fira wa kike ni kati ya nyoka wachache sana wajulikanao kuwa hutengeneza kiota. Yeye hukusanya majani na kuyaweka kwenye shimo la karibu sentimeta 30 na kutaga mayai 20 hadi 50 ndani yalo. Kisha anaupinda mwili wake kulizunguka shimo na kubaki hapo, bila chakula, kwa karibu miezi miwili ya kuatamia, yule wa kiume mara nyingi huwa karibu pia. Fira wengine, bila kutayarisha kiota, hubaki karibu na mayai yao ili kuyalinda.
Watoto wa nyoka hutumia sehemu ya pua, ambayo hukatika baadaye, ili kufungua gamba la yai na kutoka nje. Watokapo nje wao hujitegemea kabisa wakiwa na tezi za sumu na meno yaliyokua vya kutosha. Wao hutoatoa ndimi zao nje mara nyingi, huonja mazingira, na kupeleka habari za kikemikali hadi kwenye kile kiitwacho kiungo cha kunusia kilicho katika kaakaa la mdomo. Kiungo hiki kimeunganishwa na hisi ya kunusa; muungano wa ladha na harufu humwezesha kufuatia windo lake, kupata mwenzi, au kuwatoroka washambulizi.
Nyoka mchanga hukua upesi sana na baada ya muda mfupi hutoa ngozi yake ya nje, ambayo imekuwa yenye kubana sana. Jambo hili la ajabu hurudiwa kwa ukawaida, kwa kuwa fira huendelea kukua kwa muda wote wa maisha yake, ambao waweza kuwa zaidi ya miaka 20. Kwa juma moja au mawili kabla ya kutoa ngozi, huyo nyoka hulala sana, ngozi yake huanza kupoteza rangi, na macho yake kugeuka kuwa samawati-kimaziwa. Kisha, mara moja macho yang’aa, na kwa kusugua kichwa chake kwenye mawe, huyo nyoka hupasua ngozi yake kuanzia kifuniko changavu kwenye mdomo wake. Sasa kihalisi yeye hutambaa na kutoka ndani ya ngozi yake kwa kuwa hiyo hubambuka toka upande wa ndani kuelekea nje, kuanzia kwenye macho yake na kuendelea hadi kwenye mkia. Akiwa sasa nyoka mwenye nguvu, mwangavu, na mwenye sura mpya yu tayari kuendelea na shughuli zake za kawaida.
Halijoto ya hewa huathiri sana fira. Halihewa inapozidi kuwa baridi, wao hupunguza utendaji wao na hata kuwa bwete, wakianza kutenda tu wakati halijoto inapopanda. Joto jingi sana laweza kuwaua. Isipokuwa kwa mfalme fira alaye nyoka wengine, chakula chao ni panya, buku, vyura, mijusi, ndege, na wanyama wengine wadogo. Windo linaposhikwa, kulidunga kwa sumu hulifanya lisiweze kutembea. Humezwa likiwa zima, kwa kuwa fira hawezi kutafuna chakula. Unyumbufu wa ngozi na kubadilikana kwa kinywa humwezesha fira kummeza mnyama aliye mkubwa mara mbili au tatu kuliko kichwa chake mwenyewe. Kwa kuwa kinywa huzuiwa kabisa na lile windo, huyo nyoka hupumua kwa kusongeza koromeo mbele ya palipo kizuizi, kama vile mwogeleaji hutumia kipumulio. Sasa safu ya meno yaliyopindika kuelekea nyuma hulisongeza windo ndani kuingia mwilini mwa huyo nyoka. Hulala mahali patulivu ili ameng’enye chakula polepole, labda bila kula tena kwa siku kadhaa. Fira waweza kuishi kwa miezi bila kula, wakitumia mafuta yaliyohifadhiwa mwilini.
Nyoka ni wenye hadhari. (Ona Mathayo 10:16, New World Translation.) Ulinzi wa fira hutokana ama na kutoroka kwake, labda kutambaa na kuingia chini ya mwamba au katika nyumba yake iliyokuwa shimo la panya, au kwa kutulia tuli, hivyo akiepuka kutambuliwa. Akishambuliwa, atasimamisha na kuvimbisha shingo yake, akitoa sauti ili kumwogopesha adui. Kuuma ni njia ya mwisho anayotumia.
Kuumwa na Nyoka
Kuumwa na nyoka katika sehemu za mashambani za Afrika na Asia mara nyingi hakuripotiwi, lakini kuuzunguka ulimwengu yaonekana kwamba watu karibu milioni moja huumwa kila mwaka na nyoka wenye sumu. India ina rekodi kubwa ya vifo—karibu 10,000 kila mwaka—huenda vingi vyavyo vikiwa ni kutokana na fira-miwani. Karibu asilimia 10 ya maumo ya fira ni yenye kufisha.
Fira ni mpole kuliko nyoka wengine; nguchiro mwepesi, mmoja wa maadui wake wakuu, aweza kumshinda. Kwa kumrukia nyoka, na kuhepa shambulio kwa kuendelea, nguchiro humfanya fira kuwa bila nguvu na mwenye kusitasita. Akimshambulia nyuma ya kichwa chake, yeye huvunja shingo yake. Nyoka wengi hushambulia wakiwa wamejipinda, ikifanya iwe vigumu kujua anapoweza kufika, lakini fira huinua mwili wake na kushambulia kuelekea chini. Umbali waweza kukadiriwa, naye mtu aweza kuondoka katika eneo awezalo kushambulia kwa ule mwendo wake ambao ni wa pole kwa kulinganishwa.
Fira wengine, kama vile swila, fira mwenye shingo nyeusi wa Afrika Kusini, na fira katika kaskazini-mashariki mwa India, hujilinda kwa kutema mate. Akiinua na kuelekeza meno yake kwa windo, huyo nyoka, pamoja na hewa inayotoka, aweza kutema minyunyizo miwili midogo ya sumu kwa zaidi ya meta mbili. Kwenye ngozi haina madhara yoyote, lakini ikiingia kwenye macho, yaweza kusababisha upofu wa muda na, isipooshwa upesi, upofu wa kudumu. Ajabu ni kwamba, huyo nyoka huonekana kuwa aweza kulenga macho.
Tuseme fira akuuma, wapaswa kufanyaje? Sumu husukumwa kutoka kwenye vifuko vyayo katika midomo ya nyoka kupitia meno mawili mafupi, yenye mashimo yaliyoko kwenye sehemu ya mbele ya kinywa cha nyoka. Meno hayo hutoboa ngozi na kuingiza sumu kama vile sindano inayodungwa chini ya ngozi ingefanya. Dawa pekee yenye uhakika ya kuumwa na nyoka ni antivenin inayotengenezwa kutokana na sumu ya nyoka wanne wenye sumu. Mapema katika karne ya 20, India ilikuwa nchi ya kwanza kutumia antivenin kwa wingi. Unga wa antivenin waweza kutumika kwa miaka mitano bila kuwekwa kwenye friji; unapochanganywa na maji huingizwa mwilini kwa kutumia sindano.
Dalili za kuumwa na fira ni maumivu na kufura mahali pa kuumwa, kutoona vizuri, kukosa kuwa imara, kupooza kwa zoloto, na kupumua kunakopungua. Kifo hutokea baada ya karibu saa mbili ikiwa kiasi kikubwa cha sumu kiliingia na matibabu yasipotolewa.
Mtumbuiza-Nyoka
Kutumbuiza watu kwa kutumia nyoka kulianza zamani sana. Hilo likifanywa sanasana katika Mashariki, baadhi ya wanasarakasi wa Magharibi wamelitia katika orodha yao ya michezo. Kwa sababu ya kichwa chake kisicho cha kawaida na hali yake ya kuchokozeka upesi, fira-miwani ndiye hutumiwa mara nyingi, hata hivyo nyoka wengine wenye kupendeza, kama vile nyoka wa kifalme na yule sundakuwili mwekundu, hutumiwa pia. Naye mtumbuizi, mwenye ustadi, achezapo paipu zake, fira hutoka kikapuni mwake na kuvimbisha shingo yake kama afanyavyo anapojilinda. Mwendo wa mtumbuizi hutokeza mwitikio kutoka kwa nyoka amwangaliapo, akiwa tayari kushambulia. Meno ya fira walio wengi wanaotumiwa na watumbuiza-nyoka yameondolewa, lakini watu wengine hujihatarisha kwa kucheza na nyoka wenye sumu.
Katika India ya kale mtumbuiza-nyoka aliyekuwa akizuru sehemu mbalimbali alikuwa pia msimuliaji wa maoni ya kidini na ngano, ambayo yalimfanya awe maarufu. Leo kuna faida zaidi za kifedha kufanya mchezo nje ya mahoteli yaliyo na watalii wengi wapiga-picha. Baadhi ya watumbuiza-nyoka hutembelea watu nyumbani na kumwambia mwenye nyumba kuwa bustani yake kubwa yaelekea ina nyoka wengi. Kwa kukubaliana kiasi fulani cha fedha, yeye hujitolea kuwashika. Hupotelea vichakani, na baada ya muda, wakati ambapo paipu zake zaweza kusikiwa, arudi akiwa na mfuko uliojaa nyoka. Bila shaka, mwenye nyumba angalikuwa mwenye hekima na kumwangalia afanyapo hilo au angalau kuchunguza ikiwa alileta mfuko uliojaa nyoka!
Mbuga za Nyoka Huelimisha
Mbuga za nyoka huchochea upendezi katika wanyama-wambazi. Hulipia utafiti unaofanywa, hufundisha juu ya kuzuia kuumwa na nyoka na jinsi ya kuponya, na huwalinda nyoka kutokana na pupa na ujinga wa mwanadamu. Fira wameuawa kwa ajili ya ngozi yao iliyo maridadi, inayotumiwa kutengeneza mishipi, vibeti, viatu, na vitu vingine vya anasa. Katika mwaka mmoja nyoka milioni kumi waliuawa katika India kwa faida ya viwanda vya ngozi. Nyoka huuawa kisha kutolewa ngozi mara moja. Rangi za majani hutumiwa katika India ili kuipa ngozi rangi nzuri, nayo hung’arishwa kama kioo na nyakati nyingine hunyunyiziwa rangi ili kuifanya ing’ae na kuzuia maji.
Thamani ya fira haiwezi kukadiriwa kupita kiasi. Yeye huokoa tani nyingi za nafaka kwa kuwaua panya na wanyama wengine waharibifu. Sumu yake hutumiwa kutengeneza antivenins, madawa ya maumivu, na madawa mengineyo. Tata Memorial Cancer Institute katika Bombay inachunguza matokeo ya sumu ya fira kwenye chembe za kansa.
Je, umefurahia kukutana na fira? Mwenye kupendeza, mwenye mafaa, mwenye hadhari, mwenye vifaa vya kujihami mwenyewe. Kumjua vyema zaidi kwaweza kutusaidia kuthamini mshiriki huyo wa dola ya wanyama asemwaye vibaya.
[Sanduku katika ukurasa wa19]
Ibada ya Fira na Ushirikina
IBADA ya fira imekuwako tangu nyakati za kale. Sanamu ya mfano wa fira imepatikana kwenye sili katika Mohenjo-Daro, mojapo staarabu za kale sana ambazo zimepata kufukuliwa na waakiolojia. Toka mileani ya tatu K.W.K. kufikia sasa, mamilioni katika India wamewapa fira staha ya kishirikina. Kwa kupendeza, nyingi kati ya hadithi za fira zaweza kutambuliwa kuwa ngano zilizopotoshwa zenye msingi wa matukio halisi ya kihistoria.
“Hadithi” ya uumbaji hueleza juu ya wakati ambapo hakukuwa na nuru katika ulimwengu wote mzima. Kutokana na maji meusi ya ulimwengu wote mzima mungu Vishnu aliumbwa kwanza, kisha mbingu, dunia, na ulimwengu wa chini. Kutokana na mabaki ya uumbaji, fira mkubwa sana aitwaye Shesha (ikimaanisha sehemu iliyobaki) aliumbwa. Ngano husema kwamba fira alikuwa na kati ya vichwa 5 hadi 1,000, nazo picha huonyesha Vishnu akiwa amemkalia Shesha aliyejipinda, akiwa chini ya himaya ya shela iliyo wazi ya vichwa vingi vya Shesha. Matetemeko ya dunia yasemwa kuwa ni tokeo la Shesha kupiga miayo, nao moto kutoka kinywani mwake au sumu yake huuharibu ulimwengu mwishoni mwa enzi fulani.
Ngano za Kihindi husema juu ya jamii ya fira inayoitwa Nagas, ambao wanaishi katika ulimwengu wa chini, Nagalok au Patala. Sokwe-mungu Hanuman hudai kwamba katika “Enzi Kamilifu,” watu wote walikuwa watakatifu, kulikuwa na dini moja tu, na hakukuwa na roho waovu wala Nagas. Nyoka wakawa walinzi wa utajiri wa dunia nao wakapata ujuzi mwingi na nguvu za kufanya mambo ya ajabu. Shesha, ambaye huitwa Vasuki nyakati nyingine, alitumiwa na miungu kusukasuka bahari ya maziwa ili kutokeza amrit, umajimaji mtamu ambao ungempa mtu kutokufa. Ulimwengu wa chini, uliokuwa ukitawalwa na Nagas, waonyeshwa kuwa mahali penye kutamanika zaidi; askari wanaokufa vitani wanaahidiwa raha isiyowazika huko.
Hata hivyo, si fira wote wa kingano wanaoonwa kuwa wenye fadhili. “Hadithi” moja hueleza juu ya kabiliano kati ya Krishna, aliyegeuka kutoka kwa Vishnu na Kaliya, fira-daimoni mkubwa, mwenye kufisha. Picha huonyesha Krishna mshindi akiwekelea mguu wake juu ya huyo nyoka mkubwa.
Manasa, au Durgamma, malkia wa Nagas, huabudiwa na wanawake ili awalinde wana wao kutokana na kuumwa na nyoka. Katika msherehekeo wa Nagapanchami, wanaoabudu nyoka humwaga maziwa na hata damu juu ya mifano ya fira na ndani ya mashimo ya nyoka. Mifano ya fira ya mawe au fedha huabudiwa na kupewa kuwa toleo katika mahekalu na wanawake wakitarajia kupata watoto wa kiume.
Fira Katika Filamu
Fira wa kingano ni kichwa chenye kupendwa sana na wengi katika filamu zilizotengenezwa katika India—zaidi ya 40 zikiwa zimetengenezwa tangu 1928. Kwa kawaida fira anaonyeshwa akiwa kama mtunzaji wa mungu-mke, msaidizi wa waabudu wake, na mwangamizaji wa waovu. Ipendwayo sana na wengi ni ile ngano juu ya fira Icchadari, ambao wanasemekana wana uwezo wa kutwaa umbo la kibinadamu. Wanasemekana kuwa wana mwenzi mwenye ujitoaji. Mwenzi huyo akiuawa, fira huyo anaweza kuona picha ya muuaji katika macho ya nyoka aliyekufa, naye hutafuta kulipiza kisasi. Huu huwa msingi wenye kuchangamsha wa filamu nyingi. Sehemu kubwa ya hadithi hizo ni dansi za nyoka; kwa kuandamana na muziki sawa na ule wa watu wenye kutumbuiza nyoka, wacheza-dansi huiga mwendo wa nyoka, hata wakitambaa kama nyoka kwenye ardhi.
Sinema ya mambo hakika, Shakti, ilifanyizwa kwenye msherehekeo katika Rajasthan, India, ambako kila Agosti mamia ya maelfu ya waabudu-nyoka hukutana jangwani. Chini ya jua kali, na kwenye halijoto zifikiazo digrii 50 Sentigredi, wao hujitandika kwa fito za chuma na kutambaa kwa matumbo yao kwa zaidi ya kilometa mbili juu ya mchanga wenye kuchoma hadi hekaluni kwa mungu-nyoka, Gogha. Mfalme fulani wa kihistoria katika karne ya kumi W.K., Gogha asemekana kuwa aliwaokoa watu wake kutokana na washambulizi Waislamu kwa kumwongoza adui kwenye eneo lenye nyoka wengi, ambako wengi katika jeshi hilo walikufa kutokana na kuumwa na nyoka.
[Sanduku katika ukurasa wa20]
Waokolewa na Fira
Familia mbili katika kijiji cha Sastur katika India zina sababu ya kuwa na shukrani kwa fira mmoja. Ziliamshwa karibu saa 9:50 usiku katika Septemba 30, 1993, kwa sauti kubwa ya fira aliyekuwa akitoka nyumbani mwao. Zilimfukuza hadi kwenye nyanda ili kumwua. Saa 10.00 za usiku, lile tetemeko la dunia lenye kuhofisha sana katika India ya kati lilibomoa kijiji chao na kuua karibu kila mtu. Hizo familia mbili ziliokoka—yote hayo kwa sababu ya mfumo wa uonyaji-mapema wa huyo fira!
[Picha katika kurasa za 16, 17]
Mwono wa nyuma na wa mbele wa fira wa Asia
Picha ndogo: Fira mweusi apanua kichwa chake anapoota jua kwenye mwamba wenye joto
[Hisani]
Picha zilizo kwenye kurasa 16 hadi 20: A. N. Jagannatha Rao, Trustee, Madras Snake Park Trust
[Picha katika ukurasa wa 18]
Mwono wa mbele na nyuma wa fira mweusi