Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 11/8 kur. 23-25
  • Kuchunguza Umaridadi wa Miaka Mingi wa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuchunguza Umaridadi wa Miaka Mingi wa
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uvutio wa Miaka Mingi wa Mbao Thabiti
  • Kurudia Tezo
  • Mwandamani Wake—Drawknife
  • Mbao za Zamani—Zatumiwa Upya
  • Madokezo Kuhusu Mbinu
  • Usanii Unaoridhisha
  • Kwa Nini Kujenga kwa Mbao?
    Amkeni!—1995
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1999
  • “Seremala”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2010
  • Je, Wajua?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 11/8 kur. 23-25

Kuchunguza Umaridadi wa Miaka Mingi wa

Mbao

Na mleta-habari wa “Amkeni!” katika New Zealand

MBAO, hasa za namna nyingi za kiasili zinazidi kuwa nadra sana kupatikana. Katika sehemu nyingi za ulimwengu, misitu inaangamizwa kwa kiwango chenye kuogofya. Ukosefu wa mbao hutokeza bei ghali za mbao, mojawapo ya bidhaa za msingi na ambayo ilipatikana kwa wingi ulimwenguni.

Inashangaza kwamba hapa New Zealand, kuna mashamba ya misonobari aina ya radiata, yaliyoanzishwa katika miaka ya 1930, na bado misitu ya asili, kama vile rimu, kauri, beech, na kahikatea, inadidimia.

Uvutio wa Miaka Mingi wa Mbao Thabiti

Kwa maelfu mengi ya miaka, mwanadamu amefurahia kuchonga mbao kuwa vyombo vyenye faida. Mara nyingi watu wamevutiwa na rangi yenyewe, nyuzi zilizo tofauti, na hata harufu inayotolewa na miti ya aina nyingi. Vyombo vyenye matumizi mbalimbali vimewaridhisha watu kwa miaka mingi, na katika visa fulani, kwa karne nyingi.

Tangu nyakati za kale, fanicha za mbao thabiti zimetumiwa katika nyumba. Kwa kutumia zana sahili, wanaume kwa wanawake wamedhihirisha vipawa na ustadi wa kuunda vitu vya msingi kama vile meza, bakuli, vibago, mapipa, masanduku, na viti.

Tekinolojia ya kisasa imeongeza mwendo wa kuunda vitu hivi leo. Vifaa vinavyotumia umeme kama vile misumeno, keekee, randa, na vifaa vya kupigia msasa, vyaweza, ingawa kwa kelele ya kadiri fulani, kuunda vizuri fanicha thabiti kutoka kwa mbao ghafi. Nchi nyingi zaweza kujivunia viwanda vya mbao vinavyotumia mashine kutokeza fanicha nyingi kwa bei nafuu.

Lakini mara nyingi fanicha hizo hukosa kudumu kwa sababu ama (1) vibadala (ubao-vene, ubao wa vibanzi) hutumiwa badala ya mbao thabiti ama (2) mbinu za kuunganisha mbao hutegemea ujenzi wa haraka, kwa kutumia mashine za kubana au misumari.

Kurudia Tezo

Katika majaribio ya kushinda unaoonekana kuwa udhaifu wa tekinolojia ya kisasa, wengine wanatafuta kutumia chombo cha kale cha useremala—tezo. Kinafafanuliwa kuwa “chombo cha kukata chenye makali membamba wenye tao uliowekwa kwenye pembe mraba kwenye mpini na hutumiwa hasa kwa kuchongea mbao.” Katika New Zealand, kabila la Wamaori walitumia tezo zilizotengenezwa kwa kito chenye rangi ya kijani kibichi ili kuchonga mitumbwi na kuunda fito ili zichongwe. Hata hivyo, tezo nyingi leo zimetengenezwa kwa chuma.

Katika karne zilizopita, maseremala walitumia tezo kusawazisha na kulainisha fremu ya nyumba na katika kujenga merikebu. Walipanga mbao pana zilizoshikiliwa kwa miguu yao, na kutumia makali yaliyopinda ya tezo kuchonga mashimo yaliyobonyea ndani ya mbao.

Mwandamani Wake—Drawknife

Kuongezea uvutio wa kitu kinachoundwa na kinachotumika kama mwandamani wa tezo ni chombo kingine cha lazima, drawknife. Hiki hutumiwa kurembesha kingo au sehemu za juu za mbao. Ni lazima tezo na drawknife zinolewe kama wembe nyakati zote.

Baada ya kupata vifaa hivi, hatua zinazofuata ni kutafuta mali ghafi zinazofaa kisha, kutengeneza fanicha unayotaka. Hapa ndipo kulingana na maseremala, mtindo wa zamani wa kishamba wa kuunda fanicha una faida nyingi kuliko mbinu za kawaida za utengenezaji.

Mbao ghafi zilizokatwa kwa msumeno, mradi zimekauka na hazijapinda, zaweza kutengeneza fanicha iliyo imara na maridadi. Mbao za namna hiyo zaweza kupatikana kwa njia nyingi: fanicha zilizotupwa (kabati za nguo, mbao za sehemu za kichwa za kitanda, sehemu za juu za meza), masanduku mazee, mihimili kutoka majengo yaliyobomolewa, na vigingi vizee vya ua.

Mbao za Zamani—Zatumiwa Upya

Mbao zilizozeeka ambazo hazijaliwa na wadudu au kuoza zaweza kung’aa na ziwe nzuri zinapofanyiwa kazi na mtaalamu.

Mawaa, mashimo ya msumari, na mabonde yaweza kutokeza sehemu zisizo za kawaida katika mbao iliyotumiwa kwa fanicha. Kikiachwa katika umbo lake la asili au kikitiwa rangi na kung’arishwa, kitu chako ulichotengeneza kwa mbao kitakuletea uradhi na raha kikiwa kitu ambacho kimetengenezwa vizuri na chenye kudumu.

Kama mtunza bustani alimaye ardhi, mfinyanzi anayekanda udongo, na mfumaji anayesokota kitani, seremala anayeunda na kurembesha kipande cha mbao akitumia tezo au drawknife hulipata kuwa jambo linaloridhisha zaidi. Ndiyo, ni kazi ngumu. Ndiyo, itachukua muda mrefu kuliko njia za kisasa. Hata hivyo, kutambua kwamba kazi yako itakuwa chanzo cha kukuridhisha na kwamba fanicha yako iliyoundwa kwa ustadi italeta miaka yenye faida kwa watumizi wake huchangia shangwe inayoletwa na useremala.

Madokezo Kuhusu Mbinu

Tezo haifai kutumiwa kwa mbao zote. Kwa kawaida nyuzinyuzi zinazopatikana katika mbao ngumu za kitropiki hukinza tezo. Kwa kawaida, mbao nyororo, au hata—yenye nyuzinyuzi itachongeka vizuri zaidi kwa kutumia tezo. Si lazima mafundo yasumbue. Kwa kutumia patasi iliyopindika, unaweza kuyachonga au kuyafukua, hivyo ukibuni sura ya kipekee kwenye uso wa mbao unayoifanyia kazi.

Baadhi ya rangi bora kabisa mara nyingi hupatikana katika mbao zilizokatwa kutoka sehemu ya katikati kabisa ya mti. Fanicha zilizotengenezwa kutokana na mbao hizi hutiwa rangi kwa nadra sana. Hata hivyo, ikiwa unataka kuirembesha kabisa mbao isiyokuwa na rangi, kuna rangi za aina mbalimbali zitakazofaa upendezi wako.

Hata hatua hii haipaswi kuwa ghali. Watu fulani wamesugua grisi ya gari kwenye mbao isiyo na rangi nzito wakapata kwamba inaongezea uzuri kifaa kilichoundwa kwa njia ya kustaajabisha.

Kwa kumalizia kifaa chako ulichobuni, kuna polyurethane au vanishi ziwezazo kunyunyiziwa au kupakwa kwenye fanicha. Kwa umalizio mzuri wa asili zaidi ambao unakuza mbao badala ya kuiziba, unaweza kupaka mbao mafuta ya kung’arishia yaliyotengenezwa kwa vitu vifuatavyo: sehemu tano za siki, sehemu nne za terafini, sehemu mbili za mafuta ghafi ya kitani, na sehemu moja ya methylated spirit. Yeyusha nta ndani ya mchanganyiko wako, na kuruhusu mchanganyiko huo upenye ndani ya mbao kwa siku kadhaa.

Usanii Unaoridhisha

Fanicha ya mbao iliyo thabiti ambayo imetengenezwa kwa ustadi kwa mikono yako, itakuvutia sikuzote ikaapo kwenye pembe uipendayo sana ya nyumba yako, hata nyumba yako iwe ya hali ya chini kiasi gani. Ulimwenguni pote, kwenye kasri na kwenye nyumba ndogo za kijijini, mtu aweza kujionea mifano mingi yenye kuvutia, ya fanicha zilizoundwa kwa mkono wa wasanii, nyakati fulani za tarehe za karne nyingi zilizopita. Hapana shaka huu ni ushuhuda wa ustadi, bidii, na saburi ya watu hao. Walipata uradhi na raha kwa kutokeza vitu ambavyo vilipohifadhiwa, huleta thamani yenye kutumika na uzuri. Hivi huongezea hali fulani ya kipekee kwa nyumba ambayo vinarembesha.

Katika kizazi hiki, kinachoendelea kujaza plastiki na bidhaa zenye utomvu, zawadi ya Muumba wetu ya miti bado inatumikia makusudi mengi mazuri. Mojawapo ya matumizi makubwa zaidi ya zawadi ya Mungu ya miti ni kutokezwa kwa mbao ghafi zinazomvutia msanii mwenye hamu aunde fanicha nzuri ya mbao.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Rimu

Tawa

Mwaloni

Msonobari aina ya radiata wenye mafundo-fundo

Msonobari uliong’arishwa

Msonobari uliopakwa grisi

Msonobari wenye rangi nyeusi-nyeusi

[Picha katika ukurasa wa 24]

Kutumia tezo

na “drawknife”

[Picha katika ukurasa wa 25]

Kabati ya nguo iliyotengenezwa kwa mkono

[Picha katika ukurasa wa 25]

Rafu ya pembeni

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki