Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kufanyia Wanyama Ukatili Ninawaandikia ili niwaeleze juu ya kazi nzuri sana mliyofanya kwenye makala “Maoni ya Biblia: Kufanyia Wanyama Ukatili—Je, Ni Vibaya?” (Novemba 8, 1998) Naona mlifanya vizuri sana kuonyesha kwamba Mungu hapendi wanyama watendwe kwa ukatili, hasa na watu wanaodai kuwa Wakristo.
J. L. C., Marekani
Vijana Bila Wazazi Nimeshukuru sana kwa makala “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Niishi Bila Wazazi?” (Novemba 22, 1998) Nina umri wa miaka 39 sasa. Lakini nilipokuwa na umri wa miaka 11, mama yangu alikufa na baba yangu akatoroka nyumbani. Hadi leo hii sijaweza kufanya watu waelewe maisha mabaya tuliyoishi na ndugu zangu. Lakini sasa naona kwamba wengine wanatuelewa. Asanteni.
K. Y., Japani
Baba yangu alikufa nilipokuwa na umri wa miezi tisa tu, naye mamangu akafa kabla nitimie umri wa miaka 12. Makala yenu ilikuwa yenye kufariji sana na kuonyesha jinsi mayatima wanavyohisi hasa. Ni jambo zuri kama nini kujua kwamba Yehova atawafufua wapendwa wetu waliokufa!
M. S. S., Brazili
Nina umri wa miaka 40 na nimesoma makala hiyo na hata nikarudia kuisoma. Nilibubujikwa machozi tangu mwanzo hadi mwisho, kwa kuwa nilikuwa yatima tangu nilipokuwa na umri wa miaka miwili. Kufikia leo, siwezi kutazama picha ya Mama na Baba bila kulia. Asanteni kwa kuandika makala kama hizo!
J. C. V., Ufaransa
Wazazi wangu wangali hai, lakini mimi hushuka moyo sana na kuchanganyikiwa akili na ninapenda makala yoyote inayozungumzia jinsi ya kupitia magumu. Nilitaka kuwaambia kwamba napenda masimulizi ya maisha na mashauri yanayotegemea Biblia ambayo yanapatikana katika “Vijana Huuliza . . .”
S. H., Kanada
Useremala Nimekuwa nikisoma jarida hili kwa miongo mingi, na inaonekana kwamba yaliyomo, mtindo wa kuandika, na uteuzi wa habari za kuandikwa zimeendelea kuboreka. Hata hivyo, ningependa kutaja jambo kuhusu makala “Kuchunguza Umaridadi wa Miaka Mingi wa Mbao.” (Novemba 8, 1998) Tafadhali waonyeni wasomaji ambao huenda wakataka kujaribu useremala kwamba tezo ni chombo hatari sana. Nilipokuwa nikikua katika miaka ya 1920, kilikuwa kinatumiwa sana nacho kiliitwa tezo-mguu. Kama picha yenu inavyoonyesha, mbao i katikati ya miguu, na tezo ina makali kama wembe. Lakini, kiliitwa pia msiba wa mguu kwa sababu mara nyingi wenye kukitumia walijeruhi miguu yao. Naona ni chombo hatari sana kutumiwa na mtu ambaye hajazoezwa kukitumia.
W. G., Marekani
Twathamini sana kikumbusha hiki cha kutahadharisha.—Mhariri.
Malkia Mwenye Busara Makala yenu yenye kuvutia kuhusu Catherine Parr (“Malkia Mwenye Busara Aliyemshinda Askofu Mwenye Hila,” Novemba 8, 1998) ilinikumbusha masimulizi ya Biblia ya Malkia Esta. Wanawake hao walionyesha hekima iliyoje! Japo mimi si mmoja wa Mashahidi wa Yehova, sikosi kamwe toleo la Amkeni! Mara nyingi mimi hujiuliza ni kwa nini wengine hawathamini vichapo vyenu kama ninavyovithamini.
M. D. S. F., Brazili
Nilipendezwa sana na masimulizi ya kihistoria kuhusu Henry wa Nane na mkewe Catherine Parr. Hongera. Makala hiyo ilifanyiwa utafiti vizuri sana, ikawa hususa na wazi.
C. G., Italia
Makala hiyo ilisimuliwa kwa njia ambayo ilitufanya tuhisi tulikuwa pamoja na Malkia Catherine wakati huo. Asanteni kwa kuchapa makala kama hizo ili kwamba sisi tunaoishi upande huu wa ulimwengu tupate kufahamu tamaduni za mbali.
L. G. na L. G., Venezuela