Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 11/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Mwaka Ambao Ulimwengu Ulichomeka”
  • Kalisi Nyingi Zaidi Zahitajika
  • Dola Yenye Kudhibiti
  • Kibali cha Kupora Mali
  • Mzigo wa Deni
  • Kuchukulia Kifo Kijuu-Juu
  • Rekodi Hatari
  • Ngano ya Lemming Si ya Kweli
  • Kuwanyang’anya Wagonjwa Vitu
  • Alama za Sikio
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1993
  • Je, Pesa Zinakutawala au Unazitawala?
    Amkeni!—2009
  • Ninaweza Kupangaje Matumizi ya Pesa Zangu?
    Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, Buku la 2
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 11/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

“Mwaka Ambao Ulimwengu Ulichomeka”

Jean-Paul Jeanrenaud, msimamizi wa programu ya Kimataifa ya Hazina ya Ulimwengu ya Mambo-Asili, adai kwamba “mwaka wa 1997 utakumbukwa kuwa mwaka ambao ulimwengu ulichomeka.” Mioto hatari ilitokea katika kila bara ila tu Antaktika. Kwa mfano, misitu yenye thamani ilichomeka nchini Indonesia na Brazili, katika maeneo yanayotoshana na Uswisi. Mioto hiyo huanzishwa na mambo tofauti-tofauti kama kukata miti kwa makusudi ya kilimo hadi ukame, ambao unadhaniwa kuwa umetokana na hali-hewa zenye kupita kiasi zinazosababishwa na El Niño. Kaboni dioksidi nyingi inayotokana na kuchomeka kwa vitu kama mafuta huongezea uchafuzi wa hewa na kuongeza hatari za ongezeko la joto duniani, laripoti gazeti la habari la London The Independent. Bw. Jeanrenaud aonya hivi: “Tunafanyiza duru mbaya ya uharibifu, ambako ongezeko la mioto hutokezwa na mabadiliko ya anga na mambo yanayohusu mabadiliko hayo.”

Kalisi Nyingi Zaidi Zahitajika

“Kwa sababu ya ukuzi wa mifupa yao, vijana wanahitaji kalisi zaidi,” chaonya kijarida cha Ujerumani cha Gesundheit in Wort und Bild. (Afya Katika Neno na Picha). Kiasi kinachopendekezwa kila siku ni miligramu 1,200, lakini ni asilimia 56 tu ya wasichana na asilimia 75 ya vijana wanaume wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 19 nchini Ujerumani hufikia kiwango hicho. “Kotekote katika Ulaya wasichana hawapati kalisi za kutosha,” asema Mary Fraser, wa Wakf wa Ulaya wa Kushughulikia Mifupa. Ingawa upungufu huo waweza kukaa muda mrefu bila kutambuliwa, unaweza kuchangia matatizo ya mifupa baadaye maishani. “Jibini, maziwa, mtindi, mbegu za ufuta, mbegu za amaranth, maharagwe soya, mboga za kijani-kibichi, njugu, na samaki ndivyo vyakula vyenye kalisi nyingi,” makala hiyo yasema.

Dola Yenye Kudhibiti

“Ni Wamarekani wachache tu ambao huenda wakatambua kwamba fedha nyingi zaidi za Marekani zinatumiwa nje ya nchi yao kuliko zile zinazotumiwa ndani ya Marekani,” lasema U.S.News & World Report. “Kati ya noti zenye thamani ya dola bilioni 450 pamoja na sarafu ambazo sasa zimo katika vibeti vya watu, madaftari ya hesabu, benki, na yaliyofichwa kwenye magodoro, karibu thuluthi mbili—au dola bilioni 300—ziko nje ya nchi.” Na kiasi hicho kimekuwa kikiongezeka kufikia dola bilioni 15 hadi dola bilioni 20 kila mwaka. Ingawa fedha katika Marekani huwa za noti za dola 20, fedha nyingi zilizo nje ya nchi hiyo ni noti za dola 100, jambo linaloonyesha kwamba fedha hizo hutumiwa kwa akiba na kwa biashara wala si kwa sababu ya kununua vitu vidogo-vidogo tu. Ndivyo hali ilivyo hasa katika nchi ambako kuna inflesheni kubwa na watu hawatumaini mabenki. Karibu asilimia 60 ya noti mpya-mpya za dola 100 ambazo zilichapwa mwaka uliopita zilipelekwa ng’ambo moja kwa moja. Kwa maoni ya Marekani, fedha nyingi zinazosambaa katika nchi za nje ni kama kuipa Marekani mkopo bila riba na ambao si lazima ulipwe kwa ununuzi wa bidhaa au kwa utumishi, jambo linalookoa serikali mabilioni ya dola.

Kibali cha Kupora Mali

“Viongozi wa kidini wa Katoliki ya Kiroma nchini Brazili wametetea maskini na wenye njaa, na kuwatetea wale ambao wameiba chakula ili waishi,” laripoti ENI Bulletin. Kwa sababu ya ukame mkali katika sehemu ya kaskazini-mashariki ya Brazili, watu wameruhusiwa kupora maduka makubwa na maghala ya bidhaa. Kulingana na askofu-mkuu wa Belo Horizonte, kadinali Serafim Fernandes de Araujo, “kanisa halishutumu mtu ambaye anatwaa chakula, mahali popote pale anapokipata, ili kuepuka njaa.” Na kadinali Paulo Evaristo Arns ananukuliwa akisema: “Tutapigana dhidi ya ubepari wa kisasa ambao hurundika mali mikononi mwa watu wachache waliopendelewa huku maskini wakizidi kuwa maskini.” Aliongezea: “Wakati umefika watu majijini na mashambani waamke.”

Mzigo wa Deni

“[Mkanada] wa kawaida hutumia dola 1,236 kununua zawadi, kujitumbuiza na kusafiri wakati wa sikukuu,” laripoti gazeti la habari la The Vancouver Sun, na “sehemu kubwa ya matumizi hayo yatatozwa kwenye kadi za mkopo.” Kuna msongo wa juu sana wa kihisia-moyo wa kutumia pesa wakati wa Krismasi, wasema washauri wa mambo ya kifedha, na wakati ambapo hakuna pesa, ni rahisi kuendelea kutumia pesa kwa kutumia kadi za mkopo. Mshauri mmoja aamini kwamba usalama wa kazi huonekana kuwapa wanunuzi “uhakika wa kujiingiza kwenye madeni hata zaidi badala ya kulipa madeni hayo.” Kufikia mwisho wa 1997, Wakanada waliweka rekodi ya kuwa na madeni ya dola bilioni 20.42 yasiyolipwa kutokana na matumizi ya kadi za mkopo—hiyo ikiwa maradufu ya madeni ya 1991. Wataalamu wakadiria kwamba inachukua mnunuzi wa kawaida miezi sita kulipa madeni ya sikukuu na kwamba wengi bado watakuwa na deni fulani waanzapo “kununua tena vitu kwa wingi” Krismasi ijayo.

Kuchukulia Kifo Kijuu-Juu

“Ni wazazi na walimu ambao wanapaswa kupunguza ushujaa unaoendelezwa na sinema na televisheni ili kutochukulia kifo kijuu-juu tu,” laeleza Jornal do Brasil. Uchunguzi mmoja uliofanywa katika Rio de Janeiro waonyesha kwamba watoto ambao wana umri unaopungua miaka 13 hufanya asilimia 10 ya uhalifu wote. “Watoto hawa hubeba bunduki, hushambulia, hulemaza, au huua wanashule wenzao, nao wana hatia juu ya kuwatenda vibaya kingono wale walio wachanga,” makala hiyo yasema. Mtaalamu wa akili Alfredo Castro Neto alisema: “Utamaduni wa sasa, ambao unatia moyo mashindano na ambao huonyesha katika sinema kwamba mtu aweza kuua ili apate chochote kile anachotaka, waweza tu kuongezea mvurugo wa akili wa vijana hao.” Akipendekeza vichezeo vyenye kufundisha badala ya bunduki, mwalimu Josefa Pech asema kwamba ni muhimu kumwonyesha mtoto kwamba “wonyesho wa shujaa auaye kila mtu ni upumbavu na si halisi na kwamba silaha si ishara ya uwezo, bali ni vifaa vya kuua watu.”

Rekodi Hatari

“Uvutaji wa sigareti huua Wamarekani wengi kila mwaka kuliko wale wote ambao wamekufa katika Vita ya Ulimwengu ya Pili na Vita ya Vietnam,” chasema kijarida University of California Berkeley Wellness Letter. “Kila siku zaidi ya Wamarekani 1,200 hufa kutokana na visababishi vinavyohusika na uvutaji wa sigareti, idadi inayolingana na ndege kubwa tatu au nne kuanguka na kuua kila mtu.”

Ngano ya Lemming Si ya Kweli

Je, lemming—wanyama wadogo wa jamii ya panya—hujiua kwa wingi kwa kufa maji? Watu wengi wangali wanaamini hili. Hata hivyo, kwa muda wote wanasayansi wametilia shaka na sasa Idhaa moja ya Shirika la Utangazaji la Uingereza inayoshughulikia Wanyama wa Pori, ambayo imekuwa ikipiga filamu za wanyama hao kwa miezi sita katika Aktiki ya Kanada, imeona kwamba jambo hilo si kweli. Maadamu wana chakula, lemming husitawi na kusongamana. Basi, hadithi ya kujiua kwao ilianzaje? Wanyama hao wa Norway wameonekana wakitumbukia kiaksidenti katika maji wanapohama kutoka milimani wakielekea kwenye malisho mazuri, laripoti gazeti la habari la The Guardian la London.

Kuwanyang’anya Wagonjwa Vitu

Hospitali za Ujerumani zimekumbwa na wezi. “Visa mia tatu huripotiwa kila mwaka na vyuo vya hospitali katika Cologne,” laripoti gazeti la habari la Emsdettener Tageblatt. “Shada la maua kwenye mkono mmoja, na tabasamu tosha mdomoni—na kwa mwizi aliyeingia hospitalini, amefanikiwa.” Wakijifanya kuwa wamezuru wagonjwa, wao huiba vitu vilivyo kwenye meza za kando ya kitanda na vitu vya kuangikia koti. Wagonjwa wazee-wazee hasa hurahisisha kazi ya wezi. Kwa mfano, mzee mmoja alipatikana akiwa ameweka maelfu kadhaa ya pesa za marki chini ya mto wa kitanda chake hospitalini. Kuweza kuzuru wakati wowote ule huwapa wezi uhuru mwingi na karibu kila mtu aweza kuingia hospitalini bila kusimamishwa. Kwa hiyo, wagonjwa waonywa wafungie fedha na vitu vyenye thamani katika sefu ya hospitali au kwingineko au kuwapa wengine wawawekee.

Alama za Sikio

Mwizi mmoja wa kuvunja nyumba alipopatikana na hatia karibuni katika London, ni sikio lake lililofanya atiwe hatiani. Kwa njia gani? Ingawa alikuwa mwangalifu sana asiache alama za vidole kwenye mahali pa uhalifu, yeye alikuwa na tabia ya kuweka sikio lake kwenye dirisha au kwenye tundu la ufunguo ili kuona kama kuna mtu ndani ya nyumba kabla ya kuvunja, hivyo akiacha alama za sikio. “Alama za sikio ni za kipekee kama vile tu alama za vidole,” asema Profesa Peter Vanesis, mtaalamu wa patholojia ya mahakama kwenye Chuo Kikuu cha Glasgow nchini Scotland. Lakini, tofauti na alama za vidole, masikio huendelea kukua muda wote wa maisha, kama nywele na kucha, laripoti The Daily Telegraph la London. Lakini, polisi wanajua kwamba masikio yetu, hata yawe na ukubwa gani, ni ya kipekee, kama ya yule mwizi. Alikuwa mtu wa kwanza kuhukumiwa nchini Uingereza kutokana na uthibitisho wa alama za masikio, naye alikiri mashtaka matano ya kuiba kwa kuvunja nyumba.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki