Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 4/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ni Nani Anayetaka Watoto?
  • Wakatoliki Wachawi
  • Watoto Wanene Zaidi—Kwa Nini?
  • Wakumbwa na Maumivu Makali ya Kichwa
  • Ponyo la Ukoma
  • Uchafuzi wa Moshi
  • Kuanguka Mtihani wa Unyoofu
  • Kurudi kwa Viini Vinavyoua
  • Uvutio wa Televisheni
  • Pesa na Kanisa
  • Kukabiliana na Wevi wa Magari
  • Kutoa Mimba Huua Akina Mama Pia
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1993
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1995
  • Kutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1993
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 4/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Ni Nani Anayetaka Watoto?

“Mpenzi chukua watoto, mimi nitachukua pesa.” Kichwa hicho kikuu katika Mainichi Daily News kilitaja kwa ufupi majibu ya wanawake wengi Wajapani kwa habari ya kwamba wangependa kubaki na nini ikiwa wangepata kutaliki. Kulingana na uchunguzi mmoja uliofanywa karibuni na Hakuhodo, kampuni moja ya matangazo ya biashara, mambo matatu yanayotangulizwa kwanza ni akiba ya benki, pesa, na makao ya likizo. Wana walikuwa nambari nne, wakifuatwa na mabinti, kisha makao, televisheni, vitu vya sanii, na mifuko. Akina baba pia wana wakati mchache kwa watoto wao. Uchunguzi tofauti uliofanywa na Benki ya Tokai ulipata kwamba asilimia 69 ya akina baba Wajapan wasema kwamba wana shughuli nyingi sana na kazi zao hivi kwamba hawawezi kutumia wakati kuzungumza na watoto wao. Kwa hakika, asilimia 22 walisema kwamba kwa vyovyote hawana mambo yanayofanana na ya watoto wao ili wayazungumzie.

Wakatoliki Wachawi

Kuvutiwa na mambo yanayopita uwezo wa kibinadamu kwaonekana kuwa kunaambukiza idadi inayoongezeka ya Wakatoliki. Makasisi Wakatoliki wanaomba kuondolewa kwa “marufuku ya kanisa juu ya zoea la uwasiliani roho,” lasema gazeti la kila juma la Katoliki Il Sabato. Kwa sababu ya kupendezwa kwao na uchawi, viongozi fulani Wakatoliki na wafuasi wao wanajulikana kuwa “Wakatoliki wachawi.” Wao wanasadiki kwamba wanaweza kuwasiliana na wafu, wawapige picha kwa kamera ya vidio, na kurekodi sauti zao kwa kaseti. Chuo kimoja katika chuo kikuu cha kipapa kimeandaa masomo fulani yanayopendwa sana ya mambo yanayopita uwezo wa kibinadamu. Lakini si kila mmoja anakubaliana na hilo. Myesuiti anayefundisha katika chuo kikuu kingine cha kipapa alisema hivi: “Kuna njia salama zaidi na ya kuheshimika zaidi ya kuongea na wafu: sala.” Hata hivyo, Biblia yaeleza kwamba wafu hawana ufahamu wowote na kwamba haiwezekani kuwasiliana nao, hata njia ipi itumiwe.—Mhubiri 9:5.

Watoto Wanene Zaidi—Kwa Nini?

“Watoto wa kisiku-hizi ni wanene zaidi na wazembe kuliko wakati mwingine wowote uliopita,” laripoti The Toronto Star. “Kunenepa miongoni mwa watoto kumeongezeka kwa kiwango cha kustaajabisha katika miaka 20 iliyopita,” adai Dkt. Oded Bar-Or, mkurugenzi wa lishe ya watoto katika Hospitali ya Chedoke-McMaster katika Hamilton, Kanada. Uchunguzi waonyesha kwamba hiyo ni kwa sababu ya ukosefu wa mazoezi na wa lishe bora. Mwendo huo ukizidi, madaktari wanahofu kwamba kutakuwa upungufu mkubwa katika afya ya watoto. Kulingana na gazeti Star, madaktari tayari “wametambua ukosefu wa mazoezi kuwa kisababishi kimoja cha . . . maradhi ya moyo, msongo wa juu wa damu, kisukari, na ugonjwa wa kupunguka kwa ukubwa wa mifupa.” Dkt. Bar-Or amalizia kwamba “mtoto asiyetenda anaelekea atakuwa mtu mzima mnene sana.” Yeye apendekeza mtindo wa maisha wenye utendaji.

Wakumbwa na Maumivu Makali ya Kichwa

Wataalamu wanakadiria kwamba karibu watu milioni 15 katika Jamhuri ya Muungano ya Ujerumani huugua aina mbalimbali ya maumivu ya kichwa. Moja ya maumivu ya kawaida sana ni maumivu ya kichwa kuuma upande mmoja, yanayoathiri wanawake mara nne kushinda wanaume. Maumivu ya kichwa kuuma upande mmoja huchukua karibu saa 18, na kwa ujumla imekubalika kuwa hakuna utibabu wa ugonjwa huo. Kwa kuongezea, gazeti Süddeutsche Zeitung laripoti kwamba “angalau Wajerumani milioni 1.5 huugua maumivu ya kichwa ya mara kwa mara yanayosababishwa na dawa za kutuliza maumivu.” Tatizo huanza wakati mtu anapomeza dawa hizo mara nyingi kwa miaka mingi ili kutuliza maumivu ya kichwa. Gazeti hilo laongezea kwamba kitulizo cha pekee kinachotumika kwa maumivu ya kichwa ya aina hiyo ni kuacha kutumia dawa hizo.

Ponyo la Ukoma

Je! wenye ukoma waepukwe au wasiajiriwe kazi? Sivyo, kulingana na makala moja katika jarida la Afrika Kusini Farmer’s Weekly. Okkie Kruger wa Misheni ya Ukoma alisema hivi: “Baada ya saa chache ya kutibiwa, hawawezi tena kuwaambukiza wengine na wanaweza kuendesha maisha ya kawaida na familia zao.” Wala wenye ukoma hawawezi kulemaa kabisa maishani wakipokea matibabu ya mapema vya kutosha, kwa sababu “maendeleo makubwa yamefanywa katika kutibu maradhi hayo katika mwongo uliopita,” katika tiba ya mchanganyiko wa dawa. Farmer’s Weekly liliripoti kwamba kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, watu kati ya milioni 10 na milioni 15 ulimwenguni wana ukoma.

Uchafuzi wa Moshi

Je! kuvuta sigareti hufanya uwezo wa kufikiri uwe bora? Wavutaji wengi hudai hivyo. Hata hivyo, utafiti wa karibuni katika United States waonyesha matokeo tofauti kabisa. Uvutaji hupunguza uwezo wa kukaza akili na hudhuru kumbukumbu la muda mrefu, lasema gazeti Guardian Weekly katika ripoti moja ya uchunguzi uliofanywa katika Chuo cha Washington katika Maryland. Uvutaji ulipatikana pia kuwa hupunguza uharaka wa tendo-itikio la mtu. Katika mtihani wa ustadi wa kuendesha gari, wavutaji walipatikana kuwa walikuwa na uwezekano wa kusababisha aksidenti mara 3.5 zaidi ya wasiovuta. Sababu ni nini? Madaktari wanadhani kwamba uvutaji wa muda mrefu waweza kuathiri ugavi wa damu katika maeneo ya ubongo yanayoshughulikia habari.

Kuanguka Mtihani wa Unyoofu

Lori la ulinzi lililokuwa likisafirisha mifuko ya pesa kutoka benki moja ya Jiji la New York liliangusha bila kukusudia mifuko miwili ya pesa katika moja ya barabara kuu yenye shughuli nyingi mno jijini. Magari yalisimama kwa ghafula. Mifuko “ikapasuka, ikiwamwagia wenye magari noti nyingi za dola kwa dakika kadhaa,” laripoti Newsday. Ni dola 3,500 tu zilizopatikana kati ya zile dola 300,000 zilizokuwa katika mifuko hiyo. Kwa kawaida, katika New York, ni kinyume cha sheria kuweka pesa zilizookotwa zikiwa ni zaidi ya dola 20. Akielezea kisa hicho, ofisa mmoja alisema hivi: “Ilikuwa ni kama kutupa kipande cha nyama kwa papa wengi. Watu walikuwa wakinyang’anyana tu pesa.” Mtu mmoja alidokezea msemaji wa polisi kwamba nambari ya simu ya pekee iwekwe kwa ajili ya wale ambao wangependa kurudisha pesa hizo. Inasemekana kwamba msemaji huyo “alionekana ameshtuka kidogo, kisha akacheka.”

Kurudi kwa Viini Vinavyoua

Inaonekana wanayansi walipuuza uwezo wa kurudi kwa vijidudu vyenye kusababisha magonjwa. Baada ya miaka ya ushindi uliotangazwa sana juu ya vijidudu hatari, “madaktari wanaripoti ugumu unaoendelea kuongezeka wa kutibu maambukizo fulani,” laripoti U.S.News & World Report. Gazeti hilo lilisema kwamba vijidudu fulani vinasitawisha “mbinu za uwerevu za urithi zinazoviwezesha kutangulia utengenezaji wa viua-viini.” Hospitali, vituo vya utunzaji, na vibanda vya wasio na makao zinakuwa sehemu za maongezeko makubwa ya magonjwa kama ugonjwa wa utando wa ubongo na kifua-kikuu. Sababu moja ya utendaji ulioongezeka wa viini ni kutwaliwa kwa mwendo wa kasi kwa mabara ambayo hapo awali hayakuwa yameguswa. “Kwa vile wanadamu wameenea na kuwapita wanyama wengine kwa idadi, wamekuwa ndio rahisi kushambuliwa,” lasema U.S.News & World Report. Mtaalamu mmoja asema kwamba “wanadamu sasa ni chaguo la makao ya vimelea na viini.”

Uvutio wa Televisheni

Ikiwa ungepewa dola milioni moja ili uache kutazama televisheni maisha yako yote, je, ungekubali? Kwa kupendeza, Mwamerika 1 kati ya kila 4 hawangekubali, laripoti International Herald Tribune. Kulingana na uchunguzi uliofanywa na gazeti TV Guide, nusu ya wale waliohojiwa walisema kwamba hawangeacha kutazama TV kwa pesa zinazopungua dola milioni moja. Kwa kutofautisha, 1 kati ya 4 walisema wangeacha kutazama TV maishani mwao hata kwa pesa kidogo kama dola 25,000. Watu wengi walisema wao hutazama TV mara chache kushinda walivyotazama miaka miwili iliyopita, lakini ni mtu 1 tu kwa 8 waliohisi kuwa wenye hatia ya kutazama televisheni kupita kiasi.

Pesa na Kanisa

Kulingana na jarida la Argentina La Maga, ni asilimia 3 pekee wa Wakatoliki wa Argentina huhudhuria misa. Hata hivyo, Argentina inabaki kuwa nchi ya pekee ulimwenguni yenye sheria katika Katiba yayo inayoamuru serikali kutegemeza Kanisa Katoliki kifedha. Sheria zimewekwa za kuwapa maaskofu wa Argentina na maofisa wengine wa Katoliki mishahara ya juu. Baada ya kujumlisha pesa, maondoleo ya malipo fulani, pesa za ziada, na mapendeleo mengine yanayotolewa, jumla kuu ya msaada wa serikali haipungui pesos milioni 246 (dola milioni 245, za U.S.) kila mwaka. Pesa hizo hutoka wapi? Hutoka kwa serikali. Lakini serikali huzipata kutoka kwa “Waargentina wote—hata wawe na itikadi gani za kidini,” lasema La Maga.

Kukabiliana na Wevi wa Magari

Transmita zilizofichwa, ambazo ni ndogo sana hivi kwamba zaweza kubebwa mkononi, zinawasaidia polisi kupata magari yaliyoibwa, laripoti International Herald Tribune. Kampuni moja katika United States, ambayo imetia katika karibu magari 150,000 chombo hicho chenye gharama ya dola 600, yadai kwamba asilimia 95 ya magari 3,500 yenye transmita yaliyokuwa yameibwa tangu 1986 yalipatikana. Katika kujaribu kuepuka wasikamatwe, wevi fulani sasa huendesha gari waliloiba maili kadhaa tu na kisha kuliegesha. Gari hilo lisipopatikana katika siku kadhaa, wevi hudhania gari hilo halikuwa na transmita.

Kutoa Mimba Huua Akina Mama Pia

Inakadiriwa kwamba “kila dakika mwanamke hufa kutokana na mimba au uzazi,” laripoti gazeti Choices. Gazeti hilo laongezea kwamba “zaidi ya nusu milioni ya akina mama hufa kila mwaka kutokana na matatizo yanayohusu mimba. Na kwa kila mwanamke anayekufa, 100 wengine hubaki wakiwa wagonjwa au hulemaa.” Katika Amerika ya Latini, karibu 1 kwa kila wanawake 73 hufa kutokana na matatizo ya mimba. Katika Esia, inakadiriwa kwamba 1 kati ya wanawake 54 hufa; na katika Afrika, 1 kati ya 21. Tarakimu hizo ni za juu sana zikilinganishwa na uwiano wa 1 kati ya kila 10,000 katika Ulaya ya Magharibi. Visababishi vya vifo vinavyohusu mimba vinatia ndani “kutoa mimba, kunakosababisha vifo zaidi ya 200,000 kati ya vifo vya akina mama 500,000 vinavyotukia ulimwenguni pote kila mwaka,” lasema Choices.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki