Kuutazama Ulimwengu
Wizi Katika Makanisa ya Uingereza
“Mahali pa ibada hapaonwi tena kuwa patakatifu,” laripoti The Sunday Times la London. Vinara vya mishumaa, viti vya maaskofu, vinara vya shaba vya msemaji, magudulia ya enzi ya kati, na mabirika ya kale ya maji ya ubatizo huibiwa kutoka makanisa ya Uingereza na kuuzwa kama virembeshi vya bustanini. Biashara hii isiyo halali ni ya kimataifa, huku vitu vya sanaa vikiibiwa baada ya kuagizwa na wateja. Dirisha moja lililopotea lenye kioo chenye rangi lilionekana katika mkahawa mmoja Tokyo. Hasara ya kila mwaka ya makanisa hujumlika kuwa karibu dola milioni 7. Sasa vifaa vilivyo tata vya uchunguzi vinawekwa na mashirika ya usalama yameajiriwa kulinda majumba ya makanisa.
Utoaji-Mimba Zaidi Katika Kanada
Rekodi ya juu ya utoaji-mimba 104,403 ulifanywa katika Kanada mwaka wa 1993, ambao ni ongezeko la asilimia 2.3 kupita mwaka uliotangulia. Kulingana na The Toronto Star, “hilo hujumlika kuwa utoaji-mimba 26.9 kwa kila watoto 100 wanaozaliwa.” Kwa nini kuwe na ongezeko hilo? Ingawa hilo limesemwa kuwa ni kwa sababu ya idadi yenye kuongezeka ya kliniki za kibinafsi za utoaji-mimba katika hiyo nchi, maofisa kwenye Planned Parenthood Federation of Canada huelekeza kwenye misongo ya kiuchumi kuwa “sababu kuu ya utoaji-mimba.” Anna Desilets, mkurugenzi mkuu wa Alliance for Life, kikundi chenye kutetea uhai, ahisi kwamba “kuweza kutoa mimba kwa urahisi huongoza watu wautumie kama kizuia-uzazi, kwa gharama za kodi inayolipwa na serikali.”
Watoto Walio na UKIMWI
Idadi ya watoto wa Venezuela walio na UKIMWI inaongezeka kwa kiwango chenye kushangaza, laripoti El Universal la Caracas. “Mbeleni watoto kati ya wawili hadi sita waliripotiwa kuwa na UKIMWI kila mwaka,” aeleza mtaalamu mmoja, “lakini sasa tuna visa viwili hadi sita kwa juma moja.” Asilimia ya wanawake walioambukizwa, ambao kisha hupitisha hivyo virusi kwa watoto wao, huongezeka kila siku. “Ni jambo la maana kukumbuka,” yamalizia hiyo ripoti ya gazeti la habari, “kwamba takwimu zinazoshughulikiwa na Wizara ya Afya huonyesha tu sehemu ndogo mno ya tatizo hilo.”
Wanawake Wenye Jeuri Waongezeka
“Wanawake wanahusika mara nyingi zaidi katika jeuri kuliko wakati uliopita,” adai mtaalamu wa uhalifu wa Chuo Kikuu cha Ottawa, Tom Gabor. “Jeuri,” laripoti gazeti la habari The Globe and Mail, “inafanywa kwa kuongezeka na wanawake ambao ndio wanaongoza, badala ya kuongozwa. Hawa hawachukui mahali pa wanaume waovu.” Mashtaka ya uhalifu wenye jeuri dhidi ya wanawake yamepanda kutoka 6,370 katika 1983 hadi 14,706 katika 1993. Hata hivyo, wanaume bado ndio wenye sehemu kubwa katika uhalifu wenye jeuri. Kulingana na Globe, “katika 1993, asilimia 88.6 ya watu wazima na asilimia 76.3 ya vijana walioshtakiwa kwa uhalifu wenye jeuri walikuwa wanaume.”
Makasisi na Ndoa
Gazeti la habari la Australia The Sydney Morning Herald liliripoti kwamba idadi inayoongezeka ya Wakatoliki wenye uvutano mwingi wanasababu kwamba “kukomeshwa kwa useja wa kulazimishwa kungesaidia kuzuia makasisi wasiache ukasisi.” Useja wa kulazimishwa unaonwa kuwa kizuizi kikuu kwa wanaume wachanga kuingia katika ukasisi. Likikazia tatizo hilo, Herald lilitoa tarakimu zenye kufunua mambo mengi. Kitovu kikuu cha kuzoeza makasisi cha New South Wales kilikuwa na kilele cha wastani wa walioingia ukasisi 60 kwa mwaka kutoka 1955 hadi 1965. Lakini tarakimu inayolingana na hiyo kati ya 1988 na 1994 ilikuwa waingiaji tisa tu kwa mwaka. Kaimu mkurugenzi wa chuo kingine cha kuzoeza makasisi katika Sydney alitaarifu kwamba, kwa maoni yake, kuruhusu makasisi kufunga ndoa huenda kukathibitika kuwa suluhisho “la haraka” lakini lisilodumu kwa uhaba mkubwa sana wa makasisi katika Australia.
“Wauaji Wanaongoja kwa Subira”
Umoja wa Mataifa linajaribu kuchanga dola 75 milioni ili kuanza kuondoa mabomu ya kutegwa chini ya ardhi yakadiriwayo kuwa 110 milioni katika nchi 64, laripoti International Herald Tribune. Inagharimu dola 3 hivi kutokeza bomu linalokusudiwa kuangamiza wanajeshi (AP) ambalo si kubwa kuliko pakiti ya sigareti. Lakini kupata na kuondoa bomu hilo kutoka ardhini hugharimu kati ya dola 300 hadi dola 1,000. Kuondolewa kwa hayo mabomu ya chini ya ardhi kunazuiwa na tatizo jingine. Msemaji wa Umoja wa Mataifa alisema hivi: “Kila mwaka mabomu mapya ya AP milioni 2 yanategwa kuongezea yale zaidi ya milioni 100 yaliyopo.” Wataalamu wanakubali kwamba itachukua miongo mingi kuondoa duniani pote kile jenerali mmoja wa Kambodia alikifafanua kuwa “wauaji wanaongoja kwa subira ambao hawakosi kuua.”
Ujiuaji Kimakusudi wa Kuruka Darajani
Zaidi ya watu elfu moja wamejiua kimakusudi kwa kuruka kutoka daraja lijulikanalo sana la Golden Gate Bridge la San Francisco tangu lilipofunguliwa mnamo 1937. “Kujiua kwa kuruka kutoka Golden Gate Bridge kuna uvutio wa kihisia, ushawishi. Mahali hapo ni penye kupendeza sana. Kuna fantasia mahususi inayohusika,” akasema mtaalamu wa ujiuaji kimakusudi Richard Seiden. Ni wachache wa warukaji ambao husalimika na kueleza hiyo hali, jambo ambalo halishangazi kwa kuwa wanachapa maji wakiwa kwenye mwendo wa kilometa 120 kwa saa na kwa kawaida hupasua viungo vya ndani. Uchunguzi wa watu 500 ambao wamesihiwa wasiruke ulifunua kwamba chini ya asilimia 5 hujiua hatimaye.
Vifo Vinavyohusiana na Barabara
Kukiwa na vifo 26 kwa kila wakazi 100,000, Argentina yaongoza ulimwengu sasa katika idadi ya misiba inayohusiana na barabara, kulingana na gazeti la habari la Argentina Clarín. Katika 1993 kulikuwa na vifo kama hivyo 8,116 katika hiyo nchi. Idadi hiyo ilipanda hadi 9,120 katika 1994. Lakini wakati wa miezi sita ya kwanza ya 1995, tayari kulikuwa kumekuwa na zaidi ya vifo 5,000 vinavyohusiana na barabara. Katika 1994 asilimia 25 hivi ya majeruhi ilikuwa wanaotembea. Katika mkoa wa Buenos Aires pekee, vifo vya aksidenti za barabarani viliongezeka kwa asilimia 79. Asilimia kubwa ya hizo aksidenti ilisababishwa na ukosefu wa madereva kukadiria vizuri wakati wa kupita magari mengine.
Uvutaji Sigareti wa Watoto
Ripoti ya 1993/94 yaonyesha kwamba watoto wengi zaidi wanavuta sigareti katika Uingereza. Idadi ya wavutaji wenye umri wa miaka 11 hadi 15 imeongezeka kutoka asilimia 10 hadi asilimia 12. Ongezeko hilo hurudufisha kile maofisa wa afya wa serikali walitarajia mwaka wa 1994, laonelea gazeti la habari Independent. Ingawa uvutaji wa sigareti wa watu wazima umeshuka, asilimia 29 hivi ya wanaume na asilimia 27 ya wanawake Waingereza bado wanavuta sigareti. “Huenda kupungua kwenye kutazamisha katika uvutaji wa watu wazima kukahitajika kabla ya mitazamo ya matineja kubadilika kwa njia yenye umaana,” yamalizia hiyo ripoti.
Elimu ya Afya ya Mdomo kwa Waliozeeka
“Elimu ya afya ya mdomo yaweza kuwa jambo la uhai na kifo kwa wazee-wazee,” lasema Asahi Evening News. Wanasayansi Wajapani hufikia mkataa kwamba “wazee-wazee wanaweza kupunguza hatari ya kupata mchochota wa pafu kwa kupiga meno mswaki tu.” Katika uchunguzi wa wazee-wazee 46, meno ya kikundi kimoja cha watu 21 yalipigwa mswaki sawasawa na wauguzi kila siku baada ya chakula cha mchana. Pia walichunguzwa usafi wa meno mara mbili au tatu kila juma. Baada ya miezi mitatu ilipatikana kwamba 25 ambao hawakufuata hiyo kawaida walipatwa na homa kwa siku kumi zaidi kuliko wale 21. Afya njema ilikuwa sababu ya kukosekana kwa bakteria za mdomoni. Uchunguzi wa mbeleni ulifikia mkataa kwamba “mate au vipande vya chakula ambavyo vilipumuliwa ndani mapafuni kiaksidenti mara nyingi husababisha mchochota wa pafu,” likasema hilo gazeti la habari.
Hali ya Kutoweza Kufa Yauzwa?
“Kwa Dola 35, Waweza Kupata Hali ya Kutoweza Kufa,” ndivyo linavyodai Register-Guard la Eugene, Oregon, Marekani. Mwanamikrobiolojia James Bicknell ajitolea kuhifadhi DNA yako ili, kama gazeti hilo lisemavyo, “katika karne fulani ya wakati ujao, mzao mwenye upendo aweze kutumia habari ya kibiolojia katika DNA ili kufanya nakala yako.” Dakt. Bicknell anauza kisanduku cha DNA ambacho kina vipande viwili vya shashi na kiwekeo kidogo cha kioevu. “Isugue shashi kwenye upande wa ndani wa mashavu yako,” yeye asema, “ingiza shashi katika kioevu, na uirudishe kwangu.” Kisha yeye azidua DNA kutoka chembe ambazo zilifutwa kwenye shashi na kuiweka kwenye karatasi fulani ya kichujio. Kisha karatasi hiyo huhifadhiwa katika mrija ndani ya kisanduku kidogo cha alumini chenye jina lako juu yacho ukionyeshe kama utakavyo. Guard lasema: “Yeye huona kwamba watu huhifadhi majivu ya wafu waliochomwa, nywele, na kucha za vidole vya mikono. Kisanduku cha DNA ni kitu cha kupitisha kwa wajukuu wako kurithi.”
Tiba ya Jeni Motoni
Matarajio yalikuwa juu sana miaka sita iliyopita wakati ambapo tiba ya jeni katika binadamu ilianza kwa mara ya kwanza. Wanasayansi walitarajia, hatimaye, kutibu maradhi ya kiasili ya kurithiwa kwa kudunga wagonjwa wao jeni zifaazo. Wao pia walitumaini kudunga vitu vya kiurithi ambavyo vingesababisha chembe zenye kudhuru, kama vile chembe za kansa, zijiangamize. Hata hivyo, baada ya utafiti mwingi wenye bidii, hiyo tiba inashambuliwa. Lataarifu International Herald Tribune: “Kwa kichaa hicho chote, hakujapata kuwa na ripoti yoyote iliyochapishwa juu ya mgonjwa ambaye amesaidiwa na tiba ya jeni.” Wanasayansi wakuu wanahofu kwamba utafiti huo unaharakishwa sana na mapendezi ya kibiashara na ya kibinafsi, badala ya hangaiko kwa wagonjwa. Tatizo moja ni kwamba chembe zilizotibiwa na tiba ya jeni huenda zishambuliwe na kuharibiwa na mfumo wa kinga wa mwili, ambao unaziona kama kitu kigeni.