Rafiki Yangu Mpendwa
Rafiki zako ni nani? Je, ni wale tu wa rika lako? Soma simulizi la kijana mmoja kuhusu mmoja wa rafiki zake, ambaye ni mzee kumpita kwa miongo saba hivi.
FAMILIA yetu ilihamia Aberdeen, Scotland, miaka tisa hivi iliyopita nilipokuwa na umri wa miaka sita tu. Huo ulikuwa wakati wenye kuniogopesha kwa sababu ningelazimika kuanza shule mpya na kufanya rafiki wapya. Lakini kitu fulani kilinistarehesha kwa wanana kuingia katika hali yangu mpya. Mwanamke fulani mzee zaidi, ambaye wazazi wangu walikuwa wamekutana naye wakati moja mbeleni, aliishi karibu na kwetu. Nilijulishwa kwake ifaavyo mara nikashangaa kupata kujua jinsi alivyokuwa mwenye kupendeza. Yeye alikuwa mchanga moyoni, naye alivalia kwa urembo sana.
Nyumba tulimokuwa tukiishi ilikuwa imekodiwa, kwa hiyo tukahamia nyumba ya kudumu kilometa chache hivi kutoka nyumba ya Shangazi Louie. Natumia neno “shangazi” kwa sababu ya heshima na upendo. Nilihuzunika tulipolazimika kuondoka, kwa kuwa ndugu yangu nami tulikuwa tumeanza kumtembelea kwa ukawaida.
Hata hivyo, shule niliyohudhuria ilikuwa tu karibu na nyumba ya Shangazi Louie. Kwa hiyo kila Ijumaa baada ya masomo kwisha na kabla ya kwenda kwenye mazoezi yangu ya Dansi ya Kitamaduni ya Nchi ya Scotland shuleni, nilikuwa nikienda kwa Shangazi kunywa chai. Hii ikawa kawaida yangu. Nilikuwa nikija na kimoja cha vitabu vyangu vya hadithi, naye angenisomea nilipokuwa nikila sandwichi ya bilimbi na kunywa gilasi ya maziwa baridi.
Nakumbuka kwamba Ijumaa zilikuwa zikipita polepole nilipokuwa nikingoja kwa hamu sana kengele ya saa 9:30 alasiri, ambayo ilimaanisha kukimbia kwa Shangazi Louie. Ilikuwa wakati huu ambapo nilijifunza kwa mara ya kwanza jinsi wazee-wazee wawezavyo kuwa wenye kupendeza na wenye kufurahisha. Kwa hakika, sikumwona kuwa mzee. Akilini mwangu alikuwa mchanga sana. Angeweza kuendesha gari, na alidumisha nyumba na bustani yenye harufu nzuri—ni nini kingine atakacho mtoto?
Miaka mitatu ilipita, nami nilikuwa katika mwaka wa mwisho wa shule ya msingi. Huu ndio ulikuwa wakati ambapo Shangazi Louie aliamua kwamba bustani yake ilikuwa ikimpa kazi nyingi mno na kwamba nyumba ya orofa ilikuwa chaguo la kihalisi. Wakati huo singeweza kufahamu lile wazo la kuzeeka. Nilikasirika kwamba nyumba yake ya orofa ilikuwa katika sehemu nyingine ya mji. Ijumaa hazikuwa na uvutio kwangu kama zilivyokuwa mbeleni.
Katika 1990 ilionekana kwamba nilikuwa niende kwenye shule ya sekondari. Ningefanya nini katika shule kubwa kama hiyo? Ningeweza kukabilije magumu? Ningeenda katika shule tofauti na waliyoenda rafiki zangu, kwa kuwa familia yetu iliishi katika eneo tofauti. Lakini tena Shangazi Louie alikuwapo pale kwa sababu nyumba ya orofa aliyokuwa amehamia ilikuwa karibu tu na shule ya sekondari niliyohudhuria! Nilimwomba ikiwa ningeweza kuwa nikija kwake wakati wa kipindi cha chakula cha mchana ili kula sandwichi zangu. Hivyo kawaida nyingine yenye thamani ikaanzishwa.
Naamini kwamba huu ndio wakati ambapo uhusiano wetu ulibadilika kutoka kuwa uhusiano wa mtoto na mtu mzima hadi kuwa kufurahia uandamani wa mmoja na mwenzake. Hili lilikuwa wazi katika njia nyingi, lakini njia moja hasa ilikuwa wakati ambapo tulianza kusoma uandishi bora pamoja—Jane Eyre, Villette, Pride and Prejudice, na The Woman in White—badala ya vitabu vyangu vya hadithi. Upendezi wangu ulikuwa umekomaa.
Shangazi Louie alinifundisha kwamba kupenda watu ni ustadi na ufundi. Kama si yeye, huenda singetambua hilo hadi nilipokuwa na umri mkubwa zaidi. Yeye alinifunza kusikiliza, na watu wengi katika ulimwengu huu wenye shughuli nyingi mno hawajifunzi hilo kamwe, wawe wazee au wachanga. Ninapojikunja kwenye kiti chake, yeye anisimulia hadithi za maisha yake na mambo aliyopata kuona. Nahisi kuchangamshwa na ujuzi wenye kupendeza mno ambao bibi huyu anao.
Shangazi Louie aliacha mambo mengi—ndoa, watoto, kazi-maisha—ili kutunza wazazi wake na shangazi yake waliokuwa na magonjwa yenye kutamausha. Hili lilimwezesha ndugu yake mchanga abaki katika utumishi wa wakati wote.
Kwa miaka miwili ambayo imepita, Shangazi Louie amekuwa mwenye afya mbaya, nami naweza kuona, kukata tamaa, magumu, na maumivu ambayo umri wa uzee huleta. Hivi majuzi, akiwa na umri wa miaka 84, alilazimika kuacha kuendesha gari, na hilo limemletea magumu mengi. Alizoea maisha yenye utendaji mwingi, na sasa kutoweza kutoka nyumbani kunamkatisha tamaa sana. Amelazimika kupigana na hisia kwamba anasumbua watu. Haidhuru ni mara ngapi tumwambiapo kwamba tunampenda na kwamba tungemfanyia chochote, bado yeye huhisi kuwa mwenye kustahili kulaumiwa.
Kinachofanya hali iwe mbaya zaidi sasa ni kwamba ni vigumu kwake kujiosha na kujivisha. Hata ingawa amewafanyia wengine hivyo, ni jambo gumu kwake kujipata akihitaji msaada. Hili lanifunza kwamba hata wakati watu hawawezi kujifanyia kila kitu, bado wanastahili heshima yetu.
Hata hivyo, zaidi ya yote, ono hili limenisaidia kufahamu vile kuzeeka kulivyo. Kila kitu ambacho Shangazi Louie hawezi kufanya tena hunifanya nilie. Zaidi ya yote, ninapomwona akiwa amefedheheka au katika umivu baya, nataka kulia na kulia. Ninachosikitikia hasa ni kwamba hekima yake yote huenda isifurahiwe na kuthaminiwa na mtoto mwingine mchanga zaidi yangu.
Nyakati nyingine mimi hujiuliza ikiwa namfanyia mambo ya kutosha. Je, ananifurahia na kunipenda kama ninavyompenda? Lakini niendapo kwa chakula cha mchana na kumkumbatia, shaka zote hutoweka.
Nahisi kuheshimiwa kuwa na rafiki kama huyo. Amenifunza sifa nyingi mno nzuri—zaidi ya yote amenifunza upendo. Singebadilisha urafiki wake na ule wa rafiki mia moja wenye umri sawa na wangu. Ingawa nitamaliza shule karibuni na sitakuwa nikienda tena kwa chakula cha mchana kwake, sitaacha kamwe kumpenda, kumtembelea, na kumsaidia rafiki yangu mpendwa. Yeye amenifunza kwamba maisha yanaweza kuwa yenye furaha na yenye kuridhisha ukifikiria wengine kabla ya kujifikiria.—Imechangwa.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Nikiwa na Shangazi Louie