Kutazama Ulimwengu
Ushawishi Mkubwa wa TV Duniani Pote
Televisheni inapendwa kadiri gani ulimwenguni pote? Kulingana na International Herald Tribune, kuna TV zaidi ya bilioni moja ulimwenguni pote, asilimia 50 kuliko zilivyokuwako miaka mitano iliyopita. Katika makao ya Wajapan, kuna TV nyingi kuliko vyoo vya maji. Karibu nusu tu ya makao ya Wameksiko yana simu, lakini karibu kila makao yana TV. Na Waamerika wengi wana stesheni za televisheni 25 au 30 wanazoweza kuchagua. Tribune lasema hivi: “Matokeo ya kitamaduni, kisiasa, na kiuchumi ya mapinduzi hayo ya televisheni duniani ni makubwa sana. . . . Wengine wanahangaika kwamba kutazama TV sana hivyo kutafanya ulimwengu wote mzima upoteze hamu ya kusoma, kama vile ambavyo tayari kumetukia kwa vizazi viwili vya Waamerika.”
Damu ya Familia si Salama Zaidi
Uchunguzi wa serikali wa upaji wa damu zaidi ya milioni moja katika sehemu tano kuu katika United States umefunua uwongo wa imani inayopendwa sana kwamba damu ya marafiki au washiriki wa familia ni salama zaidi ya damu ya watu usiowajua. Kwa mfano, uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba asilimia 2.6 ya upaji wa damu kutoka kwa watu wa ukoo na marafiki ulikuwa na ugonjwa wa mchochota-ini aina ya B, ukilinganishwa na asilimia 1.8 kutoka kwa watu wasiojulikana. Upaji kutoka kwa washiriki wa familia na marafiki ulipatikana pia kuwa unabeba kiwango cha juu cha kaswende, mchochota-ini aina ya C, na aina ya vairasi inayosababisha kansa, HTLV-1. “Hufanyi hali yako ya kutoweza kupatwa na ugonjwa kuwa bora zaidi kwa kuomba marafiki au watu wa ukoo wakutolee damu,” akasema Lyle Petersen wa Vituo vya Serikali vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa.
Kuisukuma Dunia Mpaka Mwisho
Ukuzi wa sasa wa idadi ya watu kila mwaka katika ulimwengu ni karibu milioni 100, na inakadiriwa kwamba kufikia mwaka 2050, idadi ya watu itakuwa imefika bilioni 10, yasema ripoti moja katika British Medical Journal. Royal Society of London na Chuo cha Kitaifa cha Sayansi cha U.S. vilitoa taarifa ya pamoja ya pekee iliyosema kwamba ukuzi kama huo unatisha mazingira kwa uharibifu usioweza kurekebishwa. Ingekuwa hivyo hasa ikiwa mataifa yanayositawi, ambako ukuzi huo unatokea zaidi, yangetumia mali-asili zayo kwa kiwango kilekile cha mataifa yaliyositawi. Vyuo hivyo vilipendekeza kutumiwa zaidi kwa sayansi na tekinolojia lakini vikasema kwamba si hekima kuzitegemea pekee “kusuluhisha matatizo yanayoletwa na ukuzi wa haraka wa idadi ya watu, matumizi mabaya ya mali-asili, na matendo yanayodhuru ya kibinadamu.” Ikiwa hakuna badiliko, taarifa hiyo inaonya, “kwa sehemu kubwa ya ulimwengu, sayansi na tekinolojia haziwezi kuzuia uharibifu usioweza kurekebishwa wa dunia au umaskini wenye kuendelea.” “Tusipojaribu kwa bidii kudhibiti idadi ya watu, kila kitu kingine kitakuwa cha pili,” akasema Bwana Michael Atiyah, msimazi wa Royal Society of London.
Misaada Isiyofika Kamwe
Ni asilimia 7 tu ya misaada ya kimataifa inayotolewa ili kupunguza njaa na umaskini katika Afrika hufikia wale waliokusudiwa, akiri Ferhat Yunes, makamu wa rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika. Msiba huo waongezwa na hali mbaya sana ya mamilioni ya watoto Waafrika. Gazeti la Kihispania El-Pai̇́s laripoti kwamba kotekote barani, kuna watoto milioni 30 wanaougua utapiamlo na milioni 40 zaidi ambao ukuzi wao umekawia kwa kutokupata lishe bora. Wawakilishi wa nchi 44 za Kiafrika, wakikutana Dakar, Senegal, walipendekeza ugawanyaji wa misaada kutoka vituo vingi badala ya kimoja tu na kupunguzwa kwa matumizi ya kijeshi kuwa njia mbili kuu za kufanya hali ya watoto hao kuwa bora.
Mavumbi ya Afrika
Mavumbi ya Afrika, yanayochukuliwa kutoka savanna na sehemu za vichaka na pepo zenye joto na zilizokauka, yanafaidi sehemu nyingine za dunia, wasema wanasayansi. Sababu moja ikiwa ukame wa muda mrefu katika Kusini mwa Afrika, tani milioni nyingi za udongo wa juu wa Afrika ziligeuzwa kuwa mawingu makubwa ya mavumbi katika 1992 pekee, laripoti International Herald Tribune. Sehemu kubwa ya mavumbi hayo huangukia Bahari ya Atlantiki, yakitoa madini—hasa chuma inayohitajiwa sana—kwa planktoni na krili, ambazo ndizo mwanzo wa mfululizo wa chakula. Mavumbi yaliyobaki huenda mabara ya Amerika. Uchunguzi katika msitu wa mvua wa Amazon waonyesha kwamba mavumbi ya Afrika yanasaidia kurutubisha tena udongo usiokuwa na rutuba huko. “Mavumbi hayo ya Afrika yanayolisha Atlantiki na mabara ya Amerika yanaonyesha jinsi mazingira makubwa sana na yaliyo mbali sana yanavyotegemeana,” asema Dkt. Michael Garstang wa Chuo Kikuu cha Virginia. “Ujumbe ni kwamba dunia yetu ina mifumo mingi inayoshikana na kutegemeana ambayo sisi wenyewe hata hatuielewi. Sasa ndipo tunaanza tu kuelewa.”
Magazeti ya Kidini Yaacha Kuchapishwa
“Magazeti mawili ya kidini yaliyo ya kale zaidi nchini, American Baptist na Christian Herald, yameacha kuchapishwa,” laripoti habari iliyotoka kwa shirika la habari la Associated Press. “Magazeti hayo mawili, lile la Christian Herald, lenye umri wa miaka 115, lililoanzishwa katika 1878 na kuwa na makao yake katika mji wa Chappaqua, N.Y., na lile la American Baptist lenye umri wa miaka 189, ambalo toleo lalo la kwanza lilitokea katika 1803, yalitaja upungufu wa mwenezo.” Mahali pa gazeti la kila mwezi American Baptist, lenye makao katika Valley Forge, Pennsylvania, patachukuliwa na barua yenye habari. Hata hivyo, jarida jingine la kidini la enzi hiyo, Mnara wa Mlinzi, linaendelea kukua. Kwanza likichapishwa kila mwezi katika 1879 katika Pittsburgh, Pennsylvania, nakala 6,000 zikitolewa kwa Kiingereza, Mnara wa Mlinzi, sasa huchapishwa mara mbili kwa mwezi katika lugha 112 kwa nakala 16,400,000 katika kila toleo.
Jeuri Katika Shule
Uchunguzi mkubwa wa shule 169 katika Hamburg, Ujerumani, ulijaribu kugundua visababishi vya ongezeko la jeuri katika vyuo vya masomo. Kwa nini shule zinaripoti vitisho vya kifedha, matisho, majeraha ya mwili, na makosa ya kingono kwa hali inayozidi kuongezeka sana? Kulingana na gazeti Frankfurter Allgemeine Zeitung, wanafunzi waliochunguzwa walitaja ujeuri katika vyombo vya habari, kupuuzwa nyumbani, mizozano na wanafunzi wa kigeni, na mkazo wa akili kuwa ndizo sababu kuu. Uchunguzi huo pia ulitaja mambo kadhaa ya kijamii yanayozuia kusuluhishwa kwa matatizo ya ujeuri shuleni. Kwa mfano, ilipatikana kwamba watoto kwa ujumla walikosa utambuzi wa hatia au kosa na walikuwa wenye ubinafsi sana, wasiovumilia na wasiojali wengine sana. Na wazazi wengi waliona utumizi wa jeuri katika kusuluhisha mizozano kuwa jambo la kawaida na walikuwa wakifunza watoto wao walipize kisasi na kujikinga.
Wapotezwa na Nektari
Ni nini hutukia nyuki wakinywa kupita kiasi nektari (maji matamu ya maua) iliyochacha? Wanatenda kama walevi. Wengine hupotea njia ya kurudi nyumbani, na wale ambao hawapotei, hukatazwa kuingia ndani ya mzinga kwa sababu ya tabia yao mbaya. Na wasipokufa kwa sababu ya baridi, matokeo ya ulevi yaweza kuwa mabaya sana hivi kwamba yaweza kufupiza uhai wao kwa nusu, laripoti gazeti la kila siku El Pai̇́s. Hata hivyo, kwa habari ya nyuki, ulevi huo si wa kujitakia. Kama ilivyoelezwa na Errol Hassan wa Chuo Kikuu cha Queensland, Australia, ongezeko la halijoto laweza kufanya nektari wanayokunywa ichache na kufanyiza kileo.
Hatari Zilizojificha
“Wavutaji sigareti waweza kuambiwa kimakosa kwamba wana afya nzuri wakati ambapo wanakabili hatari zaidi ya kupatwa na maradhi ya moyo,” yasema makala katika The New York Times. Kwa nini? Kwa sababu madhara yanayotokezwa kwa kuvuta sigareti katika mishipa midogo ya moyo inayopitisha damu hayaonyeshwi katika michunguzo ya kawaida ya moyo. Kwa hiyo wavutaji wakiwa chini ya mkazo wa kimwili au kihisia-moyo, moyo wao hukosa damu, hiyo ikiongeza hatari ya kupatwa na maradhi ya moyo. Uchunguzi mmoja katika Taasisi ya Moyo ya Iowa katika Des Moines ulionyesha kwamba hiyo ni kweli pia hata ikiwa mvutaji havuti saa hizo na kwamba tatizo hilo huongezeka wakati wa uvutaji. Mtu akiwa chini ya mkazo, mishipa midogo ya moyo hupanuka na kupitisha katika moyo damu mara nne kuliko kawaida. Lakini katika moyo wa mvutaji, damu hiyo hupunguzwa kwa asilimia 30.
Mtindo Mpya wa Usajili
“Matangazo ya biashara ya televisheni yanayoonyesha watawa wa kike wakikata nyasi na mapadri wakicheza mchezo wa vikapu ni sehemu ya jitihada mpya ya Kanisa Katoliki ya kusajili ili kuongeza idadi inayopungua ya makasisi,” laripoti gazeti The West Australian. “Matangazo hayo ya biashara ya sekunde 30 . . . yaonyesha mapadri na watawa wa kike wachanga wakizungumzia kazi yao huku wakikata nyasi, wakienda madukani, wakishiriki katika michezo, na kuzuru hospitali na magereza.” Padri Brian Lucas, msemaji wa Kanisa Katoliki la Sydney, alisema kwamba watawa wa kike na mapadri kwa kawaida walionyeshwa wakiwa wanabeba mishumaa na kusimama chini ya minara ya kanisa na kwamba kampeni hiyo ingesaidia wengine wawaone kuwa watu wa kawaida. Matangazo hayo yanaonyeshwa katika Melbourne na kisha yataenezwa katika majimbo mengine yakifaulu.