Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 12/22 kur. 23-24
  • Sanda ya Turin—Je, Ni Nguo ya Yesu ya Maziko?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sanda ya Turin—Je, Ni Nguo ya Yesu ya Maziko?
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ufafanuzi wa Kihistoria
  • Maoni Mbalimbali
  • Je, Sanda ya Turin Ndicho Kitambaa Ambacho Yesu Alifungwa Alipozikwa?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Muono-Ndani Juu ya Habari
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Kutembelea Majiji Yenye Kuvutia ya Milan na Turin
    Amkeni!—2001
  • Hadi Ufufuo Utakapokuwa Halisi
    Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha Yetu ya Kikristo—2022
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 12/22 kur. 23-24

Sanda ya Turin—Je, Ni Nguo ya Yesu ya Maziko?

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA ITALIA

Kutoka Aprili 18 hadi Juni 14, 1998, sanda au nguo, iliyosemwa kuwa iliufunga mwili wa Yesu wa Nazareti baada ya kifo chake ilionyeshwa katika Italia kwenye Kanisa Kuu la San Giovanni Battista, katika Turin. Iliwekwa katika sanduku la kioo lisiloingia hewa, lisilopenya risasi lililojazwa gesi bwete. Ikiwa hapo ilidumishwa kwenye hali zilizo imara.

WAGENI walipita mbele ya sanda hiyo yenye kulindwa vema katika njia tatu za kupitia zilizo kwenye usawa usiolingana. Hilo lilifanya wote waweze kuona vizuri. Ziara hizo zilikuwa za muda wa dakika mbili nazo zilikuwa kwa waliowekewa nafasi tu. Kulikuwa na hisia-moyo tofauti-tofauti, zile za upeo wa furaha, kutafakari kwa machozi mpaka zile za udadisi tu. Kuliripotiwa wageni wapatao milioni 2.5.

“Sanda hiyo yamaanisha nini kwako?” lilikuwa swali lililoulizwa mara nyingi. Kwa mtu yeyote anayependelea kuzungumza juu ya dini, pindi hiyo iliandaa fursa ya kuchunguza jambo hilo zaidi sana na kuzisoma kurasa za Biblia zinazorejezea maziko ya Yesu.—Ona sanduku kwenye ukurasa unaofuata.

Sanda hiyo ni nguo ya kitani yenye urefu wa sentimeta 436 na upana wa sentimeta 110 iliyo na chapa ya juujuu ya mwili wa mwanamume ambaye, yadaiwa kwamba alikabiliwa na kifo chenye jeuri. Lakini swali ni hili, Je, Sanda ya Turin ndiyo iliyotumiwa kufunga mwili wa Yesu zaidi ya karne 19 zilizopita?

Ufafanuzi wa Kihistoria

“Hakuna uthibitisho wa sanda katika karne za kwanza za enzi ya Kikristo,” chasema kitabu New Catholic Encyclopedia. Katika 544 W.K., chapa inayosemekana kwamba haikufanywa kwa mikono ya binadamu ilionekana katika Edessa, sehemu iliyo katika Uturuki ya siku ya kisasa. Chapa hiyo ilisemekana kwamba ilikuwa ikionyesha uso wa Yesu. Katika 944 W.K., ilidaiwa kwamba chapa hiyo ilikuwa Constantinople. Hata hivyo, wanahistoria wengi hawaamini hiyo ilikuja kuwa ile ijulikanayo kuwa Sanda ya Turin.

Katika karne ya 14, huku Ufaransa, sanda ilimilikiwa na Geoffroi de Charny. Katika 1453, ilimilikiwa na Louis, Dyuki wa Savoy, ambaye aliihamisha kwenye kanisa katika Chambéry, jiji kuu la Savoyard. Kutoka huko, katika 1578, Emmanuel Philibert aliipeleka Turin.

Maoni Mbalimbali

Katika 1988 aliyekuwa askofu mkuu wa Turin, Anastasio Ballestrero, aliamuru Sanda ya Turin ichunguzwe kwa kupima kiasi cha kaboni ili kujua umri wake. Uchunguzi huo, uliofanywa na maabara tatu zenye hadhi kubwa katika Uswisi, Uingereza, na Marekani, ulionyesha sanda hiyo kuwa ya enzi za kati, hivyo ikiwa ya kipindi kirefu baada ya kifo cha Kristo. Ballestrero alikubali mkataa huo, akitangaza hivi katika taarifa rasmi: “Katika kukabidhi sayansi kadirio la matokeo haya, kanisa laonyesha tena staha yake na heshima yake kwa sanamu hii ya kuheshimika ya Kristo, ambayo yabaki kuwa chombo cha ujitoaji kwa aliye mwaminifu.”

Askofu mkuu wa sasa, Giovanni Saldarini alitangaza hivi: “Hatuwezi kusema kwamba mfano huo ni mfano wa Kristo ulioteremshwa kutoka msalabani.” Hata hivyo, wakati uleule, alisisitiza: “Hakuna shaka kwamba mwamini anaweza kuona katika hiyo chapa sanamu ya mwanamume anayefafanuliwa na Gospeli.” Mei 24, 1998, wakati sanda hiyo ilipokuwa ikionyeshwa, Papa John Paul wa Pili aliuita mfano huo “chapa iliyoachwa na mwili ulioteswa wa Yule Aliyesulubiwa.”

Kama iwezavyo kuonekana, kuna uthibitisho mkubwa sana unaopinga Sanda ya Turin kuwa nguo ya Yesu ya maziko. Lakini namna gani kama ingekuwa ndiyo yenyewe? Je, ingefaa mtu anayetaka kutii mafundisho ya Biblia aheshimu nguo hiyo?

Fikiria amri ya pili kati ya zile Amri Kumi, ambayo husema, kulingana na tafsiri ya Biblia ya Katoliki: “Hutajifanyia mwenyewe mfano wa kuchongwa au chochote kinachofanana na kitu chochote mbinguni juu au duniani chini au katika maji chini ya dunia. Hutavisujudia.” (Kutoka 20:4, 5, New Jerusalem Bible) Kwa kweli, Wakristo wa kweli hutii maneno haya ya mtume Paulo: “Tunatembea kwa imani, si kwa kuona.”—2 Wakorintho 5:7; 1 Yohana 5:21.

[Sanduku katika ukurasa wa 24]

Sanda na Masimulizi ya Gospeli

Waandishi wa Gospeli husema kwamba mwili wa Yesu, baada ya kutolewa kwenye mti wa mateso na Yosefu wa Arimathea, ulikuwa umefungwa “kitani safi bora.” (Mathayo 27:57-61; Marko 15:42-47; Luka 23:50-56) Mtume Yohana aongezea hivi: “Nikodemo pia . . . alikuja akileta kikuto cha manemane na udi, karibu ratili mia zayo. Basi wakauchukua mwili wa Yesu na kuufunga kwa mabendeji pamoja na manukato, sawa na jinsi Wayahudi walivyo na desturi ya kutayarisha kwa ajili ya maziko.”—Yohana 19:39-42.

Ilikuwa desturi ya Wayahudi kuosha wafu kisha kutumia mafuta na manukato kuupaka mwili. (Mathayo 26:12; Matendo 9:37) Asubuhi iliyofuata Sabato, marafiki za Yesu wa kike walikusudia kukamilisha matayarisho ya mwili wake, ambao tayari ulikuwa umelazwa ziarani. Hata hivyo, walipowasili na ‘manukato yao kumpaka,’ mwili wa Yesu haukuwako ziarani!—Marko 16:1-6; Luka 24:1-3.

Petro alikuta nini alipokuja muda mfupi baadaye na kuingia ziarani? Shahidi wa kujionea, Yohana, aripoti hivi: “Akaona mabendeji yamelala, pia nguo iliyokuwa imekuwa juu ya kichwa chake ikiwa haipo pamoja na mabendeji bali imebiringwa mahali pamoja ikiwa pekee.” (Yohana 20:6, 7) Ona kwamba kitani bora haitajwi—ni mabendeji tu na nguo ya kichwa. Kwa kuwa Yohana anataja kihususa mabendeji na nguo ya kichwa, je, haingeelekea kwamba angekuwa ametaja kitani bora, au sanda, ikiwa ingekuwako?

Kwa kuongezea, fikiria hili: Ikiwa nguo za kaburini za Yesu zingekuwa na mfano wake, je, haionekani kwamba huo ungetambulika na kuwa jambo la kuzungumziwa? Hata hivyo, zaidi ya yale yaliyo katika Gospeli, Biblia haisemi kitu kabisa kuhusu nguzo za kaburini.

Hata wanaodai kuwa waandishi Wakristo wa karne ya tatu na ya nne, ambao wengi wao waliandika idadi kubwa ya ile iitwayo miujiza pamoja na masalia kadhaa, hawakutaja kuwapo kwa sanda iliyo na mfano wa Yesu. Ni vigumu kuelewa jambo hili, kwa kuwa watazamaji wa karne ya 15 na 16, kulingana na msomi Myahudi Herbert Thurston, “wanafafanua chapa zilizo kwenye sanda hiyo kuwa zenye mambo wazi na rangi nyangavu hivi kwamba yawezekana zilitoka tu kutengenezwa.”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]

David Lees/©Corbis

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki