Mediterania—Bahari Inayozingirwa Isiyo na Ulinzi
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UGIRIKI
Mizoga ya dolfini zaidi ya elfu moja irundamanayo ukingoni mwa bahari kutoka Ugiriki hadi Moroko, mawimbi ya maji mekundu yenye sumu katika bahari ya Aegea, mamilioni ya tani za povu la kinamasi katika bahari ya Adriatiki, kasa na sili walio hatarini mwa kutoweka, maeneo ya maji yasiyo na viumbe hai vyovyote. Ni kitu gani kimeipata bahari ya Mediterania? Je, wakati ujao itachafuliwa na kuangamizwa kabisa?
“ENEO la kwanza kabisa kukaliwa na wanadamu ulimwenguni.” Hivyo ndivyo mwanazuolojia David Attenborough aifafanuavyo bahari ya Mediterania na kingo zake. Ikitumiwa na mabara matatu, bahari hii ilitimiza fungu muhimu katika kuinuka na kuanguka kwa Misri, Ugiriki, na Roma. Utamaduni na ustaarabu mwingi tulio nao sasa ulitokana nayo. Hata hivyo, miongo ya karibuni ya maendeleo ya kupita kiasi, ongezeko kubwa la watalii, uvuvi wa kupita kiasi, na uchafuzi vimeihatarisha Mediterania. Wataalamu wanaojali na mataifa yanayoathiriwa yataharuki yakitafuta utatuzi, yakifanikiwa kidogo tu kufikia sasa.
Bahari ya Mediterania ndiyo bahari kubwa zaidi ulimwenguni iliyo barani. Pwani yake ya kilometa 46,000, iliyo mpaka wa asili wa nchi 20, ina wakazi zaidi ya milioni 160, idadi inayotazamiwa kuongezeka maradufu kufikia mwaka wa 2025. Ikiwa ni yenye joto na yenye chumvi kuliko bahari ya Atlantiki, ambako ndiko mengi ya maji yake yatokako, Mediterania ni bahari tulivu. Kwa kuwa maji yake hufanywa upya kila miaka 80 au 90 tu, yaweza kuchafuliwa kwa urahisi. “Chochote kinachotupwa ndani ya Mediterania hukaa humo kwa muda mrefu,” chasema kichapo National Geographic.
Watalii Waivamia
Fuo za kuota jua, mandhari zenye kuvutia, ukarimu wa watu wa ufuo wa Mediterania, na historia yenye tamaduni nyingi hufanya eneo hilo lote liwe mahali maarufu pa kwenda likizo. Kila mwaka, waenda-ufuoni milioni 100 wenyeji na watalii wageni huzuru huko, na idadi hiyo yatarajiwa kuongezeka mara tatu miaka 25 ijayo. Je, uvamizi huu wa kibinadamu unahusika kwa njia fulani katika kuharibu mahali pao pa kwenda likizo wakati wa kiangazi? Chunguza mambo ya hakika.
Magenge hayo ya wavamizi wa kibinadamu huja na takataka nyingi ambazo nchi za Mediterania haziwezi kukabili. Asilimia 80 hivi ya maji machafu wanayotokeza—zaidi ya tani milioni 500 kwa mwaka—humiminika baharini bila kutiwa dawa! Wengi wa watalii hao huja wakati wa kiangazi, wakichangia kuchafua maji ya eneo hilo ambayo tayari ni machache. Nayo, maji yaliyochafuliwa ni hatari kwa afya. Kuogelea katika sehemu fulani za bahari ya Mediterania kwaweza kutokeza maambukizo ya sikio, pua, na koo, bila kutaja magonjwa kama vile mchochota wa ini, kuhara damu na visa vya mara kwa mara vya kipindupindu.
Hata hivyo, uchumi wa nchi nyingi za Mediterania hutegemea biashara ya utalii. Akizungumza juu ya nchi hizi, Michel Batisse, aliyekuwa naibu mkurugenzi-mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni asema: “Rasilimali pekee waliyo nayo ni biashara ya utalii, lakini hiyo hutegemea kutoharibiwa kwa pwani zake kwa ujenzi wa kupita kiasi unaotokana na kutaka kupata faida haraka.”
Msongamano wa Meli za Shehena ya Mafuta
Bahari ya Mediterania ni njia kuu ya usafirishaji baina ya nchi za Mashariki ya Kati na za Ulaya, jambo lifanyizalo msongamano mkubwa wa meli za shehena ya mafuta. Zaidi ya asilimia 20 ya mafuta ya ulimwengu hupitia kwayo. Kiasi cha mafuta yanayomwagika kwenye bahari ya Mediterania kila mwaka kimekadiriwa kuwa mara 17 ya kiasi cha mafuta yaliyomwagwa na Exxon Valdez katika Alaska mwaka wa 1989. Kati ya 1980 na 1995, mafuta kutoka kwa meli 14 yalimwagika katika bahari ya Mediterania, na kila mwaka, tani zifikazo milioni moja za mafuta-ghafi humwagwa kutoka melini, mara nyingi zikisababishwa na ukosefu wa vifaa vya kuzolea mafuta au vya kusafisha meli bandarini.
Isitoshe, maji ambayo hutoka kwenye Mediterania na kuingia katika bahari ya Atlantiki kupitia Mlango-Bahari wa Gibraltar huwa ya kina sana. Kwa kuwa mafuta huelea juu ya maji, bahari hupoteza maji yake yaliyo chini zaidi na ambayo ni safi ikibakiza mkusanyo wa mafuta ukielea baharini. “Ule mlishano wa bahari wa Mediterania umechafuliwa na mafuta,” asema Colette Serruya, aliyekuwa mkurugenzi wa Taasisi ya Israel ya Elimu ya Bahari. “Mafuta hayo ni sehemu ya samaki na moluska wetu.” Mwaka wa 1990 Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) liliripoti kwamba asilimia 93 za samakigamba waliotwaliwa kutoka bahari ya Mediterania walikuwa na bakteria nyingi kwenye kinyesi chao zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa na Shirika la Afya Ulimwenguni.
Mfumikolojia Uliodhoofishwa
Zaidi ya uchafuzi huu wenye uangamivu, pwani ya Mediterania inapata dhara kubwa, ambayo sehemu yake kubwa ilikuwa yenye msitu mzito kufikia karne ya 15 W.K. Ukataji-miti ili kufanyiza mashamba, kupanua majiji, au kuandaa vifaa vya ujenzi wa majahazi ya Venisi, kumetokeza mmomonyoko wa udongo. Zaidi ya vitu vigumu vinavyosafirishwa na mvua, mito hupeleka uchafu baharini kama vile kemikali za kuua viini na wadudu, na madini nzito. Mto Rhône katika Ufaransa, Nile katika Misri, Po katika Italia, Ebro katika Hispania, na mingineyo hubeba uchafu mwingi wa ukulima na wa viwanda.
Mojawapo ya matokeo ya moja kwa moja ya uchafuzi huu ni yale mawimbi mekundu ambayo yameathiri sehemu fulani za bahari ya Adriatiki na ya Aegea, yakitokeza harufu mbaya na uchafu unaonata kwenye fuo za bahari hizo. Hali hiyo husababishwa na mata inayooza itumiapo oksijeni kutoka kwenye maji, hivyo ikimalizia hewa mimea na wanyama waliomo. Maeneo mengine yanayohatarishwa na hali hii isiyo ya kawaida ni pamoja na Ghuba ya Lions (Ufaransa), Ziwa la Tunis (Tunisia), Ghuba ya Izmir (Uturuki), na Wangwa wa Venisi (Italia).
Mfumikolojia wa pwani umedhoofika sana hivi kwamba, zile spishi ngeni katika bahari ya Mediterania zaweza kuchukua mahali pa spishi za asilia za humo. Mfano mzuri ni mwani, mmea “muuaji” uitwao Caulerpa taxifolia, uharibuo kabisa spishi nyinginezo za baharini. Baada ya kuletwa katika pwani ya Monako kwa makosa, sasa mmea huo umeanza kuenea sehemu ya chini ya bahari. Ni wenye sumu, na hakuna spishi yoyote ijulikanayo inayoweza kuuharibu, nao tayari umeenea sana. “Huu waweza kuwa mwanzo wa msiba mkubwa wa kiikolojia,” asema Alexandre Meinesz, profesa wa biolojia ya mambo ya baharini katika Chuo Kikuu cha Nice, Ufaransa.
Kuna habari zaidi iliyo mbaya. Kulingana na mwanabiolojia wa mambo ya baharini Charles-François Boudouresque, zaidi ya viumbehai 300 vigeni katika maisha ya baharini vimeongezwa katika bahari ya Mediterania. Vingi vilitoka Bahari Nyekundu kupitia Mfereji wa Suez. Watafiti fulani waamini kwamba uchafuzi huu wa kibiolojia hauwezi kurekebika na kwamba waweza kuwa moja ya matatizo makubwa ya kiikolojia ya karne ijayo.
Kifo Majini
Mimea ya Mediterania yakabili hatari nyingi, moja yazo ikiwa kuharibiwa kwa Posidonia, nyasi ya baharini, ambayo huzungusha hewa safi, huwa chakula, na malezi ya bahari na pia kama mahali ambapo mamia ya spishi za baharini huzalia. Viunzi na gati za meli zinazoenea kufikia mazingira ya nyasi hizo, zaweza kuziharibu, na ndivyo na zile mashua za starehe, ambazo huirarua mimea hiyo kwa nanga zake.
Wanyama wa baharini wanatishwa vilevile. Aina fulani ya sili wa bahari ya Mediterania, mojawapo ya zile spishi 12 za ulimwengu zinazotishwa zaidi, yaelekea kutoweka kabisa. Kulikuwako sili wapatao 1,000 wa aina hiyo katika bahari ya Mediterania katika mwaka wa 1980, lakini wawindaji na wavuvi wameua idadi kubwa ya sili hao, na leo wamesalia sili kati ya 70 na 80 tu. Kasa aina ya loggerhead sasa hutaga mayai kwenye ufuo wa Ugiriki na wa Uturuki, ambapo mara nyingine mayai hayo hukanyagwa na watalii. Kasa hao hunaswa mara nyingi kwenye nyavu za kuvulia samaki na mwishowe kuliwa kwenye mikahawa ya mahali hapo. Viumbe kama mantis shrimp, rough pen shell, na date mussel, sasa wao pia wamo hatarini mwa kutoweka.
Kuchukua Hatua
Ili kushughulikia hali hii ya kuhofisha, mpango uitwao Mediterranean Action Plan (MAP) ulianzishwa mwaka wa 1975 ukifadhiliwa na Shirika la UNEP. Lengo la mpango huo ni kuzifanya nchi za Mediterania, na pia washiriki wengine wa Muungamano wa Ulaya, zilinde bahari isichafuliwe na kuhakikisha kwamba kusitawi kwa mwambao wa pwani hakuhitilafiani na mazingira. Mwaka wa 1990 mradi wa Mediterranean Environmental Technical Assistance Program (METAP) ulianzishwa ukifuatiwa na METAP 2, mwaka wa 1993. Jitihada nyingine za kuanzisha hifadhi za mimea na viumbe, mbuga za kitaifa za wanyama wa baharini zimekuwa na matokeo mazuri katika kulinda dolfini, nyangumi, sili, kasa, na spishi nyingine zilizo hatarini mwa kutoweka.
Hata hivyo, ni rahisi kusema kuliko kutenda. Kufikia mwanzo-mwanzo wa miaka ya 1990 MAP ilikaribia kuanguka, kwa kuwa mataifa yenye kuchangia sana yalikosa kutoa michango yao. Kulingana na wenye mamlaka wa mradi huo, hakuna lengo hata moja la MAP ambalo lajulikana lilitimizwa. Akiripoti juu ya utayari wa mataifa ya Mediterania kuchukua hatua za kuboresha hali, Ljubomir Jeftic, naibu mkurugenzi wa MAP, alionya hivi: “Msitarajie mengi mno.” Hata nchi hizi zikikubali kutenda, huenda ikachukua makumi ya miaka kurekebisha dhara ambalo limetokea tayari. Gazeti New Scientist lataarifu hivi: “Sasa hivi, sawa na wanyama wa porini wa eneo la Mediterania, mpango wa MAP waonekana ukiwa mfu.”
Basi, bahari ya Mediterania itapatwa na nini wakati ujao? Je, itakuwa bahari isiyo na uhai, iliyojaa mwani wenye matope, unaovunda? Huenda itakuwa hivyo iwapo wakati wake ujao wategemea mwanadamu tu. Hata hivyo, Muumba wa dunia, Yehova Mungu, huijali ‘bahari aliyoifanya.’ (Zaburi 95:5) Yeye ameahidi kwamba karibuni “[ata]waleta kwenye uangamizi wale wanaoiangamiza dunia.” (Ufunuo 11:18) Baada ya kuondolewa kunakostahili kwa wanadamu wasiowajibika wachafuao bahari na vinginevyo, Mungu atarudisha usawa wa ikolojia na unamna-namna wa viumbe kwetu duniani. Kisha, “bahari na vyote viendavyo ndani yake” ‘zitamsifu’ pamoja na hali zao za asili, zisizochafuliwa bado.—Zaburi 69:34.
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 15]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
ATLANTIKI
URENO
HISPANIA
MOROKO
UFARANSA
MONAKO
ALGERIA
TUNISIA
SLOVENIA
ITALIA
KROATIA
YUGOSLAVIA
ALBANIA
MALTA
UGIRIKI
UTURUKI
LIBYA
MISRI
SAIPRASI
SIRIA
LEBANONI
ISRAELI
[Picha katika ukurasa wa 16]
Maendeleo ya kupita kiasi yametokeza uchafuzi
Lloret de Mar, Costa Brava, Hispania
Hoteli zilizoko Benidorm, Hispania
[Picha katika ukurasa wa 16]
Bahari ya Hispania iliyochafuliwa na (chini) mafuta yaliyomwagika Genoa, Italia
[Hisani]
V. Sichov/Sipa Press
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kasa aina ya loggerhead wamo katika hatari ya kuangamizwa
Sili wa Mediterania wanaelekea kutoweka
[Hisani]
Kasa: Tony Arruza/Corbis; Sili: Panos Dendrinos/HSSPMS