Je, Ni Sili wa Maji-Ujotojoto?
SILI huonyeshwa mara nyingi wakiwa katika mitandao myeupe ya barafu ya maji ya Arktiki au Antarktiki. Lakini je, ulijua kwamba sili wengine waweza kuendelea vizuri katika tabia-anga yenye ujotojoto wa kadiri, huku wakiota jua katika mchanga wa fuo zilizoachwa?
Huyu hapa ni sili mtawa-mume wa Mediterranea. Akiwa ni mwenye urefu wa meta 3.5, sili huyu wa maji-ujotojoto ana nywele fupi nene, zilizofunikwa kwa vipakupaku vyeusi, akiwa na tumbo na kifua cheupe-cheupe. Rangi hizi za kumpambanua, zifananazo na mavazi ya wanadini wa madaraja fulani, huenda zikaeleza ni kwa nini yeye huitwa jina lile.
Vifungu kadhaa vya Biblia hutaja ngozi iitwayo taʹchash (kwa Kiebrania), iliyofunika tabenakulo na vyombo katika patakatifu. (Kutoka 25:5; 26:14; Hesabu 4:8, NW) Wastadi fulani wadokeza kwamba taʹchash hurejezea ngozi ya sili. Je, ingeweza kuwa ni ngozi ya yule sili mtawa-mume wa Mediterranea? Kuwapo kwa mnyama huyu katika maji ya Mediterranea ya kale kwafanya dhana hii iwe halali.
Ngano za watu wa kale zilimhesabia sili mtawa-mume kuwa na nguvu maalumu. Wengine waliamini kwamba ngozi yake ingeweza kuepusha kando mipigo ya radi na kuzuia mvua-mawe isipige mashamba yaliyositawishwa. Kwa kusimama wima, au kulala tambarare, nywele za ngozi ya sili zilisemwa kuonyesha mwanzo au umalizio unaokaribia wa ngurumo ya radi.
Kwa sababu ya nguvu alizodhaniwa kuwa nazo, sili mtawa-mume alikaribia kufanywa atokomee kabisa na wawindaji wasio na rehema. Hata hivyo, hivi majuzi ameonekana baharini karibu-karibu na mashariki-kati ya Sardinia. Wakati upatano utakapoimarishwa kati ya mwanadamu na mnyama katika ulimwengu mpya wa Mungu, sili mtawa-mume wa Mediterranea bila shaka atamiliki tena fuo zenye utulivu na amani, ambako ataweza kuota jua bila kutishwa na wanadamu wenye pupa.—Isaya 11:6-9.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Panos Dendrinos/HSSPMS