Kukumbuka Wakati Uliopita Wenye Kuchukiza wa Utumwa
KARIBU tu na pwani ya nchi ya Afrika ya Senegal, karibu na jiji la Dakar, kuna kisiwa cha Île de Gorée. Kwa miaka 312, iliyofikia mwaka wa 1848, kisiwa hiki kilikuwa kituo cha biashara iliyonawiri ya kuuza wanadamu. Nyaraka kutoka bandari ya Ufaransa ya Nantes zaonyesha kwamba kati ya mwaka wa 1763 na 1775 peke yake, zaidi ya watumwa 103,000 waliuzwa kutoka kisiwa cha Gorée kupitia bandari ya Nantes.
Leo, wastani wa wageni wapatao 200 kwa siku huzuru Maison des Esclaves, lile Jumba la Makumbusho la Utumwa. Kiongozi wa watalii Joseph Ndiaye alisimulia baadhi ya mambo ya kuchukiza yaliyowapata wahasiriwa waliokuwa hoi: “Wazazi wetu wa kale walihamishwa, familia zao zikatenganishwa, na kama ng’ombe, wakatiwa alama kwenye ngozi kwa chuma moto.” Familia nzima-nzima zililetwa zikiwa zimefungwa minyororo. “Huenda mama akapelekwa Marekani, naye baba Brazili, nao watoto huko Antilles,” akasimulia huyo kiongozi.
“Baada ya kupimwa uzito,” Ndiaye aeleza, “thamani ya wanaume ilikadiriwa kulingana na umri wao na asili yao, huku wanaume wa makabila fulani wakigharimu fedha nyingi kwa sababu ya ukakamavu wao au kwa sababu walidhaniwa kuwa hodari katika kuzaa watoto. Kwa mfano, wanaume Wayoruba walionwa kuwa hodari kwa kuzaa.
Mateka waliokonda walinenepeshwa kama nguruwe kabla ya kupigwa mnada. Wachuuzi wa watumwa waliwachagua wanawake vijana ili wawatumie kingono kila usiku. Watumwa walioasi walining’inizwa kifuani badala ya shingoni, ili kuzidisha maumivu makali waliyopata.
Papa John Paul wa Pili alizuru Gorée mwaka wa 1992. Gazeti The New York Times liliripoti kwamba “aliomba radhi kwa sababu ya biashara ya watumwa, huku akiomba msamaha kwa ajili ya wote walioshiriki katika biashara hiyo, kutia ndani wamishonari Wakatoliki waliokubali utumwa wa Waafrika kuwa jambo la kawaida.”
Hata hivyo, si kila mtu yuko tayari kukiri kilichotendeka. Miaka miwili na nusu iliyopita, kabla ya kufukuliwa kwa rekodi za Nantes, Myesuiti mmoja Mfaransa alidai kwamba ni watumwa 200 hadi 500 tu waliokuwa wakiuzwa kila mwaka Gorée. Hadi leo, Bw. Ndiaye aonelea hivi, “ulimwengu haujakubali kamwe ubaya wenye kuchukiza sana wa uovu huu.”
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Gianni Dagli Orti/Corbis
Yann Arthus-Bertrand/Corbis
Reproduced from DESPOTISM—A Pictorial History of Tyranny