Babu na Nyanya Walio “Tofauti”
“Karibu nyumbani kwa Babu na Nyanya—Watoto Waendekezwa Unapongoja.” Ndivyo isemavyo ishara kwenye mwingilio wa makao ya Gene na Jane.
HATA hivyo, unapoingia ndani, hutawapata wenzi wazee-wazee wakiketi kwenye viti vya kubembea. Badala yake, utaona wenzi wa ndoa wenye nguvu wakiwa na umri wa miaka 40 hivi. Pasipo kuepuka madaraka yao wakiwa ‘viongozi wazee,’ Gene na Jane wamekubali kwa furaha kuwa nyanya na babu. “Kweli, hali ya kuwa babu na nyanya ni mojawapo ya ishara ndogo maishani inayoonyesha kwamba unazidi kuzeeka,” asema Gene, “lakini hii ni mojawapo ya thawabu, za kulea watoto wako—wajukuu.”
Mithali moja ya kale yasema: “Wana wa wana ndio taji ya wazee.” (Mithali 17:6) Mara nyingi babu na nyanya na wajukuu hufurahia kifungo cha kipekee cha upendo na uhusiano wa karibu. Na kulingana na jarida Generations, “watu wengi sana katika jamii ya Kimarekani ni babu na nyanya.” Sababu ni nini? “Watu wanaishi maisha marefu zaidi na kutokea kwa mitindo mipya katika maisha ya watu,” yaeleza makala hiyo. “Mabadiliko katika hali ya kufa na uwezo wa kuzaa yanamaanisha kwamba idadi inayokaribia robo tatu ya watu wazima wataishi kufikia kuwa babu na nyanya . . . Watu wengi wa umri wa makamu huwa babu na nyanya wanapokuwa na umri wa miaka 45 hivi.”
Kizazi cha babu na nyanya walio tofauti kimeibuka katika nchi fulani. Ingawa hivyo, wengi wanazidi kujipata wakihusika katika kuwatunza wajukuu wao. Kwa kielelezo, mwana wa Gene na Jane na mkwe wao wa zamani wametalikiana na wanashirikiana katika kumlea mtoto. “Tunajaribu kusaidia kutunza mjukuu wetu wa kiume huku mwana wetu akifanya kazi,” aeleza Jane. Kulingana na uchunguzi mmoja, babu na nyanya huko Marekani wanaowatunza wajukuu wao hutumia kwa wastani muda wa saa 14 kwa juma katika kazi hiyo. Muda huu unakuwa sawa na kufanya kazi yenye malipo ya dola bilioni 29 kwa mwaka!
Babu na nyanya wa siku hizi hupata shangwe zipi? Wanakabili magumu gani? Makala zinazofuata zinachunguza maswali haya.