Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 4/22 kur. 16-19
  • Mlima Sinai—Kito Kilicho Nyikani

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mlima Sinai—Kito Kilicho Nyikani
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuuchunguza Mlima
  • Kukwea Ras Safsafa Ulio Karibu
  • Ndani ya Nyumba ya Watawa
  • Kuagana kwa Huzuni
  • Kuiponyosha Codex Sinaiticus
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Sinai Mlima wa Musa na wa Rehema
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Kugunduliwa Kwa Hazina ya Biblia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
  • Patmosi—Kisiwa cha Apokalipsi
    Amkeni!—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 4/22 kur. 16-19

Mlima Sinai—Kito Kilicho Nyikani

SITASAHAU kamwe msisimuko niliohisi nilipouona Mlima Sinai wa kale kwa mara ya kwanza. Tulipokuwa tukipita katika nchi iliyo na joto, na vumbi jingi ya Peninsula ya Sinai huko Misri, kwa ghafula gari letu lilitokezea kwenye uwanda mpana uitwao Uwanda wa er-Raha. Mlima Sinai wenye kutia kicho umeinuka sana kutoka kwenye sakafu ya uwanda. Ulikuwa kama kito, kilichowekwa nyikani. Ilisisimua kuwazia kwamba huenda huu uwe mlima wenyewe ambapo Musa alipokea Sheria kutoka kwa Mungu!

Ingawa kungali kuna ubishi juu ya mahali barabara pa Mlima Sinai unaotajwa katika Biblia, wasafiri wamekuwa wakija hapa kwa karne nyingi kwa sababu wanaamini kwamba huu ndio ule mlima maarufu. Huko nyuma katika karne ya tatu W.K., watawa wa kidini walifika, wakiwa na kusudi la kujitenga wenyewe ili kutafakari mambo ya kidini. Katika karne ya sita, Maliki Jus­tinian wa Kwanza wa Byzantium aliamuru kwamba nyumba ya watawa ijengwe hapa ili kuwalinda watawa hao, na vilevile kuhakikisha kuwapo kwa Waroma katika eneo hilo. Nyumba hiyo ya watawa iliyoko chini ya Mlima Sinai wa kale, sasa inaitwa St. Catherine. Mbona usiandamane nami ninapozuru Mlima Sinai?

Kuuchunguza Mlima

Baada ya kusafiri kupitia bonde lililokauka nikiwa na mwandamani wangu, tunafika chini tu ya nyumba hiyo ya watawa ambako tunashukishwa kutoka kwenye teksi inayoendeshwa na Mbedui. Mandhari yamefanyizwa kwa majabali, nasi tunavutiwa sana na kuta zenye miti za nyumba hiyo ya watawa na bustani inayositawi. Hata hivyo tunaipita nyumba hiyo, kwa kuwa lengo letu kubwa ni kukwea na kupiga kambi usiku katika kilele kilichoko upande wa kusini. Kilele hiki, kiitwacho Gebel Musa, jina limaanishalo “Mlima wa Musa,” huhusianishwa kwa kawaida na Mlima Sinai.

Baada ya kutembea kwa muda wa saa mbili tunafika katika bonde dogo linaloitwa Bonde la Eliya, linalougawanya mara mbili mgongo wa Mlima Sinai wenye urefu wa kilometa tatu. Kulingana na mapokeo, Eliya alisikia sauti ya Mungu alipokuwa katika pango lililopo hapa. (1 Wafalme 19:8-13) Tunatua kidogo ili tupumzike chini ya mteashuri wenye miaka 500. Hapa pia pana kisima cha kale. Jinsi tunavyofurahia maji yake safi, baridi, tuliyopewa na Mbedui mmoja mwenye urafiki!

Kwa kufuata njia inayotumiwa na watalii kwa ukawaida, tunajitahidi kwa dakika 20 zaidi kupanda vile vidato 750 vya mawe hadi kwenye kilele. Hapo tunapata kanisa dogo. Watawa wanadai kwamba kanisa hilo limejengwa mahali hususa ambapo Musa alipewa Sheria. Pana ufa kwenye mwamba unaopakana na kanisa hilo na wanadai kwamba hapo ndipo Musa alipojificha Mungu alipokuwa akipita. (Kutoka 33:21-23) Lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu awaye yote anayejua mahali hususa ambapo matukio hayo yalitukia. Vyovyote vile, mwono kutoka juu ya mlima unastaajabisha! Tunatazama ng’ambo na kuona safu baada ya safu ya milima ya matale yenye rangi nyekundu ikiishia nyuma ya uwanda ulio chini na uliotapakaa miamba. Upande wa kusini-magharibi kuna Gebel Katherina, au Mlima Catherine—wenye kimo cha meta 2,637, na ambacho ni kilele cha eneo hili.

Kukwea Ras Safsafa Ulio Karibu

Siku nyingine hutokeza fursa ya kukwea Ras Saf­sa­fa ambacho ni kilele kilichoko kwenye mgongo uleule wa kilometa tatu ambao una Gebel Musa. Ras Saf­sa­fa ndicho kilele cha kaskazini, na ni kifupi kidogo kuliko Gebel Musa. Ras Safsafa huinuka wima kutoka kwenye Uwanda wa er-Raha, ambapo huenda Waisraeli walipiga kambi Musa alipoenda kupokea Sheria kutoka kwa Yehova.

Tunapokwea kuelekea Ras Safsafa kupitia nchi yenye vilima na mabonde madogo, tunapita vikanisa vilivyoachwa, bustani, na chemchemi—mabaki ya vitu vya wakati ambapo watawa zaidi ya mia moja walikuwa wakiishi katika sehemu hii kwenye mapango na katika vyumba vidogo vya mawe. Sasa kuna mtawa mmoja tu aliyebaki.

Tunakutana na mtawa huyo katika bustani iliyozingirwa kwa ua mrefu wa seng’enge. Anapoturuhusu kuingia, anaeleza kwamba amekuwa akifanya kazi kwenye bustani hii kwa miaka mitano, huku akienda kwenye nyumba ya watawa mara moja tu kila juma. Mtawa huyo anatuelekeza kwenda Ras Safsafa, nasi tunafuata njia yenye kupinda inayoelekea juu ya mlima, na hatimaye, tunafika katika kilele kirefu kupita vilele vinginevyo katika sehemu hii. Tunaona Uwanda wa er-Raha ulio mpana chini yetu. Na hasa nikiwa mahali hapa pafaapo, nawazia kuwa hapa ndipo mahali ambapo Musa alikwea mlima kutoka kwa kambi ya Waisraeli ili asimame mbele ya kuwapo kwa Mungu. Nawaona akilini Waisraeli milioni tatu wakiwa wamekusanyika “wakiukabili mlima” katika uwanda huo mpana. Akilini namwona Musa akishuka katika bonde lililo karibu, akiwa na yale mabamba mawili ya mawe mikononi mwake yakiwa na maandishi ya zile Amri Kumi.—Kutoka 19:2; 20:18; 32:15.

Jua lishukapo tunarejea kwa mwendo wa madaha kwenye hema letu tukiwa tumeridhika kwamba jitihada yetu ya kukwea imekuwa yenye faida. Kwa nuru ya moto mdogo, tunasoma sehemu za kitabu cha Kutoka zinazoeleza mambo aliyojionea Musa katika eneo hili, kisha tunaenda kulala. Kesho yake, kipindi cha asubuhi kikiwa kimeendelea sana, tunabisha mlango wa nyumba ya watawa ya St. Catherine.

Ndani ya Nyumba ya Watawa

St. Catherine huonwa kuwa mojawapo ya sehemu muhimu sana katika Jumuiya ya Wakristo. Huku ikitunzwa na watawa wa kanisa Othodoksi la Ugiriki, hiyo ni maarufu si kwa sababu tu ya mahali ilipo bali pia kwa sababu ya sanamu zake na maktaba yake. Katika historia yake yote, St. Catherine ilikuwa imejitenga sana hivi kwamba watawa waliwapenda sana wageni kwa sababu hawakuja kwa ukawaida. Watawa wangewakumbatia wageni wao, kuwabusu kwa uchangamfu, na hata kuwaosha miguu. Wageni wangezurura kwa uhuru ndani ya majengo mengi yaliyo ndani ya kuta zenye kimo cha futi 45 za nyumba ya watawa. Watawa walisema kwa upole na kwa kurudia-rudia ‘kaa hapa kwa juma moja, kwa mwezi mmoja, au kwa muda wote ule upendao.’ Hata hivyo, siku hizi, ukaribishaji-wageni wa watawa 12 hivi wanaobaki unatahiniwa sana. Siku hizi wageni wapatao 50,000 huzuru nyumba hiyo ya watawa kila mwaka.

Kwa sababu ya umati huu, muda wa kuzuru umepunguzwa hadi saa tatu kwa siku, siku tano kwa juma. Watalii wanaweza kuzuru sehemu chache sana za nyumba ya watawa—ua lenye Kisima cha Musa (kulingana na mapokeo hapo ndipo Musa alikutana na yule ambaye baadaye alikuja kuwa mke wake), na pia Church of the Trans­fig­u­ration (linalosemekana kuwa kanisa la kale zaidi ulimwenguni lenye kutenda), na duka la vitabu. Watalii pia huonyeshwa Chapel of the Burning Bush—watawa huwaambia watalii kwamba hapo ndipo mahali hususa ambapo Musa alishuhudia kwa mara ya kwanza kuwapo kwa Mungu. Kwa kuwa watawa hupaona hapa kuwa mahali patakatifu zaidi duniani, wageni huombwa wavue viatu vyao, kama vile Mungu alivyomwelekeza Musa afanye.—Kutoka 3:5.

Tumevunjika moyo kwa sababu ya kunyimwa ruhusa ya kutazama maktaba maarufu ya nyumba ya watawa, ambayo ndiyo hasa tulitaka kuona hapa. Ombi letu la kupewa ruhusa linakataliwa na kiongozi anayesema: “Haiwezekani! Nyumba hii itafungwa baada ya dakika chache.” Hata hivyo, baada ya muda mfupi, tuwapo mbali na kikundi cha kitalii, kiongozi atunong’onezea: “Njooni upande huu!” Tunapita chini ya kamba, kisha tunapanda ngazi, na kumpita mtawa Mfaransa anayeshangaa kutuona hapo, ndipo tufikapo katika mojawapo ya maktaba za kale zaidi na zilizo maarufu zaidi ulimwenguni! Ina vitabu zaidi ya 4,500, katika Kigiriki, Kiarabu, Kiasiria, na Kimisri. Wakati fulani, ilikuwa pia na Codex Sinaiticus yenye thamani sana.—Ona sanduku kwenye ukurasa wa 18.

Kuagana kwa Huzuni

Ziara yetu yamalizikia nje ya kuta za nyumba ya watawa tunapozuru nyumba ya kuhifadhia mifupa. Mifupa mingi ya vizazi vya watawa hurundikwa humu, ikiwa imetengwa katika marundo ya mifupa ya miguu, mifupa ya mikono, mafuvu ya vichwa, na kadhalika. Mafuvu ya vichwa yamerundamana karibu kufikia dari. Kwa nini mahali hapa pa kutisha panaonwa kuwa muhimu? Watawa wana eneo dogo sana la makaburi. Kwa hivyo mmoja wao anapokufa, inakuwa desturi yao kufukua kaburi moja la kale zaidi ili kuondoa mifupa na kwa njia hiyo wanafanyiza mahali pa kumzika aliyekufa. Kila mtawa anatazamia kwamba siku moja mifupa yake itakuwa pamoja na ile ya wenzake katika ile nyumba ya kuhifadhia mifupa.

Hivyo ziara yetu yamalizika kwa njia yenye kuhuzunisha kwa kadiri fulani. Lakini kwa hakika imestahili jitihada zetu zote. Tumefurahia kuona mandhari yenye kustaajabisha na ile nyumba maarufu ya watawa. Lakini tuondokapo, tunavutiwa sana na wazo la kwamba labda tumetembea kwenye vijia ambavyo Musa na taifa la Israeli walipitia yapata miaka 3,500 iliyopita hapa katika Mlima Sinai—kito kilicho nyikani.— Imechangwa.

[Sanduku katika ukurasa wa 18]

Ugunduzi wa Maana Sana

Katika karne iliyopita, msomi wa Biblia Mjerumani Konstantin von Tischendorf aligundua katika nyumba ya watawa ya St. Catherine hati ya Biblia ya Kigiriki ya karne ya nne, inayoitwa sasa Codex Sinaiticus. Inatia ndani mengi ya Maandiko ya Kiebrania, kutoka katika tafsiri ya Kigiriki ya Septuagint, na pia Maandiko yote ya Kigiriki. Hati hiyo ni mojawapo ya nakala kamili za kale zaidi kuwahi kupatikana za Maandiko ya Kigiriki.

Tischendorf alitaka kuchapisha mambo yaliyokuwa katika “kito hiki kisicho na kifani,” kama alivyoiita. Kulingana na Tischendorf, aliwadokezea watawa kwamba zari wa Urusi alipaswa kupewa hati hiyo—ambaye, akiwa mteteaji wa Kanisa Othodoksi la Ugiriki, angeweza kutumia uvutano wake kuisaidia nyumba ya watawa.

Kwenye ukuta wa nyumba ya watawa kuna tafsiri ya barua aliyoiacha Tischendorf, akiahidi ‘kuirudisha hati hiyo kwa Holy Confraternity ya Mlima Sinai, ikiwa imehifadhiwa katika hali nzuri na bila kuharibiwa, punde tu watoapo ombi lao.’ Hata hivyo, Tischendorf, alihisi kwamba watawa hao hawakuthamini umuhimu mkubwa wa hati hiyo wala uhitaji wa kuichapisha. Haijarudishwa St. Catherine. Ijapokuwa hatimaye watawa hao walikubali rubo 7,000 kutoka kwa serikali ya Urusi kwa ajili ya hati hiyo, hadi leo wanashuku sana majaribio ya wasomi ya kufunua hazina zao. Hatimaye ­Codex ­Si­naiticus ilifika katika Jumba la Makumbusho la Uingereza, ambako yaweza kuonwa leo.

Jambo lenye kutokeza hata zaidi ni kwamba makasha 47 ya sanamu na hati za ngozi yaligunduliwa mnamo mwaka wa 1975 chini ya ukuta wa kaskazini wa St. Catherine. Ugunduzi huo ulitia ndani zaidi ya kurasa 12 za Codex Sinaiticus zilizokosekana. Hadi leo, watu wote hawaruhusiwi kuziona kurasa hizo isipokuwa wasomi wachache sana.

[Ramani katika ukurasa wa 17]

Mlima Sinai

[Hisani]

NASA photo

Mountain High Maps® Copyright ©1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Uwanda wa er-Raha, na Ras Safsafa

[Hisani]

Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Gebel Musa na nyumba ya watawa ya St. Catherine

[Hisani]

Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.

Photograph taken by courtesy of the British Museum

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki