Mandhari Kutoka Bara Lililoahidiwa
Sinai Mlima wa Musa na wa Rehema
UNAPOFIKIRIA Mlima Sinai, labda wamkumbuka Musa. Kwa nini? Kwa sababu Musa alipokea Sheria ya Mungu kwenye mlima uliokuwa kwenye Peninsula ya Sinai. Mlima upi? Labda sana ule unaoonyeshwa juu.a
Katika sehemu ya kusini mwa peninsula hiyo, karibu katikati ya milango inayoingia Bahari Nyekundu, kuna mwinuko wenye vilele viwili. Mahali hapo kwa ujumla hufaana na masimulizi ya Kibiblia yanayomhusu Musa. Kilele kimoja kinaitwa Jebel Musa, linalomaanisha “Mlima wa Musa.”
Masimulizi mbalimbali ya Kibiblia hufanya jina hilo lifae sana. Je! wakumbuka kwamba Musa alikuwa akichunga kundi la mifugo la Yethro wakati malaika mmoja alipotokea katika kichaka chenye kuwaka moto? Hapo palikuwa wapi? Biblia husema kwamba palikuwa penye ‘mlima wa Mungu wa kweli, Horebu,’ ambao huitwa pia Mlima Sinai. (Kutoka 3:1-10; 1 Wafalme 19:8) Baada ya Musa kuwaongoza watu wa Mungu kutoka katika Misri, aliwaleta hapo. Kutoka 19:2, 3 husema kwamba “Israeli [walipiga] kambi huko wakiukabili mlima. Musa akapanda kwa Mungu, na BWANA [Yehova, NW] akamwita toka mlima ule.”
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Musa kupanda Mlima Sinai, naye hakutembea mwendo mfupi tu kwenye miteremko. Tunasoma hivi: “BWANA [Yehova, NW] akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; BWANA [Yehova, NW] akamwita Musa aende hata kilele cha mlima.”—Kutoka 19:20.
Maelfu ya watalii wa ki-siku-hizi wamejitahidi kuvipanda vijia ambavyo vimetiwa alama wakati wa usiku ili kufika kilele, wamekawia-kawia ili kuona macheo ya jua, na kisha kushuka chini kufikia adhuhuri. Sivyo na Musa. Mungu alimwambia: “Njoo huku juu kwangu mlimani, uwe huku; nami nitakupa mbao za mawe na ile sheria.” Katika pindi hiyo “Musa akawa humo katika ule mlima siku arobaini, mchana na usiku.”—Kutoka 24:12-18.
Kwa hiyo inaeleweka kwamba jina la Musa linafungamanishwa na mlima huo, lakini kwa nini “rehema” itiwe ndani? Musa alipokuwa hapo juu akipokea ile sheria, watu waliokuwa kwenye uwanda wa chini (labda kwenye ule Uwanda wa er-Raha uliomo ndani ya picha) walichukua hatua ya kipumbavu. Walimsonga ndugu wa Musa atengeneze mungu. Haruni alisema hivi: “Zivunjeni pete za dhahabu zilizo katika masikio . . . mkaniletee.” Hivyo walifanyiza ndama wa dhahabu kwa ajili ya ibada. Hilo lilimghadhabisha Mungu wa kweli likaongoza kwenye vifo vya maelfu. (Kutoka 32:1-35) Lakini Haruni alionyeshwa rehema akahifadhiwa. Kwa nini?
Elezo la Mungu kwenye Kutoka 32:10 hudokeza kwamba Mungu hakumwona Haruni kuwa ndiye mwanzilishi mkuu wa kosa la Israeli. Na wakati wa kutoa adhabu ulipofika, “wana wa Lawi wote” walichagua upande wa Mungu, Haruni akiwa miongoni mwao bila shaka. (Kutoka 32:26) Kwa hiyo ingawa Haruni alikuwa na hatia fulani, alipokea rehema ya Mungu chini ya Mlima Sinai.
Baadaye, Musa alionyesha tamaa ya kumjua Yehova vizuri zaidi na kuona utukufu Wake. (Kutoka 33:13, 18) Ingawa Musa hakuweza kuuona uso wa Mungu, Yehova alimwonyesha kadiri fulani ya utukufu wake, akikazia kwamba Yeye ‘atamrehemu yeye atakayemrehemu.’ (Kutoka 33:17–34:7) Ilifaa sana kwa Mungu kukazia rehema yake, kwani Biblia hutumia “rehema” mara nyingi zaidi kuhusu shughuli za Mungu pamoja na Israeli, ambao aliwaingiza ndani ya agano huko Sinai.—Zaburi 103:7-13, 18.
Wageni kwenye Mlima Sinai leo hupata makao ya kitawa chini ya mlima huo, ambayo yasingemkumbusha mtu hata kidogo juu ya ibada ya kweli ambayo Musa alijifunza juu yayo kwenye mlima huo. Badala yake, dini iliyomo katika makao hayo ya kitawa hukazia picha za sanamu. Ile ambayo imeonyeshwa hapa ni “Ngazi ya Paradiso.” Inategemea kitabu cha mwanamume mmoja mtawa wa Bizantini John Klimakus. Baada ya kutumia karibu miaka 40 katika chumba cha makao ya kitawa, alikuwa mkuu wa makao hayo ya kitawa akaandika juu ya ngazi ya ufananisho ya kwenda mbinguni. Lakini ebu ona kwamba makasisi wengine wanaonyeshwa wakivutwa na roho waovu kuingia mateso ya milele katika moto wa helo. Huo ni wonyesho dhahiri, lakini si wa kimaandiko!—Mhubiri 9:5, 10; Yeremia 7:31.
Kinyume cha fundisho hilo bandia, kweli ni kwamba yule Mweza Yote ni “Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli.” (Kutoka 34:6) Musa alimkaribia Mungu huyo mwenye rehema kwenye Mlima Sinai.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa picha kubwa zaidi, ona 1993 Calendar of Jehovah’s Witnesses.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.y