Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 5/8 kur. 21-24
  • Comenius—Mwanzilishi wa Elimu ya Kisasa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Comenius—Mwanzilishi wa Elimu ya Kisasa
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Malezi na Elimu
  • Kilichomfanya Aende Uhamishoni
  • “Machinjioni ya Akili”
  • Njia Mpya ya Kufundisha Yaibuka
  • Vichapo vya John Comenius
  • Ni Nini Kilichomchochea?
  • Urithi Wenye Kudumu
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—2000
  • Sitawisha Ustadi wa Kufundisha
    Faidika na Elimu ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi
  • Elimu—Itumie Kumsifu Yehova
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
  • Mashahidi wa Yehova Wana Maoni Gani Kuhusu Elimu?
    Maswali Yanayoulizwa Mara Nyingi Kuhusu Mashahidi wa Yehova
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 5/8 kur. 21-24

Comenius—Mwanzilishi wa Elimu ya Kisasa

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA JAMHURI YA CHEKI

KIWA mwalimu, John Comenius alielewa kasoro za mfumo wa shule wa karne ya 17 alimokuwa akifanya kazi. Ni kweli kwamba, hakuna mfumo wowote wa elimu uliopata kuwa bila kasoro, lakini mfumo wa shule katika karne ya 17 huko Ulaya kwa wazi ulikuwa wenye kuogofya.

Badala ya kulalamika au kulaumulaumu tu bila kuchukua hatua yoyote, Comenius aliamua kuchukua hatua. Yeye alifanya nini, na kwa nini alifanya hivyo? Zaidi ya hayo, twaweza kujifunza nini kutokana na mtu huyu anayeitwa mwanzilishi wa elimu ya kisasa?

Malezi na Elimu

John Amos Comenius (Jan Ámos Komenský, katika lugha yake ya asili ya Cheki) alizaliwa Machi 28, 1592, katika Moravia, mkoa ulioko katika nchi inayoitwa sasa Jamhuri ya Cheki. Alikuwa kitindamimba katika familia ya watoto watano, naye alikuwa mwana pekee wa wenzi wakulima waliokuwa matajiri.

Wazazi wake walikuwa washiriki wa kanisa la Unity of Brethren (ambalo baadaye liliitwa Bohemian Brethren au Moravian Church), kikundi cha kidini kilichoanza katikati ya karne ya 15 chini ya uvutano wa dhehebu la Wawaldo na baadhi ya Waleta-Mabadiliko kama vile Peter Chelčický. Baada ya kukamilisha elimu yake huko Ujerumani, Comenius alirudi katika nchi ya nyumbani. Baadaye, akiwa na umri wa miaka 24, aliwekwa rasmi kuwa kasisi wa Unity of Brethren.

Kilichomfanya Aende Uhamishoni

Mwaka wa 1618, Comenius akawa msimamizi wa parokia ndogo katika mji wa Fulnek, ulioko umbali wa kilometa 240 upande wa mashariki ya Prague. Wakati huo, upinzani wa Katoliki dhidi ya Mabadiliko ya Uprotestanti ulikuwa umeenea huko Ulaya. Uhasama kati ya Wakatoliki na Waprotestanti uliongezeka mpaka, hatimaye, ile Vita ya Miaka Thelathini ikazuka (1618-1648).

Baada ya kupigana kwa mwongo mmoja, dini Katoliki ya Kiroma ilitangazwa rasmi kuwa dini pekee iliyo halali katika Moravia. Comenius na washiriki wa matabaka ya juu walihitaji kuchagua kati ya—kukubali Ukatoliki au kuhama nchi. Kwa kuwa Comenius hakutaka kuwa Mkatoliki, yeye pamoja na familia yake walihamia ng’ambo kwenye mji mdogo wa Leszno, kituo mashuhuri cha utendaji wa dhehebu la Unity of Brethren katika Poland. Huu ulikuwa mwanzo wa uhamisho wa miaka 42. Hangerudi tena kamwe katika nchi yake ya kuzaliwa.

“Machinjioni ya Akili”

Comenius aliajiriwa kazi ya kufundisha Kilatini katika Leszno Gymnasium—shule ya matayarisho kwa wanafunzi wa chuo. Ingawa hivyo, baada ya muda mfupi, akiwa na sababu nzuri—hakupendezwa na njia zisizofaa za kufundisha zilizotumiwa.

Mfumo wa shule katika nyakati za Comenius ulikuwa wa kusikitisha. Kwa mfano, ni wanaume peke yao walioonwa kuwa wanastahili kuelimishwa, ingawa wanaume waliotoka katika familia maskini hawakuelimishwa. Mafunzo ya darasani yalikazia hasa maneno, sentensi, na sarufi ya lugha ya Kilatini. Kwa nini? Kwa sababu shule nyingi za enzi za kati zilisimamiwa na Kanisa Katoliki, ambalo lilifunza liturjia katika Kilatini. Kwa hiyo, ilikuwa muhimu kwao kufundisha Kilatini ili kuhakikisha kwamba kulikuwako wapya wanaojiandikisha kwa kazi ya upadri.

Kwa kuongezea, hawakuzingatia kuweka miradi mahususi ya elimu, wala kufundisha hakukukusudiwa kuwaongoza wanafunzi hatua kwa hatua kutoka kwa mambo sahili hadi kufikia yale yaliyo magumu kueleweka. Utiaji wa nidhamu ulifuatwa sana, nyakati nyingine ulikuwa wa kinyama, na hali ya kiadili ilikuwa mbaya sana.

Hivyo basi, haishangazi kwamba, mwelimishaji Mskoti Simon Laurie wakati mmoja aliziita shule za karne ya 17 kuwa “shaghalabaghala na ovyo kabisa” na “zisizopendeza.” Comenius alisema waziwazi hata zaidi. Aliziita shule hizo “machinjioni ya akili.”

Njia Mpya ya Kufundisha Yaibuka

Comenius hakuwa mtu wa kwanza kusema juu ya uhitaji wa mabadiliko ya kielimu. Huko Uingereza, Francis Bacon alikuwa amelaumu kukaziwa kwa lugha ya Kilatini naye akadokeza kurudishwa kwa elimu ya maumbile. Wolfgang Ratke na John Valentine Andreae wa Ujerumani pamoja na wengine walijaribu pia kuboresha hali. Hata hivyo, mawazo ya watu hawa hayakuungwa mkono na serikali.

Comenius alipendekeza mfumo ambao ungefanya kujifunza kupendeze, kusiwe kwa kuchosha. Aliuita mpango wake wa elimu pampaedia, jina limaanishalo “elimu ya ulimwenguni pote.” Mradi wake ulikuwa kuanzisha mfumo wa kufundisha hatua kwa hatua ambao ungemfurahisha kila mtu. Watoto wanapasa kufundishwa hatua kwa hatua, yeye akasema, ambapo dhana za msingi zingeongoza pole kwa pole kwa dhana zilizo ngumu zaidi kueleweka. Comenius pia alitia moyo matumizi ya lugha ya kwanza katika miaka michache ya kwanza shuleni badala ya lugha ya Kilatini.

Hata hivyo, elimu haipaswi kuwa tu ya wakati wa ubalehe lakini inapaswa iwe sehemu ya maisha ya mtu yote. Comenius aliandika kwamba kujifunza kunapaswa kuwe “kwenye kutumika kabisa, kunakopendeza kabisa, ili kufanya elimu iwe yenye kuburudisha, yaani, uwe mwanzo unaopendeza wa maisha yetu yote.” Aliamini pia kwamba shule inapaswa ikazie si kuelimishwa tu kwa akili bali kwa mtu mzima—na kwamba inapaswa itie ndani mafundisho ya kiadili na ya kiroho.

Vichapo vya John Comenius

Kichapo cha kwanza cha Comenius katika uwanja wa elimu kiliitwa The School of Infancy, kilichochapwa katika mwaka wa 1630a. Kilikusudiwa kitumiwe na akina mama na mayaya wanapowafundisha watoto nyumbani. Hiki kilifuatwa katika mwaka wa 1631 na kichapo The Gate of Languages Unlocked, ambacho kilikuwa karibu kukomesha kufundishwa kwa Kilatini. Maandishi yake yalipangwa katika safu zilizo sambamba, moja ikiwa katika Kicheki na nyingine katika Kilatini. Hivyo, lugha zote mbili zingelinganishwa kwa urahisi, jambo lililorahisisha zaidi kujifunza. Chapa yake ya kichapo hicho cha kufundishia iliyofanyiwa marekebisho, ilipokewa na wengi hivi kwamba hatimaye ilitafsiriwa katika lugha 16.

Kichapo kilichokuwa mashuhuri sana na labda sahili zaidi kuandikwa na Comenius kiliitwa The Visible World, kikiwa ni mwongozo wenye vielezi kwa watoto. Hicho pia kilikuwa muhimu sana katika historia ya elimu. Profesa wa elimu wa karne ya 20, Ellwood Cubberley, alisema kwamba kichapo hicho “hakikuwa na mshindani Ulaya kwa miaka mia moja na kumi na mitano hivi; na kilitumiwa kikiwa kitabu cha mafundisho ya kwanza kwa miaka ipatayo mia mbili.” Kwa kweli, vitabu vingi vya mafundisho na vilivyo na vielezi leo, bado hufuata muundo wa kawaida wa vichapo vya Comenius, wa kutumia vielezi vikiwa misaada ya kufundishia.

Punde si punde Comenius alisifiwa kuwa mtu mwenye kipaji. Kotekote Ulaya wasomi walimwona kuwa kiongozi nao walimwendea ili kupata shauri. Kulingana na kitabu Magnalia Christi Americana, sifa ya Comenius iliongezeka hivi kwamba katika mwaka wa 1654 alialikwa awe msimamizi wa Chuo Kikuu cha Harvard, huko Cambridge, Massachusetts. Hata hivyo, Comenius alikataa, kwa kuwa hakuwa akitafuta sifa, utukufu, au cheo cha juu.

Ni Nini Kilichomchochea?

Baada ya kuchunguza maisha ya Comenius, ni kawaida kwa mtu kutaka kujua ni nini kilichomchochea. Comenius aliiona elimu kuwa kitu cha kuwaunganisha wanadamu. Alisisitiza kwamba elimu ya ulimwenguni pote ingesaidia kuhifadhi amani ya ulimwengu.

Comenius pia alihusianisha ujuzi na mambo ya kimungu. Aliamini kwamba kwa kujipatia ujuzi, wanadamu hatimaye huelekezwa kwa Mungu. Na huenda jambo hilo liwe lilikuwa kusudi lake kuu.

Ufahamu wenye kina wa Comenius juu ya elimu bado unafaa leo. Njia zake zenye utaratibu za kufundisha, kutia ndani matumizi ya vielezi, hutumiwa ulimwenguni pote—kwa mfano, katika fasihi zinazochapishwa na Watch Tower Bible and Tract Society. Kila mmoja wetu anaweza kunufaika kwa kutumia njia zake tunapokuwa na funzo la Biblia la kibinafsi au tunapoongoza funzo la Biblia la familia. Jinsi gani?

“Wanafunzi hawapaswi kulemezwa kwa mambo yasiyofaa umri wao, ufahamivu wao, na hali zilizopo,” akaandika Comenius. Hivyo, unapowafundisha watoto wako Biblia au somo jinginelo, jaribu kuyafanya masomo yawafae. Badala ya kutumia njia ya kawaida ya maswali na majibu, mbona usiwasimulie hadithi za watu katika Biblia? Wahusishe, labda kwa kuwaruhusu wachore picha za matukio katika Biblia au kuwatia moyo waigize drama za Kibiblia. Uwe mbunifu! Jitihada zako zitakuwa na matokeo.—Mithali 22:6.

Tumia pia fasihi zenye vielezi zinazokusudiwa kuwafundisha hasa vijana hatua kwa hatua, kama vile Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia na Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi.b Na unapowafundisha wanafunzi wa Biblia wenye umri wowote, tumia fursa hiyo kufanya kujifunza kwao kuwe “kwenye kutumika kabisa, kunakopendeza kabisa.”

Urithi Wenye Kudumu

Moto ulipoukumba mji wa Leszno mnamo mwaka wa 1656, Comenius alipoteza karibu mali yake yote. Ingawa hivyo, jambo la kupendeza ni kwamba aliacha utajiri wa namna nyingine. Kitabu A Brief History of Education chasema: “Comenius . . . alibadilisha mkazo wa mafundisho kutoka kwa maneno hadi kwa vitu, naye alifanya kufundishwa kwa ujuzi wa kisayansi na wa habari muhimu za ulimwengu kuwe jambo kuu katika vichapo vyake.”

Kwa kweli, Comenius anaweza kupongezwa kwa kugeuza kazi ya kufundisha iwe stadi. Njia zake za kufundisha zilibadili kabisa namna watoto walivyofundishwa shuleni. Mwelimishaji Mmarekani Nicholas Butler alisema: “Comenius alitimiza fungu muhimu sana katika historia ya elimu. Alianzisha na kuendeleza harakati zote za kisasa katika uwanja wa elimu ya sekondari na ya msingi.” Mashahidi wa Yehova, wakiwa wanafunzi wa Biblia wenye bidii, wana sababu pia ya kumshukuru mwanzilishi huyo wa elimu ya kisasa.

[Maelezo ya Chini]

a Mwaka wa 1657, Comenius alichapisha kitabu The Great Didactic katika lugha ya Kilatini kikiwa sehemu ya Opera Didactica Omnia.

b Vimechapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

BAADHI YA KANUNI ZA KUFUNDISHA ZA JOHN COMENIUS

Kuhusu kiasi cha habari inayopasa kufundishwa: “Mwalimu anapaswa kufundisha kiasi ambacho mwanafunzi anaweza kufahamu na wala si kile ambacho yeye anaweza kufundisha.”

Kuhusu njia za kufundisha: “Kufundisha vema ni kuweza kumfundisha mtu kwa haraka, kwa kukubalika, na kikamili.”

“Mwalimu mwenye uwezo [ni] yule anayejua jinsi ya kustahimili kwa subira kutokuwa na ujuzi kwa mwanafunzi na pia anayejua jinsi ya kuondoa kutokuwa na ujuzi huko kwa matokeo.”

“Kufundisha kwamaanisha tu kuonyesha jinsi ambavyo vitu hutofautiana katika makusudi yake mbalimbali, maumbo, na vyanzo. . . . Kwa hiyo, yule anayetofautisha vitu kwa njia nzuri anafundisha vema.”

Kuhusu uhusiano wa kimantiki: “Jambo lolote lisilokuwa wazi haliwezi kueleweka wala kuthaminiwa na kwa sababu hiyo haliwezi kukumbukwa.”

“Jambo mojamoja linapokosekana, inakuwa vigumu kuelewa au kubainisha jambo na inakuwa pia vigumu kulikumbuka.”

Kuhusu Ufahamivu: “Kuelewa kitu chochote kunahusu hasa kuelewa kwa nini na jinsi gani kitu hicho kikiwa katika mojawapo ya sehemu zake kinahusiana na kitu kingine na kuelewa ni jinsi gani na ni kwa kadiri gani kinatofautiana na vitu vingine vinavyofanana nacho.”

“Imesemwa kwa kufaa kwamba tunapaswa kusoma habari mara moja ili kujua yaliyomo; na mara ya pili, ili kuielewa; na mara ya tatu, ili kuitia katika kumbukumbu letu; tunapaswa kuirudia mara ya nne kwa kimya ili tujitahini wenyewe tuone ikiwa tumeielewa kabisa habari hiyo.”

[Picha]

Ukurasa kutoka kwa “The Visible World,” chapa ya 1883

[Picha katika ukurasa wa 24]

Kitabu cha kwanza cha Ujerumani cha mwaka wa 1775, kilicho na kanuni za kufundisha za Comenius

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki