Kwa Kazi Ngumu ya Watoto
“Watoto, ambao sasa hutumiwa katika uzalishaji, wanaonwa kuwa bidhaa za kiuchumi badala ya kuwa tumaini la wakati ujao la jamii.”—Chira Hongladarom, mkurugenzi wa Taasisi ya Masuala ya Jamii, Thailand.
WAKATI ujao umnunuliapo binti yako mwanaserere, kumbuka kwamba huenda ametengenezwa na watoto wachanga huko Kusini-mashariki ya Asia. Wakati ujao mwanao apigapo mpira wa miguu, fikiria uhakika wa kwamba huenda umeshonwa na msichana mwenye umri wa miaka mitatu ambaye, pamoja na mamaye na dada zake wanne, hulipwa senti 75 za Kimarekani kwa siku. Wakati ujao ununuapo zulia, fikiria kwamba huenda likawa limefumwa kwa vidole vyepesi vya vijana wenye umri wa miaka sita wanaofanya kazi saa nyingi siku baada ya siku chini ya hali mbaya.
Kuajiriwa kwa watoto kumeenea kadiri gani? Kunaathirije watoto? Ni hatua gani iwezayo kuchukuliwa kukomesha tatizo hili?
Kuenea kwa Tatizo Hili
Kulingana na Shirika la Wafanyakazi Ulimwenguni (ILO), idadi ya watoto walioajiriwa wenye umri wa kati ya miaka 5 na 14 katika nchi zinazositawi inakadiriwa kuwa milioni 250.a Inaaminiwa kuwa asilimia 61 wako Asia, asilimia 32 katika Afrika, na asilimia 7 wako Amerika ya Latini. Kuajiriwa kwa watoto kumeenea pia katika nchi zilizositawi kiviwanda.
Katika kusini mwa Ulaya idadi kubwa ya watoto hufanya kazi ya kulipwa, hasa kazi za kimsimu, kama vile ukulima, na katika karakana ndogo. Hivi karibuni, kuajiriwa kwa watoto kumeongezeka katika Ulaya ya Kati na ya Mashariki kufuatia mabadiliko ya kutoka Ukomunisti hadi ubepari. Katika Marekani, idadi rasmi ya watoto walioajiriwa ni milioni 5.5, lakini hesabu hiyo haitii ndani idadi kubwa ya watoto wenye umri wa chini ya miaka 12 walioajiriwa kiharamu katika biashara zenye kudhulumu au wale wafanyakazi wa muda na wahamaji kwenye mashamba makubwa. Mamilioni haya ya watoto yanakujaje kuwa sehemu ya wafanyakazi?
Visababishi vya Watoto Kuajiriwa
Kuutumia vibaya umaskini. “Sababu kubwa inayowafanya watoto wafanye kazi iliyo hatari, na yenye kuumiza ni kuutumia vibaya umaskini,” chasema kichapo The State of the World’s Children 1997. “Kwa familia zilizo maskini, mchango mdogo kutoka kwa mshahara wa mtoto au usaidizi nyumbani unaowaruhusu wazazi wafanye kazi ni jambo linaloweza kuamua iwapo watapata chakula au la.” Mara nyingi wazazi wa watoto waajiriwa huwa wasioajiriwa kazi au hufanya kazi yenye mshahara mdogo. Wanatamani kupata kazi yenye mshahara mzuri. Ni kwa nini basi watoto wao wanaajiriwa badala yao? Kwa sababu watoto wanaweza kulipwa mshahara mdogo. Kwa sababu watoto ni waelekevu zaidi na watiifu—wengi wao hufanya lolote waambiwalo, bila kubisha. Kwa kuwa ni nadra sana kwa watoto kupanga migomo ya kupinga uonezi. Na kwa sababu hawalipizi kisasi wanapotendwa vibaya kimwili.
Ukosefu wa elimu. Sudhir, mvulana mwenye umri wa miaka 11 kutoka India, ni mmojawapo wa mamilioni ya watoto walioacha shule na kuanza kufanya kazi. Kwa sababu gani? “Shuleni, walimu hawakuwa wakifundisha vema,” yeye ajibu. “Tulipowaomba watufundishe alfabeti, wangetupiga. Wangelala darasani. . . . Tulipokosa kuelewa, wangekataa kutufundisha.” Inasikitisha kwamba maelezo hayo ya Sudhir juu ya shule ni ya kweli. Kupunguzwa kwa kiasi cha fedha kinachotumiwa kwa masilahi ya jamii katika nchi zinazositawi, kumeathiri sana elimu. Uchunguzi mmoja uliofanywa na Umoja wa Mataifa mwaka wa 1994 katika nchi 14 zisizositawi ulimwenguni ulifunua mambo fulani hakika yenye kustaajabisha. Kwa mfano, katika nusu ya nchi hizi, madarasa ya wanafunzi wa darasa la kwanza yana madawati ya wanafunzi 4 tu kati ya kila wanafunzi 10. Nusu ya wanafunzi hawana vitabu vya mafundisho, na nusu ya madarasa hayana ubao. Si ajabu kwamba, wengi wa watoto wanaohudhuria shule hizi huishia kuajiriwa kazi.
Mataraja ya kidesturi. Kazi izidipo kuwa yenye hatari zaidi na ngumu zaidi, inaachwa kwa makabila madogo, watu wa matabaka ya chini, wenye magumu, na walio maskini. Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa lasema hivi juu ya nchi moja ya Asia kwamba “maoni yamekuwa kwamba watu fulani wanazaliwa ili waongoze na kufanya kazi kwa kutumia akili yao huku wengine, walio wengi zaidi, wanazaliwa ili wafanye kazi kwa kutumia miili yao.” Katika nchi za Ubepari, mitazamo haiwi mizuri sikuzote. Watu wenye utajiri huenda wawakataze watoto wao wenyewe kufanya kazi hatari, lakini hawajali wakati vijana wa jamii, kabila, au vikundi vilivyo maskini wanapofanya kazi hiyo. Mathalani, katika kaskazini mwa Ulaya, watoto walioajiriwa huenda wawe Waturuki au Waafrika; huko Marekani, huenda wawe Waasia au wenyeji wa Amerika ya Latini. Kuwaajiri watoto huendelezwa na jamii ya kisasa inayokazia sana utumiaji wa bidhaa. Watu wanahitaji sana bidhaa za bei nafuu. Watu wengi hawajali kwamba huenda bidhaa hizi zinatengenezwa na mamilioni ya watoto wasiojulikana, wanaotumiwa vibaya.
Njia Mbalimbali za Kuwaajiri Watoto
Watoto huajiriwa kwa njia zipi? Kwa ujumla, watoto wengi walioajiriwa hufanya utumishi wa nyumbani. Wafanyakazi hawa hutajwa kuwa “watoto wenye kusahaulika zaidi ulimwenguni.” Kwa kweli utumishi wa nyumbani haupaswi kuwa hatari, lakini mara nyingi umekuwa hivyo. Watoto walioajiriwa nyumbani hulipwa mshahara mdogo sana—au hata hukosa kulipwa. Mabwana-wakubwa wao huweka masharti na hali za kazi yao jinsi wapendavyo. Hawaonyeshwi shauku, hawapati elimu, wakati wa tafrija, wala utendaji wa kijamii. Ni rahisi kwao kutendwa vibaya kimwili na kingono.
Watoto wengine huwa wafanyakazi wa kulazimishwa na watumwa waliotolewa kuwa dhamana. Katika Asia Kusini, na katika sehemu nyinginezo, mara nyingi watoto wenye umri wa miaka 8 au 9 tu, huwekwa rehani kwa wamiliki viwanda au wawakilishi wao ili wazazi wao wapate mikopo midogo. Utumwa wa maisha wa watoto hawa haufanikiwi kamwe kupunguza deni hilo.
Namna gani biashara ya ngono inayoharibu watoto? Inakadiriwa kwamba kila mwaka takriban wasichana milioni moja ulimwenguni pote hushawishiwa kuingia katika biashara ya ngono. Wavulana pia hutumiwa vibaya kingono mara nyingi. Madhara ya kimwili na ya kihisia-moyo yanayosababishwa na kutendwa vibaya huku—bila kutaja kuambukizwa HIV—hufanya biashara hii iwe mojawapo ya kazi zilizo hatari zaidi kwa watoto. “Jamii hutuona kuwa wazururaji,” asema kahaba mwenye umri wa miaka 15 kutoka Senegal. “Hakuna mtu anayetaka kutujua au kuonekana akiwa nasi.”b
Asilimia kubwa ya watoto walioajiriwa hutumiwa vibaya mashambani na viwandani. Watoto hawa humenyeka katika uchimbaji wa migodi unaoweza kuonwa kuwa hatari sana kwa watu wazima. Wengi wao huugua kifua kikuu, mkamba, na ugonjwa wa pumu. Watoto walioajiriwa kwenye mashamba huathiriwa na viua visumbufu, huumwa na nyoka, na wadudu. Baadhi yao wamejikata viungo vya mwili kwa miundu wanapokuwa wakivuna miwa. Mamilioni ya watoto wengine wanafanya kazi barabarani. Kwa kielelezo, fikiria Shireen mwenye umri wa miaka kumi, anayejiruzuku kwa kuokoteza takataka. Hajawahi kamwe kuhudhuria shule, lakini anajua sana kutafuta riziki. Anapouza makaratasi yaliyotumiwa na mifuko ya plastiki yenye thamani ya senti 30 hadi 50 za Marekani, yeye huweza kununua chakula cha mchana. Anapochuma fedha chache sana, yeye hukosa kula. Mara nyingi watoto wanaorandaranda mitaani, wakiwa wanaepa kutendwa vibaya au kutotunzwa nyumbani, hutendwa vibaya zaidi na kutumiwa vibaya kwenye barabara. “Kila siku mimi husali nisikutane na mtu mwovu,” asema Josie, mwenye umri wa miaka kumi anayeuza peremende kwenye barabara za jiji moja la Asia.
Maisha ya Utotoni Yaliyoharibiwa
Makumi ya mamilioni ya watoto wako katika hatari sana, kwa sababu ya kufanya kazi za aina hiyo. Huenda ikasababishwa na kazi wanayofanya au hali mbaya za kazi. Watoto pamoja na wafanyakazi wengine wachanga huelekea kupatwa na aksidenti mbaya sana kazini kuliko watu wazima. Hii ni kwa sababu mwili wa mtoto ni tofauti na wa mtu mzima. Uti wake wa mgongo au fupanyongo lake laweza kulemazwa na kazi ngumu kwa urahisi. Watoto pia, huathiriwa zaidi katika mazingira yenye dutu za kemikali hatari au na mnururisho kuliko watu wazima. Kwa kuongezea, mwili wa watoto haufai kutumiwa kwa saa nyingi kufanya kazi zenye kuchosha na zenye kuumiza, wanazofanya mara nyingi. Licha ya kwamba hawatambui hatari zinazohusika, hata hawajui tahadhari wanazopaswa kuzingatia.
Kuwaajiri watoto kunaathiri sana pia ukuzi wao wa kisaikolojia, kihisia-moyo, na kiakili. Watoto hawa hawaonyeshwi shauku. Mapigo, matusi, adhabu kwa kunyimwa chakula, na kutendwa vibaya kingono ni mambo ya kawaida sana. Kulingana na uchunguzi mmoja, karibu nusu ya takriban watoto milioni 250 walioajiriwa wameacha shule. Kwa kuongezea, imeonekana kwamba uwezo wa kujifunza wa watoto wanaofanya kazi kwa saa nyingi waweza kudhoofishwa.
Haya yote yamaanisha nini? Yanamaanisha kwamba watoto wengi walioajiriwa hubaki wakiwa maskini, wenye kutaabika, wagonjwa, wasiojua kusoma wala kuandika, na waliojitenga na jamii muda wote wa maisha yao. Au, kama vile mwandishi wa habari Robin Wright alivyosema, “licha ya maendeleo yote ya kisayansi na ya kitekinolojia, mwishoni mwa karne ya 20, ulimwengu unatokeza mamilioni ya watoto wasiokuwa na tumaini la kuishi maisha ya kawaida, sembuse kuuongoza ulimwengu kwenye Karne ya 21.” Maneno haya yenye kumfanya mtu afikiri yanatokeza maswali haya: Watoto wanapaswa kutendewaje? Je, kuna tumaini lolote la kutatua tatizo la kuwaajiri watoto?
[Maelezo ya Chini]
a Kwa kawaida, shirika la ILO huweka kiwango cha chini cha umri wa watoto wanaoweza kuajiriwa kuwa miaka 15—mradi tu haupungui umri wa kukamilisha elimu ya lazima. Hiki kimekuwa kiwango kinachofuatwa sana ili kujua idadi ya watoto walioajiriwa ulimwenguni pote sasa.
b Kwa habari zaidi juu ya kuwaharibu watoto kingono, ona ukurasa wa 11 hadi 15 wa toleo la Amkeni! la Aprili 8, 1997.
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
Kuajiriwa kwa Watoto Ni Nini?
WATOTO wengi katika jamii zote hufanya kazi kwa njia moja au nyingine. Kazi wanazofanya hutofautiana katika jamii nyingi na hubadilika baada ya muda. Kazi inaweza kuwa sehemu muhimu ya elimu ya watoto na njia ya wazazi kuwafundisha watoto wao stadi zilizo muhimu. Katika nchi fulani, mara nyingi watoto hufanya kazi katika karakana na kutoa utumishi fulani-fulani, na hatua kwa hatua wanakuwa wafanyakazi wa wakati wote baadaye maishani. Katika nchi nyingine, matineja hufanya kazi kwa saa chache kwa juma ili kuchuma fedha chache za kununulia vitu vidogo vidogo. Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa linasisitiza kwamba kazi kama hiyo “inanufaisha, ikiboresha au kuendeleza ukuzi wa mtoto kimwili, kiakili, kiroho, kiadili au kijamii bila kuhitilafiana na elimu, tafrija na pumziko.”
Kwa upande mwingine, kuajiriwa kwa watoto, hurejezea watoto wanaofanya kazi saa nyingi kwa mshahara mdogo, mara nyingi chini ya hali zenye kudhuru afya yao. Kazi ya aina hii “kwa wazi ni yenye kuumiza au kudhuru,” chasema kichapo The State of the World’s Children 1997. “Hakuna yeyote anayeweza kubisha hadharani kwamba kuwatumia watoto vibaya wakiwa makahaba ni jambo lenye kukubalika kwa sababu yoyote ile. Vivyo hivyo na ‘kuajiriwa kwa watoto wakiwa kama dhamana’, maneno yanayotumiwa kwa mapana kurejezea tendo la kuwafanya watoto watumwa ili kulipia madeni ya wazazi, au ya babu na nyanya yao. Hii inatia ndani pia viwanda vinavyohatarisha afya na usalama . . . Kwa wazi watoto wote hawapaswi kufanya kazi inayowahatarisha.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]
“Bado Tuna Mengi ya Kufanya”
SHIRIKA la Wafanyakazi Ulimwenguni (ILO) linaongoza jitihada za kukomesha namna mbaya zaidi za kuwaajiri watoto. Shirika la ILO linashawishi serikali zitunge sheria inayokataza kuwaajiri watoto wenye umri wa chini ya miaka 15. Linatia moyo pia kuanzishwa kwa mikataba mipya inayokataza kuwaajiri watoto wenye umri wa chini ya miaka 12 na kuharamisha namna hatari zaidi za kuwatumikisha watoto. Ili kuelewa zaidi mafanikio ya jitihada hizo, Amkeni! lilimhoji Sonia Rosen, mkurugenzi wa Mpango wa Kimataifa Unaoshughulikia Kuajiriwa kwa Watoto, katika Idara ya Wafanyakazi ya Marekani. Amefanya kazi kwa ukaribu katika mipango mbalimbali ya ILO. Hili ni dondoo kutoka kwa mazungumzo hayo.
Swali: Ni njia gani inayofaa zaidi kukabiliana na kuajiriwa kwa watoto?
Jibu: Hatuna njia hata moja ya kukabili tatizo hili. Hata hivyo, katika ngazi ya kimataifa, masuala tuliyozungumzia ni masuala muhimu, yaani, kutekeleza sheria kwa njia bora na kutoa elimu ya msingi kwa ulimwengu wote, itakuwa bora zaidi ikiwa itakuwa lazima kwa kila mtu na bila malipo. Kwa hakika, ni muhimu pia kuandaa fursa za kutosha za kuwaajiri wazazi.
Swali: Je, umeridhika na maendeleo ambayo tayari yamefanywa katika kukabiliana na kuajiriwa kwa watoto?
Jibu: Mimi siridhiki kamwe. Sisi husema kwamba hakuna mtoto hata mmoja apaswaye kufanya kazi chini ya hali zenye uonevu. Tumefanya maendeleo makubwa kupitia kwa mipango ya ILO. Lakini bado tuna mengi ya kufanya.
Swali: Jamii ya kimataifa inaitikiaje jitihada za kukomesha kuajiriwa kwa watoto?
Jibu: Sijui kamwe jinsi ninavyoweza kujibu swali hilo tena. Sasa tumefikia muafaka fulani ulimwenguni pote kwamba kuajiriwa kwa watoto ni tatizo linalohitaji kushughulikiwa. Nafikiri kwamba kwa sasa maswali hasa yanakuwa: Tatizo hilo lishughulikiweje, na haraka kadiri gani? Ni njia gani zinazofaa zaidi kukabiliana na namna fulani-fulani za kuajiriwa kwa watoto? Nafikiri hilo ndilo tatizo letu.
Swali: Watoto walioajiriwa wanaweza kutarajia nini wakati ujao?
Jibu: Nchi zote ulimwenguni zinatarajia kurudi Geneva mwaka huu ili kukamilisha muafaka mpya juu ya kazi zilizo mbaya zaidi kwa watoto. Kwa kweli hilo linatoa tumaini kubwa sana la utatuzi kwa —nchi zote, pamoja na mashirika yote ya wafanyakazi na ya waajiri. Tunatumaini kwamba, muafaka huo utaanzisha muundo mpya wenye shabaha ya kukomesha kabisa kazi zilizo mbaya zaidi kwa watoto.
Si wote wenye matumaini kama ya Sonia Rosen. Charles MacCormack, msimamizi wa shirika la Save the Children, ana mashaka. “Serikali hazina nia ya kufuata makubaliano hayo na wala watu wote hawana ujuzi wa kutatua tatizo hilo,” yeye asema. Kwa nini? Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa linasema hivi: “Mara nyingi kuajiriwa kwa watoto ni suala gumu. Uvutano wa watu wenye mamlaka unaliendeleza, kutia na waajiri wengi, wale wanaojinufaisha kwa kuwaajiri watoto na wataalamu wa uchumi wanaopendekeza wawe huru kuwaajiri watoto, na wafuata-mapokeo wanaoamini kwamba cheo au tabaka la watoto fulani-fulani huwanyima haki.”
[Picha]
Sonia Rosen
[Picha katika ukurasa wa 5]
Historia yenye kuhuzunisha ya kuajiriwa kwa watoto inatia ndani kumenyeka kwenye migodi na viwanda vya kutengeneza pamba
[Hisani]
U.S. National Archives photos
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kuokoteza takataka
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kufanya kazi ngumu ya kukusanya kuni
[Hisani]
UN PHOTO 148046/ J. P. Laffont-SYGMA
[Picha katika ukurasa wa 7]
Waajiriwa kwenye kiwanda cha kusokota nyuzi
[Hisani]
CORBIS/Dean Conger
[Picha katika ukurasa wa 8]
Watoto wanaouza barabarani hulipwa mshahara mdogo wa senti sita za Marekani kwa siku
[Hisani]
UN PHOTO 148027/Jean Pierre Laffont
[Picha katika ukurasa wa 8]
Wafanya kazi ngumu katika karakana ya useremala
[Hisani]
UN PHOTO 148079/ J. P. Laffont-SYGMA
[Picha katika ukurasa wa 9]
Wajitahidi kutafuta riziki
[Hisani]
UN PHOTO 148048/J. P. Laffont-SYGMA