Kuishi Maisha Bora Bila Kiungo cha Mwili
“MPANDA-MLIMA afika tena kwenye kilele.” Ndivyo gazeti moja lilivyotangaza, Tom Whittaker alipofika kwenye kilele cha Mlima Everest. Wengi wamepanda kilele hicho kirefu awali, lakini Tom Whittaker alikuwa mtu wa kwanza aliyekatwa kiungo cha mwili kufanya hivyo! Whittaker alipoteza mguu wake kwenye aksidenti ya gari. Lakini mguu bandia, ulimwezesha arejee mchezo anaoupenda. Vifaa kama hivyo vinawezesha maelfu ya watu wengine waliokatwa viungo vya mwili wafurahie maisha bora yenye kuridhisha. Kwa hakika, ni jambo la kawaida kuwaona watu waliokatwa viungo wakishiriki riadha, wakicheza mpira wa kikapu, au wakiendesha baiskeli.
Miguu na mikono bandia ya kale ilikuwa vipande vya mbao au kulabu za chuma zenye kuumiza. Lakini maendeleo yalifanywa wakati maelfu ya watu walipopoteza viungo vya mwili vitani. Haishangazi kwamba daktari mpasuaji wa jeshi Mfaransa—wa karne ya 16 Ambroise Paré—ndiye anayedaiwa kuwa mwanzilishi wa viungo bandia vya kwanza vilivyo bora. Viungo bandia vya leo hutumia haidroliki, viungo vya goti vyenye muundo tata, miguu bandia iliyotengenezwa kwa kaboni, silikoni, plastiki, na vifaa vingine vya kisasa, vinavyowezesha watu wengi kutembea na kujongea kwa urahisi na bila matatizo kuliko ilivyowahi kudhaniwa. Maendeleo katika taaluma ya elektroni yanawezesha mikono isogezwe kwa njia ya kawaida zaidi. Umbo la viungo bandia limeboreshwa pia. Viungo bandia vya kisasa vina vidole, na hata vingine huonekana kama vina mishipa. Hata mwanamke mmoja mrembo, anayeonyesha mitindo ya nguo aliyepoteza mguu kwa sababu ya ugonjwa wa kansa, alitiwa mguu bandia ulioonekana kuwa wa asili sana hivi kwamba akaweza kuendelea na kazi yake ya kuonyesha mitindo ya nguo.
Mtazamo wa Akilini Ni Muhimu
Hata hivyo, mtaalamu wa afya ya akili Ellen Winchell atahadharisha hivi: “Unapopatwa na tatizo la kibinafsi kama vile kukatwa kiungo cha mwili, utu wako unajaribiwa sana katika kila hali—kimwili, kihisia-moyo, kiakili, na kiroho.” Fikiria William, ambaye mguu wake ulikatwa kwa sababu ya kuoza kulikosababishwa na jeraha. Yeye asema hivi: “Siri moja ya kushinda tatizo lolote maishani ni mtazamo wetu wa akilini. Mimi sijapata kamwe kuona kutojiweza kwangu kuwa kizuizi. Badala yake, nimedumisha mtazamo mzuri kuhusu matatizo yoyote ambayo nimekuwa nayo tangu nilipopata aksidenti.” Ellen Winchell, ambaye pia alikatwa kiungo cha mwili, amwunga mkono kwa kusema kuwa watu wenye maoni mazuri huelekea kukabiliana vema na tatizo la kukatwa kiungo cha mwili kuliko watu wenye maoni yasiyofaa. Ni kama vile Biblia isemavyo, “moyo uliochangamka ni dawa nzuri.”—Mithali 17:22.
Amkeni! lilihoji baadhi ya Wakristo waliopoteza viungo vya mwili ambao wamekabiliana kwa mafanikio na hali yao. Wengi wao walidokeza kwamba watu waliokatwa viungo wanahitaji kuepuka kufikiria sana au kuficha kutojiweza kwao. “Nilisumbuka sana wakati wengine walipohisi kwamba ni mwiko kuzungumzia jambo hilo,” akasema Dell, aliyepoteza mguu chini tu ya goti lake la kushoto. “Naona kwamba jambo hilo humtahayarisha kila mtu.” Wataalamu fulani hupendekeza kwamba ikiwa huna mkono wa kulia na unajulishwa kwa mtu fulani, unapaswa kumsalimu kwa mkono wa kushoto. Na ikiwa mtu anaulizia habari za kiungo chako bandia, mweleze juu yake. Unapostarehe unawafanya watu wengine wahisi wamestarehe. Kwa kawaida, mazungumzo hubadilika upesi.
Kuna “wakati wa kucheka.” (Mhubiri 3:4b) Mwanamke mmoja aliyepoteza mkono asema hivi: ‘Zaidi ya yote, uwe mcheshi! Ni lazima tukumbuke sikuzote kwamba mtazamo wa watu juu yetu hutegemea sana mtazamo tulionao juu ya hali yetu.’
“Wakati wa Kulia”
Hapo mwanzoni, baada ya kupoteza mguu, Dell alijiambia, “Kwisha. Maisha yamekwisha.” Florindo na Floriano walipoteza viungo vya mwili kutokana na mabomu ya kutegwa ardhini huko Angola. Florindo asema kwamba alilia kwa siku tatu mchana na usiku. Floriano pia alisumbuliwa na hisia-moyo. “Nilikuwa na umri wa miaka 25 tu,” yeye aandika. “Siku moja ningeweza kufanya kitu chochote, na siku ifuatayo singeweza hata kusimama. Nilivunjika moyo na kushuka moyo sana.”
Kuna “wakati wa kulia.” (Mhubiri 3:4a) Ni kawaida kuhuzunika kwa kipindi fulani unapokumbwa na msiba. (Linganisha Waamuzi 11:37; Mhubiri 7:1-3.) “Njia ya kukabiliana kwa mafanikio na huzuni hiyo ni kutoficha hisi hizo,” aandika Ellen Winchell. Kumweleza msikilizaji mwenye hisia-mwenzi jinsi unavyohisi mara nyingi husaidia sana. (Mithali 12:25) Lakini hisi za huzuni haziendelei milele. Kwa muda fulani baada ya kupatwa na msiba wa kukatwa kiungo cha mwili, huenda watu mmoja mmoja wakawa wenye kukasirika upesi, wenye kuchambua-chambua, wenye mahangaiko, au wenye kujitenga. Hata hivyo, kwa kawaida hisia hizi hupungua. Ikiwa sivyo, huenda akawa amepatwa na mshuko-moyo mbaya—ugonjwa unaohitaji kutibiwa na daktari. Washiriki wa familia na marafiki wanapaswa kuwa macho kuona dalili zozote zinazoonyesha kwamba mpendwa wao anahitaji msaada wa daktari.a
W. Mitchell, ambaye amepooza miguu yote miwili, aandika hivi: “Sote twahitaji watu wanaojali. Mtu anaweza kuvumilia karibu kila hali mradi anahisi akiwa na marafiki wengi na washiriki wa familia, na kwa upande mwingine mtu anayejaribu kukazana maishani peke yake hushindwa na tatizo dogo. Na marafiki hawaji tu kimwujiza, jitihada inahitajiwa ili kuwapata na kudumisha urafiki nao, kama sivyo unaharibika.”— Linganisha Mithali 18:24.
Kuishi Maisha Bora, Bila Kiungo cha Mwili
Watu wengi waliopoteza viungo vya mwili wameweza kuishi maisha bora licha ya ulemavu huo. Kwa kielelezo, Russell alizaliwa akiwa na sehemu ya juu tu ya mguu wa kushoto. Sasa akiwa na umri wa miaka 78, yeye bado hufanya mazoezi kwa ukawaida naye anaishi maisha yenye kuridhisha, ingawa sasa anatembea kwa msaada wa mkongojo. Russell ambaye kwa asili ni mchangamfu, alikiri kwamba kwa muda mrefu aliitwa jina la utani Happy, (Mwenye Furaha).
Douglas, aliyepoteza mguu wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, hutembea kwa msaada wa mguu bandia wa kisasa. Akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, ametumikia kwa furaha akiwa painia wa kawaida, mweneza-evanjeli wa wakati wote, kwa miaka sita. Na je, wamkumbuka Dell, ambaye alifikiri kwamba maisha yake yalikuwa yamekwisha alipopoteza mguu? Yeye pia anaishi maisha ya kuridhisha akiwa painia, naye anajiruzuku.
Ingawa hivyo, watu waliopoteza viungo vya mwili hukabilianaje na hali katika nchi maskini au zile zenye vita? Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lasema hivi: “Leo, ukweli ni kwamba ni idadi ndogo tu ya watu wasiojiweza wanaopata msaada.” Wengi wao hulazimika kutumia fimbo na mikongojo isiyofaa ili kutembea. Hata hivyo, nyakati nyingine msaada huwapo. Floriano na Florindo, waliopoteza viungo vya mwili kutokana na mabomu ya kutegwa ardhini huko Angola, walipewa viungo bandia na Shirika la Msalaba Mwekundu na serikali ya Uswisi. Floriano hutumikia kwa furaha akiwa mtumishi wa huduma katika kutaniko la Mashahidi wa Yehova katika eneo lao, naye Florindo anatumikia akiwa mzee na mweneza-evanjeli wa wakati wote.
Shirika moja linalowashughulikia walemavu hueleza vizuri hivi: “Watu walemavu ni wale tu waliovunjika moyo!” Kwa kupendeza, Biblia imetimiza fungu muhimu katika kuwatia moyo watu walemavu. “Kweli za Biblia nilizojifunza nilipokuwa nikipata nafuu zilinisaidia sana,” asema Dell. Vivyo hivyo, Russell asema hivi: “Tumaini langu linalotegemea Biblia limenisaidia kuvumilia magumu sikuzote.” Biblia ina tumaini gani kwa walemavu?
[Maelezo ya Chini]
a Ona makala “Jinsi ya Kusaidia Walioshuka Moyo Wapate Shangwe Tena,” katika toleo la Mnara wa Mlinzi la Machi 15, 1990.
[Sanduku katika ukurasa wa 8]
Maumivu Bandia
Hisi ya kuwa na kiungo hurejezea hisi halisi inayokufanya uhisi una kiungo chako ulichopoteza. Ni hisia ya kawaida ambayo watu waliokatwa viungo huwa nayo baada ya kukatwa, na ni halisi sana hivi kwamba kijitabu kwa ajili ya watu waliokatwa viungo vya mwili husema hivi: “Jihadhari na hisi ya kuwa una kiungo chako unapotoka kitandani au kitini bila kiungo chako bandia. Sikuzote tazama chini ili ukumbuke kwamba huna mguu.” Mgonjwa mmoja aliyepoteza miguu yote miwili aliinuka ili amsalimu daktari wake, lakini badala yake, akaanguka kwenye sakafu!
Tatizo jingine ni maumivu bandia ya kiungo kilichopotezwa. Haya ni maumivu halisi ambayo mtu huhisi kana kwamba yanatoka kwa kiungo kilichokatwa. Ukali, aina, na muda wa maumivu bandia hutofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Kwa uzuri, hisi ya kuwa na kiungo na maumivu bandia kwa kawaida hupungua baada ya muda.
[Picha katika ukurasa wa 6]
Viungo bandia vya kisasa hufanya maisha ya watu wengi walemavu yawe yenye kupendeza
[Hisani]
Photo courtesy of RGP Prosthetics
[Picha katika ukurasa wa 7]
Ni jambo la kawaida kuhuzunika baada ya kupatwa na msiba mbaya
[Picha katika ukurasa wa 8]
Watu wengi walemavu hufurahia maisha bora