Kupoteza Kiungo cha Mwili—Je, Waweza Kupatwa na Hali Hiyo?
Benjamin alikuwa nje akifurahia jua lililoangaza jiji la Sarajevo wakati wa majira ya kuchipua, alipokanyaga bomu lililotegwa ardhini. Mguu wake wa kushoto ulilipuliwa. “Nilijaribu kusimama,” Benjamin akumbuka. “Nikashindwa.” Benjamin ni mmojawapo wa watu 20,000 wanaokufa au kulemazwa kila mwaka kutokana na mabomu ya kutegwa ardhini.
MABOMU ya kutegwa ardhini yapatayo milioni 15 yametapakaa katika nchi ya Angola—zaidi ya bomu moja kwa kila mwanamume, mwanamke, na mtoto katika nchi hiyo. Sasa Angola ina watu 70,000 ambao wamepoteza kiungo fulani cha mwili. Nchi ya Kambodia, ambayo ina mabomu yaliyotegwa ardhini yapatayo milioni nane hadi kumi, ina uwiano mkubwa zaidi ulimwenguni wa watu waliopoteza viungo fulani vya mwili—inakadiriwa kuwa mtu 1 kati ya kila 236 hana kiungo fulani cha mwili. Imeripotiwa kwamba Bosnia na Herzegovina ina zaidi ya mabomu milioni tatu yaliyotegwa ardhini—mabomu 152 katika kila eneo la kilometa 59 za mraba.
Lakini si katika nchi zenye vita tu ambako watu hupoteza viungo vya mwili. Kwa mfano, huko Marekani watu wapatao 400,000 wamepoteza viungo fulani vya mwili. Kinachowafanya watu wazima wengi kati ya idadi hiyo wapoteze viungo vya mwili ni maradhi sugu ambayo kwa ujumla yanaitwa “maradhi ya mishipa,” au PVD. Neno hili lawakilisha magonjwa mbalimbali. Kamusi ya Taber’s Cyclopedic Medical Dictionary hueleza PVD kuwa neno la ujumla linalotia ndani “maradhi ya ateri na vena za miisho ya mwili, hasa maradhi yanayoathiri mzunguko wa damu kwenye miisho ya mwili.” Kisababishi kikuu cha PVD ni ugonjwa wa kisukari. Kulingana na The World Health Report 1998, “idadi ya watu wazima wenye kisukari ulimwenguni pote itaongezeka zaidi ya maradufu kutoka milioni 143 mwaka wa 1997 hadi milioni 300 mwaka wa 2025.”
Huko Marekani, majeraha—yanayosababishwa na aksidenti za magari, mashine, vifaa vya umeme, na bunduki—ndiyo kisababishi kikuu cha pili cha kupoteza viungo vya mwili, yakisababisha asilimia 20 hadi 30 ya visa vyote vya kukatwa viungo vya mwili. Visababishi vingine vya kupoteza viungo vya mwili hutia ndani uvimbe (takriban asilimia 6) na kasoro za kuzaliwa (takriban asilimia 4).
Wazo la kupoteza kiungo muhimu cha mwili ni baya sana. Je, kuna njia yoyote ya kupunguza hatari hiyo? Na ikiwa tayari umepoteza kiungo cha mwili, unawezaje kufurahia maisha bora? Makala zifuatazo zinazungumzia swali hili na mengineyo.