Kuutazama Ulimwengu
Idadi ya Wasiojua Kusoma na Kuandika Ulimwenguni Yaongezeka
“Takriban sehemu moja kwa sita ya watu bilioni 5.9 ulimwenguni hawajui kusoma wala kuandika,” gazeti la The New York Times laripoti. Kulingana na shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF), idadi ya wasiojua kusoma na kuandika inatarajiwa kuongezeka. Kwa nini? Kwa sababu watoto 3 kati ya 4 katika nchi maskini zaidi ulimwenguni hawaendi shuleni siku hizi. Mbali na kusababisha matatizo ya kiuchumi yanayokumba ulimwengu, mapambano ya kikabila yamewanyima mamilioni ya watoto elimu. Shule huharibiwa wakati wa vita na pia hufanya watoto wengi wawe wanajeshi badala ya wanafunzi. Bila shaka, kutojua kusoma na kuandika, huchangia pia matatizo ya kijamii. Ripoti ya shirika la UNICEF yenye kichwa The State of the World’s Children 1999 yasema kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kutojua kusoma na kuandika na kuzaliwa kwa watoto wengi. Kwa mfano, katika nchi moja ya Amerika Kusini, “wanawake wasiojua kusoma na kuandika wana watoto 6.5 kwa wastani, nao akina mama wenye elimu ya sekondari wana watoto 2.5 kwa wastani,” gazeti Times likasema.
Kichaa cha Milenia
“Serikali ya [Israeli] imetenga dola milioni 12 ili kuimarisha ulinzi katika eneo la Temple Mount” kwa kuwa inatazamia ujeuri wakati wa milenia, gazeti la Nando Times laripoti. Polisi wanahofia kuwa huenda Wayahudi au “Wakristo” washupavu wakajaribu kubomoa misikiti iliyoko katika eneo hilo la Temple Mount ili wajenge upya hekalu la Kiyahudi. Madhehebu fulani ya “Kikristo” yanaamini kuwa hilo litaharakisha mwisho wa ulimwengu na kurudi kwa Kristo. Kulingana na ripoti hiyo, Temple Mount, inayoitwa na Waislamu al-Haram al-Sharif, “huonwa kuwa eneo hatari zaidi katika mzozo wa Mashariki ya Kati.” Eneo hilo liko katika “Jiji la Kale la Yerusalemu lenye kuta, lililotekwa na Israeli kutoka kwa Jordan wakati wa vita ya 1967 ya Mashariki ya Kati.” Imeripotiwa kwamba tayari “Wakristo” kadhaa wamekodi sehemu kwenye Mlima wa Mizeituni wakitazamia kurudi kwa Kristo.
Aspirini kwa Ajili ya Maumivu ya Mimea?
Huenda mimea isihisi maumivu kama watu, lakini hujikinga kutokana na madhara kwa kutokeza asidi ya yasmoni. Baadhi ya mimea hata hutokeza kemikali zinazohusiana na yasmini zinazofanya mimea mingine ijikinge. “Kwa miaka mingi, watafiti wamegundua kwamba kwa njia fulani aspirini huzuia mimea kutokeza asidi ya yasmoni,” gazeti la Science News lataarifu. Sasa wanasayansi wa Arizona State University wamefumbua sehemu ya utendaji huu usioeleweka. Aspirini hudhoofisha kimeng’enya muhimu katika mimea kupitia kwa utendaji wa kemikali ulio sawa na ule inayotumia kudhoofisha kimeng’enya tofauti katika wanadamu. Hata hivyo, uhusiano uliopo kati ya utendaji wa aspirini katika mimea na watu bado haueleweki, kwa kuwa vimeng’enya vyote viwili vinaonekana kuwa tofauti kabisa.
Je, “Wachawi” Waliouawa Wasamehewe?
Mnamo mwaka wa 1994 papa aliliomba Kanisa Katoliki ‘lichunguze historia yake ya kutekeleza haki.’ Tokeo moja limekuwa kuanzishwa kwa tume ya Kikatoliki katika Jamhuri ya Cheki—ya kwanza kabisa ya aina hiyo—ili iamue iwapo mamia ya watu walioteketezwa wakiwa hai kwa dai la kuwa wachawi watasamehewa. Kama tokeo la jitihada zilizoidhinishwa na kanisa za kuwasaka wachawi, maelfu mengi ya watu waliuawa Ulaya ama kwa kuteketezwa au kuteswa, kati ya karne ya 12 na 18. Baada ya Papa Innocent wa Nane kuchapisha amri dhidi ya wachawi mnamo mwaka wa 1448, wachawi walisakwa sana, na njia zaidi ya 30 za kutesea zilitumiwa ili kuwanasa walioshukiwa kuwa wachawi. Hata watoto wachanga waliteswa ili kuwalazimisha watoe ushahidi dhidi ya wazazi wao. Wachawi walio wengi zaidi walichomwa huko Ujerumani, lakini kesi za aina hiyo zilienea sana huko Ufaransa na Uingereza pia. Huenda kanisa likafikiria kuwasamehe waliouawa, gazeti la The Sunday Telegraph la London laripoti.
Kuudhibiti Mto Yangtze
Ujenzi wa bwawa la Three Gorges Dam kwenye Mto Yangtze wa China utakapokamilika, litakuwa kituo kikubwa zaidi ulimwenguni cha kutoa nguvu za umeme. Bwawa hilo litakuwa na kimo cha meta 185, na upana wa kilometa 2.3, na litazalisha kilowati milioni 18.2 za umeme. Hata hivyo, sababu kuu ya kujenga bwawa hili si kuzalisha nguvu za umeme, bali ni kusaidia kudhibiti kufurika kwa Mto Yangtze. Ujenzi ulianza mwaka wa 1994 na unatarajiwa kukamilika mwaka wa 2009. Kwa ujumla, mradi huu mkubwa utahusisha kuchimbwa kwa kyubiki-meta milioni 147 za udongo na mwamba, na kumwagwa kwa zaidi ya kyubiki-meta milioni 25 za saruji, na kuunganishwa kwa feleji zenye uzito upatao tani milioni mbili. “Hata hivyo, kazi ngumu zaidi ni kuwahamishia makao mapya zaidi ya watu milioni 1.1 wanaoishi katika maeneo yanayotumiwa kwa mradi huo,” gazeti China today lasema.
Ugonjwa wa Pumu Waongezeka
Shirika la Afya Ulimwenguni linaripoti kwamba katika mwongo uliopita, kumekuwa na ongezeko la asilimia 40 katika kuenea kwa ugonjwa wa pumu na katika idadi ya watu wanaolazwa hospitalini kwa sababu ya ugonjwa huo ulimwenguni pote. Kwa nini kumekuwa na ongezeko hilo? Wanachama wa American College of Chest Physicians walitaja kuongezeka kwa wanyama vipenzi wanaofugwa, kutia ndani na mwelekeo wa sasa wa kuishi katika vyumba vyenye kusongamana, visivyokuwa na hewa safi. Mtu aweza kushikwa na ugonjwa wa pumu kwa sababu ya “magamba (kutoka kwenye ngozi, au manyoya) ya wanyama, wadudu wa mavumbini, kuvu, moshi wa sigareti, chavuo, vichafuzi vya mazingira na harufu kali,” gazeti la The Toronto Star lasema. Hata hivyo, manyoya ya paka ndiyo kizio kikubwa zaidi. Gazeti hilo la habari lilisema kuwa ugonjwa wa pumu unahangaisha hasa kwa sababu vifo vingi vinavyosababishwa nao vyaweza kuzuiwa. Wakati huu, kuna takriban watu milioni 1.5 wanaougua pumu huko Kanada, na takriban watu 500 kati yao hufa kila mwaka kutokana na ugonjwa huo.
Halihewa Yasababisha Hasara Kubwa Sana
Misiba iliyosababishwa na halihewa katika miezi 11 ya kwanza ya mwaka wa 1998, ilitokeza hasara kubwa ya dola bilioni 89 ulimwenguni pote. Hasara iliyotokea “ilizidi sana hasara ya dola bilioni 55 ya mwongo wote wa miaka ya 1980,” ripoti ya Shirika la Habari la Associated Press yasema. Ripoti hiyo yasema hivi: “Hata kiwango cha infleshoni kinapozingatiwa, hasara ya miaka ya 1980, ya dola bilioni 82.7, bado ni ndogo sana ikilinganishwa na ile ya miezi 11 ya kwanza” ya mwaka wa 1998. Mbali na kupoteza vitu vya kimwili, inakadiriwa kwamba watu wapatao 32,000 walikufa kutokana na misiba ya kiasili kama vile dhoruba, mafuriko, mioto, na ukame. “Na zaidi ya hayo,” Seth Dunn wa Worldwatch Institute asema, “mwanadamu analaumika kuhusiana na hasara ya misiba ya kiasili.” Jinsi gani? Kulingana na Dunn, ukataji wa miti umechangia tatizo hilo kwa kuacha bara likiwa bila miti na bila maeneo yenye maji, ambayo huhifadhi maji kiasili.
Familia Zenye Mkazo
Uchunguzi wa hivi karibuni uliohusisha Wakanada unaonyesha kwamba familia leo zinahisi zikiwa na mkazo zaidi wa kifedha na kihisia-moyo kuliko familia za baada ya vita, nusu karne iliyopita. Gazeti la National Post huorodhesha talaka na mvunjiko wa familia kuwa visababishi vikuu vya mkazo. Kwa kufuata utaratibu huo, gazeti hilo linaorodhesha visababishi vingine vya mkazo kuwa “wazazi kufanya kazi ngumu sana kwa muda mrefu, hali za kazi zinazohatarisha usalama, kutozwa kodi kupita kiasi, na ukosefu wa staha kwa jitihada za wazazi za kuwalea watoto.” Waliohojiwa walisema kwamba familia nyingi zenye mzazi mmoja zina mikazo zaidi.
Kukusanya Vilima vya Barafu
“Kwa muda mrefu wakazi wa Newfoundland wameyaona maji ya vilima vya barafu kuwa safi sana,” lasema Financial Times la London, lakini sasa wanakusanya “rasilimali hii ya muda mrefu inayoelea kwenye fuo zao.” Baada ya kufunga kilima cha barafu kinachoelea kwa nyavu, meli ya kuvutia huvuta kilima hicho wakati wa bamvua kuelekea ufukoni. Meli hiyo husonga kwa kasi sana, kisha kwa ghafula hupiga kona kali inapokaribia pwani, na mara huachilia nyavu na kuvurumisha kilima hicho cha barafu ufukoni. Kilima hicho cha barafu hubaki kwenye bara, maji yanapopungua ufukoni. Ndipo kirini kubwa inapopasua kilima hicho cha barafu katika vipande vikubwa na kuvipakia katika mashua kubwa “ambamo vinapondwapondwa, kuyeyushwa na kuchujwa kabla ya kusafishwa kwa miali ya urujuanimno.”
Jeuri Dhidi ya Wanawake
“Katika Brazili, asilimia 63 ya visa vyote vya jeuri dhidi ya wanawake hutukia nyumbani, na ni thuluthi tu vinavyoripotiwa,” gazeti la habari la O Globo lataarifu. Gazeti hilo laongezea hivi: “Wanawake maskini ndio hasa wanaofanyiwa jeuri nyumbani, nao mara nyingi ndio huripoti jeuri kwa polisi. Si kawaida kwa wanawake matajiri kuripoti.” Nchi nyingine huripoti takwimu kama hizo. Kwa mfano, kulingana na ripoti moja iliyochapishwa na U.S. Justice Department, “zaidi ya nusu ya wanawake wote Marekani wameshambuliwa pindi fulani maishani mwao, na takriban mwanamke 1 kati ya 5 amebakwa au akaponea chupuchupu jaribio la kubakwa,” lasema shirika la habari la Reuters. Katibu wa Afya na Huduma za Jamii wa Marekani Donna Shalala asema hivi: “Kila tarakimu katika ripoti hii inawakilisha binti zetu, mama zetu, na jirani zetu.”