Kuelewa Pumu
PUMU ni ugonjwa wa ulimwenguni pote. Hapa katika New Zealand, inakadiriwa kwamba mtu 1 kati ya 10 anasumbuliwa nao. Vijana na wazee pia, watu wa mjini na watu wa mashambani, wafanya kazi wa mikono na wafanya kazi wa ofisini, ni miongoni mwa wenye kusumbuliwa.
Hata hivyo, pumu haieleweki sana, hasa na wale wasiosumbuliwa nao. Hata wagonjwa wa pumu mara nyingi hawaelewi linalowapata, na hii inaweza kufanyiza wasiwasi unaoongeza ubaya wa hali ile. Labda maelezo yanayofuata, yenye msingi wa maono na uchunguzi katika New Zealand, yatasaidia kupunguza kidogo ukosefu wa uelewevu.
Pumu Ni Nini?
Katika shambulio halisi la pumu, msumbukaji anajisikia amekabwa na kitu kifuani. Akikokota pumzi na kukohoa, anajitahidi kupumua. Ono hilo linaogopesha! Shambulio la pumu linaweza kuwa kali au pole sana. Dalili huenda zikatofautiana, hali moja na mara za kutokea-tokea kwa mashambulio. Sikuzote watu fulani wana dalili hizo, ingawa zinatofautiana ukali.
Ni nini kinachosababisha hisia hizi zisizopendeza? Kama vile labda unajua, hewa inaelekezwa ndani ya mapafu yetu kupitia mirija ya hewa. Katika wagonjwa wengi wa pumu, hali zenye kudhuru mwili wa mtu kwa urahisi zinasababisha wepesi wa kuwasha matata katika mirija hii. Huenda misuli iliyo katika ukuta wa mirija ya hewa ikakazika, huenda ule utando wenye kutandaza mirija hiyo ukafura, na tezi katika ukuta wa mirija ya hewa huenda zikatokeza ukamasi wa kupita kiasi. Tokeo ni nini? Mirija inakuwa myembamba zaidi. Si ajabu mgonjwa anakuwa na ugumu wa kupumua!
Ni Nini Kinachosababisha Pumu?
Ni nini kinachofyatusha shambulio la pumu? Labda ni ambukizo, udhiko la maono ya moyoni, au wepesi wa kutiwa madhara makali na kitu fulani. Hata hivyo, mara ugonjwa huo ukiisha kufyatushwa katika mtu, huenda kukawa na vitendeshaji kadhaa, au vitu fulani hususa, vitakavyotokeza wepesi unaopita kiasi wa kuwashwa katika mirija ya hewa. Nayo mirija ya hewa ikiisha kutiwa wepesi wa kuwashwa na vitu hivyo, mambo mengine, kama mabadiliko ya halijoto, unyevu unaotofautiana katika hali ya hewa, maudhiko katika maono ya moyoni, au mazoezi, huenda pia yakasababisha mashambulio.
Huenda madaktari wakaweza kutambua vingine vya vitendeshaji vinavyoleta shambulio la pumu, lakini mara nyingi haiwezekani kuvipata vyote. Na hata vikipatikana, si sikuzote inapowezekana kuviepuka. Uchunguzi wenye kufanywa kweli kweli ili kupata visababishi vya pumu na njia bora kabisa ya kushughulika nao huenda ukachukua wakati. Huenda ukahusisha subira nyingi upande wa msumbukaji na daktari. Lakini inaelekea wakati huo unaotumiwa utatokeza uwezo mkubwa zaidi wa kuzidhibiti dalili.
Jinsi ya Kuepuka Mashambulio
Vitu vingi vinawasha mapafu na vinaweza kuamsha shambulio katika msumbukaji wa pumu. Jaribu kuepuka mgusano na vitu vinavyofuata.
Moshi wa Tumbako: Usivute sigareti, na epuka vyumba vilivyojaa moshi. Madaktari wanaacha upesi kuwaonea huruma wagonjwa wa pumu wanaosisitiza kuvuta sigareti. Na marafiki za mtu mwenye kusumbuliwa na pumu hawapaswi kuvuta sigareti mbele yake. Ingawa huenda mtu huyo asisumbuliwe na shambulio mara hiyo, saa kadhaa baadaye huenda mtu huyo akawa katika shida kubwa kwa sababu ya matokeo ya moshi.
Vumbi: Jaribu kuepuka maeneo ya mahali pa ndani penye vumbi, na pia utendaji unaotifua vumbi. Kazi yako ikikuleta katika mgusano na vumbi jingi, kwa uzito fikiria kuibadili. Wagonjwa fulani wa pumu wanapata kwamba dalili zao zinatukia usiku tu au katika chumba chao cha kulala. Je! hii ingeweza kuwa ni kwa sababu ya vumbi la nyumba au vijipande vidogo sana vya vumbi la nyumba? Katika visa vingi ndivyo ilivyo; basi, chumba cha kulala cha mgonjwa wa pumu kinapasa kuwekwa bila vumbi kwa kadiri inavyowezekana. Yanayofuata ni mengine ya madokezo ya kutunza nyumba yaliyokusudiwa hasa kwa wagonjwa wa pumu.
Kila siku safisha chumba cha kulala.
Kila juma, safisha na uondoe vumbi kweli kweli katika godoro, ulalio wa kitanda, blanketi, na sakafu. Sakafu za mbao ngumu ni nzuri kuliko vitambara vya kukanyagia au mazulia, na vigae vya vioo-madirisha ni vizuri kuliko vitambaa vya madirishani.
Toa vumbi kwenye fanicha, sehemu za juu za milango, fremu za madirisha, na vizingiti vya madirisha kwa kitambaa chenye umajimaji au mafuta.
Chumba kinapasa kufunguliwa hewa nyingi sana na milango na madirisha kufungwa baada ya hewa kuingia, angalau muda wa saa tatu kufika nne kabla ya mtu huyo kwenda kulala.
Godoro, blanketi, na mito haipasi kuwa ya vitambaa vinavyosababisha wepesi wa kupata madhara, na inapasa kupelekwa kwa ukawaida ikapigwe na hewa kwenye jua ikiwa inawezekana.a
Jambo moja zaidi. Usiruhusu wanyama vipenzi waingie katika chumba cha kulala. Na ikiwa kuna ushuhuda wowote kwamba wewe ni mwepesi wa kupata madhara kutokana na mnyama kipenzi chako, mtafutie makao mengine—au, angalau, sikuzote umweke nje ya nyumba.
Halijoto na Unyevu Hewani: Mabadiliko ya ghafula katika halijoto na hali zinazopita kiasi za joto na baridi huenda zikaamsha shambulio. Hali inayofaa kabisa ni kuwa na hewa yenye ujoto kidogo na uchepechepe. Basi, ikiwa wewe unasumbuliwa na pumu, enda nje kwa kadiri ndogo iwezekanavyo katika hali ya hewa yenye ukungu au baridi yenye kupenya. Epuka kupasha nyumba joto kali lenye ukavu. Ikiwa mabadiliko ya halijoto yanasababisha mashambulio wakati wa usiku, jaribu kuwa na kipasha-joto chenye kurekebishwa joto katika chumba chako wakati wa miezi ya kipupwe (baridi). Ikiwa unyevu wa hewa ndio unaotokeza dalili zako, jaribu kutumia kidhibiti-unyevu.
Mkazo wa Maono ya Moyoni na Uchovu: Lolote la mambo haya linaweza kusababisha shambulio la pumu. Ni kweli, hatuwezi sikuzote kudhibiti mkazo wa maono ya moyoni. Lakini wagonjwa wengi wa pumu wamepata kwamba kanuni za Biblia zinawasaidia katika eneo hili. Biblia inatuambia hivi: “Uhai wa mwili ni moyo mtulivu.” (Mithali 14:30, The Jerusalem Bible) Pia, wasumbukaji wa pumu walio na hekima wanajaribu kujua mipaka yao ya kimwili, kuepuka uchovu, ambao pia unaweza kufyatusha shambulio.
Chakula: Wepesi wa kufanyiwa madhara na chakula unaweza kuwa visababishi vya mashambulio ya pumu, hasa katika watoto au katika watu wazima ambao pumu yao ilianza utotoni. Hata vyakula vya kawaida, kama maziwa, mayai, na vyakula vya nafaka, vinaweza kutiliwa shaka. Lakini huenda kazi nyingi ya uchunguzi ikahitajiwa ili kujua kisababishi ni nini, hasa ikiwa ni kitu chenye kutumiwa mahali pengi, kama sukari. Na, bila shaka, ingeweza kuwa kwamba kinachohusika ni zaidi ya chakula kimoja. Wagonjwa watu wazima wangefanya vema kufikiria vileo, hasa pombe na divai, kuwa vinawezekana kuwa ni viongezea tatizo.
Mazoezi: Nyakati fulani shambulio la pumu linafyatushwa na kufanya kazi kupita kiasi, kwa kawaida likitokea baada ya kazi hiyo kumalizika. Ikiwa wewe umeona hivyo, epuka mazoezi yanayohusisha matumizi ya ghafula ya nishati, kama vile mchezo wa skwoshi, na ujaribu namna ya mazoezi ya hatua kwa hatua, kama kuogelea na kuendesha baiskeli. Labda itasaidia kutumia kipuliziaji-mirija-ya-hewa (dawa ya kuondoa mjazano katika mirija ya hewa) kabla ya utendaji wowote wa kujikaza. Tabibu wa mazoezi ya mwili huenda akaweza kukusaidia kwa programu itakayoongeza uvumilio wako wa mazoezi. Hii itakuwezesha ushiriki katika utendaji mwingi zaidi bila kupungukiwa na pumzi.
Ambukizo: Mara nyingi, maambukizo madogo ya upumuaji, kama mafua au influenza, yataamsha mashambulio ya pumu au kufanya dalili ziwe mbaya zaidi. Utibabu wa kawaida kwa kitulizo cha pumu hauwi na matokeo sikuzote kukiwa na ambukizo.
Kuishi na Chavuo (Unga-Unga wa Mimea): Ingawa miezi ya kipupwe inasababisha matatizo mengi kwa wale walio na ugonjwa wa upumuaji, wengi wanasumbuka kutokana na ile inayoitwa pumu ya majira. Vijipande vya chavuo isiyoonekana kwa macho inayoelea hewani wakati wa kiangazi vinaweza kusababisha huzuni na usumbufu usioelezeka kwa wenye kusumbuliwa na pumu. Haiwezekani kuondolea mbali vyanzo vya chavuo hii, lakini hatua fulani za kutumia akili zinaweza kusaidia. Kwa mfano, jaribu kuepuka viwanja ambavyo vimekatwa nyasi sasa hivi, na pia maeneo ya jangwa au nchi katika majira ya chavuo, na utumie chombo kinachopepea hewa vizuri ikiwezekana.
Kuishi na Kungu: Maelfu ya kungu, au kuvu, zinakaa katika mazingira yetu. Kungu na mbegu (vizalishaji) za kuvu juu ya mboga au wanyama. Pia hivyo ni tele juu ya ngano, oti, mahindi, manyasi, na majani. Ingawa ni idadi ndogo tu ambayo imeonyeshwa kuwa inasababisha matatizo kwa wasumbukaji wa pumu, uchunguzi mmoja katika New Zealand ulidokeza kwamba huenda mbegu zikawa ni kisababishi kikubwa cha wepesi wa kupatwa na madharaa. Basi, ingawa haiwezekani kuondolea mbali mbegu zilizo hewani, hatua zinazofuata huenda zikasaidia:
Epuka sehemu za chini ya nyumba na majengo yaliyo na uchepechepe.
Usikokote majani au nyasi kavu kwa reki wala usiviteketeze.
Tia dawa ya kuua maambukizo vitu vyovyote vyenye kungu au uviharibu.
Usiweke mimea ndani ya nyumba wala usiweke mahali pa kurundika takataka za kuzoea bustanini.
Ua viini vibaya katika maeneo ya nyumba yaliyoambukizwa ukuvu.
Je! Mtoto Wako Ni Mgonjwa wa Pumu?
Ikiwa ndivyo, atahitaji utegemezo wako. Wewe, na pia walimu wake, mtahitaji kuelewa tatizo lake na kumsaidia akabiliane nalo. Ni lazima mtoto asisukumwe kufanya mengi kuliko yale anayoweza, lakini pia asiruhusiwe kujificha nyuma ya pumu yake na kuepuka kufanya mambo ambayo yangemfaidi.
Utendaji wake wa kimwili ungekuwa afadhali uwe usio wa mashindano, ingawa watoto wengi wenye pumu wanaweza kucheza kadiri nyingi za michezo wakati wasipokuwa na dalili za ugonjwa. Hata hivyo, mtoto mwenye pumu ya wakati wote huenda akaweza kuonea shangwe utendaji wa kiasi tu, na watu wazima wanapaswa kuwa waangalifu wasimsukume kujaribu kwa bidii mno. Utumizi wa akili wa utibabu huenda ukamsaidia aonee shangwe utendaji wa ukawaida kama vile elimu ya kuzoeza mwili, na mfundishaji anapaswa kujua ni wakati gani na jinsi gani ya kutumia kipuliziaji mirija ya hewa.
Watoto wachache wanashikwa vikali sana na pumu hivi kwamba wanaendelea kuwa na ugumu wa kupumua na kukokota pumzi mara nyingi. Mara nyingi watoto wa jinsi hao ni wenye wasiwasi na hangaiko, na wazazi na walimu wao wanafanya wasiwasi sana juu yao. Mara nyingi watoto hao wanakosa kwenda shuleni na huenda wasiweze kujiunga katika michezo.
Huenda mzazi akalinda sana mtoto wa jinsi hiyo. Ikiwa mtoto anatoka nyumba ambako kuna mambo ya kuhangaisha daima na mabishano, huenda akakosa utegemezo, upendo, uelewevu, na kitia-moyo anachohitaji sana. Wazazi wanaofuata maoni yenye afya na kutazamia mazuri kwa habari ya pumu wanasaidia kupunguza wasiwasi katika mtoto, wakipunguza ukali wa kasoro hiyo.
Ikiwa Mtu Fulani Ana Shambulio . . .
Mpeleke mahali patulivu na umpe uhakikishio. Anaweza kusimama au kuketi akiegemea mbele, mara nyingi hiyo ikiwa ndiyo hali ya kustareheka zaidi wakati wa shambulio, naye anapaswa kutumia kipuliziaji-mirija-ya-hewa chake mara hiyo. Ikiwa kipuliziaji mirija ya hewa ni cha kuvuta hewa, huenda kikafanya kazi upesi zaidi na hivyo kiwe na matokeo kuliko dawa yenye kumezwa mdomoni. Ikiwa shambulio ni kali—hasa ikiwa msumbukaji hawezi kuongea inavyofaa—anapasa kupelekwa kwa daktari upesi iwezekanavyo. Na isisahaulike, mgonjwa anapoteza umaji mwingi wakati wa shambulio kwa sababu ya kutweta na kuhema. Kwa hiyo, mpe kinywaji tele.
Kutibu Mgonjwa wa Pumu
Utibabu wa mazoezi ya mwili ni msaada wa maana katika kusaidia mgonjwa wa pumu, hasa katika kumwonyesha jinsi ya kupumua inavyofaa (kwa kutumia kiwambo cha moyo) na jinsi ya kutuliza mtweto wa kukosa pumzi. Tabibu wa mazoezi anaweza pia kumfundisha kutuliza wasiwasi, kuwa na mkao mzuri, na kufanya mazoezi yanayosaidia kudhibiti pumu. Matibabu yanatofautiana. Kwa kawaida daktari ndiye mwenye anayestahili zaidi kudokeza matibabu yaliyo bora zaidi katika visa kimoja kimoja.
Matibabu ni kutia ndani utumizi wa dawa za kulevya, kama vile sodiamu kromolini na steroidi, na pia namna kadhaa za vipulizaji-mirija-ya-hewa. Bila shaka, kukiwa na utumizi wa dawa za kulevya, inawezekana ziambatane na madhara fulani. Huenda daktari akaweza kupendekeza matibabu mengine.
Pumu inatatanisha. Watu wa ukoo na marafiki ni lazima waelewe jambo hili ikiwa kweli wataweza kusaidia. Epukeni kusema mambo kama, ‘Wewe ondoa akili yako kwenye jambo hilo’ au, ‘Kwa maoni yangu unaonekana vizuri sana.’ Wasumbukaji wa pumu wanaojifunza kuelewa ugonjwa wao wanaweza kufarijika kwa kujua kwamba hata kabla ainabinadamu hawajaponywa magonjwa yote katika ulimwengu mpya wa Mungu, wanaweza kutayarishwa vizuri zaidi kwa mashambulio ya pumu, kutayarishwa vizuri zaidi kwa vifaa vya kuepuka mambo yenye kuyafyatusha, na kupunguziwa mkazo, wasiwasi, na hangaiko lao kwa kadiri kubwa. (Isaya 33:22, 24)—Imechangwa na msumbukaji wa pumu.
[Maelezo ya Chini]
a Nyakati fulani huenda mgonjwa wa pumu akawa mgonjwa mno kutoweza kufanya kazi hizi za nyumba. Kwa madokezo yenye msaada, tafadhali angalia ile makala “Makao Safi Japo Afya Mbaya” katika Amkeni! la Februari 22, 1982 (Kiingereza).
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 23]
HALI YA KAWAIDA
Musuli iliyolegea vizuri
Utando-ukamasi
Njiahewa isiyozuiliwa
SHAMBULIO LA PUMU
Musuli iliyokazika
Utando-ukamasi uliowashwa
Njiahewa isiyozuiliwa
Belghamu (kikohozi)