Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Ibada ya Maliki Katika makala yenu “Maziko ya Aliyekuwa Mungu” (Juni 8, 1990), lawama lenu liliwekwa mahali pasipofaa kuhusu pambano kati ya Japani na Magharibi. Jambo hili lilitokana na majaribio ya Magharibi kutawala Esia. Kuinuka kwa Japani ikiwa serikali kubwa ya ulimwengu kulizuia jambo hili. Maliki Hirohito hakuwa mungu, hapana, lakini labda Bwana alimtumia kuwa njia ya kuongoza watu wa Esia wenye kuonewa wafikie uhuru.
T. M., United States
Si jambo la akili kukata shauri kwamba ni Mungu aliyekubalia uharibifu mkubwa ulioletwa na pambano hilo. (Habakuki 1:13) Utawala wenye msiba wa Maliki Hirohito ulitumiwa kutoa kielezi cha kwamba utawala wa kibinadamu huumiza binadamu na kwamba binadamu ahitaji utawala wa Mungu tu. (Mhubiri 8:9)—MHARIRI.
Je! makala hizo zilikuwa njema na zenye kufaa kusomwa na Mkristo? Kwa kusoma hata mambo yale madogo-madogo juu ya Maliki Showa, je! ‘akili zetu haziko juu ya kazi za uovu’?—Wakolosai 1:21, NW.
Y. F., Japani
Ni jambo lenye kueleweka kwamba, makala hizo zingeweza kuamsha kumbukumbu zenye maumivu, hasa miongoni mwa wasomaji walioishi muda wa matukio yaliyosimuliwa humo. Hata hivyo, makala hizo ziliandikwa ili kufunua ujinga wa kuabudu binadamu yeyote na kuelekeza wasomaji kwenye “Mungu aliye hai.” (Matendo 14:15)—MHARIRI.
Kuchagua Kazi-Maisha Asanteni kwa shauri lenu kwa vijana juu ya thamani ya elimu ya chuo kikuu. (Februari 8, 1990) Kwa miaka 22 iliyopita, mimi nimekuwa profesa kwenye chuo kikuu cha mkoa mkubwa, nami naweza kuhakikishia wasomaji wenu wachanga kwamba zaidi ya kufanya yale mafikirio mazito juu ya hali ya kiroho, mengi yafunzwayo kwenye vyuo vikuu siku hizi hayana thamani yenye kutumika. Viwango vya masomo vimeshuka, na mara nyingi wahitimu hawawi na stadi nyingi za kuweza kupata kazi.
Pia, wakati uliopita, watu fulani walikuwa wamekata shauri kwamba Mkristo kijana alipaswa kulaaniwa vikali kwa kujiandikisha katika mitaala ya chuo kikuu chini ya hali zozote. Kwa hiyo mimi nathamini maoni yenye usawaziko yaliyoelezwa katika makala yenu.
F. S., United States
Ni lazima wazazi waamue ni kiasi gani cha masomo kiwafaacho watoto wao. Na ingawa kazi-maisha katika huduma yapendekezwa kwa vijana Wakristo, mazoezi fulani ya kazi yapitayo yale yatolewayo katika shule ya sekondari si mabaya hayo yenyewe. Katika mabara fulani, huenda ikafaa au hata ikahitajiwa kupokea mazoezi hayo. Ni lazima wazazi wapime uzito wa manufaa zilizopo dhidi ya athari ambazo mazoezi hayo yaweza kuleta juu ya hali ya kiroho ya watoto wao. Vyovyote vile, jambo la kutangulizwa na Mkristo lazima liwe ni kusogeza mbele masilahi za Ufalme, si faida ya kifedha. (Mathayo 6:33)—MHARIRI.
Wazazi wangu walikuwa wakiniambia nijifunze ustadi fulani shuleni, lakini mimi nikawa nikiisahau tu. Tangu niliposoma makala yenu, mimi nafanya mitaala itakayonisaidia kupata kazi nipendayo wakati niachapo shule. Lakini hata kama nitajifunza ustadi gani, mimi napanga kuifanya huduma iwe kazi-maisha yangu.
V. L., United States
Kuvuta Sigareti Kwa kweli jalada la toleo lililohusu “Kifo Chauzwa” (Machi 8, 1990) lilivuta uangalifu wa watu. Mimi humzuru kwa ukawaida mwanamke mzee-mzee ambaye huvuta mfululizo. Kwa miaka kadhaa yeye amekuwa na andikisho la Amkeni! lakini ni mara haba ambapo yeye huzisoma makala. Hivi majuzi, nilimtembelea nikaona kwamba hatimaye ningeweza kupumua nikiwa nyumbani mwake. Ndiyo, alikuwa akijaribu kuacha kuvuta sigareti. Alipoona toleo hilo, alilisoma kutoka jalada hadi jalada na sasa ataka kujifunza Biblia na kuja kwenye Jumba la Ufalme. Asanteni kwa uvutio wa macho ulio katika magazeti yetu!
C. P., United States