Maziko ya Aliyekuwa Mungu
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Japani
Baada ya kutawala kwa miaka zaidi ya 62, Maliki wa Japani Hirohito alikufa Januari 7 mwaka juzi. Alikuwa na miaka 87. Wawakilishi kutoka nchi 164 walihudhuria maziko yake mnamo Februari 24. Hata hivyo, wengi walitatizika kwa uchungu juu ya kama wahudhurie au wasihudhurie. Kwa nini? Nacho kifo cha Hirohito kina uhusiano gani na lile swali kwenye jalada letu: Je! Mungu Wako Yuko Hai?
“MALIKI HIROHITO alionwa kuwa mungu aliye hai,” lilisema Japan Quarterly mapema mwaka jana. Kodansha Encyclopedia of Japan kinamworodhesha kuwa mzao wa kibinadamu wa 124 wa mungu-mke-jua Amaterasu Omikami, ambaye anatambuliwa kuwa “mungu mkuu wa hekalu la miungu wote wa Shintō.”
Kwa hiyo wakati askari-jeshi Wajapani walipoulizwa wadhabihu maisha zao kwa ajili ya huyu “mungu aliye hai,” walifanya hivyo kwa ari yenye kustaajabisha. Hakukuweko wapiganaji wakali zaidi wakati wa vita ya ulimwengu ya pili kushinda wajitoaji Wajapani ambao walipigania mungu wao, maliki huyo.
Hata hivyo, kwa kuzidiwa na maejshi ya kivita yenye hesabu kubwa, Wajapani walishindwa vita hiyo. Miezi inayopungua mitano baadaye, mnamo Januari 1, 1946, Hirohito, katika amri yenye kufanyiza historia, alikanusha mbele ya taifa “wazo bandia kwamba Maliki ni wa kimungu.” Yeye alisema kwamba “hadithi tu za kimapokeo na za kitamaduni” ndizo zilisababisha imani hiyo.
Ilishtua kama nini! Mamilioni ya Wajapani waliduwaa sana. Kwa miaka zaidi ya 2,600 maliki alikuwa ameonwa kuwa mungu!a Na sasa si mungu tena? Binadamu huyu ambaye wakati mmoja alitukuzwa sana hata kwamba hawangeinua macho yao wamtazame, yeye si mungu? Kuiacha imani hiyo iliyokuwa imeshikiliwa muda mrefu kwamba maliki huyo alikuwa wa kimungu haikuwa rahisi. Kwa kweli, askari-jeshi Wajapani kadhaa wa milki ya hapo zamani walijiua walipopata habari za kifo cha Hirohito, kwa kufuata utamaduni wa karne nyingi.
Kwa kweli, Hirohito alikuwa nani? Na nini kilichofanya fungu lake katika historia kutokeza ubishi? Mnamo Februari 24, 1989, gari lenye kuchukua jeneza lake likitoka kwenye Makao ya Milki katika Tokyo na likiwa linaelekea bustani ya Shinjuku Gyoen kwa ajili ya maziko ya serikali, mamilioni ya watazamaji wa televisheni na watazamaji wapatao 200,000 kando ya barabara walipata fursa ya kufikiria maswali hayo.
Mtu Huyo na Utawala Wake
Hirohito, linalomaanisha “Mkarimu Mwenye Akili Pana,” ndilo jina alilopewa mwana wa Maliki Taisho alipozaliwa mnamo Aprili 29, 1901. Siku ya Krismasi 1926, babake alipokufa, Hirohito alichukua mahali pake kuwa maliki. Jina lililochaguliwa na wasomi wa baraza la enzi ya utawala wake lilikuwa Showa, au Amani Yenye Maarifa. Kwa hiyo baada ya kifo chake, akaja kuitwa, si Maliki Hirohito, bali Maliki Showa.
Hata hivyo, sehemu ya mapema ya utawala wa Hirohito haikuwa yenye amani yenye maarifa, tukifikiria hatua za kijeshi za Kijapani katika Manchuria na China katika miaka ya 1930, uvamizi wa India-China ya Ufaransa mnamo 1940, na shambulizi juu ya United States mnamo 1941. Jina la utawala wa Hirohito ni kinyume hasa wakati mtu anapofikiria kwamba wakati wa miaka ya mapema, kwa halisi mamilioni ya uhai yalikomeshwa na vita vilivyopiganwa kwa kibali chake.
Ijapokuwa kusitawi kwa uchumi wa Japani baada ya vita si kila mtu anayefikiria kipindi cha amani ambacho Japani imeonea shangwe kuwa amani yenye maarifa. “Ninapoangalia nyuma kwenye Enzi ya Showa, naona ubatili,” alisema mtunzi Mjapani, Sue Sumii mwenye miaka 86. Tangu Japani ishindwe vitani, nafikiri nchi imekuwa ikizorota . . . ufanisi wa Japani ni mazingaombwe.
Mchanganyiko wa Hisia
Nyingi za nchi ambazo Japani ilipiga ubwana na kupigana dhidi yazo zililazimika kuridhiana kwa kupeleka wawakilishi kwenye maziko ya Hirohito. Kwa kielelezo, Wakorea, walikuwa wangali wanatambua ‘hitilafu iliyoachwa kwenye nchi yao’ na upigaji ubwana wa Japani kwenye Peninsula ya Korea “katika jina la Maliki.” Katika magazeti ya Uingereza, kulikuwako wito maziko hayo yagomewe. Wengi hawangeweza kusahau kwamba wafungwa wa vita Waingereza wapatao 27,000 walikufa mikononi mwa jeshi la maliki huyo.
Hali ilikuwa moja katika United States, ambako lawama kubwa ya uchokozi wa jeshi la Japani inawekelewa juu ya Hirohito. Ni kama makala ya mhariri ya New York Times ilivyosema wakati wa kifo chake: “Katika cheo chake cha kutukuzwa, yeye angeliweza kuuepusha ulimwengu na msiba mkubwa.”
Hata katika Japani, ambako Hirohito kwa ujumla ametukuzwa kuwa maliki mpenda-amani, wengine wanahisi kwamba ana lawama kubwa. Katsuro Nakamura akumbuka kwamba alipopata habari za kifo cha kakake katika vita, babake alisema: “Mwanangu aliuawa na yule jamaa Hirohito.” Mwanamume mwingine mzee Mjapani, Masashi Inagaki, alieleza: “Kwa muda mrefu nilimlaumu yeye kwa ajili ya vita ambamo tulilazimika kuteseka sana.” Lakini yeye aliongeza hivi: “Hisia zangu za uchungu zilianza kupungua nilipotambua kwamba maliki mwenyewe alilazimika kubeba mambo ya jadi maishani mwake mwote.”
Itibari Inapowekwa Pasipofaa
Yaweza kusemwa kwamba mamilioni ya Wajapani walitoa maisha zao kwenye madhabahu ya mungu huyu wa Shinto, bila kutaja uhai wa mamilioni ya wengine waliotolewa kwenye madhabahu hiyo hiyo na majeshi ya maliki huyo. Wale walioamini waliingizwa katika vurugu ya hatua za kijeshi katika jina la mungu wao, ndipo tu wakatambua baadaye kwamba kumbe hakuwa mungu. Ni kama Asahi Evening News lilivyosema: “Mamilioni ya Wajapani walikuwa wamedhabihiwa na uelewevu huo wenye makosa.”
Itikio la waumini lilikuwa nini wakati mungu wao alipokanusha yeye si mungu mnamo 1946? Mmoja aliyekuwa amepigania maliki huyo alisema kwamba alihisi kama “mashua iliyopoteza usukani wake katikati ya bahari kuu.” Itikio lake liliwakilisha wengi. Wale waliookoka vita “ghafula walitupwa ndani ya shimo tupu,” aomboleza Sakon Sou, mtunga mashairi Mjapani. Wangeweza kujazaje utupu huo?
“Nilikuwa nimepumbazwa kabisa. Nilikuwa nimepigana si kwa ajili ya Mungu bali kwa ajili ya binadamu wa kawaida,” asema Kiyoshi Tamura. “Sasa baada ya hilo ningeamini nini?” Kiyoshi alifanya kazi juu-chini apate mali, lakini zikashindwa kumliwaza. Imani yako inapovunjwa-vunjwa, thamani zenye ubatili zaweza kuingia haraka kujazia utupu huo.
Somo laweza kupatikana kwa kufikiria juu ya Maliki Showa na maziko yake. Ni kwamba kuabudu ‘usichokijua’ kunaleta msiba. (Yohana 4:22) Wewe unaabudu nani? Je! wewe una msingi imara wa kuamini kwamba mtu huyo ndiye Mungu na kwamba yeye anastahili ibada yako?
Sisi sote tunahitaji kulifikiria jambo hilo, kwa kuwa hata leo watu fulani, kama vile Dalai Lama, wanaonwa kuwa Mabuddha walio hai, nao wanaabudiwa na watu waliojitoa kwao. Wengi wanaodai Ukristo wamefundishwa kuamini katika Utatu, na kwa hiyo wanamwabudu Mungu wa utatu ambaye anadhaniwa anashirikisha Baba, Mwana, na roho mtakatifu. Chunguza katika makala inayofuata jinsi Wajapani walivyoongozwa waamini mungu ambaye kwa kweli siye Mungu, na uone tunayoweza kujifunza kutokana na hilo.
[Maelezo ya Chini]
a Ingawa wamaliki wa mapema katika ile orodha ya 124 (125, kuhesabu Akihito, mwanaye Hirohito) inabainika ni wa hadithi ya kimapokeo, kuanzia angalau karne ya tano W.K. au mahali hapo, wamaliki wamekuwa ni watu halisi. Hilo linafanya mpango wafalme wa kurithi wa kimilki wa Japani kuwa wa kale zaidi katika ulimwengu
[Picha katika ukurasa wa 2]
Maandishi ya Kijapani (juu kushoto) yamaanisha “mungu”
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Hirohito (ng’ambo nyingine): U.S. National Archives photo