Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 8/8 kur. 29-30
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • KATEKISIMU MPYA YASHAMBULIWA
  • UKIMWI—TAZAMIO LISILO NA MATUMAINI
  • “MGODI WA DHAHABU” YA MITI-SHAMBA?
  • AMBUKIZO LA UVUTAJI SIGARETI
  • UVUMBUZI MPYA WA MIANZI
  • WAKATI UHAI UNAPOLETA KIFO
  • KUMBUKUMBU ZA MISRI ZAHATARISHWA
  • JAMII MPYA YA WANYAMA YAGUNDULIWA
  • MATOKEO MAZITO JUU YA MAISHA YA FAMILIA
  • Mfumo Tata wa Viumbe
    Amkeni!—2001
  • UKIMWI—Matokeo Yenye Msiba Mkubwa kwa Watoto
    Amkeni!—1992
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1992
  • Utafutaji Wenye Kusisimua wa Dawa Zilizo Mpya
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1991
g91 8/8 kur. 29-30

Kuutazama Ulimwengu

KATEKISIMU MPYA YASHAMBULIWA

Vatikani, kwa mara ya kwanza tangu karne ya 16, inasahihisha katekisimu yake. Lakini ule muhtasari wa kurasa 434 wa fundisho la Roma Katoliki umeshambuliwa na baadhi ya maaskofu katika United States. ‘Waliiambia Vatikani kwamba ile katekisimu mpya inatumia elimu ya kale kabisa ya kibiblia na semi za kuonyesha uume au uke na hubadili maendeleo ambayo yamefanywa na maaskofu wa ulimwengu mzima katika miongo ya karibuni,” yasema U.S.News & World Report. “Maaskofu waliiona ikiwa na kasoro kwa kuchukua habari za uumbaji kwa uhalisi na kwa kutumia mistari fulani ya Agano Jipya kama ‘ripoti ya moja kwa moja ya kihistoria.’” Maoni mabaya yanatolewa, wakasema maaskofu, “kwamba sehemu zote zinalingana umaana.” Walitoa hoja kwamba mafundisho “ya muhimu” ya kanisa, kama vile ufufuo wa Yesu, yanapaswa yatofautishwe na mafunzo ambayo, kwa maoni yao, hayaaminiki sana, kama vile kuwapo kwa malaika na kushuka kwa Kristo katika helo. Wakati itakapokamilishwa, katekisimu hiyo mpya “itatumika kama mwongozo tu kwa viongozi wa kanisa katika kila nchi kwa jinsi wanavyounda katekisimu zao wenyewe,” yasema U.S.News & World Report.

UKIMWI—TAZAMIO LISILO NA MATUMAINI

Watu milioni nane kufikia kumi duniani wameambukizwa ile vairasi ya UKIMWI, laripoti WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni), ongezeko ambalo laonyesha ukuzi wa mpisho wa vairasi hii kati ya watu wa jinsia tofauti wanaofanya ngono. “Ni wazi sasa kwamba idadi ya maambukizo ya HIV kuzunguka tufe lote inakuwa mbaya kwa haraka sana, na hasa katika nchi zinazoendelea kusitawi,” asema Dkt. Michael H. Merson, mkurugenzi wa shirika hilo. Shirika la Afya Ulimwenguni linatabiri kwamba ongezeko katika maambukizo litaleta kifo kwa angalau wanawake na watoto milioni tatu katika miaka ya 1990, zaidi ya mara sita idadi ya watu waliokufa kwa UKIMWI katika miaka ya 1980. Idadi ya wanaume watakaokufa kutokana na UKIMWI wakati wa mwongo huo inatarajiwa iwe ya juu hata zaidi. Mamilioni ya watoto wasioambukizwa watakuwa yatima baada ya kupoteza wazazi wao. Kulingana na ripoti hiyo, UKIMWI tayari ndicho kisababishi cha kwanza cha vifo vya wanawake wa miaka 20 kufikia 40 katika majiji makubwa katika Amerika, Ulaya Magharibi, na maeneo ya Afrika yanayokaribia kuwa jangwa, mahali ambako karibu 1 katika 40 ya wanaume na wanawake wa umri mkubwa wanasemwa kuwa wameambukizwa.

“MGODI WA DHAHABU” YA MITI-SHAMBA?

Je, nchi kama Brazili zingeweza kufanya misitu yazo yenye mvua nyingi iwe yenye faida? Labda, kulingana na nakala moja katika Scanorama (gazeti la Mfumo wa Ndege Skandinevia): “WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni) ladokeza . . . kufanya kilimo cha bustani za miti-shamba na kuuza mimea iliyo dawa. Ole Hamann Mholanzi mwenye elimu ya mimea asema kwamba yeye huona miradi hiyo kuwa yawezekana kuwa ‘mgodi wa dhahabu’ kwa nchi zinazositawi.” Namna gani hivyo? Wingi wa mimea katika misitu yenye mvua nyingi, katika visa vingi ikiwa bado kujaribiwa kuonwa kama ina uwezo wa kuwa dawa, ni mwito wa ushindani kwa wavumbuzi. Mimea kama 250,000 tayari imetambulishwa, lakini “wenye elimu ya mimea wanakadiria kwamba aina ya mimea mingine 30,000 sana-sana ikiwa ya kitropiki, bado haijajulikana na wanasayansi.” Mingi ya mimea hii huenda ikathibitika kuwa yenye faida katika kukinga magonjwa mbalimbali, kwa sababu, “kati ya dawa zote za kuagizwa na daktari Magharibi, angalau asilimia 25, na labda kukaribia zaidi nusu, zina visehemu-sehemu vya asili vinavyopatikana katika mimea.”

AMBUKIZO LA UVUTAJI SIGARETI

“Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, utumizi wa tumbako umeongezeka katika tufe lote kwa karibu asilimia 75,” laripoti JAMA (Jarida la Shirika la Kitiba la Kiamerika), na “ni kisababishi cha vifo karibu milioni 2.5 kwa mwaka vinavyopita kiasi au vifo vinavyotokana na kujifungua mapema—karibu asilimia 5 ya vifo vyote.” Ingawa maagizo ya bidhaa za tumbako yamepunguka katika nchi zilizositawi kiuchumi, mataifa yanayositawi, hasa katika Asia ya Kusini-mashariki, Afrika, na Amerika ya Kilatini, yameona mwinuko katika idadi ya watu wanaovuta sigareti. United States, kwa mfano, imejipata yenyewe katika hali yenye aibu ya kuunga mkono kampeni ya kutovuta sigareti kwa watu wake yenyewe huku ikitilia mkazo kufunguliwa kwa masoko mapya ya kigeni kwa ajili ya bidhaa zake za tumbako ili kusaidia kupunguza kasoro za biashara. Kulingana na ripoti hiyo, kwa kukadiria watoto milioni 200 walio chini ya miaka 20 sasa mwishowe watakufa kutokana na utumizi wa tumbako, na vifo vya kansa ya mapafu vitaongezeka ulimwenguni pote viwe milioni mbili ufikapo mwaka 2000.

UVUMBUZI MPYA WA MIANZI

Mianzi. Kulingana na Asiaweek robo moja ya idadi ya watu ulimwenguni inaitegemea kwa chakula, kilaji cha wanyama wa kufugwa, samani (fanicha), majukwaa ya kujenga juu, na bidhaa za karatasi. Panda wakubwa husitawi kwayo. Ni yenye nguvu, haiozi, na ni myepesi. Lakini aina nyingi za mianzi huchanua na kuzaa mbegu mara moja tu, ikichukua kutoka miaka 12 kufikia 120 kufanya hivyo, bila shaka ikiwa ni kulingana na saa iliyopangiliwa ndani yayo, na baada ya haya, kichaka chote cha mianzi kinakufa. Kufikia sasa kitabia hiki kimezuia majaribio ya kisayansi kufanyiza aina bora zaidi, kwa sababu aina ambayo ni ya maana sana kiuchumi huchukua miaka 30 kuchanua na hivyo basi mara nyingi huishi zaidi ya wale wanasayansi wanaohusika. Gazeti Nature lataarifu kwamba wenye elimu ya mimea sasa wanasema kwamba wamegundua njia ya kuishinda ile saa katika aina mbili za mianzi na kuchochea mchanuo wa mapema ambao unaweza kufanya mazao ya aina bora zaidi yawezekane na kupata mwandalio wenye kuendelea wa mbegu za kupanda. Kwa kuweka mimea michanga katika mchanganyo maalumu wa ukuzi, maua mazima kabisa yalitokezwa katika muda wa majuma machache, na yaliyo mengi yalizaa mbegu baada ya kuchanua.

WAKATI UHAI UNAPOLETA KIFO

“Wazia,” asema mtaalamu mmoja mwenye elimu ya mimba na ukunga Malcolm Potts, “kwamba kila muda wa saa sita, siku nenda, siku rudi, jumbo jeti moja huanguka, na wote waliomo kwenye ndege hiyo hufa. Abiria hao 250 ni wanawake, wengi wao wakiwa katika upevu wa maisha yao, wengine wakiwa bado katika miaka yao ya utineja. Wote ama ni waja-wazito au ndiyo sasa tu wamezaa mtoto. Wengi wao wana watoto wanaokua nyumbani, na familia zinazowategemea.” Kifananishi hicho kinaonyesha wanawake nusu milioni duniani mwote kila mwaka wanaokufa wakati wa mimba au wanapokuwa wakizaa. “Vyote isipokuwa asilimia moja ya vifo hivi vya uzalishaji vinatukia katika ulimwengu unaositawi,” yasema New Scientist. “Wauaji wakubwa zaidi ni mvujo wa damu, maambukizo, sumu ya viini vya ugonjwa damuni, kuzibwa kwa uzalishaji na utoaji mimba usiofanywa kwa ustadi.” Mimba zisizotakwa huongoza kwenye uuaji mkubwa wa kila mwaka wa mama wengi na viinitete. “Kila mwaka kati ya wanawake milioni 40 na 60 hutafuta utoaji mimba,” gazeti hilo lasema.

KUMBUKUMBU ZA MISRI ZAHATARISHWA

Ule ujenzi wa Aswan High Dam katika miaka ya 1960 “ulileta badiliko kubwa katika mazingira ya Bonde la Naili,” yasema New York Times. “Maji ya ardhini chini ya nguzo za sanamu yamepanda; hewa ina joto lenye unyevunyevu zaidi kwa sababu ile mifereji ya kunyunyizia maji haiishi maji kamwe; aina za chumvi katika udongo zinavutwa kupitia upande wa mbele wa nyumba za kale, zikiibandua kutoka kwa jiwe lililoko chini; mifereji ya maji machafu imeharibu udongo.” Kama tokeo, hazina za kiakiolojia za Misri—zenye eneo kubwa zaidi ulimwenguni—na ambazo zimezidi kuwapo kwa mileani nyingi sasa zinatishwa vikali. Ithibati imeongezeka ikionyesha kwamba hata maeneo yasiyochimbuliwa bado, ambayo hapo mwanzoni yalifikiriwa kuwa salama na yenye ulinzi, tayari yameharibiwa. Wastadi wametatizwa na ukubwa wa tatizo hilo, wasijue la kufanya. “Kuna maziara (makaburi) zaidi ya 2,000, nguzo za sanamu, piramidi, nguzo ndefu zilizochongoka juu,” asema Sayed Tawfiq, mkurugenzi wa tengenezo la uhifadhi wa vitu vya kale vya Misri katika Cairo (Shirika la Vitu vya Kale Katika Cairo). “Kama ungepatia kila ziara miaka miwili ya kutengenezwa, hiyo ingekuwa miaka 4,000.”

JAMII MPYA YA WANYAMA YAGUNDULIWA

Kila mwaka wanasayansi wanagundua jamii mpya zaidi ya 10,000 za mimea na wanyama. Idadi kubwa ya hizi ni wadudu, kukiwa na wanyama wapya watano kufikia kumi wa kunyonyesha na idadi kama hiyo ya ndege wenye kutambulishwa kila mwaka. Hata hawa waonekane wakiwa wengi jinsi gani, wanabayolojia bado wana mwendo mrefu wa kwenda. Kuna idadi inayokadiriwa ya jamii 50 za mimea na wanyama milioni 50 katika ulimwengu, na chini ya milioni 1.5 zimegunduliwa na kuorodheshwa. Ugunduzi wa mnyama mpya anayenyonyesha, tamarini-simba (nyani) mwenye uso mweusi, juzijuzi ulivuta uangalifu, kwa vile aligunduliwa akiwa si zaidi ya kilometa 320 kutoka mji ulio wa tatu kwa ukuu ulimwenguni, kando ya fuo za bahari za Brazili zenye watu wengi sana. Misitu ya kitropiki inapotokomea, inahofiwa kwamba aina za wanyama na mimea zitatoweka haraka sana kuliko vile zinavyoweza kupatikana.

MATOKEO MAZITO JUU YA MAISHA YA FAMILIA

“Muundo wa familia unategemea sana afya ya watoto na maendeleo,” yasema nakala moja katika The Wall Street Journal. Takwimu za kutoka “uchunguzi wa kiserikali wa U.S. juu ya afya na hali za moyoni za watoto kama 17,000 wenye kadiri ya miaka kuanzia uchanga kufikia 17” zilifunua kwamba “watoto wanaoishi katika familia zisizo na wazazi wa asili walikuwa na matatizo makubwa kuliko wale walioishi na wazazi wote wa asili.” Hatari ya kupata aksidenti au umizo mwakani kabla ya uchunguzi huo ilikuwa asilimia 20 kufikia 30 zaidi kwa watoto walioishi na mama aliyetalikiwa au aliyeolewa tena. Wakilinganishwa na wale walioishi na wazazi wote wawili wa kibayolojia, watoto hao walielekea zaidi kurudia darasa kwa asilimia 40 kufikia 75. Watoto kutoka ndoa zilizovunjika walielekea zaidi kufukuzwa kwa muda au hata kwa kudumu kutoka shuleni kwa asilimia 70; na wale ambao mama zao hawakuwa wameolewa walielekea kwa mara mbili kupatwa na matatizo hayo. Watoto walio katika familia zenye kuongozwa na mama walielekea zaidi kwa asilimia 50 kupatwa na ugonjwa wa pumu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki