Mazingira-Jinsi Yanavyoathiri Afya Yako
HIVI karibuni, Dakt. Walter Reed, wa shirika la World Resources Institute, aliiambia Redio ya UM kwamba athari ambayo mwanadamu amesababisha kwenye mifumo ya kimazingira sasa ni ya kiwango kikubwa sana ambapo mwanadamu “anavuruga mizunguko hii sana.” Dakt. Reed asema kwamba mvurugo huu wa kimazingira, unachangia vitisho vya afya ulimwenguni pote. Katika makala iliyokuwa ikipitia kitabu World Resources 1998-99, gazeti Our Planet, linalochapishwa na Umoja wa Mataifa, linaorodhesha baadhi ya vitisho hivyo kwa afya ya watu. Miongoni mwake ni kama vifuatavyo:
□ Uchafuzi wa hewa ndani na nje ya nyumba umehusianishwa na maambukizo ya upumuaji ambayo husababisha vifo vya watoto takriban milioni nne kila mwaka.
□ Ukosefu wa maji safi na usafi wa afya huchangia kuenea kwa maradhi ya kuharisha ambayo husababisha vifo vya watoto milioni tatu kila mwaka. Mathalani, kipindupindu, kilichokuwa kimemalizwa kabisa kutoka Amerika ya Latini, kiliibuka tena katika sehemu hiyo na kuua watu 11,000 katika mwaka wa 1997 peke yake.
Inaripotiwa kwamba kila siku zaidi ya watoto 30,000 katika maeneo yenye umaskini zaidi ulimwenguni hufa kwa sababu ya maradhi yanayohusiana na mazingira. Ebu wazia watu—30,000 kila siku katika mwaka, wanaotosha kujaza viti vyote vya ndege aina ya jumbo jet zipatazo 75!
Hata hivyo, vitisho vya kimazingira kwa afya, havipo tu katika nchi zinazositawi. Gazeti Our Planet lasema kwamba “zaidi ya watu milioni 100 katika Ulaya na Amerika Kaskazini wangali wanapumua hewa isiyo salama,” ambayo huchangia kuongezeka kwa ugonjwa wa pumu. Wakati huohuo, ongezeko la safari na biashara ya kimataifa limechangia kuibuka kwa maradhi mapya yenye kuambukiza yapatayo 30 katika nchi zilizositawi. Kwa kuongezea, gazeti hilo liliripoti kwamba maradhi ambayo yalikuwa yamedhibitiwa hapo awali “yameibuka tena kwa kiwango kikubwa sana.”
Jambo lenye kuhuzunisha ni kwamba mengi ya maradhi haya yanayohusiana na mazingira yanaweza kuzuiwa kwa kutumia tekinolojia iliyopo na kwa gharama ya chini kiasi. Kwa kielelezo, maendeleo yenye maana yangeweza kufanywa kwa kuandalia watu wote maji safi na usafi wa afya. Ni pesa ngapi zingehitajiwa kutimiza mradi huo? Redio ya UM yaripoti kwamba kulingana na Human Development Report 1998 ya Umoja wa Mataifa, kuandalia kila mtu maji safi na usafi wa afya kungegharimu dola bilioni 11—hicho ni kiasi cha pesa kinachopungua pesa ambazo Wanaulaya hutumia kwa aiskrimu kwa mwaka mmoja!
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
Picha: Casas, Godo-Foto