Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 7/8 kur. 14-19
  • Sydney—Jiji la Bandari Lenye Pilikapilika

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sydney—Jiji la Bandari Lenye Pilikapilika
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mahali pa Kuadhibia Wafungwa Pawa Jiji Lenye Kusitawi
  • Jiji Laanza Kuibuka
  • ‘Bandari Pana Yenye Kuvutia’ ya Sydney
  • Daraja la Bandari ya Sydney—Uhandisi Bora
  • Kito cha Sydney Kwenye Bandari
  • Jinsi Jumba la Opera Linavyofanana Ndani
  • Usikose Kutembelea Makao ya Wanyama!
  • Wasafirishwa Hadi Botany Bay
    Amkeni!—2001
  • Vijana Wakatoliki Wahimizwa Watoe Ushahidi
    Amkeni!—2009
  • Usiku Mmoja Kwenye Opera
    Amkeni!—1994
  • Kupiga Moyo Konde Kulinisaidia Nifanikiwe
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1987
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 7/8 kur. 14-19

Sydney—Jiji la Bandari Lenye Pilikapilika

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

WEWE hukumbuka nini usikiapo maneno “Sydney, Australia”? Je, wewe hufikiria mara moja jumba la kipekee la opera kwenye ukingo wa maji, na lenye paa zinazochomoza kama tanga za mashua au kama magamba makubwa? Ikitegemea upendezi wako, hiyo ndiyo picha uwezayo kuwazia.

Yasemekana kwamba Sydney—ambalo ni jiji kuu la kuingia Australia—ni mojawapo ya majiji yenye kuvutia zaidi ulimwenguni. Sydney ni jiji kuu la mkoa wa New South Wales, ambao ndio mkoa wenye watu wengi zaidi. Lakini jiji kuu la taifa ni Canberra, ambalo liko katikati hivi baina ya Sydney na Melbourne.

Kwa kawaida wakazi wa Sydney, ambao hupenda kuitwa Sydneysiders, ni wapole na wenye urafiki. Sydney hurejezewa mara nyingi kwenye nyimbo zinazopendwa kuwa “Sydney Town,” nalo ni mashuhuri kwa angalau mambo matatu: (1) bandari ya asili yenye kilindi, (2) daraja la bandari lenye kuvutia sana na ambalo halina nguzo za katikati, na (3) jumba la kipekee la opera.

Hali ya hewa ni yenye kiasi, na wastani wa joto katika mwezi wa Februari, ambao ndio mwezi wenye joto zaidi, ni nyuzi 22 Selsiasi, huku Julai ambao ni mwezi baridi zaidi, ukiwa na wastani wa nyuzi 12 Selsiasi. Mvua nchini Australia hunyesha ghafula-ghafula nayo haitabiriki, lakini wastani wa milimeta 1,140 za mvua hunyesha kwa mwaka Sydney, mvua nyingi ikinyesha wakati wa miezi ya kiangazi (Desemba hadi Machi).

Utasikia mengi zaidi kuhusu Sydney katika miezi ijayo kwa sababu limeteuliwa kuwa jiji la kufanyia Michezo ya Olimpiki mwaka wa 2000.

Mahali pa Kuadhibia Wafungwa Pawa Jiji Lenye Kusitawi

Sydney ni jiji changa likilinganishwa na majiji mengine makubwa ya ulimwengu kwa sababu lilianza miaka 200 tu iliyopita mnamo mwaka wa 1770, wakati mvumbuzi wa Uingereza Kapteni James Cook alipoweka historia kwa kutia nanga kwenye Ghuba ya Botany. (Sasa kuna uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sydney kwenye ufuo wa kaskazini wa Ghuba ya Botany.) Alipoabiri kilometa chache kuelekea kaskazini, alipita bandari ya asili yenye kilindi ambayo aliiita Port Jackson. Lakini hakuingia kwenye lango lililokuwa katikati ya rasi mbili la kuingilia bandari.

Kisha mwaka wa 1788, Gavana Arthur Phillip alifika kutoka Uingereza kwa Meli za Kwanza zilizowabeba wafungwa wa Uingereza. Alishukia hapo akaanzishe makao kwenye Ghuba ya Botany lakini akaamua kwamba mahali hapo hapakufaa. Basi akachukua mashua tatu akaabiri kuelekea kaskazini akatafute mahali bora.

Na kwa kweli alipoenda kilometa chache tu, akagundua ghuba pana ajabu na yenye kilindi ambayo Cook alipita bila kujua. Katika taarifa yake ya dharura na iliyo maarufu ambayo alimpelekea Lord Sydney, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza, Phillip alisema hivi kuhusu Port Jackson: “Tulifurahi . . . kupata bandari nzuri zaidi ulimwenguni, ambamo meli elfu moja zaweza kufuatana pamoja kwa usalama kabisa.” Kwa heshima ya Lord Sydney, Phillip aliiita ghuba hiyo Ghuba ya Sydney naye akaanzisha makao ya kwanza hapo. Jina Sydney likadumu hadi leo hii.

Wafungwa wote wa kiume wakashuka na mara moja wakaanza kazi ya kufyeka na kujenga vibanda. Meli hizo zilibeba wafungwa wengi na vilevile wake kadhaa na watoto, na wote hao walilazimika kung’ang’ana na maisha katika “makao” hayo mapya waliyoshurutishwa kuja na ambayo yalikuwa maelfu ya kilometa kutoka nchi yao. Kwa miaka 20 iliyofuata, makao hayo yalikuwa tu mahema na vibanda kwa kuwa awali kusudi lilikuwa kwamba mahali hapo pawe tu mahali pa kuadhibia wafungwa. Lakini, mwaka wa 1810, Gavana Lachlan Macquarie alifika Sydney, na kukaa kwake hapo kwa miaka 11 kulitokeza mabadiliko ya haraka kwenye makao hayo.

Jiji Laanza Kuibuka

Chini ya mwelekezo wa Macquarie, msanifuujenzi mmoja ambaye alikuwa ameandamana naye kutoka Uingereza, akisaidiwa na mfungwa mmoja aliyekuwa ameachiliwa huru na ambaye pia alikuwa msanifuujenzi, alitayarisha michoro ya majengo mengi katika Sydney na vitongoji vyake. Jambo hilo likawafanya wafungwa wawe na hisia ya udumifu wa makao hayo. Hakukuwa na tatizo la wafanyakazi kwa kuwa wafungwa walijaa tele. Na vilevile mawe-mchanga yaliyofaa sana ujenzi yalijaa tele.

Mwandishi Portia Robinson, afafanua mageuzo ya haraka yaliyotokea katika kitabu chake The Women of Botany Bay: “Wageni, walowezi, maofisa, wanajeshi, na wafungwa waliofika New South Wales katika miaka ya baadaye ya Macquarie [1810-1821] walishangaa kuona ‘ustaarabu wake’ kwa kuwa walitarajia kupata ufasiki, ulevi na ukosefu wa adili kingono, tabia ambazo ziliaminiwa huko Uingereza kuwa zilikuwa zimekolea kwenye makao haya. Badala ya vibanda waliona majumba yenye fahari ‘ambayo yangestahili kuwa Hanover Square . . . barabara ndefu za mjini kama Barabara ya Oxford,’ makanisa na majengo ya umma yenye fahari, barabara na madaraja, maduka na biashara za kila aina, nyumba ndogo-ndogo nzuri za vibarua, na magari mazuri ya matajiri . . . ‘hungedhani kamwe kwamba hayo ni makao ya wafungwa’.”

Basi kufikia wakati Gavana Macquarie alipoondoka mwaka wa 1821, tayari Sydney lilikuwa na majengo 59 ya mawe-mchanga, 221 ya mawe, na nyumba 773 za mbao, bila kuhesabu nyumba za serikali na majengo ya umma. Leo, jiji la Sydney ambalo lina wakazi milioni nne hivi, ni wonyesho wa uwerevu wa wafungwa, walowezi na familia zao na busara za magavana wa awali wa koloni hiyo.

‘Bandari Pana Yenye Kuvutia’ ya Sydney

Japo Sydneysiders huita Port Jackson Bandari ya Sydney, bandari yenyewe imegawanyika mara tatu hasa—Bandari ya Kati, Bandari ya Kaskazini, na Bandari ya Sydney. Mto Parramatta na Mto Lane Cove huingia bandarini yakitoka mashambani.

Bandari ya Sydney ni mojawapo ya bandari nzuri zaidi ulimwenguni, ikiwa na ufuo wa mawe-mchanga unaoenea kwa kilometa 240. Umbali wenyewe kutoka lango la bandari hadi mahali inapoungana na Mto Parramatta ni kilometa 19, na eneo lake la maji ni kilometa 54 za mraba. Kina cha bandari hiyo ni mojawapo ya mambo yake yenye kutokeza zaidi, na mahali penye kina zaidi ni meta 47. Lango lenye kuvutia kutoka kwenye Bahari ya Pasifiki lina rasi mbili ambazo zimesimama wima—Rasi ya Kaskazini na Rasi ya Kusini. Rasi hizo mbili zimetenganishwa na kilometa mbili tu, na huwezi kujua ukubwa halisi wa bandari hiyo mpaka uingie ndani kabisa. Labda hiyo ndiyo sababu Kapteni Cook hakuchunguza kwa makini kile alichodhani ni ghuba nyingine tu.

Kule nyuma mwaka wa 1788, Gavana Phillip alinukuliwa akisema hivi kuhusu Bandari ya Sydney: ‘Mweneo wake na usalama wake washinda bandari yoyote ile ambayo nimepata kuona, na mabaharia stadi zaidi niliokuwa pamoja nao walikubaliana nami kabisa kwamba ilikuwa bandari pana yenye kuvutia na ambayo ina nafasi ya kutoshea meli zilizo kubwa sana, na nafasi ya kutoshea idadi yoyote ile ya meli kwa usalama kabisa.’

Daraja la Bandari ya Sydney—Uhandisi Bora

Kule nyuma mwaka wa 1815, uhitaji wa kujenga daraja la kuvuka bandari hiyo kutoka kaskazini kuelekea kusini ulifikiriwa kwa uzito, lakini rekodi ya kwanza ya mchoro wa daraja hilo ilitokea baadaye mwaka wa 1857. Leo, daraja hilo laanzia Dawes Point kwenye upande wa kusini wa bandari na kufikia Milsons Point kwenye ufuo wa kaskazini—mahali hususa ambapo palidokezwa kwa mara ya kwanza! Daraja hilo ambalo ni mojawapo ya madaraja yasiyo na nguzo yaliyo marefu zaidi ulimwenguni lilijengwa kwa miaka tisa na kugharimu takriban dola milioni 20 za Australia—kiasi kikubwa sana wakati wa mshuko wa uchumi mapema katika miaka ya 1930. Lilifunguliwa rasmi Machi 19, 1932.

Utao mkubwa wa katikati una urefu wa meta 503, na kimo cha meta 134 juu ya maji. Kuna meta 50 hivi katikati ya daraja na maji, jambo linalowezesha meli kubwa-kubwa kupitia chini ya daraja kwa usalama. Daraja lenyewe lina upana wa meta 49 na awali lilikuwa na reli mbili, njia mbili za tramu, barabara yenye nafasi sita za magari, na njia mbili za miguu. Mwaka wa 1959, Sydney lilianza kutumia mabasi badala ya tramu, na hivyo basi njia za tramu zilibadilishwa kuwa barabara. Sasa kuna barabara yenye nafasi nane za magari, mabasi, na malori. Urefu wote wa daraja hilo, kutia ndani mahali linapoanzia ni meta 1,149.

Kufikia miaka ya 1980, magari yalikuwa yakisongamana sana kwenye daraja hilo hivi kwamba kukawa na wazo la kujenga kivuko kingine cha bandari. Wakati huu ilikuwa bora kwenda chini ya maji. Basi, mnamo Agosti 1992, handaki la bandari lenye barabara yenye nafasi nne za magari lilifunguliwa.

Ukitembea kwenye daraja hilo unaona mandhari nzuri sana ya Sydney. Kwenye upande wa kaskazini wa bandari, ambao una miteremko yenye miti, kuna Makao ya Wanyama katika Hifadhi ya Taronga. Kwenye upande mwingine wa bandari na karibu chini ya daraja, kwenye Bennelong Point, kuna lile jumba kuu la opera la Sydney.

Kito cha Sydney Kwenye Bandari

Jumba la Opera la Sydney limeitwa “kito cha Bennelong Point,” nalo limezingirwa kwenye pande tatu na maji ya samawati ya Bandari ya Sydney. Kwa kweli jumba hilo hufanana na kito kwenye jua jangavu. Wakati wa usiku magamba yake ya kikale hung’aa kabisa kwenye taa za jumba hilo la opera.

Dibaji ya kitabu A Vision Takes Form hufafanua jinsi mtu huvutiwa anapoona jumba la opera: “Jumba la Opera la Sydney limekuwa mojawapo ya majengo ambayo hubadilika-badilika kulingana na mahali alipo mtu na kulingana na badiliko la nuru. . . . Ukungu wa asubuhi au mionzi ya jua ya jioni zaweza kuangaza magamba yake ili yafanane na kofia kubwa za majitu kwenye hadithi za hekaya.”

Michoro ya jumba hilo la opera ilifanyizwa na msanifuujenzi wa Denmark Jørn Utzon na hatimaye uliteuliwa katika mashindano ya uchoraji miongoni mwa zaidi ya michoro 200 iliyotoka mataifa mbalimbali. Lakini ilionekana haiwezekani kutumia sehemu fulani-fulani za michoro yake nazo zikabadilishwa sana.

Gazeti Architects’ Journal la London lilitaja mchoro huo kuwa “upeo wa ubuni wenye kuvutia sana ulio mkubwa sana.” Lakini, kujenga kwenyewe kutokana na wazo hilo kulikuwa jambo gumu sana kwa wahandisi. Wahandisi wawili, Sir Ove Arup na Jack Zunz, walisema: “Jumba la Opera la Sydney ni . . . mwito mkubwa sana wa ujenzi. . . . Kwa sababu linajengwa chini ya hali zisizo za kawaida kabisa, na kwa vile lina matatizo makubwa sana, limetokeza hali za kipekee . . . za kukuza mbinu mpya. Nyingi za mbinu hizo tayari zimetumiwa katika madaraja ya kawaida na majengo mengi.”

Kadirio la awali la gharama ya jumba la opera lilikuwa dola milioni 7 za Australia, lakini kufikia wakati lilipomalizika mwaka wa 1973, gharama hiyo ilikuwa imeruka kufikia dola milioni 102!

Jinsi Jumba la Opera Linavyofanana Ndani

Tuingiapo sebuleni, twaona kwamba nuru ya jua yapitia tabaka mbili za kioo kwenye midomo ya yale magamba. Jumba hilo limezingirwa kwa kioo cha kipekee kilichotengenezwa Ufaransa chenye jumla ya meta 6,225 za mraba. Kisha twaingia ndani ya ukumbi wa michezo. Tunapokuwa tumesimama upande wa nyuma tukitazama viti 2,690 vinavyoelekea jukwaa, twashangaa kuona kinanda kiitwacho tracker organ kinachoendeshwa na mashine ambacho ndicho kikubwa zaidi ulimwenguni, kikiwa na zumari 10,500.a Dari yafikia meta 25 kutoka chini ikifanya ukumbi uwe na uwezo wa meta 26,400 za kyubiki. Jambo hilo “hufanya kuwe na mwangwi kwa karibu sekunde mbili na kuruhusu muziki wenye kupatana usikike kikamili zaidi,” yasema broshua moja rasmi ya mwongozo.

Kumbi nyinginezo tatu zinavutia vilevile, nazo zilikusudiwa kwa ajili ya opera, maonyesho ya muziki, dansi aina ya ballet, sinema, kukariri mashairi, drama, muziki wa ala, maonyesho, na mikusanyiko. Kuna jumla ya vyumba 1,000 katika jumba la opera, kutia ndani mikahawa, vyumba vya kubadilishia mavazi, na vyumba vya mambo mengine.

Usikose Kutembelea Makao ya Wanyama!

Kama unapanga kuzuru Sydney, hakikisha kwamba umepangia kuabiri kwa boti au feri kwenye bandari hiyo. Utafurahia sana. Panda feri uelekee Makao ya Wanyama ya Taronga. Si wageni wote wanaozuru Australia ambao hupata wakati wa kuona pori za Australia na wanyama wake. Basi kuzuru makao ya wanyama kwa siku moja kwaweza kufaa ili uone sehemu za “mashambani” za Australia. Makao hayo ya wanyama yana wanyama wa kipekee wa Australia, kama vile kangaruu, koala, platipasi na dingo. Makao hayo yako karibu na katikati ya Sydney, na inachukua dakika chache tu kwa kutumia feri kutoka kwenye kituo cha feri kilicho karibu na jumba la opera. Inasemekana kwamba makao hayo ni mojawapo ya makao bora zaidi ulimwenguni. Unapokuwa kwenye eneo la bandari, furahia bila malipo vitumbuizo vinavyoandaliwa na watu mbalimbali—wanasarakasi, Wenyeji wa Australia wanaocheza ala iitwayo dijeridu (ala ya muziki ya wenyeji wa Australia), au bendi ya muziki aina ya jazi.

Tuna uhakika kwamba utafurahia sana kukaa Sydney—jiji ambalo kwa kweli ni lenye pilikapilika na ambalo liko kwenye bandari ya kustaajabisha ya rangi ya samawati ya Pasifiki Kusini. Ni nani ajuaye, labda utakaribishwa kwa vinono!

[Maelezo ya Chini]

a Hiyo tracker ni mfumo unaoendeshwa na mashine ambao huingiza hewa kwenye zumari na kumruhusu mcheza kinanda aguse tu kidogo kinanda.

[Ramani katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Sydney

Ufuo wa Manly

Port Jackson

Daraja la Bandari ya Sydney

SYDNEY

Ghuba ya Botany

[Picha katika ukurasa wa 15]

Eneo kuu la biashara la Sydney

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mfano wa meli “Bounty” katika Ghuba ya Botany

[Picha katika ukurasa wa 15]

Gari-moshi la juu jijini Sydney

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Jumba la Opera la Sydney pamoja na daraja la bandari

[Picha zimeandiliwa na]

By courtesy of Sydney Opera House Trust (photograph by Tracy Schramm)

[Picha katika ukurasa wa 17]

Ndani ya Jumba la Opera, likiwa na kinanda chenye zumari 10,500

[Picha zimeandilwa na]

By courtesy of Australian Archives, Canberra, A.C.T.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Ufuo wa Manly, Sydney

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki