Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 7/22 kur. 11-13
  • Je, Unaweza Kutumaini Kuishi Milele?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, Unaweza Kutumaini Kuishi Milele?
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kujibu “Swali Muhimu Kuliko Yote”
  • Kisababishi Halisi cha Kifo
  • Hukumu na Ahadi
  • Jinsi ya Kurefusha Maisha Yako—Milele
  • Jinsi Unavyoweza Kuishi Milele
    Amkeni!—1995
  • Je, Kweli Uhai Udumuo Milele Wawezekana?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Je, Unaweza Kuepuka Kuzeeka?
    Amkeni!—2006
  • Kwa Nini Tunazeeka na Kufa?
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 7/22 kur. 11-13

Je, Unaweza Kutumaini Kuishi Milele?

“KUNA jambo fulani linaloendelea ndani ya mwili wa mwanadamu linalofanya iwezekane kuishi muda wa miaka 115 hadi 120,” asema Dakt. James R. Smith, profesa wa biolojia ya chembe. “Maisha yana kikomo—lakini hatujui kinachoamua kikomo hicho.” Mwanabiolojia Dakt. Roger Gosden asema kwamba si ajabu kuwa “wanasayansi bado hawajapata njia ya kurefusha maisha, na hakuna yeyote anayewazia jambo hilo.” Je, jambo hilo litawezekana?

Kujibu “Swali Muhimu Kuliko Yote”

Japo kuna nadharia chungu nzima zinazoahidi kukomesha kuzeeka, wataalamu wengi hukubaliana na Dakt. Gene D. Cohen, msimamizi wa chama cha Gerontological Society cha Marekani, kwamba “nadharia zote zilizoahidi kukomesha kuzeeka zimekuwa bure.” Kwa nini? Kwanza, asema mwandikaji wa sayansi Nancy Shute, katika U.S.News & World Report, “bado hakuna mtu awaye yote anayejua kisababishi cha kuzeeka na tokeo lake lisiloepukika, kifo. Na kutibu ugonjwa usiojua kisababishi chake ni kufanya mambo kihobelahobela tu.” Dakt. Gosden ataarifu pia kwamba kuzeeka bado ni fumbo: “Hutupata sote lakini bado hatuelewi hali yake.” Asema kwamba “swali muhimu kabisa la kwa nini kuzeeka hutukia” halishughulikiwi.a

Kwa wazi, kama kulivyo na mpaka wa kiasi cha mwendo wa kasi ambao wanadamu wanaweza kukimbia, kimo wanachoweza kuruka, na kina wanachoweza kufikia wanapopiga mbizi, vivyo hivyo kuna mpaka wa kiasi cha mambo ambayo uwezo wa wanadamu wa kufikiri na kusababu unaweza kueleza. Na kujibu “lile swali muhimu kuliko yote la kwa nini” kwa wazi kunapita mpaka huo. Kwa hiyo, njia pekee ya kupata jibu ni kugeukia chanzo kinachopita mipaka ya ufahamu wa wanadamu usioelekezwa. Kitabu cha kale cha hekima, Biblia, kinapendekeza ufanye vivyo hivyo. Inapozungumza juu ya Muumba, “chemchemi ya uzima,” Biblia hutuhakikishia hivi: “Nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi.” (Zaburi 36:9; 2 Mambo ya Nyakati 15:2) Hivyo basi, uchunguzi wa Neno la Mungu, Biblia, hufunua nini juu ya sababu halisi inayofanya mwanadamu afe?

Kisababishi Halisi cha Kifo

Biblia hutuambia kwamba Mungu alipowaumba wanadamu wa kwanza, aliweka “hisi ya umilele katika mioyo yao.” (Mhubiri 3:11, Beck) Hata hivyo, Muumba aliwatia wazazi wa kwanza wa mwanadamu zaidi ya tamaa ya kuishi milele, aliwapa pia fursa ya kuishi milele. Waliumbwa wakiwa na mwili mkamilifu na akili kamilifu, na walifurahia kuishi katika mazingira yenye amani. Muumba alikusudia kwamba wanadamu hawa wa kwanza waishi milele na kwamba baada ya muda dunia ijazwe wazao wao wakamilifu.—Mwanzo 1:28; 2:15.

Hata hivyo kuishi milele kulitegemea masharti fulani. Kulitegemea utii wao kwa Mungu. Iwapo Adamu angekosa kumtii Mungu, ‘angekufa hakika.’ (Mwanzo 2:16, 17) Kwa kusikitisha, wanadamu wa kwanza walikosa kutii. (Mwanzo 3:1-6) Kwa kutotii, wakawa wenye dhambi, kwa kuwa “dhambi ni uasi-sheria.” (1 Yohana 3:4) Basi matokeo yakawa kwamba hawakuwa tena na tazamio la kuishi milele, kwa maana “mshahara ambao dhambi hulipa ni kifo.” (Waroma 6:23) Kwa hiyo, alipokuwa akitangaza hukumu ya wanadamu wa kwanza, Mungu alisema: “Kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.”—Mwanzo 3:19.

Hivyo, baada ya wanadamu wa kwanza kufanya dhambi, athari za dhambi zilizotabiriwa zilipigwa chapa katika jeni zao, na basi maisha yao yakawekewa mpaka. Basi wakaanza kuzeeka, na matokeo yakawa kifo. Kwa kuongezea, baada ya kufukuzwa kutoka kwa makao yao ya kwanza ya Paradiso, yaliyoitwa Edeni, wanadamu wa kwanza walikabili tatizo jingine ambalo liliathiri sana maisha yao—mazingira nje ya Edeni yaliyokuwa kama kiunzi. (Mwanzo 3:16-19, 23, 24) Muungano huu wa urithi wenye kasoro na mazingira mabaya uliathiri wanadamu wa kwanza na wazao wao wa baadaye pia.

Hukumu na Ahadi

Kwa kuwa mabadiliko haya yenye kudhuru maishani mwao yalitukia kabla ya wanadamu wa kwanza kuzaa watoto, wangeweza tu kutokeza wazao waliokuwa kama wao—wasio wakamilifu, wenye dhambi, na wanaozeeka. “Kifo kikasambaa kwa watu wote kwa sababu wote walikuwa wamefanya dhambi,” Biblia yasema. (Waroma 5:12; linganisha na Zaburi 51:5.) “Tunabeba hati zinazoidhinisha kifo chetu katika muundo wa chembe zetu,” chasema kitabu The Body Machine—Your Health in Perspective.

Hata hivyo, hili halimaanishi kwamba hakuna tumaini la kuishi bila kikomo—maisha bila kuzeeka na kifo. Kwanza, ni jambo la akili kuamini kwamba Muumba mwenye hekima yote aliyeanzisha uhai wa mwanadamu pamoja na namna nyinginezo nyingi sana za uhai anaweza kuponya kasoro zozote za urithi na kuandaa nishati inayohitajika ili kuendeleza maisha ya mwanadamu milele. Pili, hivyo ndivyo Muumba ameahidi kufanya. Baada ya kuwahukumia kifo wanadamu wa kwanza, Mungu alifunua mara kadhaa kwamba kusudi lake la wanadamu kuishi milele duniani halikuwa limebadilika. Mathalani, yeye atoa uhakikishio huu: “Wenye haki watairithi nchi, nao watakaa humo milele.” (Zaburi 37:29) Unahitaji kufanya nini ili upate utimizo wa ahadi hii?

Jinsi ya Kurefusha Maisha Yako—Milele

Kwa kupendeza, baada ya mwandikaji wa sayansi Ronald Kotulak kuwahoji zaidi ya watafiti wa kitiba 300, yeye alitaarifu: “Kwa muda mrefu wanasayansi wamejua kwamba riziki, kazi, na elimu ndiyo mambo muhimu sana yanayoamua afya ya watu na muda ambao wataishi. . . . Lakini ni elimu inayoibuka kuwa jambo muhimu la kurefusha maisha.” Akaeleza: “Kama vile chakula tunachokula kinavyoupa nguvu mfumo wetu wa kinga ili kupambana na viini vinavyohatarisha uhai, ndivyo elimu hutulinda dhidi ya kufanya maamuzi yenye kudhuru.” Kama vile mtafiti mmoja alivyosema, “ukiwa na elimu unajifunza jinsi ya kuishi” na jinsi ya “kushinda vitu vinavyoweza kuwa vizuizi.” Kwa hiyo, kwa njia fulani, elimu ni, kama vile mtungaji Kotulak anavyosema, “ufunguo wa maisha marefu yenye afya.”

Hatua ya kwanza ya kupata uhai udumuo milele wakati ujao ni elimu—elimu ya Biblia. Yesu Kristo alisema: ‘Hii yamaanisha uhai udumuo milele, wao kuendelea kutwaa ujuzi juu yako wewe, Mungu pekee wa kweli, na juu ya yule uliyemtuma, Yesu Kristo.’ (Yohana 17:3) Kutwaa ujuzi juu ya Yehova Mungu, Muumba, juu ya Yesu Kristo, na juu ya mpango wa fidia ambao Mungu ameandaa ndiyo elimu pekee ambayo itamtayarisha mtu kuchukua hatua ya kwanza katika barabara iongozayo kwenye uhai udumuo milele.—Mathayo 20:28; Yohana 3:16.

Mashahidi wa Yehova huongoza programu ya elimu ya Biblia inayoweza kukusaidia kupata ujuzi huu wa Biblia unaotoa uhai. Zuru mojawapo ya Majumba ya Ufalme yao ili ujifunze zaidi juu ya programu hii bila malipo, au waombe wakuzuru wakati unaokufaa. Utaona kwamba Biblia ina uthibitisho thabiti kwamba wakati u karibu ambapo maisha hayatazuiwa na viunzi na muda mfupi wa kuishi. Ni kweli kwamba kifo kimemiliki kwa milenia nyingi, lakini hivi karibuni kitaondolewa milele. Hilo ni tazamio lililoje kwa watu wazee na vijana pia!

[Maelezo ya Chini]

a Wachunguzi wa hali ya kuzeeka wamebuni nadharia nyingi (ripoti moja ilionyesha zaidi ya 300!) ambazo hueleza jinsi kuzeeka kunavyoweza kutukia. Hata hivyo, nadharia hizi hazielezi kwa nini kuzeeka kunatukia.

[Picha katika ukurasa wa 13]

Hatua ya kwanza ya kupokea uhai udumuo milele ni elimu ya Biblia

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki