Kuutazama Ulimwengu
Maradhi Kumi Kuu ya Kuambukiza Yanayosababisha Vifo
Ulimwenguni pote, mamilioni ya watu hufa kila mwaka kutokana na maradhi ya kuambukiza. Kulingana na gazeti Natural History, maradhi yafuatayo ya kuambukiza yalikuwa hatari zaidi katika mwaka wa 1997. Maambukizo hatari ya mapafu, kama vile kichomi (nimonia), yaliongoza kwa kusababisha vifo vya watu milioni 3.7. Kifua kikuu kikawa namba mbili, kikisababisha vifo vya watu milioni 2.9. Kipindupindu na maradhi mengine ya kuhara yakawa namba tatu, yakisababisha vifo vya watu milioni 2.5. UKIMWI ukasababisha vifo vya watu milioni 2.3. Kati ya watu milioni 1.5 na milioni 2.7 walikufa kutokana na malaria. Surua ikasababisha vifo vya watu 960,000. Mchochota wa ini aina ya B ukasababisha vifo vya watu 605,000. Kifaduro kikasababisha vifo vya watu 410,000. Watu wengine 275,000 walikufa kutokana na pepo punda. Na watu 140,000 wakafa kutokana na kidingapopo cha kuvuja damu. Japo jitihada bora za mwanadamu, maradhi ya kale ya kuambukiza yangali yanatisha uhai wa wanadamu kotekote ulimwenguni leo.
Matumizi Mabaya ya Vileo Nchini Venezuela
Kwa wastani, watu wa Venezuela hunywa vileo zaidi ya nchi nyingine yoyote ya Amerika ya Latini, laripoti gazeti la habari El Universal, la Caracas. Inakadiriwa kwamba kila mtu nchini Venezuela hunywa kati ya lita 60 na 70 ya vileo kwa mwaka. Wizara ya Afya yakadiria kwamba nusu ya mauaji yote na visa vya ujiuaji ambavyo hutukia eneo la jiji la Caracas huhusu vileo. Lakini, uchunguzi mmoja uliofanywa na Chuo Kikuu cha Central cha Venezuela, Kituo cha Amani, na Polisi, unadai kwamba zaidi ya mauaji ya ukatili 9 kati ya 10 ambayo hutukia katika eneo hilo huhusu vileo. Ili kusaidia kudhibiti matumizi mabaya ya vileo, warsha zimepangwa ili kufundisha wanafunzi wajue jinsi ya kukinza msongo wa marika wa kunywa vileo na wajue utendaji wa badala unaofaa na vilevile kutia moyo kuwe na mawasiliano mazuri kati ya wazazi na watoto.
Bahari Zakabiliwa na Matatizo
Ulimwenguni kote, matumbawe yanaharibiwa na vivimbe, majeraha, maambukizo, na matisho mengine, laripoti Science News. Mwanabiolojia wa majini James Cervino asema kwamba angalau hali mpya 15 zimetokea katika kipindi kinachozidi miaka 20 ambazo zinaua matumbawe. Aina nyingine za uhai wa baharini zinazotishwa zatia ndani nyasi za bahari, samakigamba, kasa, na nguva. “Asilimia 95 ya sehemu za ulimwengu zenye uhai ni bahari,” asema mtaalamu wa bahari Sylvia Earle. “Bahari zikiwa na matatizo, basi hata sisi tuna matatizo. Na kwa kweli bahari zina matatizo.”
Usomaji wa Kijuu-Juu
Si kila mtu ambaye amejaza vitabu kwenye rafu zake ni msomaji mwenye bidii. Kwa mfano, mwenye-duka mmoja Chris Mattheus akiri: “Napenda kuwa na vitabu vingi, lakini mimi husoma kwa nadra.” Sasa Mattheus atoa suluhisho rahisi kwa tatizo hilo. Akiwa pamoja na mwenzake, wamefungua duka la kwanza nchini Ujerumani ambalo linauza vitabu vya miigo, laripoti gazeti la habari Weser-Kurier. “Vichwa vipatavyo 2,800 vya vitabu vya miigo” vya nyanja za sanaa, falsafa, na sayansi vinauzwa. Vitabu hivyo vya miigo huchongwa kwa njia mbalimbali, tokea vitabu sahili vya kadibodi hadi mifano ya vitabu halisi iliyochongwa kwa mbao bora ya msaji. Miigo yenye kuvutia ya vitabu vya uchoraji, ambavyo kwa kawaida ni ghali sana, inagharimu dola 10 hadi 15 tu. Mattheus asema: “Bei inategemea ukubwa wa mwigo wa kitabu, bali si yaliyomo.”
Michezo ya Vidio Yenye Kufaa
Ukitaja “michezo ya vidio” watu wengi hufikiria michezo ambayo imejaa jeuri. Lakini, watafiti wamegundua kwamba “michezo inayofaa inaweza kuzoeza watoto wenye ugonjwa wa kisukari na pumu waweze kudhibiti hali zao,” laripoti Technology Review. Kituo cha Kitiba cha Chuo Kikuu cha Stanford kilifanya utafiti kwa watoto wapatao 60 ambao wana ugonjwa wa kisukari wenye umri wa kati ya miaka 8 na 16. Nusu ya watoto hao walicheza michezo ya kawaida ya vidio. Nusu nyingine ya watoto ikacheza mchezo uitwao Packy & Marlon ambao unahusu tembo wawili wanaosaidia wachezaji kuchagua vyakula vinavyofaa kuliwa, kuchunguza kiwango cha sukari katika damu yao, na kutumia dawa ya insulini ifaavyo. Katika kipindi kinachozidi miezi sita, wale waliocheza mchezo wa tembo “walipunguza ziara zao za dharura kwa daktari na kwenye vyumba vya dharura kwa asilimia 77” kuliko wale waliocheza michezo ya kawaida, lasema Technology Review. Michezo mingine kama hiyo imetayarishwa ili kuwasaidia watoto wadhibiti ugonjwa wa pumu na kuepuka kuvuta sigareti.
UKIMWI Wasababisha Madhara Makubwa
Katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa Sahara katika miaka kumi ambayo imepita, matarajio ya muda wa kuishi tokea wakati wa kuzaliwa yamepungua kwa karibu miaka sita, na muda huo watazamiwa kupungua hata zaidi. Kwa nini kuna mabadiliko hayo? Kwa sababu katika nchi zilizo katika eneo hilo “Ukimwi waendelea kuwaka,” laripoti The UNESCO Courier. Kwa wakati huu, zaidi ya asilimia 10 ya watu katika eneo hilo wameambukizwa virusi HIV, ambavyo husababisha UKIMWI. Nchi zilizokumbwa vibaya zaidi ni Afrika Kusini, Botswana, Malawi, Msumbiji, Namibia, Zambia, na Zimbabwe. Isitoshe, shirika la Umoja wa Mataifa lasema kwamba “kuna mazishi 5,500 yanayohusu watu waliokuwa na UKIMWI kila siku katika Afrika,” laripoti The New York Times.
Katekisimu—Imekuwa Msiba
Katika barua moja ya karibuni ya kanisa, askofu mkuu wa Siena, Gaetano Bonicelli, alisema kwamba hata baada ya kuhudhuria masomo ya katekisimu, watu wenye umri wa miaka 20 “hawajui tofauti iliyoko kati ya Utatu na Maria Mtakatifu.” Hali kama hiyo ya kutojua mafundisho ya Katoliki ni wonyesho wa kile ambacho askofu mmoja wa cheo cha juu, Kadinali Ratzinger, alichokiita “msiba wa katekisimu ya kisasa,” laripoti Corriere della Sera, la Milan, Italia. Askofu Mkuu Bonicelli apendekeza kurudia kueneza evanjeli. “Utume, yaani kueneza evanjeli, ndio njia ya pekee kwa kanisa katika mileani ya tatu.”
Je, Maadili Yanarudi?
Uchunguzi uliofanywa karibuni nchini China ulifunua kwamba “japo watu wazima wa China hawaoni kama kufanya ngono nje ya ndoa ni jambo kubwa, matineja wengi bado wanapinga tabia hiyo,” laripoti gazeti China Today. Magunduzi hayo yalitegemea mahojiano na watu 8,000. “Sehemu tatu kwa tano ya matineja walikubali kwamba watu wanaoharibu ndoa za wengine kupitia uhusiano wa kimapenzi wanapasa kuadhibiwa ama kifedha ama kwa njia nyingine yoyote,” uchunguzi huo ukaonyesha, “huku asilimia 70 ya watu wenye umri wa kati ya miaka 37 na 45 wanaona hakupaswi kuwe na adhabu yoyote kwa matendo kama hayo.”
Kuvalia Nguo Zisizofaa Kanisani
Nchini Marekani, idadi inayoongezeka ya watu wanavalia isivyofaa wanapoenda kanisani, laripoti shirika la habari la Associated Press. Wahudumu fulani wanasumbuliwa wanapoona waenda-kanisani wakivalia suruali fupi, jeans, au nguo nyinginezo zisizofaa wakati wa ibada ya kanisa. Wakuu wa kanisa wametatanika—wao hawataki kuwafukuza washiriki wapya wala hawataki kuwaepuka waabudu wa kawaida ambao hawataki kuvalia vizuri. Kulingana na uchunguzi mmoja, “asilimia ipatayo 30 ya Wamarekani hupendelea ibada za kanisa ambazo si rasmi lakini zinazopatana na hali za wakati huu,” kwa kulinganisha na asilimia 21.5 ambao hupendelea ibada za kanisa za kizamani.
Mimba za Matineja Zakubaliwa
“Jambo linalochangia sana ongezeko la daima la idadi ya wanawake wanaopata watoto bila kuwa na waume [ni] kwamba jambo hilo lakubaliwa na jamii,” lasema The News, la Mexico City. “Inaonekana kwamba jamii inajitahidi sana ili kuondoa maoni mabaya juu ya mimba za matineja. Kwa kufanya hivyo, huenda jamii hata inatia moyo jambo hilo.” Je, ongezeko hilo laweza kurekebishwa? Makala hiyo yasema: “Ikiwa mashirika ya utangazaji yanaweza kubadili mtazamo wa watu ili waache kumwona mvutaji wa sigareti kuwa mtu wa kisasa na kuanza kumwona kuwa chukizo, na ikiwa Wamarekani wanaweza kubadili mlo wao kwa kuacha kula vyakula vyenye mafuta na waanze kula vyakula vya makapi, basi hata mawazo ya matineja yanaweza kubadilishwa ili waone kupata watoto wakiwa shuleni kuwa jambo la kipumbavu na lenye ubatili.”
Kurekodi Fadhili
“Kwa msingi watoto hujifikiria wenyewe tu hadi wanapofikia angalau umri wa miaka 4 hivi, wakati ambapo wao huanza kuwa na uwezo wa kuonyesha hisia-mwenzi,” yasema ripoti moja iliyonukuliwa katika The Toronto Star. Ili kusaidia watoto wasitawishe hali ya kuhangaikia wengine, inapendekezwa kwamba wazoezwe nyumbani kuonyesha matendo ya fadhili. Labda kila mshiriki wa familia anaweza kuweka rekodi kwenye chati angalau mara mbili ambazo wameonyesha fadhili bila kuombwa. Wazazi wanaoona tendo la fadhili ambalo mtoto wao ametenda wanaweza kuongeza tendo hilo kwenye chati. Shule kadhaa zinatumia chati kama hizo katika jitihada za kukinza kudhulumiana shuleni. Watoto wanaombwa warekodi matendo ya fadhili ambayo wameona watoto wengine wakifanya. Kulingana na ripoti hiyo, “jambo hilo huwasaidia watoto watambue hisia-mwenzi, ambayo ni hatua muhimu ya kujifunza jinsi ya kuwa mwenye hisia-mwenzi na kuionyesha.”