Magonjwa ya Kuambukiza Husababisha Misiba Japo Yanaweza Kuepukwa
HUKU matetemeko ya dunia na mafuriko yakiripotiwa kama vichwa vikuu vya habari, magonjwa ya kuambukiza kwa kawaida hayaripotiwi kama mambo ya maana. Hata hivyo, “idadi ya vifo vinavyosababishwa na magonjwa ya kuambukiza (kama vile UKIMWI, malaria, magonjwa ya mfumo wa kupumua na kuharisha) inazidi ile ya vifo vilivyosababishwa na misiba ya asili ya mwaka uliopita kwa mara 160,” yasema taarifa kwa waandishi wa habari ya Shirika la Msalaba Mwekundu na la Mwezi Mwekundu ya Juni 2000. “Na hali inazidi kuwa mbaya zaidi.”
Kuna visababishi viwili vikuu vya idadi hiyo inayoshtua. Kimoja ni kuenea kwa UKIMWI ambao unaua watu 300 baada ya kila saa moja. UKIMWI “si ugonjwa tena, bali ni msiba,” asema Peter Walker, msimamizi wa mipango ya kupambana na misiba wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na Shirika la Mwezi Mwekundu. “Ugonjwa unaoenea sana hivyo huwamaliza wafanyakazi na kuuzorotesha uchumi.” Kisababishi kingine ni kuzorota kwa huduma za afya kwa umma. Jambo hilo limesababisha magonjwa yaliyokuweko zamani yatokee tena kama vile kifua-kikuu, kaswende, na malaria. Kwa mfano, siku hizi nchi moja ya Asia huwa na visa vipya 40,000 vya kifua-kikuu kila mwaka. Katika nchi moja ya Ulaya Mashariki, ugonjwa wa kaswende unaambukizwa mara 40 zaidi ya ilivyokuwa katika mwongo uliopita.
Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kwamba japo magonjwa ya kuambukiza yamekuwa misiba, hiyo ni misiba inayoweza kuepukika zaidi. Kwa kweli, ripoti hiyo yasema kwamba kati ya vifo milioni 13 vilivyosababishwa na magonjwa ya kuambukiza katika mwaka wa 1999, vingi “vingeepukwa iwapo afya ya kila mtu ingetunzwa kwa kutumia dola 5 za Marekani.” Iwapo serikali za ulimwengu zingejitolea kutumia dola 5 za Marekani kwa kila mtu mmoja ili kutunza afya—jumla ikiwa dola bilioni 30 za Marekani—watu wengi sana hawangekufa ovyoovyo!
Ingawa hizo zinaonekana kuwa fedha nyingi, si nyingi sana zikilinganishwa na zile zinazotumiwa ulimwenguni kwa ajili ya huduma nyinginezo. Kwa mfano, katika mwaka mmoja hivi karibuni, dola bilioni 864 za Marekani, yaani dola 144 za Marekani kwa kila mtu mmoja, zilitumiwa kuendeleza shughuli za kijeshi ulimwenguni pote. Hebu fikiria jinsi fedha nyingi zaidi zinavyotumiwa ili kujitayarishia vita badala ya kuzuia kuenea kwa magonjwa! Huenda mwanadamu asiweze kuondoa magonjwa ya kuambukiza—si kwa sababu amekosa fedha, bali kwa sababu kubwa hata zaidi. Kwani, serikali za wanadamu hata haziwezi kupangia mambo yanayofaa kutangulizwa.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Picha ya eksirei: New Jersey Medical School—National Tuberculosis Center
Picha ya mtu anayekohoa: WHO/Thierry Falise