Siagi ya Karanga Mtindo wa Kiafrika
NA MLETA-HABARI WA AMKENI!
KATIKA JAMHURI YA AFRIKA YA KATI
KATIKA nchi za Magharibi siagi ya karanga mara nyingi huonwa kuwa kitu cha kupakia kipande cha mkate tu. Hata hivyo, katika nchi fulani za Afrika, hiyo hutimiza sehemu muhimu sana ya maisha ya kila siku. Jinsi gani?
Katika Afrika ya kati, vyakula vingi vipendwavyo hupikwa kwa siagi ya karanga. Huku, kama vile sehemu nyingine zinazositawi, unga wa ngano na unga mwororo wa mahindi—vifaa vinavyotumiwa kufanya mchuzi uwe mzito—haupatikani kwa urahisi. Hivyo, ni jambo la kawaida kutumia siagi ya karanga badala yake.
Hata hivyo, haipatikani kwa kwenda tu dukani na kununua chupa ya siagi ya karanga. Huko, hiyo huuzwa kwa kijiko kidogo cha chai, na ni ghali sana. Kwa hiyo, wanawake wengi Waafrika huona ni afadhali wajitengenezee yao wenyewe. Jinsi kazi hii ya jasho inavyotimizwa ni jambo lenye kuvutia sana. Habari ifuatayo ilikusanywa kwa kuongea na wanawake kadhaa Waafrika.
Ulimaji wa Karanga
Ni dhahiri kwamba si vigumu kutunza karanga. Sehemu iliyo ngumu ni ile ya kutayarisha mchanga. Hilo hufanywa mwanzoni mwa majira ya mvua wakati mchanga ungali mkavu na mgumu. Mwezi wa Aprili mbegu hupandwa kwa mkono, na mvua ikija mapema, “njugu” zaweza kuvunwa mwishoni mwa Agosti au mwanzoni mwa Septemba.
Kwa kweli karanga si njugu bali ni jamii ya kunde. Karanga hazikui mtini, kama vile huenda ikawa ulifikiri; badala yake, hukua katika mimea mifupi, ambayo ina njia ya pekee ya kutokeza karanga chini ya mchanga. Hivyo, karanga zajulikana sana kuwa njugu.
Katika Afrika ya kati wastani wa shamba la kukuza karanga huenda likawa na meta 90 kwa 50 hivi. Watu wengine wamezipanda katika shamba dogo karibu na nyumba zao. Jembe fupi na panga hutumiwa kulimia shamba hilo. Hilo laweza kutia ndani jitihada yenye kuchosha mgongo! Mmea huo huhitaji kutunzwa sana, angalau mwanzoni. Shamba lahitaji kulindwa ili wanyama wasichimbue mbegu na kuzila. Na mchanga wahitaji kulegezwa na kuondolewa magugu.
Shamba lahitaji kulindwa hasa karibu na wakati wa mavuno. Huenda watoto wakawekwa walinde wakati wa mavuno ukaribiapo. Mwanamke mmoja aliripoti kwamba jirani yake alikuta mimea yake ya karanga ikiwa juu ya miti iliyokuwa karibu na hapo. Tumbili walikuwa wameibeba huko juu na wakafurahia karamu kwa hasara yake!
Mara nyingi familia yote huhusishwa wakati wa mavuno. Kila mtu huenda shambani kusaidia. Mimea hiyo hung’olewa kwa mkono na kuachwa ikauke, kisha karanga hutolewa na kuletwa kijijini kwa mabakuli makubwa, yanayobebwa kichwani na wavunaji.
Halafu karanga hufanywaje? Baada ya kusafishwa, huchemshwa ndani ya maji yenye chumvi. Nyingine huliwa bila kukawia na familia, lakini zilizo nyingi huwekwa zitumiwe baadaye kwa upishi. Hizo hutandazwa chini karibu na nyumba na kuachwa zikauke kabisa. Lazima mtu azilinde zisiliwe na mbuzi wenye kuzurura-zurura.
Baada ya karanga kukaushwa, hizo huwekwa katika ghala iliyotengenezwa kwa nyasi na udongo na kujengwa kwenye milonjo. Hiyo hufanya karanga zibaki zikiwa kavu, pia huepushwa na wanyama na watoto ambao huenda wakawa wanatafuta chakula Mama anapokuwa akifanya kazi shambani.
Kuanzia Karanga Hadi Siagi ya Karanga
Lazima njugu hizo ziambuliwe kabla ya kufanywa siagi ya karanga. Kisha hukaangwa, mara nyingi katika kikaangio kipana kilicho bapa, kwenye moto mdogo wa kuni uliokokwa mchangani. Hiyo hufanya ziwe na ile ladha yake na kuzifanya ziwe rahisi kuambuliwa ngozi. Karanga hizo huachwa zipoe, na ngozi yake hufikichwa. Mashine ya kusagia hutumiwa kuponda-ponda karanga zilizokaangwa mpaka ziwe siagi yenye rangi ya krimu. Ikiwa mashine haipatikani, mke nyumbani atazitandaza kwenye jiwe kubwa lililo bapa, na kuziponda-ponda kwa chupa au jiwe la kusagia.
Hivi punde siagi ya karanga itatumiwa ifaavyo kuwa kikolezo cha kufanya mchuzi uwe mzito, kwa kawaida katika chakula kinachopikiwa katika chungu kimoja na kuliwa na mhogo, ndizi, au wali. Ikiwa wajiuliza jinsi chakula kilichopikwa kwa siagi ya karanga kinavyoonja, kwa nini usijaribu kukipika?
Waweza kufuata mapishi ya kawaida na kutayarisha mchuzi wa nyama, vitunguu, kitunguu saumu, na nyanya nzito. Upike hadi nyama ziwe laini, na uongezee spinachi zilizokatwa-katwa ukipenda. Wakati chakula hicho kingali jikoni, koroga siagi ya karanga ndani ya maji kidogo uifanye iwe nzito—kikombe kimoja hivi kwa kila kilo moja ya nyama—na uikoroge ndani ya mchuzi huo. Ipike kwa dakika kumi au zaidi kwenye moto mwingi ili ladha ya siagi ya karanga isikolee mno. Kama mchuzi si mzito vya kutosha kama upendavyo, ongeza tena siagi ya karanga. Tia chumvi ya kutosha. Ikiwa wapenda viungo, unaweza kutia ndani pilipili.
Wengi huona chakula hicho kikiwa kitamu sana kinapoandaliwa kwa wali! Na ijapokuwa yako huenda isiwe halisi, utaona matumizi ya moja kwa moja ya siagi ya karanga—mtindo wa Kiafrika!
[Picha katika ukurasa wa 26]
Karanga huvunwa, kisha kupelekwa nyumbani ziambuliwe na kupondwa-pondwa