Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 9/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Wagonjwa wa Kutoganda Damu Walioambukizwa, Walipwa Ridhaa
  • Kuzuka kwa Kipindupindu cha Kufisha
  • Mioyo Iliyopuuzwa
  • Uwezo wa Wanaume wa Kuzaa Unapungua
  • “Maradhi Yasiyoonekana”
  • Homa ya Mafua Ingali Inaua
  • Kipepeo-Maliki Atishwa
  • Je, Kutenda Vibaya Watoto Kunazidi Kujulikana?
  • Kutamani Sana Magari
  • Tatizo la Elimu
  • Damu Yenye Viini Vibaya Hupewa Wasioganda Damu
    Amkeni!—1994
  • Hali ya Afya Ulimwenguni—Mwanya Unaozidi Kukua
    Amkeni!—1995
  • Magonjwa ya Kuambukiza Katika Karne ya 20
    Amkeni!—1997
  • Ugonjwa Ulioogopwa Zaidi Katika Karne ya 19
    Amkeni!—2010
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 9/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Wagonjwa wa Kutoganda Damu Walioambukizwa, Walipwa Ridhaa

Mahakama ya Madai ya Roma imeagiza Wizara ya Afya ya Italia iwalipe ridhaa watu 385 wenye ugonjwa wa kutoganda damu walioambukizwa mchochota wa ini au virusi vya UKIMWI kutokana na damu yenye viini, wakiishtaki kwa “kukosa uangalifu na udhibiti” na pia “kuchelewa kuondoa vitu [vilivyoambukizwa].” Thuluthi moja kati yao tayari wamekufa. Kulingana na wakili Mario Lana, msimamizi wa shirika la Italian Forensic Union for the Safeguard of Human Rights, “hukumu hii inatambua uhusiano dhahiri uliopo kati ya mwenendo wenye kulaumika na usio na busara wa Serikali ya Italia na madhara waliyopata wagonjwa wa kutoganda damu.” Nchini Italia, wagonjwa wapatao 2,000 wa kutoganda damu, wameambukizwa virusi vya UKIMWI na takriban 5,000 wakaambukizwa mchochota wa ini-C. Waitalia 1,246 wamekufa kwa sababu ya kutiwa vitu hivyo vyenye damu iliyoambukizwa.

Kuzuka kwa Kipindupindu cha Kufisha

Kuzuka kwa kipindupindu cha kufisha mnamo Februari kulilazimu baraza la mji wa Lusaka, Zambia, kupiga marufuku “uchuuzi wa barabarani wa vyakula vyote visivyotiwa kwenye mikebe,” laripoti Times of Zambia. Kwa kuongezea, hoteli na mikahawa “ililindwa kwa muda wa saa 24 huku idadi ya vifo vyenye kusababishwa na kipindupindu katika mji mkuu ikiongezeka kwa haraka na kufikia 42,” yasema ripoti hiyo. Maafisa wa afya walihangaika kwamba maradhi ya kuharisha pia “yalizidi katika sehemu nyinginezo za nchi.” Ili kutatua tatizo hilo, maafisa wa Wizara ya Afya na Elimu walianzisha kikundi cha wafanyakazi ili kuajiri wakusanyaji takataka zaidi na kutia dawa ya klorini kwenye visima visivyo na kina kirefu, ambavyo huchafuliwa kwa urahisi na maji yaliyo chini ya ardhi. Daniel M’soka, msemaji wa Baraza la Mji wa Lusaka, alisema: “Mradi wetu ni kupunguza pigo la kipindupindu.”

Mioyo Iliyopuuzwa

“Badala ya kuchukua hatua za kuboresha afya yao, wanawake Wakanada hawatunzi mioyo yao ifaavyo,” lasema gazeti la habari la The National Post. Uchunguzi wa hivi karibuni uliofanyiwa wanawake Wakanada 400 wenye umri wa kati ya miaka 45 hadi 74, uliodhaminiwa na Shirika la Moyo na Mshtuko wa Akili la Kanada, ulipata kwamba “ni asilimia 30 tu waliodumisha uzito unaofaa, asilimia 36 walikuwa watendaji, na asilimia 74 walisema kwamba walikuwa na mkazo kwa sababu ya madaraka mengi waliyo nayo sasa.” Msemaji wa shirika hilo Elissa Freeman alikata kauli kwamba “wanawake wanawatunza waume zao zaidi ya wanavyojitunza wenyewe.” Kulingana na ripoti hiyo, “maradhi ya moyo na mshtuko wa akili yanasababisha asilimia 40 ya vifo miongoni mwa wanawake—zaidi ya 41,000 kila mwaka.”

Uwezo wa Wanaume wa Kuzaa Unapungua

“Wastani wa shahawa ya wanaume huko Marekani na Ulaya umepungua kwa kiwango cha asilimia 50 tangu mwisho-mwisho wa miaka ya 1930,” laripoti gazeti World Watch. “Uchunguzi huo unaunga mkono hangaiko linaloendelea kwamba uwezo wa wanaume wa kuzaa huenda ukawa unadidimia na kwamba kisababishi chaweza kuwa vichafuzi vya mazingira.” Mkataa huo wategemea uchunguzi 61 uliochapishwa tangu 1938, unaotia ndani washiriki zaidi ya 14,000. Inadhaniwa kwamba kemikali fulani za kimazingira huvuruga mfumo wa tezi wa mwili na kuvuruga uwezo wake wa kudhibiti ukuzi na kuzaa. Kuna kemikali zipatazo 60 ambazo zinasemekana kuwa husababisha mvurugo huo. Hata hivyo, “ni asilimia ndogo sana ya kemikali zinazokadiriwa kuwa 80,000 zinazotumika sasa ambazo zimekaguliwa ili kuonekana ikiwa zina madhara yanayovuruga mfumo wa tezi,” lasema World Watch.

“Maradhi Yasiyoonekana”

“Watoto wapatao milioni 15 hadi 18 katika nchi zinazositawi wanaathiriwa na risasi nyingi sana iliyo katika damu yao,” laripoti Shirika la Habari za Kimazingira. Kwa mfano, nchini India imethibitishwa kuwa, kuna uhusiano kati ya uwezo wa akili wa watoto na kiasi cha risasi walichotumia. Kulingana na Dakt. Abraham George, watoto “hupoteza uwezo wao wa akili . . . kuwa katika mazingira yenye risasi kwa muda mrefu huathiri ubongo wao,” laripoti The Indian Express. Chanzo kikubwa cha sumu ya risasi katika majiji ya India ni magari ambayo yangali yanatumia petroli yenye risasi. Kwa kuwa sumu inayosababishwa na risasi haigunduliwi mara moja kwa kulinganishwa na matatizo kama vile umaskini na njaa, Dakt. George aiita “maradhi yasiyoonekana.”

Homa ya Mafua Ingali Inaua

Zaidi ya wataalamu mashuhuri 300 wa homa ya mafua hivi majuzi walikusanyika kwenye makao makuu ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) huko Geneva, Switzerland, kujadili namna ya kukabili maradhi haya ya kufisha. Licha ya hatua kubwa katika miaka 50 iliyopita, homa ya mafua inazidi kuua mamia ya maelfu ya watu kila mwaka, yaripoti Idara ya Habari za Umma ya Umoja wa Mataifa. Ili kuboresha uzuiaji na udhibiti wa homa ya mafua, shirika la WHO litachapisha mpango unaokusudiwa kusaidia kile wanachoita “kuenea kwa ghafula kwa homa ya mafua.” Mkurugenzi mkuu wa shirika la WHO, Dakt. Gro Harlem Brundtland, alisema: “Muda wa kukabiliana nayo waweza kuwa mfupi—kuanzia kutambuliwa kwa aina ndogo mpya na kuanza kwa mweneo mkubwa sana.”

Kipepeo-Maliki Atishwa

Kila majira ya vuli mamilioni ya vipepeo-maliki huhamia umbali wa kilometa zaidi ya 3,200 kutoka Kanada hadi kwenye makao yao ya baridi katika California na katika milima ya Sierra Madre iliyoko Mexico ya kati. Hata hivyo, hivi karibuni, makao ya maliki hao katika Mexico yametishwa na mmomonyoko wa udongo na ukataji haramu wa msonobari aina ya oyamel (mti wa mbao wa jamii ya Abietaceae). Tokeo limekuwa kwamba, “katika miaka miwili iliyopita, idadi ya maliki wanaokuja kwenye makao haya baridi imepungua kwa asilimia 70,” laripoti The News la Mexico City. Ingawa utalii huandaa mapato kwa baadhi ya wenyeji, wengine wamekuwa wakijipatia riziki kwa kubeba miti mingi inayolindwa usiku. “Uharibifu huo ukiendelea,” lasema The Times, “huenda maliki wa majira ya kiangazi wa Amerika Kaskazini wakakaribia kutoweka kabisa.”

Je, Kutenda Vibaya Watoto Kunazidi Kujulikana?

Kulingana na El Universal, gazeti la habari la Caracas, asilimia ya watoto wanaotendwa vibaya kingono katika Venezuela imeongezeka kutoka mtoto 1 kati ya watoto 10 katika 1980 hadi watoto 3 kati ya watoto 10 leo. Katika 1980 wastani wa watoto waliotendwa vibaya ulikuwa kati ya 12 na 14. Leo wengi wao wana umri unaopungua miaka mitatu. Ni nani wanaochochea uhalifu huo wenye kuogofya? Wazo la kwamba ni wageni wajanja wanaozunguka-zunguka kwenye viwanja vya shule wakingoja kuwashawishi watoto kwa kuwapa peremende si halisi. Gazeti El Universal lasema kwamba asilimia 70 ya wakosaji ni watu wa jamaa au marafiki wa familia. Zaidi ya nusu ya watu hao ni wazazi wa kambo, na wengineo kwa kawaida ni watu fulani wenye mamlaka, kama vile kaka, binamu, au mwalimu.

Kutamani Sana Magari

Kulingana na Shirika la Watengenezaji Magari la Marekani, hivi majuzi Marekani ilifikia kiwango cha milioni moja katika utengenezaji magari. “Ilichukua muda wa miaka 25 kutokeza magari milioni moja kwa mara ya kwanza,” laripoti gazeti Compressed Air. Hata hivyo, leo, “kiwango cha utengenezaji cha sasa ni magari 30 ya abiria na lori na mabasi kumi kwa dakika moja kila siku ya kazi.” Ukizingatia viwanda vya kuunganisha sehemu za magari, viwanda vinavyotengeneza sehemu hizo, wauzaji na watu wa kuyatunza, na madereva walio stadi, kiwanda cha magari nchini Marekani kinaajiri takriban mtu 1 kati ya kila watu 7 walioajiriwa. Inakadiriwa kwamba sasa kuna takriban magari milioni 40 nchini Marekani.

Tatizo la Elimu

“Nchi zinazositawi zinakabili tatizo la elimu kukiwa na watoto milioni 125 wengi wao wakiwa ni wasichana, ambao hawaendi shuleni na wengine zaidi, milioni 150 wakiacha shule kabla hawajajua kusoma na kuandika,” laripoti shirika la England News Unlimited. Kwa sasa, katika nchi zinazositawi, mtu mzima 1 kati ya 4, au watu milioni 872 hawajui kusoma na kuandika. Isitoshe, tatizo la elimu linakuwa baya zaidi wakati nchi zenye idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma na kuandika zinapokopa pesa kutoka nchi tajiri zaidi. Kwa nini? Kwa sababu pesa zinazohitajika sana kwa ajili ya elimu mara nyingi hutumiwa kulipia madeni. Hivyo tatizo la kutojua kusoma na kuandika linarudiwa, jambo ambalo huongeza umaskini.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki