Janga la Vita
KATIKA Imperial War Museum huko London, Uingereza, wageni huvutiwa sana na saa ya pekee na kihesabio cha tarakimu. Saa hii si ya kupima wakati. Kusudi lake ni kuwafahamisha watu juu ya athari kubwa ya sehemu kuu ya karne hii—vita. Kadiri akrabu ya saa inavyozunguka, ndivyo kihesabio kinavyoongeza tarakimu nyingine kwenye hesabu yake baada ya kila sekunde 3.31. Kila tarakimu inawakilisha mwanamume, mwanamke, au mtoto ambaye amekufa kwa sababu ya vita katika karne ya 20.
Kihesabio hicho kilianza kuhesabu mwezi wa Juni 1989. Kuhesabu kutakoma saa sita usiku Desemba 31, 1999. Hesabu itakuwa imefikia milioni mia moja, ambayo ni kadirio la wastani la watu ambao wamefia vitani muda wa miaka 100 iliyopita.
Hebu wazia—watu milioni mia moja! Idadi hiyo ni zaidi ya maradufu ya idadi ya watu huko Uingereza. Lakini, tarakimu hiyo haifunui lolote juu ya hofu kuu na maumivu ya wahasiriwa. Wala haielezi mateso ya wapendwa waliofiwa—mamilioni yasiyohesabika ya akina mama na baba, dada na kaka, wajane na mayatima. Tarakimu hiyo inaonyesha tu kwamba: Karne yetu imekuwa yenye uharibifu mkubwa zaidi katika historia yote ya wanadamu; ukatili wake hauna kifani.
Historia ya karne ya 20 inaonyesha pia kadiri ambavyo wanadamu wamekuwa stadi katika kutekeleza mauaji. Katika historia yote utengenezaji wa silaha mpya ulikuwa wa polepole hadi karne ya 20 ilipofika, ambayo imetokeza rundo kubwa la silaha. Vita ya ulimwengu ya kwanza ilipolipuka mnamo 1914, majeshi ya Ulaya yalifanyizwa na wanaume wapanda-farasi wenye fumo mikononi. Leo, makombora yanayoongozwa na sensa za setilaiti na mifumo ya kompyuta, yanaweza kuua watu katika sehemu yoyote ya dunia pasipo kukosea. Katika miaka iliyopita kumekuwa na utengenezaji na uboreshaji wa bunduki, vifaru, nyambizi, ndege za kivita, silaha za viini na za sumu na, bila shaka, “bomu.”
Jambo la kushangaza ni kuwa, wanadamu wamekuwa stadi sana katika vita hivi kwamba vita vimekuwa pambano ambalo wameshindwa kumudu. Sawa na hadithi ya kubuni ya Frankenstein, ambamo dubwana humwangamiza aliyelifanya, vita inatisha kuangamiza wale walioianzisha. Je, dubwana hili linaweza kudhibitiwa au kuangamizwa? Makala zifuatazo zitachunguza swali hili.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
U.S. National Archives photo
U.S. Coast Guard photo
By Courtesy of the Imperial War Museum