Kuzuru Bustani ya Pekee
MAMA yangu alipenda maua ya waridi. Aliyakuza. Nilipokuwa mtoto nilitumia muda wa saa nyingi pamoja naye katika bustani yake, niking’oa magugu, nikipogoa, nikikata, na kutunza mimea hiyo. Alinifunza kwamba kilimo cha bustani ni shughuli inayopendeza. Alinifanya nipendezwe sana na kazi hiyo maishani mwangu mwote.
Kazi yangu ya kilimo cha bustani ilifikia kikomo nilipoondoka nyumbani na kujiunga na Chuo Kikuu cha California huko Berkeley. Nilipokuwa nikijifunza uhandisi, nilithamini bustani maridadi katika eneo la chuo. Vita ilikuwa imepamba moto huko Vietnam, na punde si punde maisha yangu yangebadilika kabisa.
Niliamua kujiandikisha katika kikosi cha kuleta amani na nikapelekwa katika Chuo Kikuu cha Washington ili kuzoezwa. Eneo la chuo hicho lilikuwa kama paradiso. Popote nilipotazama palikuwa na maziwa, bustani, viwanja vyenye nyasi zilizotunzwa vizuri, na milima iliyofunikwa na theluji. Kisha, mnamo 1964, nilihamia La Paz, Bolivia, kufanya kazi ya ualimu katika Chuo Kikuu cha San Andres. Mambo yalikuwa tofauti kama nini! Nilitoka kwenye eneo la usawa wa bahari hadi eneo lenye kimo cha meta 3,500 juu ya usawa wa bahari. Ni mimea michache sana iliyokua huko na sikuweza kuendeleza kilimo cha bustani.
Baada ya kuishi Bolivia kwa miaka miwili, niliajiriwa kazi ya ualimu huko Hawaii, katika shule ya Intermediate School katika jiji la Wahiawa. Niliishi katika nyumba ndogo ufuoni kwenye rasi ya Sunset Point, na nilivutiwa sana na michikichi na mimea mingine ya kitropiki. Nilijihisi nikiwa katika paradiso. Ndipo nilipofikiri juu ya kujihusisha na kilimo cha bustani ya michikichi baadaye.
Nilirejea San Diego, kisha nikasafiri kwa miezi 18 iliyofuata kutoka California hadi Tierra del Fuego, Argentina. Wakati huo nilianza kuisoma Biblia. Nilipokuwa nikisafiri, nilitumia muda mrefu katika misitu, bustanini, na mbugani nikitafakari mambo niliyokuwa nikisoma katika Biblia. Hatimaye, nilirejea San Diego mnamo 1972 na nikaanza kazi ya muda mrefu na yenye kuridhisha ya kufunza hisabati katika Coronado, California. Ndipo hamu yangu ya kulima bustani yenye mimea ya kitropiki katika ua wangu ilipoanza kuongezeka.
Bustani Yangu ya Kwanza
Katika Mei 1973, nilinunua nyumba ndogo karibu na Bahari ya Pasifiki, katika manispaa ya Ocean Beach, California. Nilikuwa na nyumba ndogo—juu ya mlima, yenye ua mkubwa, na nilitamani kilimo cha bustani. Hali hizo zilifaa kabisa mradi wangu, bustani yangu ya pekee.
Mwanzoni, bustani yangu ilikuwa shaghalabaghala. Ulikuwa mradi usiofua dafu. Nilinunua na kupanda mmea wowote ulionivutia. Niliendelea tu kupanda mmea wowote ulionivutia na kunipendeza. Niliitazama ikikua—miti ya matunda, misonobari, miti inayopukutika majani, miti isiyokauka, vichaka, pori, maua. Nilipanda mimea yoyote ile.
Mingi ya mimea hiyo ni ile niliyokuwa nimeiona utotoni. Kazi ya kutunza mimea ilikuwa yenye utulivu, ya kupendeza, yenye kuboresha afya ya kiakili na kimwili, na yenye kuthawabisha. Nilitafakari juu ya umaridadi, ubuni, utata, na kusudi la mimea hiyo.
Sikupendezwa na kila mmea wala si yote iliyonifaa kazini, kwa hiyo nilitupa mimea mingi. Nilikuwa nikitafuta umaridadi wa pekee. Mimea iliyokua pasipo utaratibu na yenye kukua haraka-haraka haikunipendeza. Mimea hiyo ilihitaji kazi kubwa na utunzi mwingi! Pia, nilitaka mimea isiyo ya kawaida tu—wala si ile inayokua katika bustani yoyote. Nilihitaji mimea ya pekee. Kisha ikawa hivyo!
Mchikichi Wangu wa Kwanza
Mnamo 1974, nilizuru bustani ya miche ya karibu, na humo nilipata mmea niliokuwa nikitafuta. Ulikuwa maridadi, ukiwa na kilele kinachovutia cha vitawi vyenye umbo la tao vya rangi ya buluu na kijani kibichi. Ulikuwa Butia capitata, unaoonwa na wengi kuwa mchikichi maridadi zaidi ulimwenguni. Nyakati nyingine huitwa jelly palm kwa sababu ya mbegu zake tamu zifananazo na tunda. Unatoka Amerika Kusini, ni rahisi kuutunza, na hukua kufikia kimo cha meta tano. Hatimaye, bustani yangu ilikuwa na mimea ya pekee—michikichi iliyo adimu kutoka ulimwenguni pote! Nilikuwa nimechagua kilimo cha “mimea Bora katika jamii ya mimea.”
Punde si punde nilianza kukusanya michikichi iliyo adimu au ya pekee kutoka kwa bustani mbalimbali za miche. Katika pembe ya bustani moja ya miche, mbele yangu tu niliona mchikichi mwingine wa kuvutia sana—mchikichi wa Mexican blue fan. Una jani gumu, lenye umbo la kipepeo, lenye rangi ya buluu na kijani kibichi, ambalo linaenea kutoka kwenye ncha iliyo shinani na kufanyiza kilele. Miiba iliyo kwenye mbegu ya ua huchomoza juu na kufanyiza matao maridadi sana ya rangi ya manjano hafifu. Mchikichi uliokomaa hukua kufikia kimo cha meta 12 hivi.
Kwa kweli nilivutiwa sana na michikichi. Ningepata wapi mimea mingine adimu kama hii? Nilianza kutafutatafuta katika eneo la San Diego bila mafanikio yoyote. Ndipo nilipopata chanzo cha habari muhimu—Tawi la Kusini mwa California la Shirika la Kimataifa la Kilimo cha Michikichi. Shirika hilo lina maelfu ya wanachama katika nchi 81. Lina habari chungu nzima juu ya kila mchikichi unaojulikana—zaidi ya jamii 200 na spishi zipatazo 3,000! Tawi la Kusini mwa California huchapisha jarida The Palm Journal kwa ajili ya wanachama wake, jarida hilo huwa na habari muhimu ya karibuni zaidi.
Kuwa mwanachama kumeniwezesha kupata na kukuza zaidi ya aina 150 za michikichi katika bustani yangu ndogo. Ninaiita ndogo kwa sababu ina ukubwa wa meta 650 za mraba. Michikichi niliyo nayo ni michache sana ikilinganishwa na spishi ambazo zimepata kugunduliwa kufikia sasa. Ni ipi ninayoipenda sana?
Baadhi ya Michikichi Maridadi Katika Bustani Yangu
Kwa kweli, ninapenda mimea yote niliyo nayo, lakini michache ni yenye kutokeza sana. Mingine hunivutia sana hasa kwa sababu ya umbo lake la pekee sana au kwa sababu ya ngozi yake yenye miiba; mingine, kwa sababu ya rangi yake au ukubwa au hata kazi ya kuikuza katika tabia ya nchi ya kusini mwa California inayofanana na ya Mediterania.
Mojawapo ya michikichi ya pekee kwangu hutoka Madagascar, nje kidogo ya pwani ya mashariki ya Afrika. Mchikichi huo unaitwa Bismarckia nobilis. Mbona ninaupenda? Kwa sababu ya rangi yake ya pekee ya zambarau-zambarau yenye buluu, kuadimika kwake, na umbo la jani lake. Kila kitawi kina uzito wa kilogramu tisa, jambo linalofanya mchikichi huu uwe mojawapo ya michikichi mikubwa zaidi ulimwenguni.
Mchikichi mwingine ninaoupenda sana, mchikichi wa fishtail, unatoka katika maeneo ya mlimani kaskazini mwa India, Myanmar, na Sri Lanka. Michikichi ya aina hii niliyoipanda hapa San Diego inafanya vyema licha ya majira ya baridi kwa kulinganishwa. Kwa hakika, ninapenda kazi ngumu ya kukuza michikichi hapa. Hiyo ndiyo sababu ninafurahi sana kuwa na mchikichi utokao Borneo katika bustani yangu—unaitwa Arenga undulatifolia. Una majani mapana yenye mapinde ya kutokeza.
Hivi karibuni nilipanda mchikichi wa Burretiokentia hapala kutoka New Caledonia, eneo la Ufaransa lililo ng’ambo katika Pasifiki ya Kusini. Kwa sasa unanawiri. Naweza kutaja pia michikichi mingine iliyo ya pekee kwangu, kama vile Pritchardia hildebrandii, au mchikichi wa loulu, kutoka Hawaii, wenye majani ya manjano na kijani kibichi yenye umbo la kipepeo. Hufanya vyema juani na kwa hakika ni mchikichi wa pekee.
Mchikichi wenye kuudhi ni Trithrinax acanthacoma, au mchikichi wa spiny fiber. Shina lake lina miiba yenye umbo la sindano, yaonekana ni kama inasema, “Usisonge karibu sana!”
Hivi karibuni nilianza kukuza cycad. Cycad ni mmea mdogo wenye umbo sawa na mchikichi ijapokuwa si wa jamii hiyo. Mchikichi mwingine ninaoupenda ni Encephalartos gratus, una kitawi cha ajabu kinachoonekana ni kama kinaruka hewani. Huvutia kila mtu. Kwa kawaida maganda ya kokwa, huwa makubwa na hukua pembeni mwa mmea huo. Hufanana na nanasi au na sonobari.
Je, michikichi yangu huvutia watu? Bila shaka ndiyo! Mara kwa mara mimi hukutana na watu wanaozuru na kustaajabia mimea yangu. Wanapokuwa kwenye kijia kinachoelekeana na nyumba, wao huweza kuona bustani ya pekee ya kitropiki kwenye mteremko wa kilima. Katika Machi 1997 bustani yangu ilikuwa mojawapo ya bustani tatu zilizofunguliwa kwa wageni na Tawi la Kusini mwa California la Shirika la Kimataifa la Kilimo cha Mchikichi. Ilielezwa kuwa “mahali pa kupata elimu ya mkusanyo maridadi wa michikichi mbalimbali.” Bustani hii imeletaje baraka kwangu na kwa wengine?
Bustani Yangu Hutoa Ushahidi
Nilibatizwa mwaka wa 1991 baada ya kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova. Nimestaafu sasa kutoka kwa kazi ya ualimu, lakini mimi huwa na shughuli nyingi sana nikiwa mzee Mkristo na mhudumu painia. Ni jambo la kupendeza kutumia bustani yangu kuwa chanzo cha mazungumzo juu ya Muumba pamoja na watu ninapoeleza ubuni wa ajabu wa miti mbalimbali na mimea niliyo nayo. Nyakati nyingine, mimi huanza mazungumzo kwa kueleza kwamba michikichi [mitende] hutajwa katika Biblia. (Waamuzi 4:5; Zaburi 92:12) Kwa kweli bustani hii imenisaidia kumkaribia Mungu na kuelewa kusudi lake la ajabu sana la kuwawezesha wanadamu watiifu waje waishi katika paradiso. Kwa vyovyote, Paradiso ya kwanza ya Edeni ilikuwa bustani maridadi kabisa.—Mwanzo 2:8.
Kulingana na unabii wa Biblia, hali hiyo ya Paradiso itarudishwa Yehova atakapowaangamiza wale wanaoiangamiza dunia sasa. (Ufunuo 11:18; 16:14, 16) Ndipo sote tutakapoweza kushiriki kazi ya kuifanya tena dunia iwe paradiso yenye kustaajabisha. Kwa wakati wa sasa, shamba langu dogo linaendelea kumsifu Muumba.—Imechangwa.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mchikichi wa “Mexican blue fan”
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mchikichi wa “Fishtail”
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Kushoto hadi kulia: “red pandanus,” mchikichi wa “royal,” mchikichi wa “traveler” (si ukubwa halisi)
[Picha katika ukurasa wa 17]
“Encephalartos ferox”
[Picha katika ukurasa wa 17]
Ua kwenye mchikichi wa “shaving brush”
[Picha katika ukurasa wa 18]
Vifaa vyangu vya kilimo cha bustani