Kokwa ya Tagua—Je, Yaweza Kuokoa Tembo?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA EKUADO
NI MARAFIKI wasio wa kawaida. Mmoja ana uzito wa gramu kadhaa; mwingine, ana uzito wa tani kadhaa. Mmoja ni mmea; mwingine ni mnyama. Wanaishi katika kontinenti tofauti. Na bado, kokwa ndogo ya tagua ya Amerika Kusini yaweza kuokoa tembo mkubwa wa Afrika kutokana na uchinjaji ulioenea. Kokwa ya tagua ni nini, na imekuja kuwaje rafiki ya tembo?
Mchikichi wa Ajabu
Kokwa ya tagua ni mbegu ya jamii fulani ya mchikichi inayopatikana hasa kaskazini mwa Amerika Kusini. Miti hiyo inayokua polepole huwa na vitawi vyenye kuvutia sana vinavyochomoza juu ya ardhi. Hakuna shina linaloonekana kwa miaka mingi. Mchikichi wa tagua uliodumu kwa angalau miaka 35 hadi 40 huwa na shina lenye kimo cha meta mbili. Vichala vikubwa vyenye nyuzinyuzi hukua chini ya vitawi. Kwa kawaida, kichala kimoja huwa na uzito wa kilogramu 10, na huwa na matunda yaliyosongamana yenye nyuzinyuzi. Kwa kawaida kila tunda huwa na mbegu zipatazo nne hadi tisa, zilizo na ukubwa na umbo linalofanana na la yai la kuku. Katika hatua ya kwanza ya ukuzi, mbegu huwa na maji kama ya nazi yenye kukata kiu. Katika hatua ya pili, maji hayo huganda na kuwa nyama tamu inayolika. Katika hatua ya tatu na ya mwisho, nyama hiyo hukomaa na kuwa dutu nyeupe ngumu inayoshabihi sana pembe ya tembo.
Sababu Inayofanya iwe Rafiki ya Tembo
Kokwa ya tagua inapotumiwa badala ya pembe za tembo kwa kweli inaweza kuitwa rafiki ya tembo. Uwindaji haramu wa kikatili wa wanyama kwa ajili ya pembe umehatarisha tembo wa Afrika. Hata hivyo, kokwa ya tagua ni kibadala kinachofaa, kwa kuwa pembe yake inayotokana na mmea hufanana na pembe ya tembo, ni ngumu sana, ina mng’ao wa hali ya juu, na hufyonza rangi kwa utayari. Kokwa ya tagua hufanana sana na pembe ya wanyama hivi kwamba mara nyingi wasanii huacha magamba machache ya kikahawia kwenye bidhaa zao ili kuthibitisha kwamba hawatumii pembe za tembo—ambazo zimepigwa marufuku ulimwenguni pote.
Pembe inayotokana na mimea haikugunduliwa hivi karibuni. Zamani sana mwaka wa 1750, mtawa wa Amerika Kusini Juan de Santa Gertrudis alitaja kokwa za tagua katika tarihi zake, akizilinganisha na “mabonge ya marumaru” yaliyotumiwa katika uchongaji wa sanamu. Kufikia mapema miaka ya 1900, Ekuado, chanzo kikuu cha tagua, ilikuwa ikiuza nje maelfu ya tani za kokwa hizo kila mwaka, hasa kwa ajili ya utengenezaji wa vifungo. Baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, kutokea kwa plastiki mpya zenye gharama nafuu nusura kukomeshe biashara ya tagua. Hivi karibuni kwa kipindi cha miezi 18, tani 1,650 za tagua kutoka Ekuado ziliuzwa Italia, Japani, Marekani, Ujerumani na katika nchi nyingine 18 huo ukiwa uthibitisho wa kurudi kwa pembe inayotokana na mimea.a Tagua hutayarishwa na kutumiwaje leo?
Tagua Hutumiwa kwa Njia Nyingi
Mbegu zake huanikwa katika jua la kitropiki ili zikauke kwa muda wa mwezi mmoja hadi miezi mitatu, ikitegemea umajimaji wake. Baadaye, humenywa na mashine, huainishwa kulingana na ukubwa, na hukatwa kwa vipande vinavyotumiwa kutengenezea vifungo. Kwa kweli, vifungo vya “pembe” vilivyotengenezwa kwa tagua huremba baadhi ya mavazi bora kabisa ulimwenguni. Hata hivyo, tagua haitumiwi tu kwa vifungo. Mapambo ya vito, kete za chesi, tete za ala za muziki za kupulizwa, vibao vya piano, na mipini ya miavuli ni baadhi ya bidhaa mbalimbali zinazofanyizwa kwa tagua.
Lakini mchikichi wa tagua una matumizi zaidi! Poda laini inayobaki baada ya utayarishaji hutumiwa kuboresha vyakula vya wanyama. Hutumiwa pia katika uchomaji wa makaa. Majani ya mchikichi wa tagua hufanyiza vifaa vya paa visivyovuja. Kwa kuongezea, uvunaji, utayarishaji pamoja na uuzaji nje wa tagua hutokeza fursa za kuajiri watu wengi.
Zaidi ya yote, pembe inayotokana na mimea yaweza kuchangia sana uhifadhi wa tembo wa Afrika. Kwa hiyo ikiwa unatamani umaridadi wa pembe, huhitaji kutafuta tu katika uwanda wa savanna ya Afrika. Tafuta katika misitu ya mvua ya Amerika Kusini ambamo pembe ni tele ajabu hivi kwamba zinakua mitini! Naam, fikiri juu ya kokwa ya tagua, rafiki ya tembo.
[Maelezo ya Chini]
a Kati ya Januari 1, 1994, na Juni 15, 1995.
[Picha katika ukurasa wa 24, 25]
1. Mchikichi wa “tagua”
2. Vichala vya matunda ya “tagua”
3. Mbegu za “tagua” zaonekana penye mkato
4. Mbegu za “tagua” hukauka na kuwa kokwa ngumu
5. Vifungo vya “tagua”
6. Kito cha “tagua” kilichopambwa kwa lulumizi
7. Sanamu za “tagua”